read

Somo La Nane: Urithi Wa Mbora Wa Mitume

Akili Na Ukamilifu Wa Mwanadamu

Mtume (s.a.w.w.) alielezea kuhusu akili, majukumu yake na nafasi yake katika maamrisho na majukumu ya mwanadamu, nafasi yake katika matendo na malipo, hivyo akabainisha sababu za kukua na kukamilika kwa akili akasema: “Hakika akili ni kitanzi dhidi ya ujin- ga na nafsi ni sawa na mnyama mbaya, hivyo iwapo hakufungwa kitanzi hucharuka, basi akili ni kitanzi kuliko ujinga.

“Mwenyezi Mungu aliumba akili kisha akaiambia nenda mbele ikaenda mbele. Rudi nyuma, ikarudi nyuma. Hapo Mwenyezi Mungu akaiambia: Naapa kwa nguvu Zangu na utukufu Wangu, sikuumba kiumbe muhimu kuliko wewe, wala kitiifu kuliko wewe. Kupitia wewe nitaumba na nitarudisha, na kwa ajili yako nitalipa thawabu na nitaadhibu, hivyo uvumilivu ukatokana na akili, na elimu ikatokana na uvumilivu, na uongofu ukatokana na elimu. Utawa ukatokana na uongofu, na kujimiliki kukatokana na utawa, na aibu ikatokana na kujimiliki na heshima hutokana na haya.

“Heshima husababisha kudumu ndani ya heri na kuchukizwa na shari, hivyo kumtii mshauri kunatokana na kuchukizwa na shari. Haya ni makundi kumi katika aina za kheri na katika kila kundi kuna aina kumi za kheri….”1

Elimu Ni Uhai Wa Nyoyo

Mtume (s.a.w.w.) alijali sana elimu na maarifa akabainisha nafasi ya elimu na jukumu lake katika maisha akasema: “Kutafuta elimu ni faradhi kwa kila mwisilamu. Fuateni elimu toka kila sehemu mnayodhani mtaipata. Jifunzeni toka kwa wenyenayo hakika kujifunza kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni wema na kuitafuta ni ibada, kujikumbusha elimu hiyo ni tasbihi na kuitumia ni jihadi, kumfunza yule asiyejua ni sadaka na kuieneza kwa wahusika ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa sababu elimu ndio alama ya halali na haramu, na minara ya watu wa peponi na ndio mfariji wakati wa upweke na rafiki wakati wa ugeni na upweke, na ndio msemeshaji wakati wa siri na upekee. Ni alama ijulishayo mambo ya siri na ya kudhuru, ni silaha dhidi ya maadui, na ni pambo kwa vipenzi.

Mwenyezi Mungu huwainua watu kupitia elimu, hivyo huwafanya viongozi bora ambao athari zao hunufaisha na vitendo vyao hufuatwa, mawazo yao hutegemewa huku malaika wakipenda urafiki wao, huwapangusa kwa mbawa zao na huwabariki katika Swala zao. Kila kibichi na kikavu huwaombea msamaha. Pia viumbe vya baharini na nchi kavu, kuanzia vidogo hadi vikubwa navyo huwaombea msamaha.

Hakika elimu ni uhai wa moyo dhidi ya ujinga na ni nuru ya macho dhidi ya kiza na ni nguvu ya mwili dhidi ya udhaifu. Humfikisha mja nafasi ya wenye heri na vikao vya watu wema na daraja la juu hapa duniani na huko Akhera. Kuitaja tu huwa sawa na kufunga, na kuisoma ni sawa na kusali Swala za usiku. Kupitia elimu Mola hutiiwa na undugu huunganishwa na haramu na halali hujulikana. Elimu huwa mbele ya vitendo na vitendo hufuata elimu.

