Table of Contents

Sura Ya Pili: Mahusiano Kati Ya Alama Za Kubaleghe Na Suala La Hedhi

Mara nyingi upatikanaji wa damu ya mwezi kwa wasichana hutokea kati ya umri wa miaka kumi na mbili hadi miaka kumi na nne.

Tofauti hii inatokana na sababu za kimazingira, kijografia na kinasaba. Hivyo katika nchi zenye baridi damu ya mwezi huchelewa kuonekana mpaka kwenye umri wa kati ya miaka kumi na sita hadi kumi na nane. Na katika nchi zenye joto huonekana mapema kwenye umri wa kati ya miaka kumi hadi kumi na mbili.

Msichana anapotimiza miaka tisa ya mwandamo analazimika kumrejea mwanachuoni mwenye daraja ya ijtihad aliyetimiza masharti.

Atamrejea mwanachuoni huyo ili amfuate katika nadharia zake na rai zake zinazohusu sharia katika namna ya utekelezaji wa wajibu wa kisharia, kuanzia Swala, swaumu na sharia nyinginezo.

Bila shaka vigawanyo vya damu ambayo huiona mwanamke ni vigawanyo saba, na kila kimoja kati ya hivyo kina kanuni zake mbalimbali za kisharia. Sisi tutavitaja vigawanyo hivi na kisha baada ya hapo tutazifafanua kanuni za wajibu.

1. Aina za Damu:

A- Damu ya majeraha itokayo toka ndani ya kizazi.

B- Damu ya vidonda vinavyo patikana kwenye ngozi.

C- Damu ya puani ambayo hutoka puani.

D- Damu ya bikira. (Damu inayosabishwa na kufanya tendo la ndoa kwa mara ya kwanza).

E- Damu ya hedhi. (Damu inayotoka kwenye kizazi).

Damu ya istihadha. (Hii ni damu ambayo hutoka kabla au baada ya hedhi au nifasi)

Damu ya nifasi (Hii ni damu ambayo hutoka baada au wakati wa kujifungua).

Mas’ala Mawili:

Damu inayosamehewa ni ile yenye kiwango cha upana wa dirhamu inapokuwa kwenye vazi au mwili, na Swala inasihi hata ukiwa nayo.

Damu hiyo ni damu ya jeraha la kawaida peke yake (ndiyo inayo sameheka) na wala si damu nyingine zinazo wahusu wanawake.

Damu ya kawaida ya mwili inapochanganyika na najsi au na kitu kingine, basi hapo haihusiki na msamaha huu wala ruhusa hii.

2: Majosho Ya Wajibu, Nayo Ni Saba:

Josho la janaba
Josho la istihadha
Josho lanifasi Josho la janaba
Josho la maiti1
Josho la kumgusa maiti
Josho la sunna ambalo huwajibika kwa nadhiri au kiapo.

Kwanza: Kanuni Za Hedhi:

Mwenyeezi Mungu anasema: “Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Waambie: Huo ni uchafu, basi jitengeni na wanawake katika hedhi….”2

Maana Ya Hedhi:

Hedhi ni Damu anayoiona mwanamke katika baadhi ya siku, aghlabu huwa ndani ya kila mwezi.
Na ndani ya siku za kutoka kwa damu hiyo, mwanamke huitwa Mwenye Hedhi.

Alama Za Damu Ya Hedhi:

Damu ya Hedhi ni nyekunde yenye kuelekea kwenye weusi, au nyekundu nzito, yenye msukumo, joto na harara3

Sharti:

Balehe ya kisharia, nayo ni kutimiza miaka kumi ya mwandamo. Uchache wa Hedhi ni siku tatu.

Wingi wake ni siku kumi, hivyo kila damu aionayo mwanamke chini ya siku tatu au iliyozidi baada ya siku kumi, siyo hedhi.

Kauli yenye nguvu ni kuwa, kipimo ni siku tatu zenye kufuatana, na hilo haliharibiwi na ukatikaji wa muda mchache.

