read

Somo La Kumi Na Tisa: Urithi Wa Az-Zahrau (A.S.)

i. Imepokewa toka kwa Fatima binti wa Mtume (s.a.w.w.) kuwa yeye Fatima aliingia nyumbani kwa Mtume (s.a.w.w.), hapo Mtume (s.a.w.w.) akatandika nguo kisha akamwambia akae juu yake, kisha akaingia Hasan, Mtume (s.a.w.w.) akamwambia kaa pamoja na mama yako. Akaingia Husein, Mtume (s.a.w.w.) akamwambia kaa nao. Kisha akaingia Ali (a.s.) akaambiwa na Mtume (s.a.w.w.) kaa nao. Kisha Mtume (s.a.w.w.) akashika pembe za nguo na kuwafunika na kusema: “Ewe Mwenyezi Mungu; wao wanatokana na mimi na mimi natokana na wao, ewe Mwenyezi Mungu waridhie kama nilivyowaridhia.”1

ii. Kutoka kwa Muhammad bin Umar Al-Kannasiy kutoka kwa Jafar bin Muhammad kutoka kwa baba yake kutoka kwa Ali bin Husein kutoka kwa Fatima mdogo kutoka kwa Husein bin Ali kutoka kwa Fatimah binti Muhammad alisema: “Alitujia Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Hakika Mwenyezi Mungu amejifaharisha kwenu, hivyo akawasamehe nyinyi wote kwa ujumla na akamsamehe Ali mahsusi, na hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, si mwenye kuogopwa kwa ajili ya watu wangu na ni mwenye kupendwa kwa sababu ya kizazi changu. Huyu hapa Jibril ananipa habari kuwa: Mwema wa kweli ni yule atakayempenda Ali wakati wa uhai wangu na baada ya kifo changu.”2

iii. Kutoka kwa Ali (a.s.) kutoka kwa Fatima (a.s.) alisema: “Mtume aliniambia: Ewe Fatima, atakayekuombea rehema wewe basi Mwenyezi Mungu atamsamehe na atamkutanisha na mimi peponi sehemu yoyote nitakayokuwepo.”3

iv. Kutoka kwa Zaynab binti Ali kutoka kwa Fatima binti wa Mtume (s.a.w.w.) alisema: Mtume alisema kumwambia Ali: “Ewe Ali! Wewe na wafuasi wako ni watu wa Peponi.”4

v. Fatima (a.s.) alisema: “Mtume aliniambia: Hivi huridhii kuwa mimi nimekuoza kwa mwislamu wa kwanza kuamini, mwenye elimu nyin- gi kuliko wao. Hakika wewe ni mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni kama Mariam alivyokuwa mbora kuliko wanawake wote wa kaumu yake.”5

vi. Kutoka kwa Sahl bin Saad Al-Answariy amesema: “Fatima binti wa Mtume (a.s.) aliulizwa kuhusu Maimam. Akajibu: Mtume alikuwa akimwambia Ali: “Ewe Ali! wewe ni Imam na khalifa baada yangu, na wewe una haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao, hivyo akipita Hasan ni mwanao Husein ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Husein ni mwanae Ali bin Husein ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Ali ni mwanae Muhammad ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Muhammad ni mwanae Ja’far ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Jafar ni mwanae Musa ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao.

Akipita Musa ni mwanae Ali ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Ali ni mwanae Muhammad ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Muhammad ni mwanae Ali ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Ali ni mwanae Hasan ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Akipita Hasan ni mwanae Mahdi ndiye mwenye haki zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao. Mwenyezi Mungu atafungua Mashariki ya ardhi na Magharibi yake kupitia yeye. Wao ndio Maimam wa haki na ndimi za kweli, atanusurika atakayewanusuru, atatelekezwa atakayewatelekeza.”6

v. Aliashiria makusudio ya sheria ya kiislamu kwa kusema: “Mwenyezi Mungu ameweka imani kwa ajili ya kuwatakasa dhidi ya shirki. Swala kwa ajili ya kuwaepusha na kiburi. Zaka kwa ajili ya kuitakasa nafsi na kuongeza riziki. Funga kwa ajili ya kuimarisha ikhlasi. Hija kwa ajili ya kuimarisha dini. Uadilifu kwa ajili ya kuziunganisha nyoyo. Utiifu wenu kwa ajili ya nidhamu ya sheria. Uimamu wetu kwa ajili ya kusalimika na mfarakano. Jihadi kwa ajili ya kuupa heshima Uislamu. Subira ni msaada ili muwajibike kupata malipo. Kuamrisha mema ni masilahi ya wote. Kuwatendea wema wazazi wawili ni kinga dhidi ya adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Kuunga undugu ni kuongeza umri na kuongeza idadi. Kisasi ni kwa ajili ya kuhifadhi damu. Kutekeleza nadhiri ni kwa ajili ya kuomba msamaha. Kutimiza vipimo na mizani ni kwa ajili ya kuondoa ulaghai. Kukataza kunywa pombe ni kwa ajili ya kuwatakasa dhidi ya uchafu. Kujiepusha kutuhumu ugoni ni kwa ajili ya kuzuia laana. Kuacha wizi ni kwa ajili ya kupelekea nafsi kujimiliki. Mwenyezi Mungu akaharamisha ushirikina kwa ajili ya kumnyookea Yeye tu kwa Umola wake.”

