read

Sura Ya 12: Kifo Cha Khadija-Tul Kubra Na Abu Talib - A.D. 619.

Mashujaa watano wa Makka waliukanyaga mkataba wa Maquraysh wa kuwasusia Banu Hashim. Shukurani kwa uungwana na ushujaa wao, Bani Hashim wameweza kurudi mjini, na kuishi kwenye nyumba zao kwa mara nyingine tena. Lakini, kabla hata hawajatulia na kuanza kusa­hau ugumu wa maisha ya maficho ya milimani kwa miaka mitatu, Khadija, mke, sahaba na rafiki wa Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mfadhili wa Uislamu na Waislamu aliugua. Ugonjwa wake ulikuwa wa muda mfupi lakini wa kufisha. Maisha yake yote aliyoishi katikati ya maisha ya kujitosheleza na ya anasa, lakin miaka mitatu aliyoishi uhamishoni ulikuwa wakati wa kushikilia sana maadili kwake ambao bila kuepukika uligharimu maisha yake.

Kama ambavyo imeandikwa kwenye kurasa za nyuma, Khadija alikuwa mwanamke wa kwanza kutangaza kwamba Muumbaji ni Mmoja na kwamba Muhammad alikuwa Mjumbe Wake.

Utukufu na heshima ya kuwa Muumini wa Kwanza duniani pote, ni yake daima.

Wakati Uislamu ulipoanza kupata upinzani mkali kutoka kwa maadui zake, Khadija alijitolea kwa kusahau raha zake zote, utajiri na familia yake ili auhami Uislamu, na sasa ilionyesha kama vile alikuwa tayari kuyatoa mhanga maisha yake. Bila shaka kama angeishi kwenye nyum­ba yake ya starehe Makka, akiwa amezungukwa na watumishi wake, labda angeishi kwa miaka mingi. Lakini alipendelea kumsaidia mume wake na ukoo wake na kushiriki maisha machungu pamoja nao.

Kipindi cha kuzingira Waislamu, si tu kwamba alivumilia uchungu wa njaa na kiu, bali na joto kali la kiangazi na baridi ya majira ya kipupwe, hata hivyo hakulalamika kwa mumewe kwa hayo yote. Ima hali iwe nzuri au mbaya; mahitaji ya kutosha au hakuna kabisa kitu, wakati wote alikuwa na furaha. Hali mbaya ya maisha na ufukara kamwe havikumkatisha tamaa. Mwenendo huu ndio ulikuwa chanzo imara cha raha, ujasiri, umadhubuti wa mume wake wakati mbaya sana katika maisha yake.

Katika kipindi cha kuzingirwa Waislamu. Khadija alitumia utajiri wake wote kwa kununua mahitaji muhimu kama chakula na maji kwa ajili ya ukoo wa mumewe. Aliporudi nyumbani kwake Makka, senti yake ya mwisho ilikwishatumika na alipofariki dunia hapakuwepo hata hela ya kununua sanda. Joho la mume wake lilitumika kama sanda.

Muhammad Mustafa kamwe hakuoa mke mwingine wakati wa uhai wa Khadija, na kama asingekufa, uwezekano ni mkubwa kabisa kwamba hangeoa kabisa.

Edward Gibbon

Katika kipindi cha miaka 24 cha ndoa yao, mume wa Khadija ambaye alikuwa bado kijana aliepusha na haki ya mitala, na fahari au upendo wa mjane kamwe haukufedheheshwa na jamii ya upinzani. Baada ya kifo chake, Mtume alimweka kwenye daraja la wanawake wanne ambao ni bora zaidi, dada wa Musa, mama wa Isa (Yesu) na Fatima, binti yake aliyependwa sana.

(The Decline and Fall of the Roman Empire)

Muhammad bin Ishaq, mwandishi wa maisha ya Mtume, anasema kwamba wakati Wahyi kutoka kwa Mungu uliponza tena baada ya kuko­ma kwa muda baada ya kutembelewa mara mbili na malaika Jibril kati­ka pango la Hira, Khadija alipokea sifa na salamu za amani kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t). Ujumbe uliwasilishwa na malaika Jibril kupi­tia kwa Muhammad, na alipoufikisha ujumbe kwa Khadija alisema: "Mwenyezi Mungu ni Amani (as-Salaam), na Amani yote hutoka kwake na amani iwe kwa Jibril."

