Table of Contents

Jedwali La Hukumu Za Damu Ya Istihadha

Aina ya Damu Chache Wastani Nyingi
Alama


Damu ilowanishe ichafue pamba bila kupenya ndani Damu ilowanishe ichafue panda zote mbili za pamba bila kutoka nje Damu itembee kutoka kwenye pamba mpaka nje(kiasi cha kutapakaa kwenye pendi au kitambaa
Hukumu ya Swala


Kila Swala:
1. Kubadili pamba au pendi

2. Kutia Udhu

3. Kutoharisha mavazi na mwili sehemu iliyona jisija moja

Pamoja na kutenda mambo matatu yenye kushirikiana, pia anawajibija kuoga kila siku mara Pamoja na wajibu wa kutenda mambo matatu yenye kushirikiana pia:
1. Kuoaga kabla ya Swala ya asubuhi

2. Kuoaga kabla ya Swala ya adhuhuri na alasiri(kwa sharti iwapo atazikusa nya pamoja

3. Kuoga kabla ya magharibi na isha (kwa sharti iwapo atazikusanya pamoja)

Hukumu ya Swaumu
Sahihi wala haihi taji udhu Sahihi kwa sharti ya kuoga josho la wajibu la kila siku Sahihi kwa sharti ya kuoga majosho ya wajibu ya kila siku

Mas’ala Muhimu:

a. Iwapo baada ya Swala ya asubuhi istihadha chache itaongezeka na kuwa ya wastani, basi atawajibika kuoga kwa ajili ya Swala za adhuhuri na alasiri. Na iwapo itaongezeka baada ya Swala za adhuhuri na alasiri, basi atawajibika kuoga kwa ajili ya Swala za magharibi na isha.

b. Iwapo istihadha ya wastani itabadilika na kuwa nyingi, basi ni lazima kuoga kwa ajili ya kila Swala (yaani atende matendo ya mwenye istihadha nyingi).

c. Istihadha itakapokatika, ni wajibu kutekeleza mambo ya wajibu ambayo yanahusu istihadha husika kwa ajili ya Swala ya kwanza tu, na wala si kwa Swala zitakazofuata. Kwa hiyo iwapo damu ya mwenye istihadha ya wastani au nyingi itakatika ni lazima aoge.

Lakini ikiwa ametenda mambo ya wajibu wakati wa kuoga kwa ajili ya Swala iliyotangulia; hatowajibika kuoga mara nyingine iwapo damu yoyote haijadhihiri.

Na iwapo Mwenye istihadha chache atatoharika kutokana na Damu basi atatumia Kanuni zake kwa ajili ya Swala ya kwanza atakayoitekeleza baada ya kusafika, na atatumia utaratibu wa kawaida kwenye Swala zitakazofuatia.

Nukta Muhimu:

Hukumu zilizotajwa hapo juu kuhusu damu ya istihadha ndizo fat’wa za Wanachuoni wengi Wakuu wa Madhehebu ya Shia Imamiya, na wala hakuna tofauti kubwa kati yao kuhusu mas’ala hayo.

Tatu: Nifasi:

Maana Yake:

Nifasi au damu ya uzazi ni damu inayoonekana wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua. Inapoonekana na isikatike mpaka siku kumi tokea alipojifungua, basi huitwa damu ya nifasi. Na ndani ya istilahi ya sharia ya ki-Islamu mwanamke huyo anayeona damu ya uzazi nifasi huitwa Mwenye Nifasi.

Alama Zake:

1. Damu ya nifasi huenda ikaonekana kwa kiasi cha muda mchache tu baada ya kujifungua au (kuharibu mimba). Ama damu inayoonekana baada ya siku kumi tangu kujifungua haihesabiki kuwa ni nifasi.

