read

Somo La Tano: Tabia Na Mwonekano Wa Hitimisho La Manabii (S.A.W.W.)

Ndani Ya Qur’ani Tukufu

Hakika Muhammad bin Abdullah alisifika kwa sifa nzuri na maadili bora ambayo yalimtofautisha na kila aliyeishi katika zama zake au kabla yake au aliyekuja baada yake, hivyo ndio maana akawa ni mbora wa manabii. Hakika ukamilifu wake umeelezwa wazi na Qur’ani kupitia maelezo yake matukufu. Qur’ani imeelea ukamilifu wa akili yake na ubora wa maadili yake kwa kusema: “Kwa neema ya Mola wako wewe si mwenda wazimu.* Na kwa hakika una malipo yasiyokatika.* Na bila shaka una tabia njema tukufu.”1

Utumwa wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu umeonyeshwa na kauli ya Mwenyezi Mungu: “Utukufu ni wake ambaye alimpeleka mja wake usiku kutoka msikiti mtukufu mpaka msikiti wa mbali.”2

Ama ukunjufu wa kifua chake umeashiriwa na Aya: “Je hatukuku- panulia kifua chako?”3 Ama kumfuata kwake Mwenyezi Mungu katika kila kitu huku akimwogopa na kumnyenyekea yeye tu kumeelezwa na Aya: “Sifuati ila ninayofunuliwa kwa wahyi. Hakika mimi naogopa nikimwasi Mola wangu adhabu ya siku iliyo kuu.”4 Ushahidi mwingine ni Aya: “Wale wanaofikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kumwogopa yeye wala hawamwogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye atoshaye kuhesabu.”5

Ama huruma yake na upole wake kwa walimwengu huku akiwahangaikia watu ili kuwaongoza waelekee kwa Mwenyezi Mungu kumeelezwa na Aya: “Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu.6 Na akasema: “Bila shaka amekufikieni Mtume kutoka miongoni mwenu, yanamhuzunisha yanayokutaabisheni, anakuhangaikieni, kwa waumini ni mpole, mwenye kuwaonea huruma.7 Na Aya isemayo: “Enyi watu wa kitabu, hakika amek- wisha kufikieni mtume wetu, anayekubainishieni mengi mliyokuwa mkiyaficha katika kitabu, na kusamehe mengi”8 inaonyesha msamaha wake.

Ama Aya isemayo: “Sema: Hii ndiyo njia yangu ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa ujuzi, mimi na wanaonifuata, na Mwenyezi Mungu ametakasika na kila upungufu wala mimi simo miongoni mwa washirikina”9 inaonyesha ufahamu wake na kudumu kwake katika njia ya uongofu wa Mola wake.

Pia hali hiyo inathibitishwa na Aya isemayo: “Sema: Na uite kwa Mola wako, bila shaka wewe uko juu ya mwongozo ulio sawa”.10 Na ile isemayo: “Basi tegemea kwa Mwenyezi Mungu hakika wewe uko juu ya haki iliyo wazi.11 Pia ile isemayo: “Yeye ndiye aliyemtuma mtume wake kwa mwongozo na kwa dini ya haki ili ishinde dini zote, ingawa washirikina wat- achukia.”12 Zote hizo zinathibitisha hali hiyo.

Aya ifuatayo: “Ambao wanamfuata mtume, nabii aliyoko Makka, ambaye wanamwona ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, ambaye anawaamrisha mema na anawakataza yaliyo mabaya na kuwahalalishia vizuri na kuwaharamishia maovu, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.”13 inathibitisha kutojifunza kwake toka kwa mtu yeyote huku akimkomboa mwanadamu dhidi ya kila aina minyororo.

Ama uadilifu na usawa wake katika maadili na mwenendo wake umeashiriwa na Aya isemayo: “Na hivyo tumekufanyeni umati bora ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe shahidi juu yenu.”14

Aya ifuatayo: “Bila shaka mnao mfano mwema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana.”15

Imethibitisha kuwa yeye ndiye mfano wa kuigwa katika ukamilifu wa mwanadamu. Ama utawala wake juu ya viumbe na cheo chake juu yao umethibitishwa na Aya isemayo: “Hakika kiongozi wenu hasa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake.”16

Aya ifuatayo: “Muhammad mtume wa mwenyezi Mungu na walio pamoja naye ni imara mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao”17 inathibitisha jinsi alivyo mkali dhidi ya wapinzani na makafiri.

Ama Aya ifuatayo: “Ewe Nabii, kwa hakika sisi tumekutuma shahidi na mtoaji wa habari nzuri na muonyaji. Na muhitaji kwa Mwenyezi Mungu kwa idhini yake na taa itoayo nuru.”18 inathibitisha ufasaha wake, kuhusika kwake katika kila jukumu na kuwaongoza watu.

Ndani Ya Maelezo Ya Bwana Wa Mawasii (A.S.)

