read

B. Jahannam ( Motoni )

Maelezo juu ya Jahannam ( Motoni )

Waislamu wanatimiza nguzo ya Saumu kwa sababu waweze kuepukana na adhabu za Jahannam . Je, Jahannam ni mahala pa namna gani na humo kuna adhabu za aina gani ?

Kumeandikwa vitabu vingi vikizungumzia swala hili. Qur’an Tukufu inayo maelezo ya kutosha yanayozungumzia mateso na adhabu za kiakili na kimwili kwa ajili ya wale watakaoingizwa humo kwa kutokana kwao kutoishi vile alivyotaka Allah swt, kwa sababu wao hawakutimiza ahadi yao pamoja na Allah swt alivyokuwa amewapa, ambao hawakutimiza makusudi ya kuumbwa kwao yaani kumwabudu Allah swt na si mwingine.

Adhabu kama hizo zinaweza kuangaliwa na kurejewa katika Surah zifuatazo :

al-Baqarah,Aali-’Imran, al-Maaida, al-An’am, al-A’raf, al-Anfal, Younus, Hud, al-Ra’d, al-Hijr, al-NahI, Maryam, Taha, al-Hajj, al-Muminoon, al-Noor, al-Furqan, al’Ankabut, Luqman, al-Sajdah, al-Ahzab, Saba, al-Zumar, al-Ghafir, al-Tur, al-Hashr, al-Ma’arij, al-Buruj, al-Fajr, al-Nisaa..., Katika Surah nyingi, kwa hakika Qur’ani imeteremka kuwaonya wanaadamu dhidi ya moto wa Jahannam na kuwaelekeza katika furaha ya kudumu milele : Ufalme usiokwisha kamwe.

Je, Jahannam ina umbo gani la kuonekana ? Tupitie Ayah ya Qur’an Tukufu Surah ya Al-Balad, 90, Ayah ya 19-20 zisemazo :

Lakini waliokanusha Aya Zetu, hao ndio watu wa upande wa shari. Moto uliofungiwa (kila upande) utakuwa juu yao.

“Kufungiwa inamaanisha kufunikwa; Jahannam inaweza kulinganishwa kama mtungi, wenye kifuniko, juu ya jiko, kwamba chungu kinachomwa ndani na nje. Maana itakuwa wazi zaidi tusomapo Ayah zifuatazo za Qur’ani Tukufu Surah al-Humazah, 104, Ayah 5 – 9 :

Hasha! Bila shaka atavurumizwa katika (Moto unaoitwa) Hutama. Na ni jambo gani litakalokujulisha (hata ukajua) ni nini (Huo Moto unaoitwa ) Hutama ? Ni Moto wa Allah swt uliowashwa (kwa ukali barabara ). Ambao unapanda nyoyoni. Hakika huo (Moto) watafungiwa (wewemo ndani yake ). Kwa magogo marefu marefu

“Kufunikwa juu yao” inamaanisha sawa na vile ilivyo katika Ayah ya 90 : 20 hapo juu. Na mistari yake inaweza kumaanisha kwenda undani zaidi, na mistari hiyo ‘inaongezeka,’ kiurefu, na kwa hakika Allah swt ndiye ajuaye zaidi.

Je miale ya moto wa Jahannam iko yenye ukubwa kiasi gani ? Jibu lake tunapewa na Muumba wetu na Jahannam Qur’ani Tukufu Surah al-Mursalat, 77: Ayah ya 32: "Hakika (Moto huo) hutoa macheche yaliyo kama majumba."

Milango ya Jahannam

Katika mlango wa kwanza wa Jahannam kumeandikwa sentenso tatu: Yeyote yule atakayekuwa na matumaini katika Allah swt basi daima atakuwa mtu mwenye furaha na mafanikio; Yeyote anayekuwa na khofu ya Allah swt basi anajaaliwa usalama; mtu mwovu na aliyepotoka na mstahiki wa adhabu za Allah swt ni yule ambaye hana matumaini yoyote kwa Allah swt na wala hana khofu ya aina yoyote ile ya Allah swt.

Katika mlango wa pili wa Jahannam kumeandikwa yafuatayo: Yeyote yule asiyetaka kufanywa uchi Siku ya Qiyama, basi awavalishe nguo wale walio uchi humu duniani, Yeyote yule asiyetaka kupatwa na kiu Siku ya Qiyamah, basi awanywishe wale wenye kiu humu duniani, Yeyote yule asiyetaka kupatwa na njaa Siku ya Qiyamah, basi awalishe wale wenye njaa humu duniani.

Katika mlango wa tatu wa Jahannam kumeandikwa : Allah swt huwalaani wale wasemao uongo, Allah swt huwalaani wale walio mabakhili, Allah swt huwalaani wale wanaowanyanyasa na kuwakandamiza wanyonge.

Katika mlango wa nne wa Jahannam kumeandikwa sentenso tatu: Allah swt humdhalilisha yule ambaye anaidharau Dini ya Islam, Allah swt humdhalilisha yule anayewakashifu Ahlul Bayt a.s. ya wananyumba ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.; Allah swt humdhalilisha yule ambaye anawasaidia wadhalimu katika kuwadhulumu watu.

Katika mlango wa tano wa Jahannam kumeandikwa sentenso: Msiendekeze matamanio yenu, kwani matamanio yanapingana na tendo la kusadikisha; Musiyaongelee zaidi yale yasiyowahusu kwani mtaondoka katika Baraka za Allah swt; na kamwe msiwe wasaidizi wa madhalimu.

Katika mlango wa sita wa Jahannam kumeandikwa sentenso: Mimi nimeharamishiwa kukubalia Mujtahid (hawa ni wale ambao wamefikia upeo wa Ijtihad, uwezo wa kutoa fatwa. Rejea vitabu vya Fiqh ndipo utakapoweza kupata ilimu zaidi katika somo hili). Mimi nimeharamishiwa kukubalia wale wanaofunga saumu.

Katika mlango wa saba wa Jahannam kumeandikwa sentenso tatu: Ujihisabie mwenyewe matendo yako kabla hujafanyiwa hisabu ya matendo yako; ikaripie nafsi yako kabla wewe hujakaripiwa; na mwabudu, Allah swt aliye Mkuu na aliyetukuka, kabla ya wewe hujafika mbele yake na ambapo hautaweza tena kumwabudu na kumtukuza.