Mpaka unaotenganisha kati ya hedhi na hedhi nyingine (ambao ndio uchache wa siku za tohara) ni siku kumi, na hapo ni lazima damu mpya ipimwe kwa alama za hedhi.

Mfano: Iwapo mwanamke ataona damu baada ya vipindi viwili vya tohara ya mzunguko wa mwezi na baada ya kuwa zimepita siku kumi basi (ili ihesabike ni damu ya mwezi) ni lazima damu hii iwe na sifa zilizotajwa.

Na kama mpaka unaotenganisha utakuwa chini ya siku kumi basi damu hii haitahesabika kuwa ni hedhi hata kama itakuwa na alama za hedhi bali itakuwa ni damu ya Istihadha.4

Damu ya hedhi kama tulivyosema, hupatikana baada ya kutimiza miaka tisa ya mwandamo na kabla ya ukomo wa hedhi, na damu itokayo baada ya miaka ya ukomo wa hedhi huwa ni damu ya Istihadha.

Umri wa kukoma kutokwa na hedhi (Maana yake, Alama zake na Hukumu zake):

Maana Yake:

Mwenye kukoma kutokwa na hedhi ni mwanamke aliyetimiza umri wa miaka sitini ya mwandamo ikiwa ni mwanamke wa ki-Qurayshi, na miaka hamsini kama si mwanamke wa ki-Qurayshi.

Kutimia umri wa miaka sitini ya mwandamo kwa mwana mke wa ki-Qurayshi, taqriban ni sawa na miaka hamsini na nane na miezi miwili ya mwaka wa mawiyo5

Aidha kwa mwana mke asiyekuwa Mquraishi kutimiza umri wa miaka hamsini, taqriban ni sawa na umri wa miaka arobaini na nane na miezi mitano ya mwaka wa mawiyo.

Mwanamke mwenye kukoma kutokwa na hedhi huwa haoni damu ya hedhi, na iwapo ataona damu kwa namna ya kuendelea au ya kukata huhesabiwa kuwa ni damu ya Istihadha.

Mas’ala:

Ni upi wajibu alionao mwanamke anapokuwa ndani ya siku za kujichunguza?
Ni lazima kwa mwanamke ambaye ametimiza alama na masharti ya hedhi ajichunguze mwenyewe kwa muda wa siku tatu kuanzia pale linapotoka tone la kwanza la damu.

Nini maana ya mwanamke kujichunguza kwa muda wa siku tatu?

Jibu:

Maana yake ni kuwa: Baada tu ya mwanamke kuona tone la kwanza la damu anatakiwa kuyaacha matendo yake ya kiibada kwa muda wa siku tatu mpaka itakapobainika hali yake upande wa wajibu wa kisharia na kujua je, atatumia kanuni za hedhi au atatumia kanuni za damu ya Istihadha?

Kwa hiyo ndani ya siku hizi tatu, ni lazima kwake kuyaacha mambo yote yaliyoharamishwa kwa mwanamke mwenye hedhi.

Na iwapo damu itaendelea kwa muda wa siku tatu bila kukatika atachukulia kuwa ni hedhi, na hapo atalazimika kutumia kanuni za hedhi.

(Mfano, ikiwa siku hizi zimo ndani ya mfungo mtukufu wa Ramadhan ni lazima kwake kulipa swaumu na wala si lazima kulipa Swala.)

Na iwapo ni kinyume na hivyo basi atachukulia kuwa ni damu ya Istihadha na atawajibika kutumia kanuni zake, hivyo atalazimika kulipa saumu pia Swala iliyompita ndani ya siku hizo.

Mas’ala:

Ndani ya siku za kujichunguza ambazo bado wajibu wake kisharia haujabainika, haifai (kwake) kuswali au (kufunga) swaumu au kuingia msikitini na kila jambo linalohitaji tohara.