2. Iwapo atakuwa anaona damu leo, kisha kesho haoni, mpaka muda wa siku kumi; basi yote ataifanya kuwa ni nifasi.

3. Iwapo ataona damu zaidi ya siku kumi, na kuendelea kwa muda wa mwezi mzima, hali hiyo ina sura mbili:

a. Ikiwa mzunguko wa damu yake ya mwezi una ada maalumu, basi kati- ka hali kama hii atachukua idadi ya siku zake za damu ya mwezi afanye ndiyo nifasi, na zitakazobakia afanye kuwa ni istihadha.

b. Ikiwa mzunguko wa Damu yake ya Mwezi hauna Ada Maalumu basi katika hali kama hii Siku kumi za mwanzo atazifanya Nifasi na zilizozidi atazifanya Istihadha.

Nukta Muhimu:

Iwapo baada ya kujifungua damu itaendelea zaidi ya siku kumi, na ikawa siku ya kwanza baada ya siku ya kumi imegongana na siku ya kwanza ya damu yake ya mwezi, na akawa ni mwenye ada maalumu, na hali ya kuwa damu ina sifa za hedhi; basi siku kumi za mwanzo atazifanya kuwa ni nifasi na siku nyingine atazifanya kuwa ni siku za damu yake ya mwezi.

Kanuni:

1. Kanuni za mwenye nifasi ni sawa na za mwenye hedhi. Hairuhusiwi kumwingilia, haisihi kumpa talaka, na ni haramu kwake kusali, kufunga, kugusa andiko la Qur’ani na kusoma sura zenye Aya ya sijida ya wajibu.

2. Kila lililo wajibu au sunna au karaha kwa mwenye hedhi pia ndivyo lilivyo kwa mwenye nifasi.

3. Ni lazima kwa mwanamke baada ya kutoharika kutokana na nifasi, aoge kisha atekeleze ibada zake.

Nne: Josho La Janaba:

Mwenyezi Mungu amesema: “Na mkiwa na janaba, basi ogeni…”1

Janaba Ni Nini?

1. Janaba hupatikana kwa mwanadamu kwa moja kati ya mambo mawili:

2. Kujamiana.

Manii kutoka kwenye mwili wa mwanadamu usingizini au hali ya kuwa macho. Na ni lazima kuoga janaba kutokana na moja ya sababu hizo mbili.

Utambulisho:

Manii: Hayo ni maji yanayotoka ndani ya mwili wa mwanadamu pindi yanapopatikana matamanio, na kwa wanaume hali ya kutoka kwa manii huambatana na msukumo na (hatimaye) uchovu wa mwili.

Kwa matokeo hayo, janaba huthibiti kwa masharti yafuatayo:

a. Kutoka manii hali ya kuhisi matamanio.

b. Kutoka manii pamoja na kuwepo msukumo.

c. Kutoka manii pamoja na kupatikana uchovu wa mwili.

Kutokana na maelezo hayo ni kuwa; unyevunyevu unaotoka mwilini ambao hauna moja ya sifa hizo hauchukuliwi kuwa ni manii.

Lakini kwa mgonjwa na mwanamke halizingatiwi sharti la msukumo na uchovu wa mwili, hivyo ikiwa unyevunyevu utatoka huku akiwa na hali ya matamanio ni lazima aoge.

Hatuna budi kusema kuwa wanachuoni wetu watukufu, wengi hawazingatii nukta mbili: Ya pili na ya tatu kuwa ni sharti kwa mwanamke.

Mambo Mawili Muhimu:

i. Iwapo mtu atapatwa na hali ya matamanio na uchovu wa mwili kwa sababu ya kutazama filamu za ngono au picha za uchi (Mungu apishie mbali) na akawa na yakini kuwa manii yamemtoka, basi kanuni za janaba zitamuhusu na hivyo atawajibika kuoga.

ii. Iwapo mtu anajua kuwa, lau akitazama filamu za ngono au kusoma baadhi ya majarida au vitabu vyenye kuamsha hisia za matamanio na hatoweza kujizuia na hivyo atapata janaba, basi ni lazima kwake kujiepusha na mambo hayo.