Kwa kuwa marejeo kuhusu Jahannam yapo yanapatikana kwa wingi kutoka Qur’ani Tukufu, sisi sasa tutajaribu kurejea mapokezi na maelezo kuhusu Jahannam kutokea Ahadith za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na Ma-Imamu a.s. kuhusu adhabu, vitisho vya Jahannam , mahala palipojaa joto la hali ya juu yenye kuumiza, mahala ambapo moto wake unawekewa vipande vya kiberiti au mrututu ambayo kila moja ni kubwa kama milima mikubwa kabisa ulimwenguni. Zipo sehemu kubwa kabisa kama hizo ambapo wale waliokwisha adhibiwa hupelekwa kupoozwa na kugandishwa kama barafu. Kwa maneno mengine, wanatolewa kutoka hali moja ya moto mkali kabisa na kupelekwa katika hali nyingine ya baridi kabisa. Katika sayari yetu kuna milima yenye theluji na milima yenye kutoa volkeno ambayo hutoa miyeyuko ya mawe kama lava; na hivyo ndivyo ilivyo hali ya Jahannam : kuna hali zote mbili za joto kali na baridi kali.

Katika uk.309 ya kitabu cha al-Selek, The Divine Traditions, mkusanyiko wa Ahadith al-Qudsi, Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amenakiliwa akisema kuwa siku moja Jahannam ilimlalamikia Allah swt kwa kusema, : “Ewe Mola! Hata sehemu zangu zinateketezana!” na kwa hayo Allah swt aliiruhusu kupumua mara mbili, mara moja katika majira ya baridi na mara nyingine katika majira ya joto kali. Kwa sababu ya kupumua kwake huku ndiko kumetokezea misimu hii miwili yenye joto kali na baridi kali. Iwapo Allah swt angalikuwa ameruhusu zaidi ya mara mbili basi kusingalikuwapo na maisha ulimwenguni humu.

Chakula cha watu wa Jahannam na Jannat

Wakati wakazi wa Jannat watakuwa wakila kila aina ya matunda mazuri na yenye ladha tamu, wakazi wa Jahannam watakuwa wakila chakula kama miiba ambayo itakuwa ikiwasakhama katika koo zao, kamwe haitawafikia tumboni mwao, na wala hawataweza kutapika. Na hii ndiyo chakula mojawapo ya watu wa Jahannam . Aina nyingine ya chakula kinachotayarishwa kwa ajili ya wakazi wa Jahannam ni usaha wa majeraha ya wale wanaopata mateso katika Jahannam , na kuchemshwa katika joto la kupasua matumbo yao.

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amenakiliwa katika uk.145, J.1 ya al-Zamakhshari’s Rabee’ al-Abrar akiwa amemwuliza Malaika Jibraili a.s., “Je ni kwa nini mimi kamwe sijamwona Malaika Mikaili a.s. akicheka au kutabasamu?” Malaika Jibraili a.s. alimjibu: “Mikaili kamwe hakucheka wala kutabasamu kuanzia pale Jahannam ilipoumbwa. ” Anas, Allah swt airehemu roho yake, amenakiliwa na al-Zamakhshari akisema kuwa mfano wa kiwango kidogo kabisa cha adhabu ya Jahannam ni kama kwamba mtu anatengenezewa pea ya viatu ambavyo anapovaa bongo inachemka na kutokota. Habari zaidi kuhusu sehemu hii ya kutisha zinapatikana katika al-Zamakhshari, ambazo ni kama zifuatazo :

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema, “Katika safari yangu ya usiku wa (‘Israa), mimi nilisikia sauti kubwa mno, hivyo nilimwuliza Malaika Jibrail a.s., ‘Je sauti hii kubwa ni ya nini, Ewe Jibraili ?’ Naye alinijibu, ‘Ni jiwe lililotupwa kutokea juu kuangukia ndani mwa Jahannam , na imekuwa ikianguka kwa muda wa vipindi sabini vya baridi, na sasa ndipo ilipofika chini.”

Abu ‘Asim ‘Ubayd ibn ‘Umayr ibn Qatadah al-Laythi, Hakimu wa Makkah (d. 68 A.H.), amesema, “Jahannam hupumua mara moja kwa sababu yake Malaika na Mitume a.s. yote hutetemeka, kiasi kwamba hata Mtume Ibrahim a.s. hupiga magoti na kusema, “Ewe Mola wangu ! Nakuomba uniokoe!”

Abu Sa’eed al-Khudri amenakiliwa akisema, “iwapo milima itapigwa kwa rungu mara moja inayotumiwa na Malaika wa Jahannam , basi itavunjika vipande vipande na kuwa vumbi.”

Tawoos ibn Keesan al-Khawlani amenakiliwa akisema, “Wakati Jahannam ilipoumbwa, Malaika walishtushwa mno, na wakati nyie wanaadamu mulipoumbwa, basi walitulia.”

Al-Hasan ibn Yasar al-Basir amesema, “Kwa kiapo cha Allah swt! Hakuna hata mja mmoja wa Allah swt anayeweza kustahimili joto la Jahannam! Tumeambiwa iwapo mtu atasimama Mashariki na Jahannam ikawa upande wa magharibi na ikafunuliwa kidogo tu, basi bongo ya mtu huyo aliye Mashariki itachemka. Iwapo kama kiasi cha ndoo moja ya usaha wa Jahannam ukimwagwa juu ya ardhi hii ya dunia, basi hakuna hata kiumbe kimoja kingalibakia hai.”

Hisham ibn al-Hassan al-Dastoo’i alikuwa hazimi taa wakati wa usiku, na wakati wananyumba yake walipompinga kwa kumwambia, “Sisi hatuwezi kutofautisha baina ya usiku na mchana!” Yeye aliwajibu, “Kwa kiapo cha Allah swt! Mimi ninapozima taa wakati wa usiku, hukumbuka kiza kikali cha kaburini, na hivyo sipati usingizi.”

Adhabu katika Jahannam itakuwa kwa mujibu wa aina za madhambi zilizofanywa wakati wa maisha ya mtu humu duniani. Kwa mfano, Wale ambao walilimbikiza mapesa humu duniani bila ya kutoa Zaka na kodi zinginezo za kidini, basi hao watachomwa kwenye paji la uso kwa yale waliyoyalimbikiza, pembeni mwao, na migongoni mwao. Kwa maneno mengine, sehemu zote za mwili wao.

Abu Dhar al-Ghaffari, Allah swt amwie radhi, alikuwa akisema, “Waambieni wale ambao hupenda kulimbikiza utajiri wao kuwa watachomwa nayo juu ya paji la uso wao, pembeni mwao, na migongoni mwao hadi watakapokuwa wamejaa kwa mioto.”

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema, kama vile tuambiwavyo katika uk.243, J.8, ya Bihar al-Anwar, “Hakuna Mja wa Allah swtmwenye utajiri au mali na hataki kulipa Zaka isipokuwa kwamba atachomwa kwa vipande hivyo vya mapesa vitakavyokuwa vimepashwa moto katika moto wa Jahannam na kwamba watatumbukizwa katika adhabu hizo kuanzia juu ya vipaji vyao vya nyuso zao na migongo yao hadi pale Allah swt atakapokuwa amemaliza kupokea mahisabu na adhabu za waja wake Siku ya Qiyamah, muda ambao ni wa maelfu ya miaka kwa mujibu wa mahisabu yetu. Hapo ndipo watatumwa ama kuingia Jannat au Jahannam.”