Muhammad alimkumbuka Khadija katika uhai wake kwa hisia za mapenzi, shukrani na upendo. Wakati Khadija anaugua, usiku kucha hakulala kwa kumuuguza, kumliwaza na kumwombea. Mumewe alimwambia kwamba Mwenyezi Mungu alimuahidi furaha kamili ya Milele na alikwisha mjengea kasri ya kifalme yenye kuta za lulu huko Peponi. Ilipokaribia asubuhi mwili wake uliodhoofika haukuweza kuhimili mauvivu ya homa na roho yake iliyotakaswa na uadilifu ilion­doka hapa duniani na kuelekea kwenye kituo chake - Mbinguni ambapo iliingia kwenye kundi la walio hai milele.

Kifo chake kilimhuzunisha Muhammad sana.

Khadija alifariki tarehe kumi mwezi wa Ramadhani mnamo mwaka wa kumi baada yakutangazwa Uislamu.

Khadija alizikwa Hujun sehemu ilioko jirani na Makka. Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, aliteremka ndani ya kaburi na kulala humo kwa dakika chake. Halafu akawasaidia waombolezaji wengine kuuteremsha mwili kaburini. Baada ya maziko alisawazisha ardhi juu ya Kaburi lake (Khadija).

Kwa hiyo, Khadija alikufa akiwa mwanamke wa kwanza kuamini Upweke wa Muumbaji.

Amani iwe kwa Khadija ambaye alipelekewa salamu za amani na Mwenyezi Mungu (s.w.t).
Amani iwe kwa Khadija ambaye alijengewa kasri ya kifalme yenye kuta za lulu huko Peponi.
Amani iwe kwa Khadija, mbora sana miongoni mwa wanawake, na mkuu wa wanawake wote.

Khadija alifariki mwaka wa 619 A.D. Mwezi mmoja baada ya kifo chake, Muhammad Mustafa alipata mshtuko mwengine wa kifo cha Abu Talib, ami yake na mlezi wake na ngao ya Uislamu. Kifo cha hawa marafiki wawili-Khadija na Abu Talib - kilikuwa mshtuko mkubwa zaidi ambao Mtume wa Mungu alitakiwa avumilie katika miaka hamsi­ni ya maisha yake. Taa mbili za maisha yake zilizimika. Alizidiwa na huzuni. Aliuita mwaka wa vifo vyao "Mwaka wa Huzuni."

Mwaka wa 619 uligeuka kuwa mwaka wa huzuni kwa Muhammad Mustafa katika maana mbili. Kifo cha mpendwa wa wastu kwa kawaida ni tukio la huzuni. Lakini kwa hali ya Muhammad, kifo cha hawa marafiki wawili haikuwa tu tukio la huzuni kwake. Haikupita muda mrefu alifanywa atambue maana ya vifo vyao, kwa mfululizo wa matukio tofauti tofauti.

Muhammad bin Ishaq.

Khadija na Abu Talib walikufa mwaka mmoja, na kwa kifo cha Khadija matatizo yalikuja kwa haraka moja baada ya lingine. Alikuwa muumini wa kutegemewa naye katika Uislamu, na alikuwa anamsimulia kuhusu matatizo yake. Pamoja na kifo cha Abu Talib alipoteza chanzo cha nguvu ya maisha, ulinzi wa kabila lake. Abu Talib alifariki miaka mitatu kabla ya Muhammad hajahamia Madina, na hapo ndipo Maquraysh walipoanza kumfanyia mambo mabaya ambayo hawangeyafanya wakati wa uhai wa ami yake. Kijana baradhuli alimtupia Mtume mchanga kichwani.

Hisham kutoka kwa baba yake, Urwa, aliniambia kwamba Mtume aliin­gia nyumbani mwake na alikuwa anasema: Maquraysh kamwe hawaku­nifanyia hivi kabla Abu Talib hajafa."

(The Life of the Messenger of Allah)

Washington Irving

Baada ya kipindi kifupi, Muhammad alitambua hasara aliyopata kutokana na kifo cha Abu Talib. ambaye hakuwa tu ndugu mwenye upendo bali mlinzi madhubuti mwenye nguvu, kutokana na ushawishi wake mkubwa kule Makka.

Baada ya kifo cha Abu Talib hapakuwepo mtu ambaye angezuia uchokozi wa Abu Sufian na Abu Jahl.

Mafanikio ya Muhammad yalianza kufifia pale Makka. Khadija, mfad­hili wa kwanza, swahiba wake aliyejitolea katika faragha na upweke wake, muumini mkereketwa wa imani yake, alikufa; vivyo hivyo Abu Talib, ambaye alikuwa mlinzi wake mwaminifu na makini.
Kwa kukoseshwa kinga yenye ushawishi ya Abu Talib, Muhammad katika hali hiyo, alikuwa kama mtu mhalifu mjini Makka, aliwajibika kujificha na kuwa mzigo wa wema wa watu ambao imani yake mwenyewe ili­waingiza kwenye mateso (sic1). Kama manufaa ya dunia yangekuwa ndio lengo lake, aliweza vipi kufanikiwa?

