Somo La Kumi Na Sita: Mwonekano Wa Utu Wa Fatima Az-Zahrau
Fatima Az-Zahrau (a.s.) ni binti wa nabii mtukufu na ni mke wa Imam mtukufu na ni mama wa wajukuu wawili Hasan na Husein mabwana wa vijana wa Peponi. Hakika yeye ni uso wenye kung’ara kwa ajili ya utume wa mwisho, na ni chombo safi kwa ajili ya kuendeleza kizazi kitakasifu, na ni chimbuko safi la kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) huku akiwa ni mbora wa wanawake wote ulimwenguni.
Historia yake ni sawa na historia ya utume kwani alizaliwa kabla ya Mtume (s.a.w.w.) kuhama, na akafariki miezi michache baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.).
Aya za Qur’ani tukufu ndani ya miongo hii miwili ya historia ya Uislamu zimebeba karama na fadhila za Az- Zahrau, baba yake, mumewe na wanawe ambao walitoa mfano bora wa jihadi, subira, moyo mkunjufu na kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Ama upande wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) yeye alionyesha utukufu wa nafasi yake na daraja la kutamaniwa alilofikia katika njia ya ujumbe wa Mwenyezi Mungu huku Mtume (s.a.w.w.) akienda sawia na njia ya Qur’ani katika kueleza karama na fadhila za Ahlul-Bayt wote kwa ujumla na kueleza karama na fadhila za moyo wa Mtume (s.a.w.w.) kwa upekee.1
Az-Zahrau Mbele Ya Mbora Wa Mitume (S.A.W.W.)
Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu hughadhibi- ka kwa kughadhibika Fatima na huridhia kwa kuridhia Fatima.”2
Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Fatima ni pande la nyama yangu atakayemuudhi kaniudhi, na atakayempenda kanipenda.”3
Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Fatima ni moyo na roho yangu inayonizunguka.”4
Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Fatima ni mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni.”5
Ushahidi kama huu ni mwingi ndani ya vitabu vya hadithi na sira6 ukipokewa toka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) ambaye hatamki la matamanio yake7 wala hapendelei kwa sababu au nasaba, wala katika jambo la Mwenyezi Mungu haogopi lawama ya mwenye kulaumu.
Kwa kuwa Mtume mtukufu (s.a.w.w.) amezama ndani ya Uislamu na kwa sababu hiyo akawa ni kiigizo chema kwa watu wote ndio maana mapigo ya moyo wake, mtazamo wa macho yake, mpapaso wa mikono yake, hatua za utembeaji wake na mawazo ya fikira zake vyote vimekuwa ni mafunzo kati ya mafunzo ya dini, chanzo cha sheria, taa ya uongofu na njia ya uokovu.
Hakika ushahidi huu kutoka kwa hitimisho la mitume ni medali kwa Az-Zahrau, medali ambazo zinazidi kung’aa kila muda unavyokwenda, hasa pale tunapoangalia chanzo cha msingi ndani ya Uislamu kupitia maneno ya Mtume (s.a.w.w.) aliyomwambia Az-Zahrau kuwa:
“Ewe Fatima, tenda kwa ajili ya nafsi yako, hakika mimi sitokufaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu.”8
Na kauli ya Mtume (s.a.w.w.): “Katika wanaume wamekamilika wengi lakini kwa wanawake hawajakamilika isipokuwa Mariam binti Imran, Asia binti Muzahim mwanamke wa Firaun, Khadija binti Khuwaylid na Fatima binti Muhammad (s.a.w.w.).”9
Na kauli ya Mtume (s.a.w.w.): “Hakika Fatima ni tawi la moyo wangu hunichukiza yanayomchukiza na hunifurahisha yanayomfurahisha,10 na hakika nasaba zote siku ya Kiyama zitakatika ila nasaba yangu, sababu yangu na ukwe wangu.”11
Imepokewa kuwa siku moja Mtume (s.a.w.w.) alitoka huku akiwa kamshika mkono Fatima akasema: “Anayemtambua huyu basi kishamtambua na asiyemtambua basi huyu ni Fatima binti Muhammad, na yeye ni kipande cha nyama yangu, na ni moyo wangu unaonizunguka, hivyo atakayemuudhi atakuwa kaniudhi na atakayeniudhi atakuwa kamuudhi Mwenyezi Mungu”.12
Mara nyingine akasema: “Fatima ndiye nimpendaye sana kuliko watu wote.”13
Maelezo haya ni ushahidi bora juu ya umaasumu wake baada ya Aya ya utakaso, bali yanatuchorea njia ya utambuzi dhidi ya matukio yatakayoukumba Uislamu kiasi kwamba haghadhibiki isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Az-Zahrau Mbele Ya Ahlul-Bayt, Maswahaba Na Tabiina
Kutoka kwa Imam Ali bin Husein Zaynul-Abidin amesema: “Khadija hakumzalia Mtume (s.a.w.w.) mtoto yeyote ndani ya maumbile ya kiislamu isipokuwa Fatima.”14
Kutoka kwa Imam Muhammad Al-Baqir amesema: “Hakika Mwenyezi Mungu alimwachanisha kwa elimu.”15
Kutoka kwa Imam Jafar As-Sadiq amesema: “Hakika aliitwa Fatima kwa sababu viumbe wameachanishwa na maarifa yake.”16
Ibnu Abbas amesema: “Siku moja Mtume (s.a.w.w.) alikuwa amekaa huku akiwa na Ali, Fatima, Hasan na Husein akasema: Ewe Mwenyezi Mungu hakika wewe unajua kuwa hawa ni kizazi changu na niwapendao sana kuliko watu wote, hivyo mpende atakayewapenda na umchukie atakayewachukia, mtawalishe atakayewatawalisha na umfanyie uadui atakayewafanyia uadui, msaidie atakayewasaidia, wafanye watakasifu dhidi ya kila uchafu, watakasifu dhidi ya kila dhambi na uwasaidie kwa roho mtakatifu toka kwako.”