Abu Umamah anamnakili Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. akielezea aina na vinywaji watakaopewa wakazi wa Jahannam. Anasema, “Italetwa mbele yake, naye atachukizwa nayo; na itakapoletwa karibu yake, itauchoma uso wake na kifuvu kitadondoka. Iwapo ataweza kunywa hata kidogo kutoka humo, basi matumbo yake yatakatika vipande vipande na kutokezea sehemu za nyuma ya kutokezea choo.”

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. ameripotiwa akisema, “Sala za mtu anayekunywa pombe hazikubaliwi kwa siku arobaini; na iwapo atakufa huku pombe ikawamo tumboni mwake, basi Allah swt atamlazimisha anywe sadiid, maji yatokayo kwenye sehemu za uchi wa malaya ambayo yatakusanywa katika birika huko Jahannam na kupewa watu hawa, na kwayo matumbo na ngozi zao zitachomwa.”

Riwaya hii imeelezwa na Shu’ayb ibn Waqid ambaye anamnakili al-Husain ibn Zayd ambaye anamnakili Imam Ja’fer al-Sadiq a.s. kama ilivyoelezwa katika uk. 244, J. 8, ya Bihar al-Anwar, “Wale wenye madhambi mbali na zinaa au mauaji, watapewa vinywaji vya risasi na shaba iliyoyeyushwa”, kama vile Ibn Mas’ud anavyonakiliwa katika Bihar al-Anwar akisema.

Mujahid anasema kuwa hayo yatakuwa ni usaha na damu za wale walioadhibiwa, ambapo Ibn Jubayr anasema ni ‘maji meusi; kwani Jahannam ni nyeusi, miti yake ni meusi, na nyuso na miili ya wakazi wake pia inakuwa imegeuka kuwa nyeusi.

Hoja hii inachukuliwa na al-Dhahhak. Adhabu za ziada zitakazokuwa zikitolewa Jahannam zitakuwa za nyoka na ng’e ambao makucha yao yatakuwa, kwa mujibu wa Ibn ‘Abbas na wengineo wanaripoti hivyo, makubwa na marefu kama minazi. Nyoka watakuwa wanene kama tembo, na ng’e watakuwa wakubwa kama punda weusi. Na mara kwa mara wakazi wa Jahannam watakuwa wakipigwa vipigo kwa makonde yao kama marungu: Iwapo wao watakuwa katika tabaka za juu za Jahannam, basi vipigo hivyo vitawaangusha katika tabaka zinginezo, na kila tabaka litakuwa na joto na mateso makali kuliko tabaka lililotangulia, kwa muda wa miaka sabini. Mara watakapofikia tabaka la chini, miale mikali ya moto itawatupa tena, na vivyo hivyo itakavyokuwa itaendelea. Hakutakuwa na muda wa kuomba msamaha kwa ajili yao.

Je ni mahala gani palipo pabaya zaidi katika Jahannam?

Ibn Mas’ud na Ibn ‘Abbas wamenakiliwa katika uk.241 – 242, J.8, ya al-Majlisi Bihar al-Anwar anasema kuwa wanafiki watawekwa katika tabaka la chini kabisa la Jahannam ambapo kuna adhabu kali kuliko zote. Watafungwa katika vyumba kama majiko yaliyojaa mioto mikali.

Kwa sasa turejee Nahjul Balagha na tuangalie vile Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. anavyotupatia picha ya Jahannam, tumwombe Allah swt asitutumbukize humo :

‘Janga kubwa kwa mtu ni kule kutumbukia katika Jahannam; yeye atajihisi kuwa anachemshwa mzimamzima, na ataona mateso yake yasiyo na mwisho, na kiumbe fulani kinakoroma na kupumua, viumbe vyote vilivyo humo hukosa raha na kamwe hawapati fursa ya kupumzika, na kamwe hawatapata kupumzika kutokana na adhabu zake au mauti ya uhakika. Yeye hasinzii hata kidogo wala hakutakuwa na mapumziko katiko mateso yake: Kutakuwa na maumivu yakudumu kiasi ambacho tunamwomba Allah swt atunusuru na kutusaidia.’ (Hotuba 83).

‘Kwa hakika ni mahala pabaya kabisa kuliko sehemu yoyote ile, mahala ambapo mikono ya wakazi wake yanakuwa yamefungwa shingoni mwao, na vichwa vyao vimefungwa na miguu yao kwa minyororo na mavazi yao yametengenezwa kwa lami. Mashati yao yametengenezwa kwa moto wakati ambapo adhabu zao za moto usiozimika kamwe hazitakwisha kamwe mahala ambapo mlango wake utakuwa umejazwa watu, katika moto mkali kabisa kiasi kwamba sauti zao zinasikitisha na kutisha, na miale ya moto ikipaa na kufikia kila sehemu na wala hakuna kujitoa kutoka humo na wala hakuna muda utakaokwisha, na wala haina mwisho wake kwa wale wanaoteketezwa na kuchomwa humo.’ (Hotuba 109).

‘Joto lake ni kali mno, kufikia chini kwake ni mbali mno, sakafu yake ni chuma, vinywaji vyake ni usaha.’ (Hotuba 120)

‘Siku ya Qiyamah, madhalimu wote wataletwa bila ya kuwapo na mtu yoyote wa kuwasaidia au kuwatetea, na hivyo watatumbukizwa katika moto wa Jahannam na humo atasagwasagwa kama vile machine za kusaga zifanyavyo, hadi hapo atakapojigonga kichwa katika sakafu ya chini kabisa.’ (Hotuba 164)

‘Iwapo Malik (msimamizi wa Jahannam) atakuwa mkali, husababisha sehemu yake moja kuminyana na sehemu zingine, anapogombeza, milango yake huruka juu na chini (hutema kama volkano). (Hotuba 183)

Mazungumzo juu ya Jahannam yanatudhihirishia wazi kuwa umbali, mahala na nafasi ni vitu vya uhakika katika maisha yajayo kama vile yalivyo katika maisha yetu haya. Ushahidi wa kusema kuwa Jahannam itasogezwa au kupelekwa sehemu moja kutokea sehemu nyingine, unapatikana katika Ayah ya 23 ya Surah al-Fajr (Surah namba 89 ) na katika Ayah zinginezo pia :

Basi Siku hiyo italetwa Jahannam. Siku hiyo mwanadamu atakumbuka, lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?

Kwa hakika wale watakaokuwa wakiihamisha Jahannam kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kwa Amri ya Allah swt, hawatakuwa wengine isipokuwa ni Malaika ambao sisi hatuwaoni duniani humu lakini punde tutakapo kufa, tutaanza kuwaona, naomba mazungumzo haya juu ya Malaika tuyaachilie hapa kwani yatahitaji kutungiwa kitabu kingine, na kwa sasa hivi somo hili litatuchukua mbali, Insha-Allah, tutaweza kuwatungieni kitabu kingine juu ya Malaika.

