read

Somo La Kumi Na Nne: Urithi Wa Imam Ali (A.S.)

Falsafa ya utawala na nidhamu yake

Kwanza: Utawala Ni Dharura Ya Kijamii

Uimamu ni mpangilio wa umma.
Lazima watu wawe na kiongozi, awe mwema au mwovu.

Pili: Falsafa Ya Utawala

Utawala Ni Jambo Linalokuja Na Kutoweka

Dola kama inavyokuja ndivyo inavyorudi.
Utawala wenye kuhama wenye kuondoka ni jambo dhalili jepesi.

Utawala Ni Njia Si Lengo

Ewe Mwenyezi Mungu, hakika wewe unafahamu kuwa yale yaliyoto- ka kwetu hayakuwa kwa ajili ya kugombania utawala wala kupata chochote kati ya mabaki ya kinachosagika. Lakini yalitoka kwa ajili ya kuhami mafunzo ya dini Yako na kudhihirisha wema katika nchi yako, ili wasalimike wale waliyodhulumiwa miongoni mwa waja Wako na zifanyiwe kazi hukumu Zako zilizoachwa.

Utawala Ni Sehemu Ya Kutahinia Maisha

Akili za watu hutahiniwa kwa mambo sita: Urafiki, mahusiano, utawala, kuvuliwa cheo, utajiri na ufakiri. Uwezo hudhihirisha sifa njema na mbaya.

Tatu: Majukumu Ya Dola Ya Kiislamu

Kuuelimisha Umma

Ni wajibu wa Imam kuwaelimisha anaowatawala sheria ya Uislamu na imani yake.

Kusimamia Uadilifu

Uadilifu ni nguzo ya raia. Uadilifu ni nidhamu ya utawala.
Hakuna kinachowapa hali nzuri raia isipokuwa ni uadilifu tu.
Kwa uadilifu hufuatwa sunna za Mwenyezi Mungu na dola huimarika.

Kuihami Dini

Kila dola inayozungukwa na dini huwa haishindwi. Watawala ni watetezi wa dini.
Atakayefanya utawala wake ni kutoa huduma kwa ajili ya dini yake basi kila kitu kitamnyookea.

Kutekeleza Sheria

Kuwalazimisha waja wa Mwenyezi Mungu kutekeleza hukumu za Mwenyezi Mungu ni kutekeleza haki na kila chenye manufaa.

Kati ya majukumu aliyobebeshwa Imamu na Mwenyezi Mungu ni kutekeleza adhabu kwa yule anayestahiki.

Kujitahidi Kutoa Nasaha

Imam hana jukumu lolote isipokuwa lile alilobebeshwa toka kwenye amri ya Mola Wake nalo ni kuzidisha mawaidha na kujitahidi kutoa nasaha.

Kuhakikisha Kipato Na Kuboresha Maisha

Ama haki yenu iliyopo kwangu ni kuwanasihi na kuwahakikishieni kipato chenu.
Watawala wenye hali nzuri sana ni wale ambao maisha ya watu yan- aboreka wanapoishi nao.

Kulea Umma

Ama haki yenu iliyopo kwangu ni kuwanasihi…..kuwafunza ili msiwe wajinga na kuwaadabisha kama mlivyojifunza.

Kutetea Uhuru Wa Nchi Na Heshima Ya Taifa

Katika mafunzo ya Imamu kwa magavana wake ni kauli hii: “Hifadhini mipaka yao na pembe za nchi zao.” Pia akasema: “Lazima watu wawe na kiongozi…..watakayemtumia kumpiga adui.”

Kuleta Usalama Wa Ndani

Lazima watu wawe na kiongozi…….ambaye kupitia yeye njia zote zitakuwa na amani.

Kuwasaidia Wasiyojiweza

Zaka ya mtawala ni kumsaidia asiyejiweza.

Kujali Ujenzi Wa Nchi

Ubora wa mtawala ni kujenga nchi.

Kuwatetea Madhaifu

Dhaifu huendelea kutetewa dhidi ya mwenye nguvu mpaka mwema atakapostarehe na dhaifu akastarehe dhidi ya muovu.

Nne: Sababu Za Kudumu Dola Na Sifa Ya Mtawala Wa Kuigwa

Kufahamu Mambo

Imam anahitaji moyo wenye akili.
Akili iliyojiepusha na machafu huamrisha mema.

Kuifuata Haki Na Kuidhihirisha Vitendoni

Atakayeifanya haki kuwa ndio dira basi watu watamfanya mtawala. Atakayeitawala nafsi yake
atapata utawala.

Utawala wako ukipenya hadi ndani ya nafsi yako basi nafsi za watu zitajikusanya kuelekea kwenye uadilifu wako.

Kiongozi bora ni yule ambaye matamanio yake hayamwongozi. Kiongozi mwenye akili sana ni yule anayeitawala nafsi yake kwa ajili ya raia kupitia yale yanayoangusha hoja za raia dhidi yake,
Na akawatawala raia kupitia yale yanayothibitisha hoja yake dhidi yao.

Ushujaa Katika Kutekeleza Haki Na Kusimamisha Uadilifu

Imam anahitaji moyo wenye akili na ulimi wenye kauli na moyo mpana ili asimamishe haki nzito.

Nia Njema

Mtawala bora ni yule mwenye vitendo na nia njema, mwadilifu kwa askari wake na raia wake.

