read

Sura Ya 13: Khadija - Mama Wa Waumini

Kabla ya Uislamu, Khadija alikuwa Malkia wa Makka. Wakati jua la Uislamu lilipochomoza juu ya upeo wa macho, Mwenyezi Mungu ali­furahi kumfanya pia Malikia wa Uislamu. Mwenyezi Mungu pia alifu­rahishwa kumfanya yeye Mama wa Waumini, kama Asemavyo kwenye Kitabu chake.

"Nabii yu karibu zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao wenyewe, na wakeze ni mama zao.
(Quran 33 : 6)

Maelezo ya mfasiri

"Sura hii ya (33) inathibitisha hadhi na nafasi ya wakeze Mtukufu Mtume, ambao walikuwa na ujumbe maalum na wajibu kama Mama wa Waumuini. Hawakutakiwa kuwa kama wanawake wa kawaida: wali­takiwa kuwaelekeza wanawake katika mambo ya kiroho, kuwatembelea na kuwasaidia wagonjwa au wenye dhiki, na kufanya mambo mengine mema katika kusaidia ujumbe wa Mtume." (A.Yusuf Ali)

Cheo cha Mama wa Waumini kinaonyesha kutayarishwa hususani kwa ajili ya Khadija. Bila Khadija, cheo hiki hakina maana. Yeye na yeye peke yake alionyesha mapenzi ya dhati ambayo yanatolewa na mama tu kwa waumini. Mama anaweza kuwa anahisi njaa lakini kama watoto wake wana njaa, atawapa chakula watoto wake kwanza. Kwa hakika, kama ni muhimu katika hali ya dharura atawalea na njaa huku akifurahi.

Hali hii imetokea mara nyingi katika historia, hasa zaidi wakati wa vita na njaa. Ni jambo la uhakika kwamba watoto walioshiba na kutosheka, inatosha kumfanya mama afurahi na kutosheka, inatosha kumfanya yeye (mama) asahau njaa na kiu yake.

Mapenzi ya mama hayana shar­ti; yanalenga hali zote na kujumuisha wote.

Waislamu walio wengi Makka walikuwa masikini. Hawakuwa na vyan­zo vya mapato, na walikuwa hawana namna ya kuwawezesha kujipatia riziki kwenye jiji ambalo uchumi wake ulikuwa mikononi mwa makun­di ya siri ya waubudu masanamu. Wanachama wa makundi ya siri wal­itoa agizo kwamba Mwislamu asilipwe ujira wowote kwa kazi yoyote atakayofanya na ni marufuku kununua kitu chochote kutoka kwake.

Walitambua kwamba ufukara wa mali uliathiri vibaya mwili na roho na walidhani kwamba wakati upinzani wa Waislamu utakaposhindwa, kutokana na kudhoofika kiuchumi, wangeukana Uislamu, na wangemkataa Muhammad. Lengo la sera hii ilikuwa ni kuwanyima chakula Waislamu.

Lakini Khadija aliwalisha Waislamu masikini kila siku, hivyo kwamba hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyedhikika kwa njaa, na aliwapa mahali pa kukaa. Kwake yeye, utoaji wa sadaka halikuwa jambo jipya lakini kipimo na uwezo wa msimamo ilikuwa kama ifuatavyo: alitumia fedha nyingi mno kwa ajili ya masikini na Waislamu wa Makka wasiokuwa na nyumba, hivyo alikwamisha mpan­go wa matajiri wa Makka waabuduo masanamu.

Msaada ambao Khadija aliutoa kwa jamii ya Waislamu wa Makka, ulikuwa muhimu kwa uhai wa Uislamu. Msaada wake kwa jamii ya Waislamu ulihakikishia uhai wa Uislamu wakati ulipokuwa katika hali ya mkwamo. Katika hali hii, alikuwa mtengenezaji wa historia - histo­ria ya Uislamu.

Wake zake Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, wote ni kina Mama wa Waumini; lakini kuna tofauti kubwa kati yao na Khadija. Wanawake wote walioolewa na Mtume Muhammad huko Madina walipokea ujira kutoka Hazina ya Umma. Baadhi yao walidai haki maalumu na marupurupu kutoka kwake. Walisema kwamba haki maalum zilizolipwa zilikuwa hazitoshi kwa mahitaji yao.