Lazima ikumbukwe kuwa picha yote iliyotolewa kuhusu Jahannam hatujaelezea kuhusu mateso na adhabu yanayotokana kuwa pamoja na Mashetani, Pepo mbaya na Majini waliolaaniwa ambao wote hao watakuwa pamoja na wanaadamu waliolaaniwa. Tukiangalia mateso wanayopewa viumbe hivi, makelele yao, sehemu zao zikivutwa na kunyofolewa, na wakichunwa ngozi kutoka miili yao … yanatisha mno kama Jahannam yenyewe. Kumbuka vile Allah swt alivyomwelezea mwanadamu kuwa ameumbwa kwa ubora wote. Wanaadamu watakaotumbukizwa katika Jahannam wataelewa vyema zaidi kuliko wengine, wakati ambapo wale watakaokuwa wameongoka watakuwa wamepona uhakika wa kuteswa.

Wale ambao wamesoma masimulizi ya Saint Joan of Arc (1412 – 1431), Mfaransa mashuhuri, mbali na umri wake wa kati, aliwaongoza Wafaransa katika ushindi dhidi ya majeshi ya Waingereza huko Orleans, kumbuka kuwa yeye alikuwa ni Pepo mbaya, na anapendelea kutembea juu ya miti iwakayo moto kutokea ncha moja ya dunia hadi nyingine kuliko kuangalia tu. Sasa hebu fikiria kuwa nao hawa Pepo mbaya za milele. (Yeye haoni ajabu kutembea juu ya moto, je na wewe unao msimamo kama huo…?)

Kwa kifupi hivyo ndivyo ilivyo Jahannam na adhabu na mateso yake. Kama tungaliweza kuangalia hata mara moja au kuwaangalia wakazi wake, basi kwa hakika tusingalijali kufunga saumu kila siku ya maisha yetu, na wala si katika mwezi wa Ramadhani tu, Mwezi wa Allah swt, mwezi wa msamaha na baraka, lakini maisha yetu yote.

Sababu zimfanyazo mtu kuingia Jahannam

1. Kufr na Nifaq

Hoja hii ipo ya kwanza katika mfululizo wa sababu za kumfanya mtu aingie Jahannam na sababu zote zifuatazo ndizo matawi ya Kufr na Nifaq na Allah swt amewafanyia makhususi Jahannam watu wenye sifa hizi mbili. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Nisaa, 4, Ayah 140 :

Naye amekwisha kuteremshieni katika Kitabu hiki ya kwamba mnapo sikia Aya za Allah swt zinakanushwa na zinafanyiwa kejeli, basi msikae pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo mtakuwa nanyi mfano wao hao. Hakika Allah swt atawakusanya wanafiki na makafiri wote pamoja katika Jahannam.

Vile vile Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Nisaa, 4 , Ayah 145 :

Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka ya chini kabisa Jahannam , wala hutompata yeyote wa kuwanusuru.

2. Kuwazuia wale wanaotenda kazi katika njia ya Allah swt

Kuna watu wengi ambao wanatabia ya kuzua uzushi na kuwazuia kwa njia mbali mbali wale wanaofanya tabia na kutenda matendo mema kwa mujibu wa Sunnah na tabia ya Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na Ahlul Bayt a.s. kwa hivyo watu kama hawa ndio waliowekwa katika sababu ya kwanza ya kuingizwa Jahannam. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Nisaa, 4 , Ayah 55 :

Basi wapo miongoni mwao walioamini, na wapo walioyakataa. Na Jahannam yatosha kuwa ni moto wa kuwateketeza.

3. Kutomtii Allah swt

Leo kila mzazi anataka watoto wake wamfuate na kumtii vile atakavyo yeye mwenyewe akiwa kama mzazi na vile vile kila atengenezacho mtu hutegemea kuwa kitu hicho kitamfaa na kumfanyia kazi kwa makusudio ya kukitengeneza na ndivyo vivyo hivyo Allah swt ametuumba sisi pamoja na viumbe vingine vyenye uhai na visivyo na uhai kwa sababu na makusudio maalumu, nayo ni utiifu kwa Amri Zake na kumfuata Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. pamoja na Ahlul Bayt a.s.

Hivyo kwa kutomtii Allah swt na Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. pamoja na Ahlul Bayt a.s. ni dhambi kuu na ndicho kitakachotutumbukiza Jahannam moja kwa moja. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Jinn, 72 , Ayah 23 :

….. Na wenye kumuasi Allah swt na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannam wadumu humo milele.

Vile vile twaambiwa na Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Nisaa, 4 , Ayah 115 :

Na anayempinga Mtume baada ya kudhihirikia uwongofu, na akafuata njia isiyokuwa ya Waumini, tutamuelekeza aliko elekea, na tutamwingiza katika Jahannam. Na hayo ni marejeo maovu.

4. Kudhihaki Ayah za Allah swt

Kuna baadhi yetu tunayo tabia ya kuzifanyia dhihaka Ayah, amri na hukumu za Allah swt ambavyo ni tabia ovu kabisa na hatimaye humtumbukiza Jahannam bila ya yeye kutambua athari mbaya ya tabia yake hiyo. Upeo wetu wa ilimu na maarifa ni mdogo sana kiasi cha kutufanya sisi tukajivunia na kufanya ufakhari mbele ya Allah swt na tukajifanya hodari mbele ya maamrisho yake. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Kahaf, 18, Ayah 106 :

Hiyo Jahannam ni malipo yao kwa walivyokufuru na wakafanyia kejeli Ishara zangu na Mitume wangu.

5. Kutotumia viungo vya mwili dhidi ya Allah swt

Tunaonywa kuwa tusivitumie viungo vyetu vya mwili kama macho, mdomo, masikio, miguu na mikono, n.k. dhidi ya Allah swt katika kutenda maasi na madhambi. Tunaelewa vyema kabisa kuwa Siku ya Qiyamah viungo vyote hivi vitatoa ushahadi wa kipekee kwa kila kilichotenda humu duniani na Allah swt amesema wazi wazi katika Sura al-Ya-Sin kuwa Siku hiyo ya Qiyamah hakuna nafsi yoyote ile itakayolipwa mema au kuadhibiwa isipokuwa kwa yale waliyoyatenda tu.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-‘A’raf, 7, Ayah 179 :

Na tumeiumbia Jahannam majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika.

6. Kumtii na kumfuata Shaitani

Humu duniani watu wengi mno tumekuwa wafuasi na mashabeki wakubwa wa Shaitani kiasi kwamba hata Allah swt tumemsahau kama yupo na anayajua yale yote tuyafanyayo. Sisi tunayakimbilia kila yaliyo maovu bila hata ya kuyafikiria matokeo yao kama yatatunufaisha au kutudhuru. Na kwa hakika mambo mengi mno tuyafanyayo sisi kimatokeo ni kutudhuru tu.

