Somo La Kumi Na Nane: Fadhila Na Mwonekano Wa Az-Zahrau (A.S.)
Imani Na Ibada Zake Kwa Ajili Ya Mwenyezi Mungu
Kumwamini Mwenyezi Mungu ndio alama ya mwanadamu mkamilifu, na ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndio ngazi ya kufikia kilele cha ukamilifu. Na hakika manabii wamepata makazi bora katika nyumba ya heshima kutokana na daraja lao la imani na juhudi zao za kuchuma mema hapa duniani na moyo mkunjufu katika ibada kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Qur’ani ndani ya Sura Ad-Dahri imethibitisha ukamilifu wa moyo mkunjufu wa Az-Zahrau na unyenyekevu wake kwa Mwenyezi Mungu, ukubwa wa imani yake Kwake na siku ya mwisho, imani ambayo imetengeneza mfano bora wa kuigwa kama alivyothibitisha hilo Mtume (s.a.w.w.) kwa kusema: “Hakika binti yangu Fatima moyo wake na viungo vyake vimejazwa imani na Mwenyezi Mungu mpaka kwenye mfupa wa ubongo, hivyo akatetemeka kwa ajili ya kumtii Mwenyezi Mungu.”1
Akasema tena: “Hakika anaposimama mihrabuni mbele ya Mola wake nuru yake huwang’aria malaika wa mbinguni kama nuru ya sayari inavyowang’aria watu wa aridhini, hapo Mwenyezi Mungu huwaambia malaika wake:
Enyi malaika Wangu, hebu mtazameni mja wangu wa kike Fatima, mbora wa waja wangu wote wa kike, amesimama mbele yangu huku viungo vyake vikitetemeka kwa kuninyenyekea, amenielekea kwa moyo wake akiniabudu, nawathibitishieni kuwa nimewasalimisha wafuasi wake dhidi ya moto.”2
Hasan bin Ali (a.s.) amesema: “Nilimwona mama yangu Fatima amesimama mihrabuni kwake usiku wa Ijumaa, aliendelea kurukuu na kusujudu mpaka ikachomoza asubuhi huku nikimsikia akiwaombea heri waumini wa kiume na wa kike, akiwataja kwa majina yao, huku akizidisha kuwaombea ilihali yeye mwenyewe hajajiombea chochote. Nikamwambia: Ewe mama yangu mpendwa! Kwa nini hujiombei kama unavyowaombea wengine? Akajibu: “Ewe mwanangu mpendwa! Kwanza jirani kisha wa ndani.”3
Saa za mwisho za mchana wa Ijumaa alikuwa akizifanya ni maalumu kwa ajili ya dua. Pia alikuwa halali lifikapo kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Alikuwa akiwahimiza wote waliyomo nyumbani kwake kuuhuisha usiku huo kwa ibada na dua. Hasan Al-Basri amesema: “Hakutokea mtu mfanya ibada sana ndani ya umma huu kama Fatima, alikuwa akisimama kufanya ibada mpaka nyayo zake zinavimba.4 Alikuwa akihema ndani ya Swala yake kwa ajili ya kumwogopa Mwenyezi Mungu.”5
Je ndani ya maisha yake Fatima aliwahi kutoka kwenye mihrabu yake? Hapana. Hakika humwabudu Mwenyezi Mungu nyumbani kwake kwa kuwa mke bora na kuwalea wanawe malezi bora huku akimtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza huduma zote za jamii, aliwasaidia mafakiri na kuwapendelea kuliko nafsi yake hata kama hana cha kujitosheleza.
Mapenzi Na Huruma Yake
Az-Zahrau (a.s.) alichukua mapenzi, upendo na huruma toka kwa baba yake, hivyo alikuwa mwana mwema kwa Mtume (s.a.w.w.). Alimpenda Mtume (s.a.w.w.) kwa dhati, hivyo akampendelea kuliko nafsi yake. Alikuwa akihudumia nyumba ya baba yake huku akitekeleza ayatakayo Mtume (s.a.w.w.), hivyo anatekeleza yanay- omfaa Mtume (s.a.w.w.), yanayompa raha na utulivu huku akiharak- isha kutenda kila linalomridhisha baba yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Anamwandalia maji ya kuoga, chakula, anafua nguo zake, zaidi ya hapo anashirikiana na wanawake wengine kubeba chakula na vinywaji kwa ajili ya kuhudumia na kuwatibu majeruhi.
