read

Somo La Kumi Na Saba: Fadhila Na Mwonekano Wa Az-Zahrau (A.S.)

Hakika yeye ni binti wa nabii aliyezikomboa na kuziongoza akili zama zote. Pia yeye ni mke wa Imam ambaye alikuwa nguzo miongoni mwa nguzo za haki na mwendelezo wa nabii mtukufu katika historia ya mwanadamu.

Hakika Fatima (a.s.) alipata akili kamilifu, roho nzuri, na dhamira safi, hivyo kwa msimamo wake na urithi wake akatuchorea sifa za njia bora ambayo dini imepita. Hivyo yeye Fatima (a.s.) akawa nguzo kati ya nguzo za dini, kwa ajili hiyo huwezi kujua historia ya Uislamu vizuri bila kujua historia yake.

Hakika Az-Zahra (a.s.) alikuwa mfano bora wa mwanamke katika ubinadamu, utawa, heshima na utukufu, ukiongeza uelevu wa juu na elimu pana aliyokuwa nayo. Fahari hii inatosha, nayo ni kulelewa ndani ya shule ya unabii na kuhitimu masomo yake toka chuo cha utume.

Akanywa toka kwa baba yake Mtume mwaminifu yale aliyokunywa baba yake toka kwa Mola wa ulimwengu.1

Hakika Fatima (a.s.) alisikia Qur’ani toka mdomoni mwa nabii mtukufu na toka kwenye sauti ya Ali (a.s.), hivyo akamwabudu Mola wake baada ya kuzitambua sheria zake, faradhi zake na sunna zake, utambuzi ambao haukufikiwa na yeyote mwingine mwenye sharafu na karama. Na hapa ndipo tunapojua siri ya maneno aliyotamka Aisha kuwa: “Hajampata mwanamke aliyependwa sana na Mtume (s.a.w.w.) kuliko Fatima.” Japokuwa yeye Aisha alibadili hilo akasema: “Sikumwona mtu mkweli mno kuliko Fatima isipokuwa tu yule aliyemzaa.”2

Hivyo ndivyo alivyogeuka Az-Zahrau sura halisi ya mwanadamu mkamilifu ambaye waumini wananyenyekea kwa kumtakasa.

Elimu Yake Na Maarifa Yake

Fatima (a.s.) hakukomea tu kwenye maarifa aliyoandaliwa na nyum- ba ya ufunuo, wala hakuishia kujing’arisha kielimu kutokana na mionzi ya elimu na maarifa yaliyomzunguka pande zote, bali alikuwa akijaribu kumywa elimu nyingine vyovyote iwezekanavyo, hiyo ni kila anapokutana na baba yake na mume wake ambaye ni mlango wa jiji la elimu ya Mtume (s.a.w.w.).
Alikuwa na utaratibu wa kudumu wa kuwatuma watoto wake Hasan na Husein kwenda kwenye darasa la Mtume (s.a.w.w.) kisha huwahoji pindi wanaporejea, hivyo ndivyo alivyokuwa akijali utafutaji wa elimu huku akijali kuwalea wanawe malezi bora. Japokuwa majukumu yake yalikuwa mengi lakini alikuwa akitoa elimu yake kuwapa wanawake wengi wa kiislamu.

Hakika juhudi hizi endelevu za kutafuta elimu na kuisambaza zimemfanya awe miongoni mwa wapokezi wakubwa wa kike wa hadithi.

Pia awe miongoni mwa wabebaji wa sunna takatifu kiasi kwamba kitabu chake kikubwa ambacho alikuwa akikijali sana kikajulikana kwa jina la msahafu wa Fatima.

Tusisahau kuwa kati ya majina yake ni Muhaddathah, yaani msemeshwa. Kwa ajili hiyo anakuwa pacha wa Mariam katika kuzungumzishwa na malaika, na hili ni chimbuko jingine la elimu yake ambayo ilihamia kwa wanawe maasumina wakirithishana wao kwa wao.