Kila aina za tabia mbaya sisi tunaongoza kama kunywa pombe, bangi, madawa ya kulevya, zinaa na uasherati wa kila aina, wizi, uongo, kudhulumiana na kufanyiana khiana, n.k. na hata wengi wetu kuthubutu kusema kuwa sala, saumu havina umuhimu wowote katika Islam na maisha ya mwanadamu. Kwa hakika tunakuwa tumejawa na kasumba za Kishetani ambazo zinatuangamiza moja kwa moja. Allah swt anasema katika Ayat ul-Kursi kuwa wale wanaokufuru na wanaomfanya Shaitani kuwa kiongozi wao, basi Allah swt huwatoa katika Nuru na kuwatumbukiza katika Kiza.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-‘A’raf, 7, Ayah 18 :

Akasema : Toka humo, nawe umekwisha fedheheka, umekwisha fukuzwa. Hapana shaka atakaye kufuata miongoni mwao, basi nitaijaza Jahannam kwa nyinyi nyote.

7. Majivuno

Kwa hakika hii ni tabia mbaya kabisa katika maisha ya mwanadamu kwani anajiona yeye yu bora na afadhali kuliko watu wengine wote ama kwa kujivunia ilimu aliyoipata, uzuri, watoto, mali, siha, n.k. lakini yote hayo si ya kujivunia kwani vyote ni vitu vyenye kuangamia na kuisha pasi na sekunde hata moja. Mfano mtu kama huyo anaweza akaugua ugonjwa kwa muda mfupi atawehuka au akapoteza fahamu zake, hivyo akasahau yote aliyokuwa akiyajua. Vile vile mtu anayejivunia afya na mwili wake anaweza kupatwa na ugonjwa wa moyo, na akapooza mwili kiasi kwamba hata chakula analishwa akiwa amelala na anajisadia choo kidogo na kikubwa akiwa kitandani, hoi hawezi hata kujipangusa mwenyewe. Je majivuno yamekwenda wapi ? Na huu ni uatamaduni wa Shaitani ambao kwetu sisi ndio tunaouona kama ndio desturi nzuri. Mtu masikini akiketi karibu nawe, je utakuwa masikini au utajiri wako utamwendea huyo masikini ?

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura az-Zumar, 39, Ayah 32 :

Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule aliyemsingizia uwongo Allah swt na kuikanusha kweli imfikiapo ? Je! Siyo katika Jahannam makazi ya hao makafiri?

Na vile vile Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-A’raf, 7, Ayah 36 :

Na wale watakaokanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hao ni watu wa Motoni; humo watadumu.

8. Kuwaomba msaada Wadhalimu

Kwa kutaka misaada kutoka wadhalimu kunatupeleka katika Jahannam bila kipingamizi kwani tunaelewa wazi kabisa kuwa mdhalimu (jina linajitosheleza kwa kujieleza ) ni mtu ambaye anamdhulumu mtu au watu, hivyo hakuna kheri kwao kwani watataka kila mtu adhulumiwe tu kwa njia moja au nyingine. Na kwa kumwomba yeye msaada atajenga chuki na uhasama baina ya watu ili yeye aweze kunufaika. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Hud, 11, Ayah 113 :

Wala msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi badala ya Allah swt , wala tena hamtasaidiwa.

Vile vile Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Maidah, 5, Ayah 2 :

…. Na saidianeni katika wema na uchamungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui….

9. Kuisahau Akhera

Kwa hakika sisi binadamu tunajitumbukiza katika maasi na madhambi basi tunasahau kuwa Allah swt yupo anatuangalia na kuyajua matendo yetu yote. Na katika hali hii sisi huwa tunasahau kuwa baada ya maisha ya humu duniani na kufa kwetu, kuna Aakhera. Na kuisahau huku ndiko kunakotutumbukiza Jahannam.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Jathiyah, 45, Ayah 24 :

Na walisema:Hapana ila huu uhai wetu wa duniani – twafa na twaishi, na hapana kinacho tuhiliki (tuangamiza) isipokuwa dahari (huu ulimwengu). Lakini wao hawana ilimu ya hayo, ila wao wanadhani tu.

10. Kuiabudu Dunia

Sisi tumepotea kiasi kwamba dunia hii tumeichukulia kama kwamba ndipo tutakapoishi milele wakati tunawaona watu wanakufa usiku na mchana, wote hawa wanaiacha dunia kwa mikono mitupu. Wapo humo wanao bahatika sanda au kuzikwa na wengine humo wapo ambao hata sanda hawabahatiki na badala ya kuzikwa wanaliwa na wanyama na kuoza kama vile kufa maji, kuchomwa moto n.k.

Lakini haya yote tunayaona kama mzaha bila kuyatilia maanani kuwa nasi pia tuko njiani kwenda huko na tutayaacha yote humu humu duniani isipokuwa matendo yetu mema ndiyo yatakayotufaa katika safari yetu ya Aakhera. Al-Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. anasema Safari ndefu lakini matayarisho ya safari ni madogo. Tukiwa watumwa wa dunia basi tutatumbukia Jahannam .

Hapa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema katika Mizanul Hikmah kuwa “Mapenzi ya dunia ndiyo chanzo chote cha kila aina ya madhambi.” Na vile vile Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al - ‘Asra’, 17, Ayah 18 :

Anayetaka yapitayo upesi upesi, tutafanya haraka kumletea hapa hapa tunayoyataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannam ; ataingia humo hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa na kufurushwa.

11. Kulimbikiza utajiri wa mali na mapesa

Sisi wanaadamu tunayo tabia ya kulimbikiza utajiri yaani kulimbikiza mali na mapesa bila ya kujali haki zilizowekwa na Dini yetu Tukufu kama vile kutoa Zaka, Khums, Sadaqa, kuwasaidia jamaa na mayatima, wajane na wale wenye shida n.k. Kwa hakika Qur’ani Tukufu inatuambia waziwazi kuwa sisi tunapenda kujiongezea tu hadi hapo tutakapofika makaburini, kamwe hatukinai wala kutosheka, na tufikapo makaburini ndipo tutakapo amka na kuzindukana na usingizi wetu huo wa upotofu.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Tawbah, 9, Ayah 34 – 35 :

Enyi mlioamini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki wanakula mali za watu kwa batili na wanazuilia Njia za Allah swt. Na wanaokusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Allah swt. Wabashirie khabari ya adhabu iliyochungu.

Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahannam , na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, “Haya ndiyo (yale mali) mliojilimbikia nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya ) yale mliyokuwa mkikusanya.”

(Imeelezwa katika riwaya kuwa neno lililotumika katika Ayah hii ‘kanz’ inamaanisha mali yoyote ile ambamo zaka haijatolewa).