Mwanzo Wa Hedhi:

Kwa wasichana wengi hedhi hudhihirika kama ilivyo kwa mama zao, na kwa ujumla inakuwa kati ya umri wa miaka tisa hadi kumi na sita ya miaka ya mwandamo. Wakati huo huo suala hili lina athiriwa na sababu za kimazingira (kutegemeana) na kiwango cha joto.

Ama katika nchi za mashariki ya kati, inakuwa ni kati ya miaka kumi na moja hadi kumi na mbili. Asilimia tano ya wasichana huchelewa hadi umri wa miaka kumi na sita mpaka kumi na nane.

Hatuna budi kugusia kuwa, miezi ya mwanzo ya kudhihiri damu ya mwezi huwa haina mpangilio maalumu kwa wasichana wengi, kwani msichana anaweza kuiona damu kuanzia siku tatu mpaka tano, lakini baada ya kupita miezi miwili au mitatu damu hiyo (kwa kawaida) hutulia kwenye siku zenye mpangilio maalum.

Vigawanyo vya Hedhi:

Mwenye kuanza: Naye ni mwanamke ambaye anaishuhudia damu kwa mara ya kwanza.

Mwenye Kukoma kutokwa na Hedhi: Kama tulivyosema tangu mwanzo kuwa mwanamke wa ki-Quraysh anaingia miaka ya ukomo wa kutokwa na hedhi baada ya kutimiza miaka sitini ya mwandamo, na yule asiye Mquraysh huwa (anakoma) baada ya kutimiza miaka hamsini ya mwandamo, na mwanamke wa namna hii kwa mujibu wa wanachuoni wa sharia ya ki-Islamu, huitwa Mwenye kukoma kutokwa na hedhi.

Mwenye Ada ya Wakati na Idadi: Huyu ni mwanamke ambaye anaiona damu kwa utaratibu wa namna moja ndani ya miezi miwili yenye kufuatana. Damu inaanza kumtoka ndani ya siku maalumu na kukomea ndani ya siku maalum.

Hivyo Siku za hedhi yake zikilingana huitwa Mwenye Ada ya Wakati na Idadi. Na kwa maana nyingine ni mwanamke ambaye hedhi yake inalingana, kwa uchache (kanuni hii inapimwa) ndani ya miezi miwili yenye kufuatana.

Mwenye Ada ya Idadi: Naye ni mwanamke ambaye anaona damu kwa idadi ya siku maalum ndani ya miezi miwili yenye kufuatana, isipokuwa muda wa kuanza unapishana. Kwa mfano mwezi wa kwanza, ada yake ya mwezi inaanza siku ya tano mpaka siku ya kumi, na katika mwezi wa pili inaanza siku ya saba mpaka siku ya kumi na mbili. (Hapo idadi ya siku inalingana lakini unapishana wakati wa kuanza).

Mwenye Ada ya Wakati: Huyu ni mwanamke ambaye anaona damu ndani ya wakati maalumu ndani ya miezi miwili yenye kufuatana, isipokuwa ndani ya kila mara idadi ya siku inapishana. Kwa mfano katika mwezi wa kwanza damu inaanza siku ya kwanza mpaka siku ya tano, na katika mwezi wa pili inaanza siku ya kwanza mpaka siku ya saba. (Hapo wakati wa kuanza umelingana, na tofauti iko kwenye idadi ya siku).

Asiye na Ada Maalumu: Naye ni mwanamke ambaye tangu alipoanza kupata damu ya mwezi kwa miezi kadhaa, damu yake haina muda maalum wa kuanza wala idadi maalum ya siku.
Aliyesahau: Huyu ni mwanamke aliye sahau aina ya Ada yake.

Nukta Muhimu:

Ni vizuri kwa mwanamke kuzitambua siku za hedhi yake kulingana na kalenda maalumu katika miezi iliyopita na miezi itakayofuata ili aweze kupanga utaratibu wa matendo yake na ibada zake kulingana na kalenda hiyo. Lifuatalo ni swali ambalo tutalijibu kulingana na vigawanyo hivyo tofauti.