Hotuba mbili muhimu alizotoa baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.) zinatosha kuwa dalili juu ya hilo na juu ya ubora wa fikira zake na ukamilifu wa elimu yake.3 Hotuba moja alitoa mbele ya maswahaba wakubwa ndani ya msikiti mtumufu wa Mtume (s.a.w.w.) na nyingine nyumbani kwake. Hakika zimekusanya madhumuni ya kupendeza yanayoonyesha undani wa fikira zake, upana wa maarifa yake, uwezo wa lugha yake, ukweli wa habari zake kuhusu mwelekeo wa umma baada ya umma kuacha njia sahihi baada tu ya kifo cha baba yake. Zaidi ya hapo ni maadili yake ya juu na jihadi yake kubwa kwa Mwenyezi Mungu na katika njia ya haki.

Az-Zahrau alikuwa miongoni mwa Ahlul-Bayt, wao walimcha Mwenyezi Mungu na Yeye akawafunza,4 na hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu alivyomwachanisha kwa elimu na hivyo akaitwa Fatima, kama alivyoelekea kwa Mwenyezi Mungu hivyo akaitwa Al- Batul.

Maadili Yake Bora

Fatima (a.s.) alikuwa mwenye maadili bora, dhamira safi, nafsi safi, mwepesi wa kufahamu, mwenye matendo bora, jasiri shujaa, jasiri wa nafsi, asiyejivuna, asiyedhibitiwa na dunia danganyifu, asiyejikweza na asiye na kiburi.5

Alikuwa mvumilivu, mwingi wa subira, mnyenyekevu mtulivu, mpole mwenye huruma, mtawa mwenye kujihifadhi. Ulimi wake ulikuwa haupiti isipokuwa penye haki.

Hatamki isipokuwa ukweli, hamtaji mtu kwa ubaya, hateti wala hasengenyi. Huhifadhi siri, hutekeleza ahadi, huwa mkweli wa nasaha, anakubali udhuru, hujiepusha kumkosea mtu, na mara nyingi husamehe akosewapo, hivyo hupokea kosa kwa kulipa msamaha.

Alikuwa mbali na shari mwenye kuelemea heri, mwaminifu, mkweli katika kauli yake, mkweli wa dhati na ahadi, alikuwa katika kiwango cha juu cha utawa. Hasukumwi na matamanio yake, kwa sababu yeye ni miongoni mwa Ahlul-Bayt wa Mtume (s.a.w.w.) ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na kuwatakasa moja kwa moja.

Alikuwa aongeapo na mtu au kuhutubia wanaume basi ni lazima kuwa na pazia kati yake na wao, pazia ambayo huzuwia kati yao kwa ajili ya utawa na kujihifadhi.

Alikuwa amekinaika na hali yake akiamini kuwa tamaa hufarakisha moyo na huharibu mambo. Akishikamana na kauli aliyoambiwa na baba yake: “Ewe Fatima vumilia dhidi ya machungu ya dunia ili ufaulu kwa kupata neema za milele.”6

Hivyo alikuwa ameridhika na maisha mepesi mvumilivu dhidi ya ugumu wa maisha, mwenye kutosheka na kidogo cha halali, mwenye kuridhia, mwenye kuridhiwa, hatamani ya mtu mwingine wala hakodolei macho yasiyokuwa haki yake, wala hakujishusha kwenda kumwomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Hakika yeye alijitosheleza kama alivyosema baba yake: “Hakika utajiri bora ni utajiri wa nafsi.”7

Hakika yeye ni mbora ambaye alijielekeza kwa Mwenyezi Mungu na kuiacha dunia yake, akajiepusha na kujitenga na mapambo na udan- ganyifu wake, akafahamu maangamizi yake, akavumilia kutekeleza majukumu yake, huku akipambana na ugumu wa maisha na ulimi wake ukilowana kwa kumtaja
Mola Wake.