12. Kuikimbia Jihadi

Hapa neno hili la Jihadi linamaana mbili : moja ya kupigana vita pamoja na nafsi yake mtu mwenyewe na pili kupigana vita kwa mikono yake dhidi ya makafiri na maadui wa Islam.

Katika uwanja wa vita badala ya kuwasaidia Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na Maimamu a.s. mtu anaweza kuacha wao vitani na yeye akatoroka. Basi mtu kama huyu ataingizwa Jahannam na Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Anfal, 8, Ayah 15 – 16 :

Enyi Mlioamini! Mkikutana na waliokufuru vitani msiwageuzie mgongo.

Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo – isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi – basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Allah swt . Na pahala pake ni Jahannam, na huo ni mwisho muovu.

13. Kumwaga damu ya mtu asiye na hatia

Kwa kumwaga damu ya mtu asiye na hatia kutatufikisha katika Jahannam kwani hii itakuwa ni dhuluma na ndiyo maana kuna mahakama na vyombo vya sheria vya kufuatilia masuala ya watu anapokumbwa na matatizo na watu wengine. Haifai kwa mtu kujichukulia sheria mikononi kwani inawezekana mtu mmoja akamwua mtu mwingine kwa kudhania tu pasi na ushahidi wa kutosha au bila kufikiria vyema kwani wakati huo mtu huyo anakuwa katika hasira na jazba. Katika Islam kuna uongozi sahihi umewekwa kwa ajili ya kufuatilia kila jambo na suala.

Kwa kufuatilia maswala kwa uchunguzi na kufikia jibu au muafaka kuna dumisha upendo na amani katika jamii zetu na kwa hakika haya ndiyo yanayomfurahisha Allah swt na ndipo hapo tunapojaaliwa baraka na rehema na neema Zake. Allah swt hataki mwenye nguvu na uwezo kuwadhulumu wanyonge na dhaifu. Haki ifuatwe ipasavyo.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Maida, 5, Ayah 32 :

Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika wakiwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.

Vile vile Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Nisaa,4, Ayah 93 :

Na mwenye kumuuwa Mumiini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam humo atadumu, na Allah swt amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa.

Kwa hakika kwa mtu anayemwaga damu ya mtu asiye na hatia, huadhibiwa adhabu nne na huko Jahannam atawekwa peke yake, daima ghadhabu za Allah swt zitakuwa juu yake, laana za Allah swt zitakuwa juu yake na adhabu kubwa kabisa itamwangukia. Habari hizi pia ziko katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Ali Imran, 3, Ayah 21 :

Hakika wanaozikataa Ishara za Allah swt , na wakawauwa Manabii pasipo haki, na wakawauwa watu waamrishao Haki wabashirie adhabu kali.

14. Kupuuzia na kutokusali Sala

Watu wa Jannat watawauliza watu wa Jahannam kile kilichowaingiza Jahannam. Nao watawajibu kuwa wao hawakuwa miongoni mwa waliokuwa wakisali. Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Muddathir, 74, Ayah 39 – 46 :

Isipokuwa watu wa kuliani.

Hao watakuwa katika mabustani, wawe wanaulizana

Khabari za wakosefu:

Ni nini kilichokupelekeni Motoni (Saqar) ?

Waseme : Hatukuwa miongoni mwa waliokuwa wakisali.

Wala hatukuwa tukiwalisha masikini.

Na tulikuwa tukizama pamoja na waliozama katika maovu.

Na tulikuwa tukiikanusha Siku ya malipo.

15. Kutokutoa Zaka

15. Kutokutoa Zaka1

Katika maisha yetu Dini yetu imetuwekea masharti ya kutozwa kodi mbalimbali ambazo zimeelezwa vyema na kwa uwazi katika vitabu vya fiq-hi kwa ajili ya kutakasisha mali zetu.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Fussilat, 41, Ayah 7:

Ambao hawatoi Zaka na wanaikataa Akhera.

16. Kudhulumu haki za yatima

Duniani humu hakuna mtu ambaye anaomba watoto wake wawe mayatima na kutaabika kwa mateso yaliyopo humu duniani. Lakini kunapotokea hali ya watu wengine kuwadhulumu mayatima, basi hao hujishughulisha kwa kila hila na mbinu katika kufanikisha azma yao hiyo ya kuwadhulumu mayatima. Badala ya kuwa waangalizi wa mayatima, wao ndio wanawadhulumu na kuwafanyia maisha yao yakawa magumu kwani watoto hao watashindwa kusoma mashuleni, hawataweza kuvaa mavazi mazuri, hawataweza kuishi maisha mazuri na vile vile hawataweza kupatiwa matibabu mazuri kwa ajili ya hayo. Sasa jee! haya ndiyo yanayomfurahisha Allah swt au tunamghadhabisha na hatimaye atuadhibu ? Halafu tutasema kuwa Allah swt anatuonea.

Kwa kifupi sisi tunatakiwa tuwe walezi wa mayatima. Ipo Hadith tukufu kuwa Yatima anapotoa pumzi moja ya kusikitika, basi; Arshi-ilahi inatetemeka na Malaika huangua kilio.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Nisaa, 4, Ayah 10 :

Hakika wanaokula mali ya mayatima kwa dhuluma, hapana shaka yoyote wanakula moto matumboni mwao, na wataingia Motoni.

17. Kutoza na kupokea riba

Allah swt ameharamisha kutoza na kupokea riba kwa sababu riba inawadumaza watu kiuchumi na hatimaye hata kufilisika. Tunasikia kila mahala kunakuwapo na kilio kikubwa cha watu hata mashirika na hata nchi mbalimbali ikiwemo yetu, wote wakilia kilio cha kunyonywa kwa kutozwa riba ambayo inawawia ngumu kuilipa na hatimaye kutumbukia katika madeni makubwa makubwa ambayo kuyalipa tena ni vigumu mno.

Watu wengi wamewahi kuchukua riba lakini wameshindwa kurejesha.

Unachukua mfuko mtupu na kuurudisha ukiwa mnono au unamchukua ng’ombe aliyekonda na kumrudisha akiwa amenona sana!

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al- Baqarah, 2, Ayah 275 :

Wale walao riba riba hawasimami ila kama anavyosimama aliyezugwa na Shaitani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Allah swt ameihalalisha biashara na ameiharamisha riba. Basi aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi,, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyokwisha pita, na mambo yake yako kwa Allah swt. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu.

Allah swt huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka…

18. Kutokushukuru neema za Allah swt

Sisi wanaadamu tunayo tabia na desturi ya kutoa shukurani kwa jema lolote tunalofanyiwa na watu wenzetu. Lakini ni ujeuri wetu sisi kwamba hatutoi shukurani ipasavyo kwa Allah swt amabye ametujaalia kila aina ya neema kama macho, miguu, mikono,siha, mali, watoto, n.k. kwa hakika hatuwezi kuzihesabu neema za Allah swt (rejea Sura ar-Rahmaan ) hata tukizikalia pamoja na makompyuta zetu.