Ufasaha Wa Maneno

Imam anahitaji….ulimi wenye kauli.

Ihsani Kwa Raia

Atakayewafanyia ihsani raia wake Mwenyezi Mungu humtandazia mbawa za rehema zake na humwingiza katika msamaha wake. Atakayewafanyia ihsani watu wake anastahiki utawala.

Kueneza Uadilifu Kwa Watu Wote

Nguzo ya utawala ni uadilifu.
Atakayefanya uadilifu utawala wake hupenya.

Aliye mwadilifu katika utawala wake hatohitajia wasaidizi wake. Atakayetenda kwa uadilifu Mwenyezi Mungu atalinda utawala wake. Mwenye kuzidi uadilifu wake siku zake husifika.
Mtawala mwenye maadili bora ni yule anayewajumuisha watu kwa uadilifu wake.

Utawa Wa Nafsi

Mtawala bora ni yule mwenye kuizuia sana nafsi yake.
Mbora ni yule asiyebabaishwa wala kudanganywa huku tamaa hazimlaghai.

Uchumi Na Kuratibu Maisha

Hatoangamia yule mwenye kufanya iktiswadi. Siasa nzuri hudumisha utawala.
Uratibu mzuri na kujiepusha na ubadhirifu ni utawala bora.

Uadilifu Wa Nafsi

Uadilifu dhidi ya nafsi ni pambo la utawala. Zaka ya nguvu ni uadilifu dhidi ya nafsi.

Upole

Msingi wa utawala ni kutumia upole. Siasa nzuri ni upole.

Uvumilivu

Uvumilivu ni msingi wa utawala.

Nguzo ya utawala ni kifua kipana (uvumilivu). Msamaha ni Zaka ya uwezo.
Muadhibu mtumwa wako amwasipo Mwenyezi Mungu lakini msamehe akuasipo wewe.

Utawala wa uadilifu hupatikana katika mambo matatu: Kulainika katika jambo ulilo na uhakika nalo, kulipiza kisasi katika jambo la uadilifu na kumpendelea mwenzio katika jambo ulilokusudia.

Kutetea Dini

Ifanye dini kinga ya dola yako, na shukurani kinga ya neema yako, hivyo kila dola inayozungukwa na dini haishindwi, na kila neema inayokingwa na shukurani hainyang’anywi.

Kujizuia Kwa Bidii

Omba msaada wa uadilifu kwa kuwa na nia njema kwa raia, kupun- guza tamaa na kuzidi kujizuia dhidi ya maasi.

Kuhisi Kuwa Mamlaka Ni Amana Ya Mwenyezi Mungu Iliyo Juu Yako

Hakika mtawala ni muhazini wa Mwenyezi Mungu hapa ardhini. Hakika mamlaka yako si wito wa chakula kwa ajili yako.

Kuwa Macho

Ambaye hayajamdhihirikia akiwa macho hawatomnufaisha chochote walinzi wake.
Miongoni mwa alama za dola ni kuwa macho (kuwa chonjo) ili kulin-da mambo.

Kutojivunia Nguvu

Mwenye hadhi hajivunii cheo alichopata hata kama ni kikubwa namna gani, na dhalili hujivunia cheo chake.

Kuamrisha Yanayowezekana

Ukitaka utiiwe omba yanayowezekana.

Mgao Sahihi Wa Kazi Na Kuainisha Majukumu Ya Kila Mmoja

Kila mwanadamu kati ya watumishi wako mpe kazi yake ambayo utamwajibisha kwayo, kufanya hivyo ni bora ili wasitegeane.

Kugawa Wema

Atakayetoa wema wake atastahiki uraisi. Ukarimu ni utawala.
Anayetoa cheo chake husifika.
Pambo la utawala ni kuwapendelea watu (kabla ya nafsi yako).1

Muhtasari

Uislamu ulikuja kuanzisha dola ya Mwenyezi Mungu yenye mpangilio wa Mwenyezi Mungu na utawala wa kuigwa ambao utamhakikishia mwanadamu wema wa sasa na wa baadaye. Mtume (s.a.w.w.) kiongozi aliasisi dola na kusimamisha nguzo zake. Ama wasii wake mlinzi wa ujumbe wake alibainisha mafunzo ya dola ya kuigwa baada ya kufukuza uovu baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.).

Akabainisha sababu za kudumu dola, kukamilika na kuendelea. Akabainisha sababu za kuporomoka dola, ustaarabu wake na utamaduni wake. Ujumbe wake wa kuigwa aliyoutuma kwa gavana wake wa Misri Malik Al-Ashtar unatoa taswira halisi timilifu ya utaratibu wa utawala wa kiislamu.

Maswali

1.Elezea kwa ufupi njia za kuthibiti na kuboreka kwa utawala?
2. Kutokana na kauli za Imam Ali (a.s.) je, tunaweza kupata maeleke- zo ya kumpa baba wa familia
kwa kuzingatia yeye ni mtawala wa familia?
3. Kutokana na maelezo ya Imam Ali (a.s.) mtawala ana wajibu gani juu ya umma?
4. Kutokana na kauli za Imam Ali (a.s.) je, unaweza kuainisha mambo yanayowatoa watawala kwenye
msitari sahihi

  • 1. Tazama Ghurarul-Hikam Wa Durarul-Kalim cha Al-Amidiy, sehemu ya nne, Uk. 327 – 348.