Hakika katika vita vya Uhud alitibu majeraha ya baba yake, hivyo alipoona damu hazikatiki akachukua kipande cha mkeka kisha akakiunguza mpaka kikawa jivu kisha akamwagia jivu hilo kwenye jeraha na hapo damu ikasimama. Akamletea kipande cha mkate wakati wa kuchimba handaki, Mtume (s.a.w.w.) akamuuliza: “Ni kitu gani hiki ewe Fatima?” Akajibu: “Ni kipande cha mkate nilioutengeneza kwa ajili ya wanangu wapendwa hivyo nimekuletea kipande chake.”
Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Hakika hiki ndio chakula cha kwanza kinachoingia mdomoni mwa baba yako tangu siku tatu.”6
Hakika Az-Zahra (a.s.) aliweza kuziba pengo la mapenzi, pengo ambalo Mtume (s.a.w.w.) alilipata baada ya kufiwa na wazazi wake wawili na mkewe mtukufu Khadija (r.a.) huku akiwa katika mazingira magumu ya ulinganio wa jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na hapa tunafahamu kiini cha lile alilolikariri Mtume (s.a.w.w.) ulimini mwake kwa kusema: “Fatima ni mama wa baba yake.”7
Alikuwa akihusiana naye uhusiano wa mama, anaubusu mkono wake, anakuwa wa kwanza kumzuru aingiapo Madina na wa mwisho kumuaga atokapo Madina.
Safari na misafara yake ya kivita huanzia nyumbani kwa Fatima (a.s.), hivyo alikuwa akijiongezea baraka na upendo katika safari na misafara yake toka katika chemchemu hii safi. Pia alikuwa akirudi mara kwa mara nyumbani kwa Fatima, hivyo Fatima (a.s.) humpokea kama mama ampokeavyo mwanae, humlea, humkumbatia na humpunguzia machungu huku akimuhudumia na kumtii.
Mapambano Yake Endelevu
Fatima (a.s.) alizaliwa kipindi cha mapambano kati ya Uislamu na Ujahiliya. Akafumbua macho yake huku waislamu wakiwa katika jihadi kali dhidi ya ushirikina wenye kiburi. Maquraishi waliweka vikwazo dhidi ya Mtume (s.a.w.w.) na Bani Hashim wote, hivyo Mtume (s.a.w.w.), mkewe mpiganaji, na binti yake mtakasifu wote wakaingia bonde la Abu Twalib, humo wakawekewa vikwazo muda wa miaka mitatu, wakaonjeshwa aina za ukata na ugumu wa maisha. Pamoja na hayo yote lakini walipambana katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutetea haki na kujitolea kwa ajili ya imani tukufu.
Miaka ya vikwazo vizito na vigumu ikapita na Mtume (s.a.w.w.) akatoka huku akiwa ameshinda. Ndani ya mwaka huo huo Mwenyezi Mungu akapenda kumchagua Khadija, pia ndani ya mwaka huo aka- fariki Abu Twalib ami wa Mtume (s.a.w.w.) na mtetezi wa Uislamu, hivyo huzuni na uchungu vikachukua moyo wa Mtume (s.a.w.w.) baada ya kuwa amemkosa kipenzi cha moyo wake.
Hivyo ndivyo Fatima (a.s.) alivyopatwa na msiba huku akiwa bado hajashiba mapenzi ya mama yake, na hapo akaungana na baba yake katika machungu. Japokuwa alimkosa mama yake, chanzo cha mapenzi, lakini Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akijaribu kumpa mapenzi mbadala toka kwake badala ya mapenzi makubwa ya mama yake.
Baada tu ya kufariki ami yake na mtetezi wake Abu Twalib maquraishi walimwagia kila chuki yao na maudhi yao juu ya Mtume (s.a.w.w.) huku Az-Zahrau (a.s.) akiona kwa macho yake maudhi yote yanayofanywa na wajinga na waovu wa kiquraishi, ilihali Mtume (s.a.w.w.) akitaka kuwatoa gizani na kuwapeleka kwenye nuru.
Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akijaribu kumpunguzia machungu huku akimhimiza kuwa na subira kwa kumwambia: “Ewe mwanangu mpendwa usilie, hakika Mwenyezi Mungu anamlinda na kumnusuru baba yako dhidi ya maadui wa dini Yake na ujumbe wake”.8
Hivyo ndivyo alivyokuwa Mtume (s.a.w.w.) akipandikiza roho ya mapambano ya juu ndani ya nafsi ya binti yake huku akiujaza moyo wake subira na imani ya ushindi.