Allah swt pia anatarajia kuwa mja wake atakuwa ni mtu mwenye kumshukuru na kumnyenyekea kwa neema zote anazomjaalia, lakini sisi badala ya kufanya hivyo, ndivyo tunavyozidi kuleta ufisadi na uchafuzi humu duniani kwa neema hizo hizo anazotujaalia Allah swt kwa ajili ya mambo mema. Tunafanya kiburi na majivuno mbele ya Allah swt lakini tunasahau kuwa hatumpunguzii chochote Allah swt na badala yake iwapo tutamshukuru basi Allah swt atatuzidishia katika maslahi yetu.

Hebu zingatia kuwa kuna masikini mwombaji mmoja akiwa mlangoni mwako, utampa chochote kile ili mradi umempa. Lakini kuna mwingine anakuja mlangoni mwako na kuanza kukusifu na kukutukuza na kukuombea dua nzuri nzuri, basi bila shaka huyu utampa mambo mazuri zaidi ya yule wa kwanza. Jaribu kusoma maana ya Ayah za Sura al-Fatiha (al-Hamdu ) utaona kuwa kuna anza kumsifu na kumtukuza Allah swt kwa mpangilio maalum na hapo katikati ndiko kuna anza sisi kujiombea maslahi yetu. Sasa katika hali kama hii Allah swt kamwe hawezi kutunyima kile tumwombacho.

Tujaribu kujifunza kutoka watoto wadogo hususan wanapo omba kitu utaona wanavyobembeleza.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Ibrahim, 14, Ayah 28 – 29 :

Hebu hukuwaona wale waliobadilisha neema ya Allah swt kwa kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo ?

Nayo ni Jahannam ! Wataingia. Maovu yaliyoje makazi hayo !

19. Kuibia katika mizani

Mwanadamu hujipatia malimbikizo ya mali kwa ilimu aliyonayo. Wengine wanapenda kufanya kwa uhalali wakati wengine wanafanya kwa kuibia katika mizani yaani wanapouza huuza kwa kupunguza, au huuza kitu kisicho sahihi au huiba katika vipimo vya uzito na urefu na upana, au huchanganya mali ili kufikisha ujazo kwa mfano kuongezea changarawe katika nafaka, maji katika maziwa, mafuta tofauti huongezwa katika mafuta ya aina nyingine au kumbandika mtu mali hafifu kwa kupokea malipo ya kifaa imara, n.k. Hivyo Qur’ani Tukufu inatukanya vikali mno pamoja na Ahadith za Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. na Ma-Imamu a.s.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Mutaffifiin, 83, Ayah 1 – 10 :

Ole wao hao wapunjao!

Ambao wanapojipimia kwa watu hudai watimiziwe.

Na wao wanapowapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza.

Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa

Katika Siku iliyo kuu,

Siku watapomsimamia watu Mola Mlezi wa walimwengu wote ?

Hasha! Hakika maandiko ya wakosefu bila ya shaka yamo katika Sijjin.

Unajua nini Sijjin ?

Kitabu kilichoandikwa.

20. Kuzitafuta aibu za mtu na kumsengenya

Watu wanapokuwa hawana kazi au shughuli za kufanya, basi utawaona wengine kazi zao ni kuzitafuta aibu za wengine na kuanzisha mgumzo ya kuwasengenya watu. Kwa hakika tutambue wazi kuwa anayemsema mwinge vibaya mbele yetu basi atatusema sisi vibaya mbele ya wengine, hivyo inabidi kujiepusha na watu kama hawa. Je, ni nani aliye humu duniani ambaye hana kasoro ? Basi huyo si mwanadamu bali ni Malaika ! Huyo anayezitafuta aibu za wengine, mwenyewe anazijua aibu zake, hivyo inambidi ajichungulie vyema undani mwake kabla ya kuwasema wengine. Vile vile tutambue wazi kuwa Allah swt hatatusamehe madhambi yetu ya kumsema mtu vibaya hadi hapo huyo mtu atusamehe yeye mwenyewe kwa furaha yake.2

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Humaza, 104, Ayah 1 - 5

Ole wake kila safihi, msengenyaji !

Aliyekusanya mali na kuyahisabu.

Anadhani kuwa mali yake yatambakisha milele !

Hasha! Atavurumishwa katika Hutama

Na nani atakujuvya ni nini Hutama ?

Moto wa Allah swt uliowashwa.

Ambao unapanda nyoyoni.

Hakika huo utafungiwa nao

Kwenye nguzo zilionyooshwa.

21. Ufujaji wa Neema za Allah swt

Kwa hakika mtu anapopata neema za Allah swt inambidi amshukuru kwa kila alichopewa lakini utaona watu kila wanapozidishiwa neema basi na ukafiri ndivyo unavyozidi kumwingia. Kwa kuwa sasa anao utajiri basi ataanza uasherati wa kila aina hata kuanzisha majumba ya kunywia pombe na kuchezea kamari na kuwaweka malaya ati ni kwa ajili ya starehe zake na marafiki zake. Kwa hakika hayo yote ni ufujaji wa Neema za Allah swt kwani utamwona mtu hatosheki kwa kidogo wala hakinai kwa kingi. Tusifuje neema za Allah swt na badala yake tuzitumie itupasavyo ili tuweze kujenga Aakhera yetu kwa Neema hiyo hiyo kama kutoa misaada kwa wenye kuhitaji, kuwasaidia mayatima na wajane na walemavu, kusaidia mahospitali, kuwachimbia watu visima kwa wenye shida ya maji, kuwalipia karo wale wanaohitaji ili waweze kusoma na kuilimika, n.k.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Mumin, 23,

Ayah 43:

Hapana umma uwezao kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.

Vile vile Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Asra’, 17, Ayah 27 :

Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashaitani. Na Shaitani ni mwenye kumkufuru Mola wake Mlezi.

22. Kosa na Dhambi

Sisi tunapo neemeka basi tunaona kuwa kuna vipingamizi vingi mno kupita kiasi katika maisha na starehe zetu, hivyo ndio mwanzo wetu wa kuanza kujifanyia vile tutakavyo, na kwa kufanya hivyo ndipo tunaanza kufanya makosa na madhambi moja baada ya nyingine. Tunafikia kiwango cha kusema kuwa bila madhambi maisha hayana raha. Allah swt atuepushe na hali kama hiyo, nyoyo zitakuwa zimekufa!

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu, Sura al-Zukhruf, 43,

Ayah 74 :

Kwa hakika wakosefu watakaa katika adhabu ya Jahannam

Hawatapumzishwa nayo na humo watakata tamaa.

23. Kuvuka mipaka iliyowekwa na Allah swt

Kila Mwislamu inambidi afuate na kutekeleza kila amri ya Allah swt bila ya kuvunja hiki wala kile na kutokufuata itakavyo nafsi yake. Allah swt ametuwekea mipaka ya kila jambo.