Imepokewa toka kwa mama wa waumini Ummu Salamah kuwa alisema: “Fatima binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ndiye aliyeshabihiana sana na Mtume (s.a.w.w.) kisura na kimaumbile.”
Imepokewa toka kwa mama wa waumini Aisha kuwa alisema: “Sikumwona mtu aliyekuwa mkweli kuliko Fatima isipokuwa yule aliyemzaa.17 Alikuwa aingiapo kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) basi Mtume husimama humkaribisha na kumbusu kisha humshika mkono na kumkalisha alipokaa yeye. Na Mtume (s.a.w.w.) aingiapo kwa Fatima basi husimama toka alipokuwa ameketi kisha hubusu mikono yake na humkalisha alipokaa yeye. Alikuwa msiri wa Mtume (s.a.w.w.) na marejeo yake katika jambo lake.”18
Ibnu Swabbagh Al-Malikiy amesema: “Na yeye ni binti wa yule aliyeteremshiwa: “Utukufu ni wa ambaye alimpeleka mja wake”.19
Watatu baada ya jua na mwezi, binti wa mbora wa wanadamu, mzawa mtakasifu aliye mbora kwa kongamano la wema wote.”20
Al-Hafidh Abu Nuaim Al-Isfihaniy amesema: “Kati ya vitakaswa vya watakasifu na visafi vya wachamungu ni Fatima mbora, mtawa, pande la nyama ya Mtume na shabihi wake….. Alikuwa kajitenga mbali na dunia na starehe zake, huku akijua vizuri machungu ya aibu za dunia na maangamizo yake.”21
Abdul-Hamid bin Abul-Hadid Al-Muutazaliy amesema: “Mtume (s.a.w.w.) alimtukuza sana Fatima kinyume na watu walivyokuwa wakifikiria….. mpaka akavuka kiwango cha mapenzi ya wazazi kwa wana wao, hivyo akatamka mara kwa mara na sehemu mbalimbali, mbele ya watu maalumu na mbele ya watu wote kuwa:
“Yeye ni mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni, na hakika yeye ni pacha wa Mariam binti Imran, na kuwa atakapotaka kupita kwenye kisi- mamo cha siku ya Kiyama atanadi mwenye kunadi toka upande wa Arshi kuwa: Enyi watu mliopo kwenye kisimamo, fumbeni macho yenu ili apite Fatima binti Muhammad.”
Hii ni kati ya hadithi sahihi wala si dhaifu, kwani si mara moja Mtume (s.a.w.w.) amekuwa akisema: “Huniudhi linalomuudhi na hunighadhibisha linalomghadhibisha, na hakika yeye ni pande la nyama yangu, hunichukiza yanayomchukiza.”22
Muhtasari
Fatima ni nyota ing’aayo katika mbingu ya akida ya kiislamu na ni bendera ya uongofu kwa wanadamu. Mwenyezi Mungu amemsifia ndani ya Qur’ani huku akidhihirisha fadhila zake.
Ama Mtume (s.a.w.w.) yeye amemsifia huku akivichorea vizazi vijavyo alama za hadhi yake, nafasi yake na mchango wake na akiwahimiza waislam wampende na kumridhisha. Kisha Maimam maasumina nao wakam- sifu na kueneza nuru yake mpaka ikabainika kwa kila mwenye macho kuwa ni wajibu kueneza fadhila zake.