Yaliyoharamishwa Kwa Mwenye Janaba

a. Mwili wake kugusa Qur’an au jina la Mwenyezi Mungu, aidha ni wajibu kujiepusha kugusa majina ya manabii na maimamu (a.s.) na pia jina la bibi Fatimat Zahraa (a.s.).

b. Kuingia msikiti mtukufu (wa Makkah) na msikiti wa Mtume (s.a.w.) hata kama itakuwa ni kwa kuvuka, aidha ni wajibu kujiepusha kuingia ndani ya maeneo yalimo makaburi matukufu ya Maimamu walio takasika (a.s.) hata kama ni kwa kuvuka.

c. Kuketi na kusimama ndani ya misikiti mingine. Si vibaya kuvuka kwa kuingilia mlango mmoja na kutokea mlango wa pili.

d. Kuweka kitu msikitini hata kama ataweka akiwa nje au wakati wa kuvuka.

e. Kusoma sura nne zenye sijida ya wajibu, hata kama itakuwa herufi moja ya sura hiyo. Nazo ni:-

    • As-Sajda-Sura ya 32,

    • Al- Fuswilatu-Sura ya 41,

    • An-Najmu-Sura ya 53,

    • Al-Alaqi-Sura ya 96

Mambo Yaliyo Karaha Kwa Mwenye Janaba

    a. Kula na kunywa, na karaha yake huondoka kwa kutia udhu.

    b. Kusoma zaidi ya Aya saba za sura nyingine zisizokuwa na Aya ya sijida ya wajibu.

    c. Kugusa sehemu nyingine ya msahafu isiyokuwa na andiko, kuanzia jalada, karatasi, maelezo ya ziada na eneo lililopo kati ya mistari. Hapa tunapenda kuhimiza kuwa, uharamu wa kugusa andiko la Qur’an kwa mwenye janaba, haukomei kwenye Mashafu Tukufu tu, bali unahusu kila ilipoandikwa Aya Tukufu, sawa iwe kwenye karatasi, gazeti, kitabu (au kitu chochote).

    d. Kubeba Mashafu Tukufu. e. Kubadili nywele rangi.

    e. Kupaka mafuta kichwani na mwilini.

    f. Kulala. Na karaha yake huondoka kwa kutia udhu au kutayamamu.

Nukta Muhimu:

Iwapo mtu atapatwa na janaba kisha akaoga, basi kuanzia hapo si karaha kwake kutenda mambo yaliyotajwa hapo juu.

Tano: Josho La Maiti

Sita: Josho La Kugusa Maiti

Utangulizi:

Kwa kuwa haya mambo mawili yanahusu kanuni za maiti na mas’ala haya yana umuhimu mkubwa, basi ni vizuri dada zetu waumini wakajua angalau muhtasari wa mas’ala haya na yale yanayowahusu wao, na ili waweze kuwafunza wenzao pindi yanapohitajika au wakati wa dharura.

Kanuni Za Maiti:

1. Wakati wa kutoka roho.

2. Hukumu za baada ya kifo.

3. Josho la maiti

4. Kumpaka karafuu maiti

5. Kumvisha sanda

6. Swala ya jeneza

7. Mazishi

8. Josho la kugusa maiti

Wakati Wa Kutoka Roho.

Dakika za mwisho za uhai wa mwanadamu ambazo ndani yake alama za kifo huonekana, ni pale ambapo mwislamu anakuwa katika hali ya kutokwa na roho. Na hali hii huitwa Al-Ihtidhaar. Ndani ya dakika hizo kuna mambo ya wajibu yafuatayo:

1. Mtu ambaye yumo katika hali ya kutoka roho, alazwe chali na nyayo zake kwa ndani zielekezwe kibla, kiasi kwamba lau ataketi uso wake utakuwa umeelekea Qibla. Ni sawa sawa akiwa mwanamke au mwana mume, mtoto au mkubwa.

2. Kumwelekeza Qibla mtu anayekaribia kutokwa na roho, ni wajibu wa kutoshelezana kwa waislamu, wala jambo hili halihitajii idhini ya walii wake.

Mambo Yaliyo Sunna Kumfanyia Mtu anaye kata roho.