Mwenyezi Mungu huwapa watu wema na huwanyima waovu, hivyo ni jambo zuri sana kwa yule ambaye hajanyimwa na Mwenyezi Mungu fungu lolote la elimu. Sifa ya mwenye akili ni kumvumilia asiyejua na kumsamehe aliyemdhulumu, kumnyenyekea aliye chini yake na kushindana katika kutafuta wema dhidi ya yule aliye juu yake.

Anapotaka kuzungumza, kwanza hufikiri hivyo kama ni la heri huzungumza na kufaidika, na kama ni la shari hunyamaza na kusal- imika. Iwapo utamfika mtihani hushikamana na Mwenyezi Mungu na huzuia mkono na ulimi wake. Aonapo jambo bora hulichangamkia na hapo aibu haimzuii wala tamaa haimpeleki pupa. Basi hizo ndio sifa kumi hujulikana kwazo mtu mwenye akili.

Sifa ya mjinga ni kumdhulumu anayechanganyikana naye, kumdhulumu aliye chini yake, kumfanyia kiburi aliye juu yake. Huongea bila kufikiri, na akiongea hutenda dhambi na akinyamaza husahau. Iwapo utamfika mtihani basi huuendea pupa na kumcharua.

Huwa mzito aonapo jambo la heri huku akijitenga nalo, hana khofu dhidi ya dhambi zake za mwanzo wala hatetemeki dhidi ya umri wake uliyobaki na dhambi alizonazo. Huwa mzito na mwenye kuchelewa dhidi ya jambo la heri. Hasikitikii heri yoyote iliyompita au aliyoipoteza. Hizo ni sifa kumi za mjinga ambazo akili imenyimwa.”2

Vizito Viwili: Kitabu Na Kizazi (Ahlul-Bayt)

Mtume (s.a.w.w.) aliwachorea watu njia ya wema wa kweli akawapa dhamana ya kuufikia wema huo iwapo tu watashikamana kwa ukamilifu na mafunzo aliyoyabainisha, hivyo akawapa ufupi wa njia ya wema ambayo inawakilishwa na kitendo cha kushikamana na asili na misingi miwili ambayo hutegemeana nayo ni: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi chake, Akasema:

“Enyi watu, hakika mimi nawatangulia nanyi mtanikuta katika hodhi. Fahamuni kuwa mimi nitawauliza kuhusu vizito viwili, hivyo angalieni jinsi gani mtahusika navyo baada yangu. Hakika Mpole mtoa habari amenipa habari kuwa: Hakika hivyo viwili havitoachana mpaka vinikute.

Nilimwomba Mola Wangu hivyo na akanipa. Fahamuni hakika mimi nimewaachieni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu Ahlul-Bayt, hivyo msiwatangulie mtafarikiana, wala msiwaache mtaangamia na wala msiwafunze hakika wao ni wajuzi zaidi yenu. Enyi watu! Msiwe makafiri baada yangu ikawa baadhi yenu wanawauwa wengine hivyo mkanikuta huku mkiwa kundi dogo kama mfereji wa maji uliyoacha njia.

Fahamuni kuwa Ali bin Abu Talib ni ndugu yangu na wasii wangu, atapigania tafsiri ya Qur’ani baada yangu kama nilivyopigania uteremkaji wake.”3

Mawaidha Fasaha

Mtume (s.a.w.w.) ambaye mwenendo wake ni fasaha tupu ana semi fupifupi ambazo ni alama ya ufasaha wake, hivyo miongoni mwa mawaidha yake ni:

“Enyi watu, mazungumzo ya kweli kabisa ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na shikio imara ni neno la uchamungu, na mila bora kabisa ni mila ya Ibrahim, na mwenendo bora kabisa ni mwenendo wa Muhammad, na mazungumzo matukufu kabisa ni kumtaja Mwenyezi Mungu.

