Table of Contents

Dibaji

Rehema na amani zimwendee Mtukufu wa Daraja Mtume Muhammad (s.a.w.w.), yeye na kizazi chake watoharifu maasumina (a.s.).

Bila shaka kipindi cha ujana ndio fursa muhimu inayompa mwanadamu uwezo wa kutimiza vipaji na uwezo binafsi, kama ambavyo vijana ni hazina kubwa yenye thamani ndani ya jamii mbalimbali za wanadamu. Kuanzia hapa ndipo maendeleo yote ya nchi yoyote ile yakategemea jinsi vipaji vya vijana vitakavyotunzwa, na jinsi watakavyoelimishwa na vipaji vyao kukuzwa. Kwa ajili hiyo daima wanaharakati, viongozi wa kidini na wa kisiasa wametilia sana umuhimu wa harakati za vijana ndani ya zama zote za historia ya mwanadamu.

Katika zama zetu hizi za maendelelo ya sayansi na teknolojia, upande mmoja tunakuta kitendo cha vijana kukusanya maalumati na maarifa mbalimbali kimesaidia sana katika kuleta maendeleo ya kielimu na kiteknolojia. Upande mwingine ni kuwa watu wa manufaa na wafanyabiashara wenye masilahi binafsi ya kisiasa na kiuchumi katika ulimwengu huu, wamejiandaa kutumia fursa hii kwa lengo la kutumia vibaya vipaji vya vijana kuliko zamani, hivyo ndio maana suala la vijana limekuwa na umuhimu sana leo kuliko hapo kabla.

Bila shaka kipindi hiki cha ujana ndio ardhi munasibu yenye rutuba safi na mbolea bora ya kuweza kuhifadhi mbegu bora na hatimaye kuotesha mazao endelevu kwa ajili ya leo na kesho, kwani ndio kipindi ambacho Mwenyezi Mungu amekipa sifa ya nguvu na uwezo wa kila kitu, kiasi kwamba ubora na ufanisi upatikanao ndani ya kipindi hiki hauwezi kupatikana nje ya kipindi hiki. Mwenyezi Mungu asema:

اللَّهُ الَّذِي خَلَقَكُمْ مِنْ ضَعْفٍ ثُمَّ جَعَلَ مِنْ بَعْدِ ضَعْفٍ قُوَّةً ثُمَّ جَعَلَ مِنْ بَعْدِ قُوَّةٍ ضَعْفًا وَشَيْبَةً ۚ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْعَلِيمُ الْقَدِيرُ {54}

“Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuumbeni katika udhaifu, na baada ya udhaifu akafanya nguvu, kisha baada ya nguvu akaufanya udhaifu na uzee, huumba apendavyo, naye ni Mjuzi Mwenye uwezo.” (Sura Rum:54).

Kisha akasema tena:

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُمْ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ مِنْ نُطْفَةٍ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍ ثُمَّ يُخْرِجُكُمْ طِفْلًا ثُمَّ لِتَبْلُغُوا أَشُدَّكُمْ ثُمَّ لِتَكُونُوا شُيُوخًا ۚ وَمِنْكُمْ مَنْ يُتَوَفَّىٰ مِنْ قَبْلُ ۖ وَلِتَبْلُغُوا أَجَلًا مُسَمًّى وَلَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ {67}

“Yeye ndiye aliyekuumbeni kwa udongo, kisha kwa manii, kisha kwa pande la damu, halafu akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga, kisha ili mpate nguvu zenu kamili, kisha (akakuacheni) muwe wazee, na wengine wenu hufishwa kabla (ya uzee) na ili mfikie muda uliowekwa, na ili mpate kufahamu.” (Sura Muumin/ Ghafir: 67).