Hakika lengo la Az-Zahrau lilikuwa ni Akhera, hivyo hakukusanya furaha za dunia huku akimwona baba yake ameipa mgongo dunia na yote yaliyomo duniani kuanzia ladha, starehe na matamanio ya dunia. Subira yake juu ya matatizo ni maarufu, ukubwa wa shukurani yake wakati wa raha inajulikana, ni maarufu kwa kuridhika na matokeo ya majaliwa ya Mwenyezi Mungu mpaka akasimulia toka kwa baba yake kuwa: “Mwenyezi Mungu ampendapo mja wake humjaribu kwa matatizo, hivyo iwapo atasubiri humkweza na akiridhia humteua.”8

Muhtasari

Kama maadili ya Mtume (s.a.w.w.) ni Qur’ani basi maadili ya Az- Zahra ndio maadili ya baba
yake. Yametudhihirikia maadili bora ya Az-Zahra na utu wake wa juu unaomfanya awe kiigizo kwa
waislam wote.

Mwenyezi Mungu alimfanya bora kuliko wanawake wote wa ulimwenguni kwa sababu yeye amekunywa elimu ya Mwenyezi Mungu, akaamini ujumbe wa Uislamu, akamtii Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa moyo mmoja zaidi ya maelezo.

Aliweza kutoa nguvu zake zote katika njia ya Mwenyezi Mungu, kujenga Uislamu na kuhudumia umma wa waislam kwa ajili ya mapenzi yake kwa Mwenyezi Mungu. Alikuwa na moyo mkunjufu katika imani yake na ibada yake, akakamilika katika kila linalohusu maisha yake mpaka mapenzi yake kwa Mwenyezi Mungu na Mtume yakadhihirika katika kila hatua ya maisha yake.

Maswali

1. Elezea mazingira ya tauhidi aliyokulia Az-Zahrau (a.s.)?
2. Elezea jinsi Az-Zahrau (a.s.) alivyojali elimu na maarifa?
3. Bainisha maadili yake bora ya muhimu?
4. Taja sifa mahsusi za elimu na maarifa ya Az-Zahrau (a.s.)?
5. Elezea ni upi msahafu wa Fatima (a.s.)?
6. Hotuba mbili za Az-Zahrau (a.s.) zina hadhi gani kihistoria?

Kwa Ajili Ya Kujisomea

Az-Zahrau (a.s.) alikuwa ni mbora wa kuwapendelea wengine kuliko nafsi yake huku akimuiga baba yake katika hilo mpaka imekuwa maarufu kuwa alitoa sadaka gauni lake la harusi usiku wa kupelekwa kwa mumewe.

Maelezo yaliyomo ndani ya Sura Ad-Dahri yanatosha kuthibitisha upendeleo wake na ukarimu wake. Jabir bin Abdullah Al-Answariy amepokea kuwa: Mtume alitusalisha Swala ya alasiri na baada ya kumaliza alikaa huku kazungukwa na maswahaba zake, ghafla aka- tokeza mzee wa kiarabu akiwa kijifunga nguo chakavu akiwa dhaifu mwenye uchovu. Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) akamfuata na kumuuliza habari zake. Mzee akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi nina njaa nilishe, sina nguo nivishe na fakiri nipe masurufu.”
Mtume akajibu: “Mimi sina kitu sasa hivi lakini mwonyesha kheri ni sawa na mtenda kheri, hivyo nenda nyumbani kwa yule ambaye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda na yeye anawapenda, humtanguliza Mwenyezi Mungu kuliko nafsi yake, nenda nyumbani kwa Fatima.”

Nyumba ya Fatima ilikuwa imeungana na nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) ambayo alikuwa akiitumia kujitenga na wakeze, akamwambia Bilal: “Ewe Bilal simama umpeleke kwa Fatima.” Akaondoka bedui akiwa na Bilal na alipofika mlangoni kwa Fatima aliita kwa sauti ya juu: “Amani iwe juu yenu enyi kizazi cha Mtume, mapishano ya malaika, mashukio ya Jibril roho mwaminifu akiwa na ufunuo toka kwa Mola wa ulimwengu.”

Fatima akasema: “Waa’leykum salam, ni nani wewe?”
Akasema: “Mimi ni mzee wa kiarabu ninahisi njaa, sina nguo, na masikini. Nisaidie Mwenyezi Mungu atakurehemu.”