Swali: Iwapo mwanamke ataona damu kwa muda wa siku kumi na mbili, basi ni ipi kanuni yake?

Mwenye kuanza: Iwapo atashuhudia damu zaidi ya siku kumi zenye kufuatana, basi muda wa chini (kwa mujibu wa sharia) ni siku tatu, na wingi wa muda wa (kutoka damu) itambidi kuwarejea ndugu zake. Kwa hali hiyo atatumia kanuni ya hedhi kwa idadi ya siku za hedhi yao, na siku zitaka-zozidi atazifanya kuwa ni damu ya Istihadha.

Mfano ikiwa idadi ya siku za hedhi kwa mzazi wake ni siku saba, basi na yeye atafanya siku saba kuwa ndio hedhi yake (kwa sharti kwamba damu ile iwe na sifa na masharti yanayohusu hedhi), na siku zilizobaki atazifanya kuwa ni damu ya Istihadha. Aidha ndugu ambao mwanamke huyu atawatumia katika kanuni hii, ni wafuatao kwa kufuata utaratibu huu: Mama, dada, mama mdogo (au mkubwa), shangazi, binti wa dada na binti wa shangazi.

Mwenye Ada ya Wakati na Idadi: Iwapo mwenye ada ya wakati na idadi ataona damu zaidi ya idadi ya siku za ada yake basi zilizozidi atazifanya kuwa ni damu ya Istihadha.

Mwenye Ada ya Idadi: Aidha mwanamke huyu naye pia atafanya idadi ya siku za hedhi ya miezi iliyotangulia kuwa ndio hedhi, na zilizozidi atazifanya kuwa ni damu ya Istihadha. Mfano: Iwapo katika miezi iliyotangulia hedhi yake ilikuwa ni siku tano basi na ndani ya mwezi huu ni siku tano na siku zilizobaki ni damu ya Istihadha.

Mwenye Ada ya Wakati: Iwapo Mwenye Ada ya Wakati ataiona damu zaidi ya siku kumi, basi jambo hilo lina sura nyingi:

a. Ikiwa kutokana na sifa za damu anaweza kugundua ni ipi damu ya hedhi, na ni ipi damu ya Istihadha, basi analazimika kutenda kulingana na hali hiyo.

b. Na ikiwa hawezi kutenganisha sifa za damu basi atarejea kwa jamaa zake ambao ni (Mama, dada na mama mdogo). Kwa hiyo atatambua siku za ada yake kwa kufuata ada zao.

c. Ikiwa siku za hedhi kwa ndugu zake hazina ada maalumu, basi siku saba za mwanzo atazifanya kuwa ni hedhi, na siku zilizobaki atazifanya kuwa ni damu ya Istihadha.

Asiye na Ada Maalum: Iwapo ndani ya mwezi huu itatokea kuona damu zaidi ya siku kumi, basi atafuatilia sifa za damu. Endapo zinafanana na sifa ya hedhi, basi siku kumi za mwanzo atazifanya kuwa ni hedhi na zilizobakia atazifanya kuwa ni damu ya Istihadha. Na kama hazifanani na sifa ya hedhi, basi ni wajibu juu yake atende kulingana na vipengele viwili vya A na B vinavyohusu kanuni ya Mwenye Ada ya Wakati.

Aliyesahau: Iwapo ataona damu zaidi ya siku kumi, basi anawajibika kutenda kulingana na hukumu za kifungu cha tano, yaani cha yule Asiye na Ada Maalum.

Yaliyoharamishwa Kwa Mtu Mwenye Hedhi:

Ibada: Kwa mfano; Swala, swaumu, kutufu Al-Kaaba, kukaa itikafu na kila lile ambalo utekelezaji wake unahitajia josho au udhu au kutayammam.