Kwa upande mwengine, Khadija kamwe hakuomba kitu chochote kuto­ka kwa mume wake. Khadija aliamua mali yake iwe Hazina ya Umma kwa ajili ya Waislamu. Hapo Makka hapakuwepo Hazina ya Umma, ilikuwa ukarimu usio na mpaka na utajiri mwingi wa Khadija ambao ndio uliiokoa Jamii ya Waumini.

Alikuwa anajihusisha sana na ustawi wa wafuasi wa mume wake, hivyo kwamba aliridhika kutumia fedha zake zote kwa madhumuni haya. Mwenyezi Mungu ambariki mtumishi Wake, Khadija, Mama wa Waumini zaidi na zaidi.

Khadija kama Mama

Dk. Sir Muhammed Iqbal (d. 1938) alikuwa Mshairi Mwana falsafa wa Indo-Paksitan. Pia alikuwa kichocheo cha mwamko wa Waislamu karne ya 20.

Anasema kwamba, mama anashika nafasi ya pili baada ya Mungu Mwenyewe. Mama analeta maisha mapya hapa duniani, yaani anaumba; na tendo hilo - tendo la kuleta maisha mapya hapa duniani au tendo la kuumba, linamtaka mtu ajitolee muhanga. Katika kuleta maisha mapya hapa duniani, mama huyaweka maisha yake hatarini. Kwa hiyo, mama anastahili hadhi na heshima kubwa sana.

Kinachomfanya mama ayatoe muhanga maisha yake ni mapenzi­mapenzi kwa mwanawe. Mapenzi kwa mwanawe ni mapenzi yaliy­otakasika. Kwenye utakatifu, mapenzi ya mama kwa mwanae yanashika nafasi ya pili baada ya mapenzi ya Mungu Mwenyewe.

Khadija alikuwa mama aliyejivunia watoto watatu - watoto wanaume wawili na mwanamke mmoja, kama ilivyokwisha onyeshwa huko nyuma. Watoto wawili wa kiume - Qasim na Abdullah walifariki dunia wakiwa wachanga. Mtoto wake wa mwisho na ndiye tu aliyebaki kati­ka kuishi alikuwa Fatima Zahra.

Kama Khadija alikuwa mama bora, Fatima Zahra alikuwa binti bora.

Fatima Zahra, binti bora wa Muhammad Mustafa na Khadija, naye pia alipata kuwa mama bora. Alikuwa mama wa watoto wa kiume wawili -Hasan na Husain - na mabinti wawili- Zainabu na Umm Kulthum.

Khadija na Fatima Zahra - mama na bintiye - walikuwa wawili miongo­ni mwa wanawake wanne walio bora hapa duniani. Wote wawili wali­fanya umama utakasike. Waliufanya umama utukuke na kuheshimiwa.

Kama ambavyo imesemwa huko nyuma, katika kitabu hiki wanawake hawakuwa na hadhi kabla ya Uislamu huko Arabuni. Kwenye jamii iliy­otawaliwa na mfumo dume walikuwa wana dhulumiwa kikatili na wal­ifanyiwa mambo kama wanyama. Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alikomesha dhuluma ya wanaume kwa wanawake, na aliwapa hadhi ambayo wanawake walikuwa hawajapewa katika nchi yoyote na wakati wowote. Kuhusu wakina mama alisema:"Pepo ya mtu ipo chini ya miguu ya mama."

Maana yake ni kwamba hakuna mtu anayeweza kuwa na matumaini ya kupata pepo kama amemkasirisha mama yake. Mtu kuipata pepo lazi­ma awe na uwezo wa kufuzu kuupata wokovu, na hakuna mtu ambaye amemkasirisha mama yake akaupata wokovu.

Hivyo Mtume wa Uislamu amefanya mtu kufuzu kupata radhi ya mama -mwanamke - sharti linalo tanguliwa kabla mtu hajapata wokovu na kuingia peponi.