Ni dhahiri Aya zilizotangulia zimeonyesha thamani ya ujana na matarajio endelevu kutoka ndani ya kipindi hicho ambacho Imam Jafar As-Sadiq (a.s.) amekiwekea kikomo kwa kusema: “Mtu akizidi miaka thelathini basi ameshakuwa mzee, na akizidi arubaini basi tayari keshakuwa kikongwe.”1

Japokuwa katika zama zetu hizi kila taifa au kundi hujiwekea mwanzo na kikomo cha ujana, lakini hakuna anayeepuka umri huo uliotajwa na Imam Jafar (a.s.), na hivyo naweza kusema kuwa lengo si umri, bali lengo ni jinsi gani mwanadamu ndani ya maisha yake anaweza kutumia vizuri kipindi

chake chote cha uwezo na nguvu zenye ufanisi na ubora, kipindi ambacho bila shaka ndio kipindi cha ujana.

Sijaona msiba mkubwa katika nchi zetu za kiafrika na hasa Tanzania kama msiba huu wa vijana kutokujali kabisa kipindi chao hiki, lakini linaloshangaza zaidi ni kuona wazee ambao ni waathirika wa mafunzo ya ujana jinsi gani wameshindwa kabisa kuwaandaa watoto wao kwa ajili ya kipindi hiki chenye thamani. Kutokana na uzembe huo wa wazee vijana wengi wameshindwa kujua thamani ya ujana wao, na hivyo kusababisha baadhi ya hasara za kijamii za kujitakia ikiwemo, ujinga, viongozi mbumbumbu, ufisadi, utumiaji wa madawa ya kulevya, ulevi, ushoga, ukahaba, ubakaji, ujambazi, ufukara, umaskini, maradhi na mengine mengi yanayochangiwa sana na kitendo cha vijana wa zamani kutowaandalia mazingi- ra vijana wa sasa.

Uisilamu unatambua thamani ya ujana na athari zake za kiroho na kimwili hadi kimaada, ndipo Imam Ali (a.s.) akasema: “Hakika moyo wa kijana ni sawa na ardhi tupu, chochote kitakachotupwa hapo hukikubali.” Hapo Imam akataka vijana wapandikizwe maadili mema na mtazamo sahihi ili maadui wa ubinadamu wasiweze kutumia fursa hiyo kupanda mbegu zenye sumu kwa jamii.

Mtume (s.a.w.w.) alijali sana kuwasomesha na kuwalea vijana, hivyo jiwe lake la kwanza alilolitaka katika msingi wa Uislamu lilikuwa ni vijana, na hivyo ndivyo ilivyokuwa, na kijana wa kwanza akiwa ni Ali (a.s.) ambaye kwa ujana wake aliusimamisha Uislamu, ndipo Mtume (s.a.w.w.) akawausia sahaba zake: “Nawausia kheri kwa vijana, kwani hakika wao ni wenye vifua vyepesi, Mwenyezi Mungu alinituma niwe mbashiri na muonyaji, vijana wakaniunga mkono, na wazee wakanipinga.”

Na kwa msingi huu Imam Jafar As-Sadiq (a.s.) akamuusia Abu Jafar Al-Ahwal akimuomba kuwasambazia vijana elimu na maarifa ya Ahlul-Bait (a.s.) ili waweze kuharakisha kuelekea kwenye kila la kheri, akasema:

“Shikamana na vijana, kwani hakika wao ndio wepesi kuelekea katika kila kheri.” Na hivyo kauli hii ya Imam inaelekeza na kuwajibisha majukumu kwa walezi, wazazi, viongozi wa kidini na kisiasa, wanaharakati na viongozi wa jamii.

Mwenyezi Mungu anawapenda sana vijana, na ndio maana wafuasi shu- pavu, makini na waaminifu walikuwa ni vijana, au kwa kauli nyingine ni kuwa Manabii na Mawasii wakiwemo Maimamu wetu (a.s.) walikuwa ni sehemu ya vijana.

Basi Kitabu hiki ni sehemu nyingine ya mwongozo wa Mwenyezi Mungu na upendo Wake kwa vijana wote na hasa wa kizazi hiki ambacho kimezungukwa na kila aina ya mitego ya ufisadi, uovu na uasi.
Hemedi Lubumba Selemani
Barua Pepe:
abulbatul@yahoo.co.uk

  • 1. Biharul-An’war, Juz. 75. Uk. 253.