1. Kumtamkisha shahada mbili na kukiri Maimamu kumi na mbili (a.s.) na itikadi nyingine za haki na maneno ya faraja.

2. Kumtamkisha dua hii: “Ewe Mwenyezi Mungu nisamehe mengi miongoni mwa (maasi) niliyokuasi, na pokea kichache kutoka kwangu miongoni mwa yale niliyokutii. Ewe (Mola) ambaye anapokea kichache na anasamehe mengi, pokea kichache kutoka kwangu na unisamehe mengi, hakika wewe ni Msamehevu na Mwingi wa Msamaha. Ewe Mwenyezi Mungu! Nirehemu kwani hakika wewe ni Mrehemevu.”

3. Ili kumrahisishia utokaji wa roho, ni sunna kumsomea sura tuku- fu Yasini, As-Swafati, Al-Ahzabu na Aya ya Al-Kursiyu, Aya ya hamsini na nne ya Sura Al-Aarafu na Aya tatu za mwishoni mwa Sura Al-Baqara.

4. Mwenya kukata roho ahamishiwe kwenye mSwala wake.

Mambo Yaliyo Karaha:

1. Kumwacha huyu mwenye kukata roho peke yake.

2. Kuweka uzito juu ya tumbo lake.

3. Kukithirisha mazungumzo na kilio mbele yake.

4. Mwenye hedhi na mwenye janaba kuhudhuria mbele yake.

5. Kumgusa awapo katika hali ya kutokwa roho.

Hukumu za Baada ya Kifo:

1. Ni Sunna kumfumba macho, kumfumba kinywa na kufunga taya

2. Kuinyoosha mikono yake kwenye mbavu zake, kunyoosha miguu yake na kumfunika kwa nguo.

3. Kumuwashia taa usiku.

4. Kuwaarifu waumini ili wahudhurie mazishi yake.

5. Kuharakisha kumuandaa (isipokuwa kama kuna utata wa hali yake, hivyo atasubiriwa mpaka upatikane uhakika wa kifo chake).

6. Atakapofariki mjamzito, basi ni wajibu kumtoa mtoto tumboni (akiwa yuko hai) na ndipo azikwe.

Josho La Maiti:

Nalo ni josho la tano katika orodha ya majosho saba ya wajibu. Ni lazima kuuosha mwili wa maiti kwa maji ya aina tatu kwa kufuata utaratibu ufuatao:

1. Kwa maji yaliyochangwa na mkunazi, (maji yatawekwa mkunazi kidogo ili maji yaendelee kubakia katika hali yake halisi).

2. Kwa maji yaliyochangwa karafuu maiti, (maji yatawekwa karafuu maiti kidogo ili maji yaendelee kubakia katika hali yake halisi.

3. Kwa maji halisi.

Mambo Yanayohusu Josho La Maiti:

a. Iwapo mwanaume atamwosha mwanamke, au kinyume chake basi josho hilo ni batili. Naam; Mwanamke anaweza kumwosha mumewe kama ambavyo mwana mume anaweza kumwosha mkewe.

b. Iwapo itashindikana kupatikana mwana mke wa kuweza kumwosha maiti wa kike, basi inawezekana wanaume maharimu kufanya hivyo, angalau nyuma ya mavazi.

c. Ni lazima kutoharisha mwili wa maiti kutokana na najisi kabla ya kuanza kumwosha.

d. Mwanamke aliyefariki akiwa katika hali ya damu ya mwezi au janaba hahitajii majosho haya mawili, bali josho la maiti pekee linamtosha.

e. Iwapo itashindikana kupatikana mkunazi au karafuu maiti basi maiti ataoshwa katika josho mbili za mwanzo kwa maji khalisi, badala ya yale majosho mawili. (Lakini kwa niya ya badala.)

f. Iwapo itashindikana kupatikana maji basi atatayamamu badala ya kila josho.

g. Mtoto wa ki-Islamu wa mamba iliyotoka ni lazima kumwosha iwapo ametimiza mwezi wa nne.