Fatuma na Ali na wao walikuwa katika hali kama hiyo kwani walikuwa na siku tatu hawajakula chochote, huku tangu mwanzo Mtume (s.a.w.w.) akiwa anajua hali hiyo. Hivyo Fatima (a.s.) akaenda kuchukua tandiko la ngozi ya kondoo ambalo Hasan na Husein walikuwa wakilalia.

Kisha akamwambia: “Chukua ewe mbisha hodi hakika Mwenyezi Mungu atakubadilishia kwa kukupa kilicho bora zaidi ya hiki.”

Bedui akasema: “Ewe binti wa Muhammad, nimelalamika kwako kuwa nina njaa kisha wewe unanipa tandiko la ngozi ya kondoo nitalifanyia nini huku nikiwa na njaa kama hii?” Fatima (a.s.) aliposikia maneno haya alichukua mkufu uliokuwa shingoni mwake ambao alipewa zawadi na Fatima binti wa ami yake Hamza bin Abdul Muttalib, hivyo akauvua na kumpa bedui kisha akamwambia: “Chukua ukauuze, hakika Mwenyezi Mungu atakubadilishia kwa kukupa kilicho bora zaidi.”

Bedui akachukua mkufu na kwenda nao msikiti wa Mtume (s.a.w.w.) huku Mtume akiwa kaketi na maswahaba zake. Bedui akasema: “Ewe Mtume, Fatima amenipa mkufu huu.”
Mtume akamwambia: “Uza mkufu huo.”

Jabir anasema: Mtume akalia na kusema: “Itakuwaje Mwenyezi Mungu asikubadilishie kwa kukupa kilicho bora zaidi ilihali mkufu huo kakupa Fatima binti wa Muhammad mbora wa wanawake wote wa ulimwengu!”

Ammar bin Yasir akasimama na kusema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! je unaniruhusu kununua mkufu huu?” Mtume akajibu: “Ununue ewe Ammar kwani laiti makundi mawili (binadamu na majini) yangeshirikiana kuununua basi Mwenyezi Mungu asingeyaadhibu kwa moto.” Ammar akasema:
“Ewe bedui! unauza mkufu kiasi gani?”

Akajibu: “Kwa kipande cha mkate na nyama, kwa nguo ya kiyemeni ambayo itanitosha kujisitiri na kumwabudia Mola Wangu na dinari itakayotosha kunifikisha nyumbani kwangu.”

Ammar alikuwa amekwishauza fungu lake alilopewa na Mtume (s.a.w.w.) kutoka kwenye vita vya Khaybar, hivyo alikuwa hajabakiwa na kitu, ndipo alipomwambia: “Nakupa dinari ishirini, dirhamu mia mbili za fedha, nguo ya kiyemeni na usafiri wangu utakufikisha nyumbani kwako na nitakushibisha kwa kukupa mkate na nyama.”

Bedui akasema: “Ewe ndugu! hakika wewe ni mkarimu mno.” Hapo Ammar akaenda naye na kumpa yote aliyomdhamini. Bedui akarudi kwa Mtume (s.a.w.w.) na hapo Mtume akamuuliza: “Je, umeshiba na umevaa?” Bedui akajibu:
“Hakika nimetosheka.”

Mtume (s.a.w.w.) akamwambia: “Mlipe Fatima kwa wema wake.” Bedui akasema: Ewe Mwenyezi Mungu, hakika wewe ni Mola wa tuliyokuzushia na hatuna Mola tunayepasa kumwabudu isipokuwa wewe, na wewe ndiye mtoa riziki kwetu katika kila hali, hivyo ewe Mola, mbariki binti wa Mtume Fatima kwa kumpa neema ambayo hakuwahi mtu yeyote kuiona wala kuisikia.”