viii. Az-Zahrau (a.s.) alimuuliza baba yake: “Ewe baba yangu mpendwa, ni mambo gani yanayompata mwanaume na mwanamke anayedharau Swala?” Akajibu: “Ewe Fatima, mwanaume yeyote au mwanamke akipuuzia Swala Mwenyezi Mungu humtahini kwa kumpa mambo kumi na tano, sita hapa duniani, matatu wakati wa kifo chake, matatu kaburini, na matatu Siku ya Kiyama atakapotoka kaburini.

xi. Fatima (a.s.) alisema: Mtume aliniambia: “Jiepushe na ubahili hakika ni aibu isiyompata mkarimu. Jiepushe na ubahili hakika ni mti uliomo motoni na matawi yake yamo duniani, hivyo atakayeshika tawi moja kati ya matawi yake litamwingiza motoni. Kuwa mkarimu, hakika ukarimu ni mti kati ya miti ya peponi matawi yake yamening’inia hapa aridhini, hivyo atakayechukua tawi moja kati ya matawi yake litamwingiza Peponi.”7

x. Fatima (a.s.) alisema: “Kufurahi mbele ya uso wa muumini kunawajibisha mwenye kufurahi kupata pepo, na kutabasamu mbele ya uso wa adui mpingaji kunamkinga mwenye kufurahi dhidi ya adhabu ya moto.”8

xi. Fatima (a.s.) alisema: “Atakayepandisha ibada safi kwa Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu atamteremshia masilahi yake bora.”9

xii. Mtume (s.a.w.w.) aliwauliza maswahaba zake kuhusu mwanamke, akasema: “Mwanamke ni nini?” Wakajibu: “Ni utupu.” Akasema: “Ni wakati gani anakuwa karibu sana na Mola wake?”

Hawakujua jibu. Ndipo Fatima (a.s.) aliposikia akasema: “Huwa karibu sana na Mola wake pindi anapotawa nyumbani kwake.” Hapo Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Hakika Fatima ni kipande cha nyama yangu.”10

xiii. Alimsifia mwanamke bora kwa kusema: “Mbora wao ni yule asiyetazamwa na wanaume wala asiyetazama wanaume.”11

xiv. Kutoka kwa Ali bin Husein bin Ali (a.s.) amesema: “Hakika Fatima binti wa Mtume (s.a.w.w.) alimruhusu kipofu aingie kisha akamwekea pazia, hapo Mtume (s.a.w.w.) akamwambi: “Fatima kwa nini umemwekea pazia ilihali yeye hakuoni?” Akajibu: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! ikiwa yeye hanioni mimi namwona, na yeye ananusa harufu.” Mtume (s.a.w.w.) akasema: “Nakiri kweli wewe ni pande la nyama yangu.”12

Muhtasari

Riwaya zilizopokewa kutoka kwa Az-Zahrau (a.s.) ni ushahidi tosha juu ya upana wa maarifa yake aliyokunywa kutoka kwenye chemchemu ya utume. Az-Zahra (a.s.) ana hotuba mbili mashuhuri ambazo zinawakilisha kina cha maarifa yake na upana wa elimu zake mbalim- bali. Kupitia hizi hotuba mbili fasaha; historia imesajili nafasi yake adimu katika kugundua njama hatari zilizoukumba Uislamu, dola ya kiislamu na umma wa kiislamu baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.w.). Az-Zahrau (a.s.) alimjali mwanamke wa kiislamu na familia ya kiis- lamu kupitia msimamo wake, semi zake na maagizo yake, hivyo akawa ni mfano mzuri wa mwanamke msomi wa kiislamu na mwanadamu kiongozi na kiigizo chema kwa kila mwanamke, na kuanzia hapa akapata medali ya mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni.

Maswali

1. Taja mifano ya filosofia ya sheria ya Mwenyezi Mungu ndani ya urithi wa Az-Zahrau (a.s.)?
2. Elezea msimamo wa Az-Zahrau (a.s.) kuhusu uimamu baada ya Mtume wa Mwenyezi
Mungu (s.a.w.w.)?
3. Toa dalili inayothibitisha jinsi Az-Zahrau (a.s.) alivyojali na kutilia umuhimu hadithi za Mtume
(s.a.w.w.)?
4. Elezea mwenendo wa Az-Zahrau (a.s.) katika mahusiano yake na wanaume?
5. Muumini inampasa aweje?
6. Kutokana na maneno ya Az-Zahrau (a.s.) ni nani aliye mwema wa kweli?

Mwisho wa dua zetu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu
.
  • 1. Dalailul-Imamah, hadithi ya 2 na 3 na ya 34.
  • 2. Asnal-Matwalib cha Shamsud-Din Al-Jazriyyu, 70.
  • 3. Kashful-Ghummah, Juz. 1. Uk. 472.
  • 4. Dalailul-Imamah, hadithi ya 2 na 3. Ihqaqul-Haq, Juz.7 Uk. 307. Yanabiul-Mawadda 257.
  • 5. Asnal-Matwalib cha Allamah Al-Wasswaniy Al-Yammaniy.
  • 6. Kifayatul-Athar 193-200.
  • 7. Ahlul-Bayt cha Tawfiq bin Abu Ilmi, Uk. 130-131.
  • 8. Tafsirul-Imam 354. Na makusudio ya kipengele cha pili ni kufanya taqiyya mbele ya maadui wa Ahlul-Bayt (An-Nawaswib).
  • 9. Biharul-An’war, Juz. 71, Uk. 184.
  • 10. Biharul-An’war, Juz.43 Uk. 92.
  • 11. Hilyatul-Awliyai, Juz. 2 Uk. 40.
  • 12. Mulhaqat Ihqaqul-Haq, Juz. 10 Uk.258.