Kumpaka Karafuu Maiti:

Nalo ni jambo la wajibu, na ni sharti iwe baada ya kumwosha na iwe kwa kumpaka hiyo karafuu maiti juu ya viungo saba vya kusujudia, navyo ni paji, matumbo ya viganja viwili.
Na kwa upande wa miguu, ni magoti mawili na ncha za vidole gumba. Kitendo hiki cha kumpaka karafuu maiti huitwa Al-Hanuut. (Na ni lazima karafuu maiti hiyo iwe imesagwa na kuwa unga, na iwe mpya. Kwa hiyo kama itakuwa kuukuu ambayo haina harufu haitofaa). Na wala haisihi kutumia manukato mengine badala ya karafuu maiti.

Katika suala la kumpaka karafuu maiti, tunaweza kuashiria mambo yafuatayo:

1. Ni sunna kuchanganya karafuu maiti na kiasi kidogo cha udongo wa Imamu Huseini a.s, (kutoka ardhi ya Karbala).

2. Ni bora kumpaka karafuu maiti kabla ya kumvisha sanda.

3. Ni karaha kutumia manukato na udi kwa ajili ya maiti.

Kumvisha Sanda:

Baada ya kumwosha na kumpaka karafuu maiti, ni lazima kuuvisha sanda mwili wa maiti wa Ki-Islamu. Na kuvisha sanda hiyo kunakuwa kwa kutumia nguo tatu ambazo ni kikoi, kanzu na shuka. Na hiyo ndiyo huitwa sanda. Nukta zifuatazo zinahusiana na suala hili:

1. Kikoi chenye kusitiri eneo la kati ya kitovu na magoti, na kanzu itakayofika kwenye nusu ya muundi, na shuka itakayofunika mwili mzima.

2. Gharama za maziko na sanda ya mke ni juu ya mume, hata kama mke ni tajiri.

3. Haisihi kumvisha sanda kwa kutumia kitambaa chepesi ambacho kinaonyesha mwili.

4. Ni lazima sanda iwe safi yenye tohara, na iwe ni ya halali (isiyo ya kunyang’anya).

Swala Ya Maiti:

Nayo ni takbira tano, na katika kila baada ya takbira moja kupatikane dhikri (kisomo maalum) isipokuwa katika takbira ya mwisho. Na uchache wa kisomo cha wajibu katika swala hiyo ni kama ifuatavyo:

1. Allah Akbar. Ash-haduallah ilaha illa llah Wa ash-had anna Muhammadarrasulullah (Allah ni Mkubwa. Nakiri kwamba hakuna Mungu ila Allah, na ninakiri kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah.)

2. Allah Akbar. Allhumma swalli ala Muhammadin wali Muhammad (Allah ni Mkubwa. Ewe Mwenyezi Mungu teremsha baraka juu ya Muhammad na juu ya familia ya Muhammad).

3. Allah Akbar. Allhummaghfir lilimuminina wal-mu’minat (Allah ni Mkubwa. Ewe Mwenyezi Mungu wasamehe waumini wa kiume na waumini wa kike).

4. Allah Akbar. (Allah ni Mkubwa) Kama maiti ni mwanaume itasemwa: Allhummghfir lihadhalmayyit (Ewe Mwenyezi Mungu msamehe maiti huyu). Kwa mwanamke: Allhummghfir lihadhi-hilmayyit Ewe Mwenyezi Mungu msamehe maiti huyu).

5. Allah Akbar. Allah ni Mkubwa.

الله أكبر: اشهد أن الا الله واشهد أنّ محمدا رّسول الله

الله أكبر: اللهم قلّ على محمّد وآل محمّد

الله أكبر: اللهم اغفر للمؤمنين والمؤمنات

الله أكبر: اللهم اغفر لهذا الميّت/ لهذه الميَت 

الله أكبر

Mambo Yanayo Husiana Na Suala Hili:

A. Kisomo cha sunna katika swala hii kimetajwa kwa ukamilifu ndani ya vitabu vya dua na vitabu vya matendo ya kisharia vya waheshimiwa wanachuoni wetu.