Imam Ali (a.s.) amesema: “ ……Mpaka Mwenyezi Mungu alipomtuma Muhammad shahidi, mtoaji wa habari njema, mwonyaji, mbora wa viumbe kati ya watoto wote, na mbora wa viumbe watakasifu kati ya wakongwe wote, mtakasifu wa maadili kati ya watakasifu wote, na mbora wa ukarimu kati ya wakarimu wote.”19

“Akamteua kutokana na mti wa manabii, shubaku yenye mwanga, nywele za utosi wa watukufu…… na chemchemu ya hekima, tabibu maarufu kwa tiba yake, yuko tayari kwa dawa yake huku akifuatilia kwa hiyo dawa yake kila sehemu yenye mghafiliko na sehemu za shaka.”20

“Nakiri kuwa Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake aliyemteua kati ya viumbe Wake, aliyeteuliwa kwa ajili ya kubainisha ukweli halisi, aliyeteuliwa mahsusi kwa ajili ya miujiza mitukufu na ujumbe mtakatifu, mwenye kubainisha alama za uongofu kupitia ujumbe huo, hivyo mwenye kujitenga naye yumo katika upotevu mkubwa.”21

“Hakika Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad huku ndani ya waarabu hakuna anayejua kusoma kitabu wala anayedai unabii, hivyo akawapeleka watu mpaka akawafikisha sehemu yao, huku akiwafikisha eneo la uokovu wao, hivyo njia yao ikanyooka na sifa zao zikatulia.”22

“Hivyo akavuka kiwango katika kutoa nasaha, akafuata njia sahihi na kulingania hekima na mawaidha mazuri.”23

“Mwenye kutangaza haki kupitia haki, mwenye kuondoa mchemko wa batili, na mwenye kuangamiza ukali wa upotovu. Kama alivyobebeshwa ndivyo alivyoinuka huku akisimama kwa nguvu zote kupitia amri yake. Mwenye kuharakisha katika kupata ridhaa Zako huku akiwa haogopi kwenda vitani wala si dhaifu katika nia.

Mwenye kuhifadhi ufunuo Wako, mwenye kulinda ahadi Yako huku akiendelea kutekeleza maamrisho Yako……..Hivyo yeye ni mwaminifu mwenye kuaminika na muhazini wa elimu Yako ya siri.”24
“Imam wa atakayemcha Mwenyezi Mungu na jicho la atakayeongoka.”25

“Hivyo akapambana katika njia ya Mwenyezi Mungu dhidi ya wale waliyomkimbia na dhidi ya wale waliyojitenga Naye……..26 kwa ajili ya kutetea dini Yake, huku haumzuwii kufanya hivyo mkusanyiko wa wote wenye kumpinga na ule wa wenye kutaka kuzima nuru yake.”27

“Ilikuwa tukizidiwa na ukali wa vita tunajikinga kwa mtume, hivyo hakuna yeyote kati yetu aliyekuwa karibu na adui zaidi yake.”28

“Hivyo muige Mtume wako mbora wa watakasifu. Hakika katika kumuiga kuna kigezo chema kwa atakayeiga. Aliidokoa dunia na wala hakuitamani kabisa, hivyo yeye ndiye aliyeiacha dunia bila kuijali, na ndiye aliyeliacha tumbo tupu bila dunia…… Alipewa dunia yote akakataa kuipokea………..Alikuwa akila huku kakaa aridhini, alikaa mkao wa mtumwa huku akishona viatu vyake kwa mkono wake……..Alitoka duniani bila kustarehe na nayo, na alifika akhera akiwa salama, hivyo hakulimbikiza kitu mpaka alipofariki.”29

Imepokewa kutoka kwa Hasan bin Ali (a.s.) kuwa Hindu bin Abi Halati alitoa wasifu wa Mtume (s.a.w.w.) kwa kusema: “Huanza kumtolea salamu yule aliyekutana naye……..Daima alikuwa na huzuni, mwingi wa tafakuri muda wote, mwimgi wa ukimya, hazungumzi pasipo na haja ya kuzungumza, huzungumza yenye kutosheleza, hazungumzi yasiyo na maana wala yaliyo pungufu, si mwenye kun- yanyapaa wala si mwenye kudharau.”

Hivyo neema ndogo kwake ilikuwa kubwa, haikashifu neema yoyote. Wala dunia na kichache alichokipata havimkasirishi. Anapopewa haki hakuna anayefahamu, wala hakutenda jambo kwa ghadhabu mpaka atakapoimiliki……..Anapoghadhibika huacha na kuondoka, na anapofurahi hubana sauti yake bali alama ya kucheka kwake ni tabasamu lake.

Ndani Ya Dondoo Za Sera Yake Kijamii

Husein bin Ali (a.s.) amepokea Hadithi kutoka kwa baba yake Imam Ali (a.s.) inayozungumzia sera ya Mtume (s.a.w.w.) kijamii:

“Anapokuwa nyumbani kwake hugawa muda wake mafungu matatu: Fungu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Fungu kwa ajili ya wakeze na fungu kwa ajili ya nafsi yake. Kisha fungu lake huligawa kwa ajili yake na kwa ajili ya kuhudumia jamii.