“Visa vizuri sana ni visa vya Qur’ani, mambo bora ni maamrisho na mambo mabaya ni bidaa. Uongofu bora kabisa ni uongofu wa manabii, kifo bora ni kifo cha mashahidi, upofu zaidi ni kupotea baada ya kuongoka. Kazi bora ni ile yenye kunufaisha, na uongofu bora ni ule wenye kufuatwa. Upofu mbaya ni upofu wa moyo, na mkono wa juu ni bora kuliko mkono wa chini. Kichache kinachotosheleza ni bora kuliko kingi kisichofaa.

“Msamaha mbaya ni ule uombwao wakati kifo kimefika na majuto mabaya ni majuto ya siku ya Kiyama. Kati ya makosa makubwa ya ulimi ni uongo. Utajiri bora ni utajiri wa nafsi na maandalizi bora ya safari ni uchamungu. Msingi wa busara ni kumwogopa Mwenyezi Mungu na jambo bora uliyopewa moyo ni yakini. Kilevi husababisha moto, na pombe ni mkusanyiko wa mikasa yote. Wanawake ni kamba za ibilisi na ujana ni tawi la uwendawazimu.

“Chumo baya zaidi ni riba, na chakula kibaya zaidi ni kula mali ya yatima. Mwema ni yule anayewaidhika kupitia mwenzake. Hakika kila mmoja wenu atawekwa ndani ya dhiraa nne (Kaburini). Kipimo cha vitendo ni mwisho wake na kila lijalo basi liko karibu. Kumtukana muumini ni ufasiki na kumuua ni ukafiri. Kumla nyama yake (kumsengenya) ni maasi na mali yake imeharamishwa kama ilivyoharamishwa damu yake.

“Atakayemuomba Mwenyezi Mungu msamaha basi Mwenyezi Mungu atamsamehe. Atakayesamehe
basi Mwenyezi Mungu atamsamehe na atakayevumilia katika msiba basi Mwenyezi Mungu
atampa badala.”4

Muhtasari

Mtume (s.a.w.w.) ni mfano hai wa ukamilifu wa mwanadamu. Pia urithi wake ndio wenye thamani baada ya Qur’ani. Hakika yeye alikunywa toka chemchemu ya ufunuo mpaka akabubujisha ukamili- fu wake kwa wanadamu kwa kiwango kinachotosheleza kuwapeleka wanadamu mbele upande wa ukamilifu na kuwafikisha kileleni mwa ukamilifu.

Tumechagua mifano ya ufasaha wake na semi zake fasihi kuhusu akili, elimu na njia ya kufikia wema na ukamilifu. Tumechagua kwa kiwango ambacho kitawaangazia wenye kufuata njia yake, hivyo wale watafuta ukweli hawatojizuia kutumia madhumuni ya semi hizo.

Maswali

1. Akili ni nini? Na ina nafasi gani katika maisha ya mwanadamu?
2. Ni kipi kinachotokana na akili. Taja sifa ambazo haziachani na akili?
3. Tunatafuta elimu kutoka wapi? Na ni zipi hatua za utafutaji elimu?
4. Ni ipi nafasi ya elimu katika maisha ya mwanadamu?
5. Ni vipi hivyo vizito viwili? Na kila kimoja kina mahusiano gani na kingine?
6. Ni zipi sifa mahsusi za Qur’ani?
7. Ni ipi nafasi ya kizazi cha Mtume kwa Mtume (s.a.w.w.)?

  • 1. Tuhfatul-Uqul, mlango wa mawaidha ya Nabii na hekima zake.
  • 2. Ameipokea ndani ya kitabu Maniyyatul-Murid kutoka kwa Imam Ridhaa (a.s.) kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Tazama hadithi hii kwa urefu ndani ya kitabu Tuhful-Uqul.
  • 3. Nasikhut-Tawarikh, Juz. 3. Rejea ufafanuzi wa hotuba hii ndani ya kitabu Tarikh Yaaqubiy, Juz. 2 Uk. 109.
  • 4. Al-Bidayatu Wan-Nihayah, Juz. 5 Uk. 13, chapa ya Darul-fikri