Az-Zahra (a.s.) alihamia Madina baada ya baba yake kuhama toka anga la Makka la kutisha. Alihama na mtoto wa ami yake Ali bin Abu Twalib (a.s.) ambaye alidharau kiburi cha ujeuri wa maquraishi hivyo Az-Zahrau (a.s.) akaungana na Mtume (s.a.w.w.) huko Kuba baada ya miguu yake kuvimba kutokana na kutembea.
Kwa unyeyekevu Az-Zahrau (a.s.) akahamia kwa mumewe huko Madina baada ya baba yake kusimamisha misingi ya dola, akashirikiana na baba yake katika mapambano kwa subira dhidi ya matatizo ya maisha na misukosuko ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu huku Fatima akijaribu kutoa sura halisi ya mfano wa kuigwa katika maisha mapya ya ndoa.
Az-Zahrau (a.s.) alichangia sehemu kubwa na ya kuonekana katika kuinusuru haki na kutetea usia wa Mtume (s.a.w.w.) pale aliposimama kidete dhidi ya uendaji kinyume, akapiga kelele kwa namna isiyo na mfano huku akiwa pembeni ya kipenzi chake Ali bin Abu Twalib (a.s.) ndani ya siku ngumu za maisha yake ili ahakikishe kuwa uwanja wa ndani wa Ali (a.s.) ni imara haudhoofiki. Pamoja na hayo yote anaacha uamuzi na msimamo wa mwisho utolewe na kuchukuliwa na kiongozi wake, mume wake na Imam wake Ali (a.s.) ili aamue linalonasibiana sana na mazingira.
Az-Zahrau (a.s.) alikuwa akienda kila Jumamosi asubuhi kwenye makaburi ya mashahidi katika viwanja vya Uhud kisha akiwaombea rehema na msamaha. Hakika vitendo hivi vinaonyesha ni kwa kiwango gani Fatima (a.s.) alithamini jihadi na shahada huku vikiweka wazi thamani ya maisha yake kivitendo, maisha ambayo yalianza kwa jihadi, yakategemea jihadi, yakakomea kwa jihadi, hiyo ni ili apate cheo cha shahidi.9
Muhtasari
Az-Zahrau (a.s.) alifuata nyayo za baba yake katika kila jambo, hivyo Mtume (s.a.w.w.) anathibitisha kuwa Mwenyezi Mungu ameujaza moyo wake na viungo vyake vyote imani kwa ajili yake. Pia walioishi naye wamethibitisha kuwa alikuwa mtu wa ibada sana kuliko watu wote.
Pia amefahamika kwa huruma kwa baba yake mpaka akampendelea kuliko nafsi yake, wanawe, hivyo baba yake akampa jina la: Mama wa baba yake.
Alibeba jukumu la jihadi katika njia ya Mola Wake kabla na baada ya kuolewa. Akasimama imara mbele ya matatizo baada ya kufariki baba yake ili aing’arishe njia ya haki kwa wapitaji.
Maswali
1. Toa wasifu wa ibada ya Az-Zahrau (a.s.)?
2. Az-Zahrau (a.s.) alishiriki na baba yake katika vita gani?
3. Elezea jinsi Az-Zahrau (a.s.) alivyompunguzia machungu baba yake?
4. Elezea sifa za Az-Zahrau (a.s.) kama mama?
5. Ni upi mchango na nafasi ya Az-Zahrau (a.s.) katika kuimarisha ujumbe wa Mtume (s.a.w.w.)?
- 1. Biharul-An’war, Juz. 43 Uk. 46 na 56-58
- 2. Biharul-An’war, Juz. 43 Uk. 46 na 56-58.
- 3. Amaali As-Suduq, Al-Majlis 24, Uk. 100.
- 4. Iddatud-Dai, Uk.139.
- 5. Iddatud-Dai, Uk.139.
- 6. Awalimul-Uluum, Juz. 1 Uk. 244 amenukuu toka kwenye kitabu Majmauz-Zawaid, Juz. 1 Uk. 312.
- 7. Rejea Usudul-Ghaba, Juz. 5 Uk. 520. Al-Istiaab, Juz. 4 Uk. 380.
- 8. Siratul-Mustafa, Uk. 295
- 9. Tazama Fatimatuz-Zahrai Witri fi Ghumdi, utangulizi wa Sayyid Musa As- Sadri