Kila lililo haramishwa kwa mtu mwenye janaba; kwa mfano: kugusa andiko la Qur’an, kuingia Msikiti Mtukufu wa Makkah6 na Msikiti wa Mtume (s.a.w.). Hairuhusiwi hata kama itakuwa ni kwa namna ya kupita, kukaa ndani ya Msikiti wowote ule usiyokuwa hiyo miwili. Si ruhusa pia (kuingia na) kuweka kitu Msikitini, kusoma moja ya Sura zenye Aya ya Sijida ya Wajibu, hata ikiwa baadhi yake kama vile Bismillahi au herufi yoyote ya Sura hizo (kwa nia ya kuwa ni sehemu yake). Kujamiana kati ya Wanandoa. (Na uharamu wake unahusu pande zote mbili, yaani mume na mke).

Mas’ala:

Kafara ya kujamiana ndani ya theluthi ya kwanza ya siku za hedhi ni dinari moja,7 na ndani ya theluthi ya pili ni nusu dinari, na ndani ya theluthi ya mwisho ni robo dinari. Na inawezekana kutoa thamani hiyo kwa fukara mmoja au kwa mafukara watatu.

Mas’ala Muhimu Kuhusu Hedhi:

Ndani ya siku za hedhi haisihi kutekeleza Swala za wajibu za kila siku, na wala mwanamke hawajibiki kuzilipa. Ama swaumu nayo pia haisihi, lakini ni lazima kuilipa. Iwapo mwanamke atapatwa na hedhi akiwa ndani ya Swala, basi Swala yake inabatilika.

Iwapo mwanamke ataichelewesha Swala na muda wa kuweza kuitekeleza Swala nzima ukampita, (mfano baada ya adhana ya adhuhuri akawa ameichelewesha Swala kwa muda wa kuweza kutimiza rakaa nne), kisha ndipo hedhi ikaanza kumtoka, basi katika hali kama hiyo ni lazima kulipa Swala hiyo iliyompita.

Iwapo Mwanamke atatoharika na akawa ana muda wa kutosha kuoga na kufanya vitangulizi, kuanzia kuandaa mavazi na mengineyo na kutekeleza rakaa moja ya Swala au zaidi ya moja, basi katika hali kama hiyo atalazimika kuoga na kutekeleza Swala, na kama hatofanya hivyo basi atalazimika kulipa Swala hiyo.

Mwanamke mwenye hedhi baada ya kutoharika analazimika kuoga na kisha kutia udhu pindi anapotaka kusali au kufanya ibada nyingine, na bora ni kutia udhu kabla ya kuoga iwapo anataka kusali. Talaka inayotolewa kwa mwanamke akiwa katika hedhi ni batili, (isipokuwa katika baadhi ya hali, lakini inasihi kuolewa).

Ni sunna kwa mwanamke mwenye hedhi kubadili pamba (na kujiweka katika hali ya unadhifu) kisha kutia udhu ndani ya kila wakati wa Swala (unapoingia) halafu akae chini (kwa kiasi cha) muda wa kuweza kutekeleza Swala nzima huku akiwa ameelekea Qibla hali ya kuwa akimtaja Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Pili: Damu Ya Istihadha: Maana Yake:

Hii ni moja ya damu ambazo humtoka mwanamke. Na pindi inapomtoka, basi mwanamke huyo huitwa Mwenye Istihadha.

Alama Zake:

Kwa kawaida damu ya Istihadha huwa ya njano, yenye baridi, tena nyepesi, wala haitoki kwa nguvu na wala haichomi, japokuwa inaweza ikawa na sifa za hedhi.

Vigawanyo Vya Damu Ya Istihadha:

Istihadha Nyingi
Istihadha ya Wastani
Istihadha Chache.

Jinsi Mwanamke Atakavyo Tambua Kanuni Za Damu Ya Istihadha

Iwapo mwanamke hajui damu yake ni ya kifungu kipi, basi anaweza kulala chali kisha ainue nyayo zake na kuingiza kipande cha pamba ndani ya utupu wake, kisha asubiri kidogo na ndipo akitoe.

Iwapo pamba itachafuka (italowana) kwa damu bila damu kupenya ndani ya pamba ile, na bila kuonekana upande wa pili, basi hiyo ni Istihadha chache.

