read

Neno La Mchapishaji

Kitabu kilichoko mikononi mwako ni mkusanyo wa tarjuma ya vitabu viwili vya Kiarabu. Cha kwanza ni, al-Imam al-Mahdiyyu fii Riwayati Ahli's-Sunnah, kilichoandikwa na Sayyid Abdul Rahim al-Musawi. Sisi tumekiita, Imam Mahdi katika Riwaya za Sunni. Na cha pili ni: al- Mahdawiyyah 'Inda Ahli 'l-Bait kilichoandikwa na Sheikh Abdul Karim al-Bahbahani . Sisi tumekiita: Umahdia katika Ahlul Bait. Tumevikusanya pamoja kwa vile tumeona maudhui yao yanafanana.

Vitabu hivi ni matokea ya utafiti wa kielimu pamoja na hoja zenye nguvu na utumiaji sahihi wa akili uliofanywa na wanachuoni wandishi wa vitabu hivi.

Kwa Waislamu, imani ya kuja kwa Mahdi (Muhudi) karibu ya mwisho wa dunia ni imani ambayo ina asili katika dini. Waislamu wote bila kujali tofauti za madhehebu zao wanakubaliana juu ya imani hii kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.) alisema: “Hata iwe imebakia siku moja tu kwa dunia hii kufikia mwisho wake Allah atairefusha siku hiyo ili kumwezesha Imam huyo kutawala na kuujaza ulimwengu huu uadilifu, amani na utulivu wakati ambapo ulikuwa umejaa ufisadi na dhulma.”

Kitu cha kuvutia ni kwamba imani hii haiko kwa Waislamu tu bali hata katika dini nyingine wana imani kama hii kwamba atatokea mtu wakati wa mwisho ambaye ataondoa dhulma na ufisadi na kuujaza ulimwengu huu uadilifu, amani na utulivu.

Mkusanyo wa vitabu hivi ni wenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote. Kutokana na ukweli huu, Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kuvichapisha vitabu hivi kwa lugha ya Kiswahili, kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili, ili kuongeza ujuzi wao katika masuala ya kidini na ya kijamii.

Tunamshukuru ndugu yetu, Hemedi Lubumba Selemani kwa kukubali jukumu hili la kuvitarjumi vitabu hivi. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam, Tanzania.