(The Life of Muhammed)

Washington Irving amekosea kwa kusema kwamba Muhammad "alikuwa mzigo wa wema wa watu ambao imani yake mwenyewe ili­waingiza kwenye mateso." Kamwe Muhammad hakuwa mzigo kwa yeyote. wakati wowote. Watu wa ukoo wake Bani Hashim waliona fahari na upendeleo kumlinda yeye na kuutetea Uislamu, vyote hivi vilikuwa hazina yao kubwa mno.

Walitambua kwamba akiwepo Muhammad miongoni mwao, walikuwa wapokeaji wa neema za Peponi na hawakuwa na nia ya kuzipoteza neema hizo kwa jinsi yoyote ile.

Ni nani mwengine isipokuwa ukoo wa Banu Hashim ambaye angemlin­da Muhammad na Uislamu? Muhammad alikuwa musuli na damu yake, na Uislamu ulikuwa uhai na mapenzi yake.

Kosa lingine ambalo mtaalamu huyu mashuhuri wa historia amelifanya lipo ndani ya swali ambalo ameliuliza: "Kama manufaa ya dunia yangekuwa lengo lake, aliweza kuyapata jinsi gani?"

Manufaa ya dunia hayakuwa madhumuni ya Muhammad. Quraysh walikuwa tayari kumpa yeye manufaa ya dunia; walitaka kumpa utajiri, utawala na starehe. Vyote hivyo wangempa kama angevitaka. Lakini alivikataa katakata. Je, wangeweza kumpa chochote kingine zaidi ya hivyo?

"Muhammad alikuwa na lengo moja tu, nalo ni kufanya kazi aliyoamri­wa na Mwenyezi Mungu (S.w.t.), yaani kutangaza Uislamu - Dini ya Mwenyezi Mungu"

Sir William Muir

Kujitoa muhanga ambako Abu Talib na familia yake walifanya kwa ajili ya mpwa wake, ingawa bado hajasadiki ujumbe wake, ameikiri tabia yake kuwa ni nzuri ya kipekee na ni mkarimu si mchoyo na mbinafsi. Hapo hapo wanadiriki kuhoji uthibitisho madhubuti wa uaminifu wa Muhammad. Abu Talib hangefanya hivyo kwa mpenda uwongo; na alikuwa na njia nyingi za kuchunguza.

(The Life of Muhammed, London, 1877)

Sir William Muir anasema kuhusu jambo hili: "Kama kweli isingekuwa kwa sababu ya ushawishi na ulinzi mkali wa Abu Talib, ni dhahiri kwamba nia ya uchokozi wa Maquraysh inge­hatarisha uhuru na pengine uhai wa Muhammed."

(The Life of Muhammed, London, 1877).

Turji Zaydan

Sababu iliyomfanya Abdul Muttalib amshawishi Abu Talib kufanya kazi ya kumlea Muhammad, ilikuwa, Abu Talib na Abdullah walikuwa wato­to wa mama mmoja. Bila shaka, ulinzi wa Abu Talib ulikuwa sababu kubwa, si tu kwa ushindi wa ujumbe wa Muhammad lakini pia kwa sababu ya usalama wake mwenyewe.
Abu Talib alikuwa na hadhi kwa Maquraysh, na mtu mwenye kuheshimika sana. Muhammad aliishi ndani ya nyumba yake kama mmojawapo wa watoto wake…

(Complete Works, published by Dar. ul-Jeel, Beirut, Lebanon, Volume 1 page 91, 1981).

Luteni Generali Sir John Glubb ameandika kwenye kitabu chake, the Life and Times of Mohammad.
Kwamba Abu Talib hafikiriwi na Waislamu kuwa shujaa kwa sababu alikufa kabla hajasilimu. Lakini anaongezea, "Hata hivyo, kama isingekuwa kwa ujasiri wa kumlinda mpwa wake, inawezekana Uislamu ungesambaratika ukiwa katika siku zake za mwanzo.