Hapo Mtume (s.a.w.w.) akaitikia dua yake na kisha akawageukia maswahaba na kuwaambia: “Hakika Mwenyezi Mungu ameshampa Fatima hayo hapa duniani kwani: Mimi ndiye baba yake wala hakuna yeyote ulimwenguni mfano wangu, na Ali (a.s.) ndiye mumewe na laiti asingeumbwa Ali (a.s.) basi milele Fatima asingepata wa kumstahili, na akampa Hasan na Husein wala hakuna yeyote ulimwenguni aliyeruzukiwa watoto mfano wao, wao ni mabwana wa vijana wa wajukuu wa manabii na mabwana wa vijana wa Peponi.”

Mbele yake alikuwepo Mikdad, Ammar na Salman, Mtume (s.a.w.w.) akawaambia: “Je, niwaongezee?” Wakajibu: “Ndiyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.” Akasema: “Jibril amenijia akaniambia kuwa: Atakapozikwa Fatima malaika wawili watamuuliza: Ni nani Mola wako? Atawajibu: “Allah ndio Mola wangu.” Watamuuliza: “Ni nani nabii wako?” Atasema: “Baba yangu.” “Na ni nani walii wako?” Atajibu: “Ni huyu aliyesimama mdomoni mwa kaburi langu.”

Mtume akasema: “Je, niwaongeze fadhila zake? Hakika Mwenyezi Mungu amemuwekea walinzi kati ya malaika wanamlinda mbele na nyuma, kushoto na kulia, wako naye katika uhai wake, kifo chake na ndani ya kaburi lake.

Wanazidisha kumwombea rehema na amani yeye na baba yake, mume wake na wanae, hivyo atakayenizuru mimi baada ya kifo changu atakuwa kanizuru wakati wa uhai wangu, na atakayemzuru Fatima atakuwa kanizuru mimi, na atakayemzuru Ali bin Abu Twalib atakuwa kamzuru Fatima, na atakayewazuru Hasan na Husein atakuwa kamzuru Ali, na atakayevizuru vizazi vyao wawili hawa atakuwa kawazuru wao wenyewe.”

Hapo Ammar akaenda kuupaka mkufu manukato na kuuweka ndani ya kitambaa cha kiyemeni. Alikuwa na mtumwa aliyemnunua kutokana na fungu lake alilopata toka Khaybari, hivyo akampa mtumwa wake ule mkufu na kumwambia: “Chukua mkufu huu umpelekee Mtume na wewe uwe miliki yake.” Mtumwa akauchukua mkufu ule na kumpelekea Mtume (s.a.w.w.) na kumwambia aliyoambiwa na Ammar. Mtume akamwambia: “Chukua mkufu huu umpelekee Fatima na wewe uwe miliki yake.”

Mtumwa akauchukua mkufu ule na kumpelekea Fatima na kumwambia aliyoambiwa na Mtume (s.a.w.w.). Hapo Fatima akapokea mkufu kisha akamwacha huru mtumwa huku kijana yule akicheka. Fatuma akamuuliza: “Ewe kijana! ni kitu gani kinachokuchekesha?”

Akajibu: “Unanichekesha ukubwa wa baraka za mkufu huu, kwani umemshibisha mwenye njaa, ukamvisha asiye na nguo, ukamtajirisha fakiri, ukampa uhuru mtumwa na mwisho ukarejea kwa mwenyewe.”9

  • 1. Ahlul-Bayt cha Tawfiq Abu Ilmi, Uk.116.
  • 2. Ahlul-Bayt cha Tawfiq Abu Ilmi, Uk.116.
  • 3. Tazama hotuba hizo mbili ndani ya kitabu Al-Ihtijaj cha At-Tabarasiy
  • 4. Anaashiria kauli ya Mwenyezi Mungu: “Mcheni Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atawafunza” Sura Al-Baqarah: 282.
  • 5. Ahlul-Bayt cha Tawfiq Abu Ilmi, Uk.132 - 134.
  • 6. Ad-Durrul-Manthur, Juz. 6, Uk. 261.
  • 7. Nahjul-Fasaha, neno la 2382.
  • 8. Tazama Ahlul-Bayt cha Tawfiq Abu Ilmi, Uk.137.
  • 9. Ahlul-Bait, Uk. 138.