Maswahaba na wanafunzi wa maswahaba, waandishi, watu wa hadithi na wanahistoria wote wamemtukuza na kuinua nafasi yake huku wakitamka fadhila zake na sifa zake.
Maswali
1. Taja Aya za Qur’ani zinazozungumzia fadhila za Az-Zahrau?
2. Mtume wa Mwenyezi Mungu amekutanisha ridhaa na ghadhabu ya Az-Zahrau na ridhaa na
ghadhabu yake. Nini maana ya kauli hiyo?
3. Toa hadithi tatu toka kwenye maelezo ya Maimam maasumina kuhusu fadhila za Az-Zahrau?
4. Ni ipi nafasi ya Az-Zahrau mbele ya waandishi na wanahistoria?
- 1. Rejea yaliyopokewa kuhusu tafsiri ya Sura Al-Kawthar, Aya ya utakaso, Aya ya mapenzi kwa watu wa karibu, Aya ya maapizano, Sura Dahri na maelezo ya Mtume (s.a.w.w.) kuhusu Az-Zahrau na Ahlul-Bayt ndani ya kitabu Aalamul-Hidayah, Juz. 3.
- 2. Kanzul-Ummal, Juz. 6 Uk. 219. Al-Mustadraku alas-Sahihayni, Juz. 3, Uk. 153. Mizanul-Iitidal, Juz. 3, Uk. 72.
- 3. As-Swawaiqul-Muhriqah Uk. 107 na 138. Sahih Bukhar kitabu cha mwanzo wa uumbaji. Kanzul-Ummal, Juz. 6, Uk. 22. Sahih Muslim kitabu cha fadhila za sahaba. Khasais cha An-Nasaiy, Uk. 35. Sahih Tirmidhiy, Juz. 2, Uk. 319.
- 4. Faraidus-Samtwayn, Juz. 2, Uk 66.
- 5. Musnad Abi Dawdi, Juz. 6 hadithi za wanawake. Hilyatul-Awliyai cha Abu Naim, Juz. 2, Uk. 29. Mushkilul-Athar, Juz. 1 Uk. 48. Shar’hu Nahjul- Balaghah cha Abul Hadid, Juz. 9, Uk. 193. Al-Awalim, Juz. 11, Uk. 46 na 49.
- 6. Kanzul-Ummal, Juz. 7, Uk. 92. Musnad Ahmad, Juz. 6, Uk. 296 na 323. Mustadrakus-Sahihayni, Juz. 3 Uk. 148 na 151. Sahih Bukhar kitabu cha kuomba idhini. Sahih Tirmidhiy, Juz. 2, Uk. 306. Hilyatul-Awliyai cha Abu Naim, Juz. 2, Uk. 42. Al-Istiaab, Juz. 2, Uk. 720 na 750.
- 7. Ameashiria hilo ndani ya Sura An-Najmi: 3.
- 8. Fatumatuz-Zahrau witri fi Ghamdi, Utangulizi wa Sayyidi Musa As- Sadri
- 9. Ameipokea mwandishi wa kitabu Al-Fusulul-Muhimmah kutoka kwenye Sahih Tirmidhiy, Uk. 123. Na rejea Tafsirul-Wusuul, Juz. 2, Uk.159. Musnad Ahmad, Juz. 2, Uk. 511.
- 10. Mustadrakul-Hakim, Juz. 3, Uk. 154. Kanzul-Ummal, Juz. 12, Uk. 111, hadithi ya 3424.
- 11. Musnad Ahmad, Juz. 4, Uk. 323 na 322. Al-Mustadrak, Juz. 3, Uk. 58.
- 12. Al-Fusulul-Muhimmah, Uk. 128. Na ameipokea ndani ya kitabu Al- Mukhtaswar kutoka kwenye Tafsir At-Thaalabiy, Uk. 133.
- 13. Aamal cha Tus, Juz. 1 Uk. 24. Al-Mukhtaswar, Uk. 136.
- 14. Rawdhatul-Kafiy, Uk. 536.
- 15. Kashful-Ghummah, Juz. 2, Uk. 99.
- 16. Biharul-An’war, Juz. 43, Uk. 65.
- 17. Kashful-Ghummah, Juz. 2, Uk.97 na 99.
- 18. Ahlul-Bayt cha Tawfiqi Abu Ilmi, Uk. 144.
- 19. Al-Israi:1.
- 20. Al-Fusulul-Muhimmah, Uk.143 chapa ya Beirut.
- 21. Hilyatul-Awliyai cha Abu Naim, Juz. 2, Uk. 39, chapa ya Beirut.
- 22. Shar’hu Nahjul-Balaghah, Juz. 9, Uk. 193.