Allah swt anatuambia katika Qur’ani Tukufu , Sura al-Nisaa, 4, Ayah 14 :

Na anayemuasi Allah swt na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Allah swt) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha.

Madhambi Yamfanyayo Mtu Kuingia Jahannam

Makala haya yametarjumiwa na kushereheshwa na:

Amiraly M.H.Datoo P.O.Box 838 Bukoba – Tanzania (8/7/2000)

Hadithi hii ilisomwa na : Sheikh Akmal Hussein Taheri – Bukoba

Mwanadamu yupo daima anatenda madhambi kutokana na nafsi yake mwenyewe. Malaika walipomwabia Allah swt kuwa mjumbe wake huyu atakuwa mtenda madhambi; Naye Allah swt akawaambia kuwa yeye ayajua zaidi kuliko wao.

Mtu kuchuma mali na kurundika

Mtu yule ambaye atakusanya fedha na kuziweka mahala pamoja bila ya kufaidika yeye wala kuwasaidia wengineo ambapo wapo ndugu zake Waislamu wenye shida ambapo maisha yao yamewawia magumu. Mtume s.a.w.w. amesema kuwa “ufukara ni mbaya zaidi ya ukafiri”. Vile vile Imam Ali a.s. amesema Daima muchunge kuwa mwenye “shida masikini asikuijie bali ni wajibu wako wewe uwafikie”.

Wakati mwingine mwanadamu hufikia kukufuru ama kwa kukusudia au bila kukusudia. Siku moja mtu mmoja alikuwa akisafiri kwenda mji mwingine kwa ndege. Ndugu yake ambaye alikuwa akimsindikiza uwanjani hapo alimwuliza “Ewe ndugu yangu! Je, hautakuwa na shida ya fedha wakati ukiwa safarini ?” Ndugu yake ambaye alikuwa akisafiri alimjibu “Naam Ndugu yangu ! Mimi sitakuwa muhtaji wa Allah swt kwa muda wa juma moja hivi.” Ndege iliruka na katika muda wa nusu saa hivi kulipatikana habari kuwa ndege hiyo imeanguka na wasafiri wote wameuawa.

Hapa siwezi kusema kuwa watu wote hao wamekufa kwa sababu ya kuadhibiwa mtu mmoja aliyetoa maneno ya kashfa dhidi ya Allah swt. Na kwa maana hii ndipo tunapoambiwa kuwa sisi tusijihusishe na mahala ambapo panapotendeka maasi na madhambi kwa sababu inawezekana adhabu za Allah swt zikateremshwa hapo na wewe ukakumbwa pamoja humo.

Kisa cha Kijana mwenye Madhambi

Ma'adh anasema: "Siku moja nilikuwa nkijiandaa kwenda kwa Mtume s.a.w.w. na mara nikamwona kijana mmoja akilia mno, basi hapo nilimwuliza sababu ya kilio chake hicho. Huyo kijana alinijibu kuwa yeye ni mwenye dhambi kubwa mno. Basi hapo nilimwambia aje pamoja nami kwa Mtume s.a.w.w. ili amwombee msamaha kwa Allah swt. Hapo huyo kijana alisema kuwa alikuwa akiona aibu kuja mbele ya Mtume s.a.w.w. kwa sababu ya dhambi zake." Hapo Ma'adh aliendelea na safari yake hadi kwa Mtume s.a.w.w. na kumwelezea yale yaliyotokea. Basi Mtume s.a.w.w.alimwambia akamlete yule kijana.

Alipofika mbele ya Mtume s.a.w.w. aliulizwa, 'Je imekuwaje, walia kwa nini? Hapo huyo kijana akasema, "Ewe Mtume wa Allah swt! Dhambi langu ni kubwa mno!" Hapo Mtume s.a.w.w.aliendelea kumwuliza, "Je, kosa lako kubwa au mbingu?" Akajibu, 'Kosa langu!'

'Je kosa lako kubwa au dunia nzima? Akajibu, ‘kosa langu!’ Je, kosa lako kubwa au msamaha wake Allah swt? Hapo huyo kijana akasita na hatimaye kukubali kuwa 'Msamaha wa Allah swt ni mkubwa!’ Basi hapo Mtume s.a.w.w., alisema, ‘sasa niambie kosa lako’.

Huyo kijana akaanza kusema: "Ewe Mtume wa Allah swt! Palitokea kufariki kwa binti mmoja mzuri mno wa kabila la ansaar, na mimi nilikwenda usiku ule kulifukua kaburi ili kutaka kuiba sanda aliyokuwa amevishwa huyo maiti, shetani alinighalibu na kunifanya nikatenda tendo la kinyama kwa maiti huyo, binti aliyekuwa uchi mbele yangu.

Hapo ndipo maiti hiyo ilipotoa sauti ya masikitiko na kunilaani kwa kuniambia kuwa Allah swt ataniingiza motoni na kuniunguza humo kuteketea. Ewe mtume wa Allah swt, kwa hakika, baada ya matamshi hayo ya maiti huyo, mimi nimekosa furaha ya kila aina na nimeingiwa na woga na nadhani nitaweza kuangamia katika hali kama hii iwapo itaendelea kunisumbua. Hapo Mtume s.a.w.w. alimwambia huyo kijana: "Ondoka haraka mbele yangu kwani inawezekana moto wa Jahannam ukanikumba nami pia." Je, kwa nini Mtume s.a.w.w. alisema hivyo? kwa sababu dhambi lilikuwa kubwa mno!

Kwa mujibu wa riwaya, kijana huyo baada ya kuambiwa hivyo, aliondoka akiwa amesikitika mno na kuelekea katika milima ya mji wa Madina, huko alikaa kwa muda wa siku arobaini akiwa akilia na kuomba Toba kwa Allah swt. Baada ya siku arobaini kupita, alisema: "Ewe Allah swt! Iwapo umeshakwisha kuikubalia Toba yangu, basi naomba unijulishe kwa kumpitia Mtume wako. Na iwapo bado haujaikubali Toba yangu, basi naomba uniteremshie miale ya moto kutoka mbinguni ili inichome na kuniunguza ili niteketee kabisa!"

Basi hapo iliteremka Aya ya 135 ya sura Ali Imraan (3):

"Na wale ambao, wanapofanya tendo la kuaibisha au kudhulumu nafsi zao, wakamkumbuka Allah swtna kuomba msamaha wa madhambi yao, na ni nani awasamehee madhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu? Na ambao hawabakii (kwa kukusudia) katika yale waliyoyafanya maovu hali walikuwa wakiyajua hayo,"

  • 1. Nipo ninakitayarisha kitabu juu ya maudhui haya.
  • 2. Iwapo utapenda kusoma habari zaidi juu ya maudhui haya ya Tawbah, jipatie kitabu nilichokitafsiri cha Syed Dastaghib Sirazi
    kinachozungumzia kwa marefu na mapana kuhusu somo hili.