Mwenendo wake katika kuhudumia umma ulikuwa ni kuwatanguliza wale wenye ubora huku akigawa ubora wao kulingana na ubora wao katika dini.

Alikuwa akizuia ulimi wake isipokuwa katika yale yanayomuhusu huku akiwaunganisha pamoja bila kuwasambaratisha. Humheshimu mheshimiwa wa kila kundi huku akimtawalisha juu yao. Hujihadhari na kujilinda dhidi ya watu bila ya kupunguza bashasha yake wala tabia yake. Huwatafuta maswahaba zake wasipoonekana huku aki- ulizia matatizo ya watu.

Hulisifia jema na kulipa nguvu, na hulisifu kwa ubaya lile lililo baya huku akilishusha thamani. Jambo lake huwa wastani wala haghafiliki na kitu….Hapunguzi wala hazidishi huku aliye mbora mbele yake ni yule mwenye kuwanasihi sana waislam.

Na mwenye hadhi kubwa sana mbele yake ni yule mwenye kuwasaidia na kuwanusuru watu. Hakai wala hasimami ila akimtaja Mwenyezi Mungu. Humpa kila aliyekaa naye fungu lake, hivyo anapokaa na mtu humvumilia mpaka mtu yule aondoke mwenyewe.

Amwombaye haja yoyote humjibu kwa kumtekelezea haja yake na kwa kauli tamu. Kikao chake ni kikao cha heshima, ukweli na uaminifu. Muda wote alikuwa ni mwenye bashasha, mwenye tabia nyepesi, mpole, asiye mkali wala si mkavu wa tabia. Hakuwa mchekaji ovyo wala mtukanaji, hakuwa mwaibishaji au mwongeza chumvi katika kusifia.

Hujighafilisha na yale asiyoyapenda, hivyo alikuwa akinyamaza kwa sababu ya mambo manne: Kwa sababu ya busara, tahad- hari, ridhaa, na tafakari.”30

Muhtasari

Mwenyezi Mungu katoa wasifu wa Mtume Wake Muhammad (s.a.w.w.) kwa kueleza sifa zake za ukamilifu wa kibinadamu, hivyo akamfanya mbora wa mitume, hitimisho lao, na kigezo chema amba- cho watakiiga wanadamu ili wanadamu hao wafikie kilele cha ukamilifu. Mwenyezi Mungu kawafafanulia waigaji sifa zake na maadili yake mazuri mema.

Kizazi chake ambacho ndio kijuacho zaidi yale yaliyomo nyumbani kimetoa wasifu wa mbora wao na mjumbe mwaminifu kupitia maneno yaliyo timilifu yaliyokusanya sifa zote. Huku maneno hayo yakitoa taswira ya ukamilifu na sifa ambazo zimemfanya awe ni kiigizo chema kwa wanaomfuata na bendera kwa wenye kuongoka.

Maelezo hayo yaliyonukuliwa kutoka kwa kizazi chake yametoa taswira ya adabu ya hali ya juu ya Mtume (s.a.w.w.) na sera yake binafsi na ya kijamii ya hali ya juu.

Maswali

1. Andika Aya inayoonyesha kuwa Mtume (s.a.w.w.) kapambika na sifa ya utumwa kwa ajili ya
Mwenyezi Mungu tu?

2. Elezea jinsi Qur’ani ilivyotoa taswira ya shakhsia ya Mtume wa mwisho (s.a.w.w.)?

3. Ni sifa zipi muhimu za Mtume (s.a.w.w.) ambazo zimetajwa ndani ya Nahjul-Balaghah?

4. Linganisha sifa za Mtume (s.a.w.w.) zilizoelezwa na Qur’ani na zile zilizoelezwa na Nahjul-Balaghah?

5. Ni mambo gani unayoyapata katika sera ya Mtume (s.a.w.w.) kupitia maelezo ya Maimam Hasan na Husein (a.s.)?

 • 1. Al-Qalam: 2 -4.
 • 2. Al-Israi: 1.
 • 3. Al-Inshirah: 1.
 • 4. Yunus: 15.
 • 5. Al-Ahzabi: 39.
 • 6. Al-Anbiyai: 107.
 • 7. At-Tawba: 128.
 • 8. Maidah: 15.
 • 9. Yusuf: 108.
 • 10. Al-Hajj: 67.
 • 11. An-Namlu: 79.
 • 12. At-Tawba: 33.
 • 13. Al-Aa’raaf: 157.
 • 14. Al-Baqarah: 43.
 • 15. Al-Ahzabi: 21.
 • 16. Al-Maidah: 55.
 • 17. Al-Fat’hu: 29.
 • 18. Al-Mulk: 26.
 • 19. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 105.
 • 20. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 108.
 • 21. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 178.
 • 22. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 33.
 • 23. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 95.
 • 24. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 72.
 • 25. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 116.
 • 26. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 133.
 • 27. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 190.
 • 28. Kashful-Ghummah, Juz. 1, Uk. 9.
 • 29. Nahjul-Balaghah, hotuba ya 160.
 • 30. Tazama kitabu Sunanun-Nabiyyi, Uk. 14 na 17.