B. Kwenye Swala ya maiti, mwenye kusali atasimama huku ameelekea Qibla hali ya kuwa jeneza likiwa juu ya ardhi, huku kichwa cha maiti kikiwa kuliani mwa mwenye kuswali na miguu ikiwa kushotoni mwake.

C. Ni wajibu kumsalia maiti mwislamu aliyetimiza miaka sita. d. Udhu si sharti katika Swala ya maiti.

Mazishi:

Baada ya kumwosha ni lazima kumpaka karafuu maiti kisha kumvisha sanda, halafu kumswalia na hatimaye mwili kuzikwa ardhini kwa namna ambayo itazuia harufu kutoka nje, au kufukuliwa na wanyama.

Katika Mazishi Kuna Mas’ala Kadhaa, Miongoni Mwa Hayo Ni:

1. Hairuhusiwi kumzika mwislamu kwenye makaburi ya makafiri, wala kumzika kafiri kwenye makaburi ya waislamu.

2. Mwili wa mwana mke utawekwa kaburini kupitia mmoja wa maharimu wake au mwana mke mwenzake.

3. Maiti hulalia ubavu wake wa kulia awekwapo kaburini kiasi kwamba uso wake na mwili wake utaelekea Qibla, na nyuma ya mgongo wake huwekwa mto wa udongo ili asilale chali, huku mikono yake ikiwekwa juu ya udongo.

4. Hairuhusiwi kufukua kaburi la maiti ya ki-Isilamu kwa lengo la kumzika mwislamu mwingine.

5. Ni sunna kusali swala ya (rakaa mbili ambayo ni) zawadi kwa ajili ya maiti usiku ule wa mazishi. Ndani ya rakaa ya kwanza atasoma Al-Hamdu na Ayatul-Kurusiyy mara moja, na katika rakaa ya pili atasoma Al-Hamdu na Suratul-Qadri mara kumi,

kisha baada ya swala aatasema: “Ewe Mwenyezi Mungu teremsha baraka kwa Muhammad na familia ya Muhammad na peleka thawabu zake kwenye kaburi la fulani.” Atataja jina la marehemu huyo.

Nukta Muhimu:

Ndani ya vitabu vya dua na vitabu vya matendo ya kisharia vya waheshimiwa wanachuoni wetu wakuu, kumepatikana mafunzo na sunna nyingi zinazohusiana na mazishi. Miongoni mwa vitabu hivyo, ni kitabu kiitwacho Mafatihul-Jinani cha Sheikh Abasi Al-Qummi. Kwa mwenye kutaka ziyada arejee humo.

Josho La Kumgusa Maiti:

Nalo ni josho la sita katika orodha ya majosho saba ya wajibu:

1. Iwapo sehemu ya mwili wa mwanadamu itagusa mwili wa maiti baada ya mwili wake wote kupoa na kabla hajaoshwa, basi ni wajibu kuoga josho la kumgusa maiti.

2. Josho hili si wajibu iwapo umegusa maiti ya mimba iliyotoka ambayo haijatimiza miezi minne.

3. Josho hili ni wajibu kwa mama aliyetoa mimba ambayo imetimiza miezi minne.

4. Josho hili pia ni wajibu iwapo mwanadamu atagusa kipande kilichokatika kutoka kwenye mwili wa maiti kabla maiti hajaoshwa.

5. Namna ya kuoga josho la kumgusa maiti, ni kama namna ya kuoga janaba.

Majosho Ya Sunna Ambayo Huwa Wajibu Kwa Sababu Ya

Nadhiri Au Kiapo:

Sehemu ya saba ya majosho ya wajibu ni pindi mwenye kulazimikiwa na sharia atakapoweka nadhiri ya kisharia (kama ilivyo fafanuliwa ndani ya vitabu vya Fiqihi. Au akaapa kiapo cha kisharia kuwa ni lazima aoge moja kati ya majosho ya sunna, basi hapo josho hilo la sunna linakuwa wajibu juu yake.

  • 1. Al-Maida: 6.