Iwapo Damu itapenya ndani ya pamba na kuonekana upande wa pili lakini bila kutiririka kutoka kwenye pamba, basi hiyo ni Istihadha ya wastani.

Na iwapo itatiririka toka kwenye pamba mpaka nje ya pamba basi hiyo ni Istihadha nyingi.

Hukmu Zinazo Shirikiana Kati Ya Vigawanyo Vitatu:

Kutia udhu kwa ajili ya kila Swala. Kwa hiyo Swala ya Adhuhuri inahitaji udhu wake, na Swala ya alasiri itahitaji udhu mwingine.

Kubadili pamba, na kuyatoharisha mavazi ambayo yamepatwa na najisi hata kama ni chache.

Kuutoharisha mwili kutokana na najisi iliyompata mwilini.

Hukmu Makhsusi Kwa Kila Kifungu:

Hukmu ya Istihadha Chache: Ni kutenda mambo matatu yenye kushirikiana ambayo yametajwa hapo nyuma kwa ajili ya kila Swala. (Inakusudiwa kutia udhu, kubadili pamba au pedi, na kuyatoharisha mavazi yaliyo najisika, na sehemu ya mwili iliyopatwa na najisi).

Hukmu ya Istihadha ya Wastani: Hukmu ya mwenye istihadha hii pamoja na kutenda mambo matatu yenye kushirikiana kwa ajili ya kila Swala; pia ni lazima kila siku kuoga kwa ajili ya Swala ya kwanza baada ya kupatwa na istihadha. Kwa mfano iwapo ataoga josho la istihadha ya wastani kwa ajili ya Swala ya asubuhi, basi siku ya pili ataoga kwa ajili ya Swala hiyo hiyo ya asubuhi. Na iwapo ataoga kwa ajili ya Swala ya adhuhuri, basi pia siku ya pili ataoga kwa ajili ya Swala ya adhuhuri, na hali itakuwa hivyo hivyo iwapo (ataanza kuoga kwa ajili ya) Swala nyingine. Ama katika Swala zitakazobaki ataendelea kutenda mambo matatu yenye kushirikiana.

Hukumu ya Istihadha Nyingi: Hukmu ya istihadha nyingi ni pamoja na kutenda mambo matatu yenye kushirikiana kwa ajili ya kila Swala, piaataoga kwa ajili ya kila Swala.

Kwa hiyo basi, ataoga kwa ajili ya Swala ya asubuhi, na kama anakusanya Swala, basi ataoga kwa ajili ya Swala za adhuhuri na alasiri na ataoga tena kwa ajili ya Swala za magharibi na isha iwapo atazikusanya.

Kusihi kwa josho moja katika kukusanya Swala ya adhuhuri na alasiri na magharibi na isha ni kwa sharti asitenganishe baina ya Swala mbili.

Kinyume na hivyo atalazimika kuoga kwa ajili ya kila Swala huku akitenda yale mambo matatu ya wajibu yanayo shirikiana.

Nukta Muhimu:

Kwa ajili ya kufafanua hukumu zinazohusu vigawanyo vya damu ya istihadha tumeweka jedwali la vigawanyo kama ifatavyo:

  • 1. Majosho haya mawili (Josho la Maiti na Josho la Kugusa Maiti) yanamuhusu Maiti. Katika uchambuzi ujao tutatoa baadhi ya ufafanuzi kuhusu hilo.
  • 2. Al-Baqara: 222
  • 3. Tahriril-Wasilah: 44.
  • 4. Somo la Damu ya Istihadha litakufikia muda mfupi ujao.
  • 5. Mwaka wa mawiyo ni mwaka uliozoeleka na unaojulikana kama mwaka wa kizungu. (Mtarjuma)
  • 6. Huu ni Msikiti uliyoko Makkah. Ama Msikiti wa Mtume ni ule uliyoko Madina.
  • 7. Dinari moja ni sawa na gramu kumi na tisa za Dhahabu Safi.