Wote wawili, Sir William Muir na Sir John Glubb na wataalam wengine wengi wamejiingiza katika kusema kwamba Abu Talib alikufa kabla hajasilimu. Kama wakitakiwa kuthibitisha madai yao wangekimbilia kwenye maandishi ya Imam Bukhari. Bukhari anasema kwenye "hadithi" yake kwamba; wakati Abu Talib alipokuwa taabani kitandani, Mtume alimsisitizia asilimu, lakini alisema kwamba kufanya hivyo kungemuaibisha yeye na rafiki zake Maquraysh.

Waandishi wa "hadithi" hii walisahau kitu kimoja. Abu Talib alikuwa anakufa na alijua kwamba hangewaona tena rafiki zake, Maquraysh.

Alitambua kwamba alikuwa anakwenda kukutana na Muumba wake. Kwenye kipindi kama hiki hangewajali Maquraysh. Shauku yake wakati wote ilikuwa kufuzu kumfurahisha Mwenyezi Mungu. Alithibitisha hilo kwa vitendo vyake zaidi kuliko mtu mwingine yeyote ambaye angeweza kuthibitisha kwa maneno yake kwamba imani yake kuhusu Upweke wa Mungu na kwenye ujumbe wa Muhammad kama mjumbe Wake, ilikuwa imani imara thabiti na ngumu kama mwamba usiotikisika.

Amin Dawidar, mtaalam wa historia wa zama za sasa wa Misri, anase­ma kwamba Abu Talib alikuwa kama ngome ya Muhammad ambayo ilimhifadhi yeye (Muhammad) kutokana na joto lote na baridi yote na shutuma na ukaidi wa walimwengu. "Na Abu Talib alipofariki," anase­ma: "Muhammad alijikuta ana kwa ana na adui kwa mara ya kwanza katika maisha yake. Bila shaka, kifo cha Abu Talib kilikuwa msiba kwake."

Hakuwa na lingine la kufanya ila Abu Talib aliamua kuwa Mwislamu na Muumini. Hakuna mtu anayeweza kumpenda Muhammad na masana­mu kwa wakati mmoja; mapenzi haya mawili hayaendi pamoja hata kidogo. Na hakuna mtu anayeweza kumpenda Muhammad na auchukie Uislamu. Kumpenda Muhammad na kuchukia Uislamu ni vitu visivy­oweza kuwekwa pamoja.

Yeyote anayempenda Muhammad, lazima apende Uislamu. Kama kuna kitu chochote kisichokuwa na shaka kati­ka historia ya Uislamu, ni mapenzi ya Abu Talib kwa Muhammad. Kama ambavyo imeandikwa kwenye kurasa za nyuma, Abu Talib na mke wake, walimpenda Muhammad zaidi ya walivyowapenda watoto wao. Mapenzi hayo yalikuwa na chemchem moja tu - yaani kukubali kwamba Uislamu chanzo chake cha asili ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Abu Talib alijivuna kwamba Mwenyezi Mungu alimteua Muhammad mtoto wa ndugu yake, Abdullah, katika Uumbaji wote, kuwa awe mjumbe Wake wa mwisho na Mjumbe mkubwa kabisa kwa watu wote. Muhammad alikuwa pendo kubwa kabisa na fahari kubwa kabisa ya ami yake, Abu Talib.

Kwenye Kitabu Chake, Mwenyezi Mungu (s.w.t) alitambua mwenyewe ulinzi ambao Abu Talib alimpa Muhammad Mustafa, kama ulinzi wake mwenyewe kama isemavyo Aya ifuatayo: "Je! Hakukukuta yatima akakupa makazi (mazuri ya kukaa)" (Quran 93: 6)

Mwenyezi Mungu alimpa ulinzi na ulezi (uangalizi) Mtume Wake Muhammad Mustafa, kupitia kwa mtumishi Wake Abu Talib.

Abu Talib alifanya kazi Makka kwa ajili ya Utukufu na Uwezo wa Uislamu na alikuwa mlezi wa maadili.

Kwa muda wa miaka 10 alikien­desha chombo cha Uislamu wakati wa ujinga na matatizo mbali mbali kwa ustadi, akiona mbali na imani ambayo iliwakasirisha walezi wa masanamu ya wapagani wa Arabuni. Matendo yake ni sehemu muhimu ya simulizi ya Uislamu, pia ni uthibitisho usiopingwa wa imani yake kwa Mwenyezi Mungu na mjumbe Wake - (imani ) ya Uislamu.

Mwenyezi Mungu na awabariki waja wake wapendwa, Khadija na Abu Talib. Wote wawili waliuweka utii kwake Yeye mbele kuliko kitu cho­chote kingine katika maisha.

  • 1. Sic- Japo kwa makosa. Maana yake ni kukataa maneno ya mwandishi aliyenukuli­wa