Kwa Waislamu, imani ya kuja kwa Mahdi (Muhudi) karibu ya mwisho wa dunia ni imani ambayo ina asili katika dini. Waislamu wote bila kujali tofauti za madhehebu zao wanakubaliana juu ya imani hii kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.) alisema: "Hata iwe imebakia siku moja tu kwa dunia hii kufikia mwisho wake Allah atairefusha siku hiyo ili kumwezesha Imam huyo kutawala na kuujaza ulimwengu huu uadilifu, amani na utulivu wakati ambapo ulikuwa umejaa ufisadi na dhulma." Kitu cha kuvutia ni kwamba imani hii haiko kwa Waislamu tu bali hata katika dini nyingine wana imani kama hii kwamba atatokea mtu wakati wa mwisho ambaye ataondoa dhulma na ufisadi na kuujaza ulimwengu huu uadilifu, amani na utulivu.