read

Sura Ya 14: Khadija, Mwanamke Mkamilifu

Kumekuwepo na wanawake wengi katika historia ya ulimwengu huu ambao walipata kuwa wakubwa na maarufu kwa sababu ya matendo yao makubwa. Jamii ya kibinaadamu inaweza kujivunia kwa haki kabisa kutokana na (wanawake) hawa. Lakini katika historia ya ulimwenguni wote, wako wanawake wanne tu ambao wangeweza kufikia vipimo vya daraja ya juu vya ukubwa wa kweli na ukamilifu uliowekwa na Uislamu. Walifikia kwenye vipimo hivi kutokana na huduma zao kubwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Muhammad Mustafa, Mtume wa Uislamu, Mpokeaji wa Ufunuo (Wahyi) kutoka mbinguni, na Mfasiri wake, aliwatambua. Nao ni:

1. Asiya, mke wa Firauni,

2. Maryam, mama wa Isa, (Yesu)

3. Khadija, binti wa Kuwaylid na

4. Fatima Zahra, binti ya Muhammad Mustafa (s.a.w.w)

Muhammad Mustafa aliwaona wanawake wanne tu walio bora katika jamii ya dunia nzima. Baina ya hao wanne, wawili wa mwisho wanato­ka nyumba moja; wao ni Khadija, mama wa Fatima, na binti yake, Fatima. Khadija alikuwa mfano kwa roho iliyo bora na iliyokamilika.
Katika jamii iliyosalia hapa duniani, wanawake wengine tu ambao wanaweza kufuzu kuwa wanawake wenye sifa ya ubora, wangekuwa ni wake zake wengine wa Muhammad Mustafa. Lakini yeye mwenyewe alitoa hukumu kuhusu jambo hili, na hukumu yake haifutiki haibadili­ki. Alimtaja Khadija tu miongoni mwa wake zake kwamba ni mwanamke bora, na kwa hiyo aliwatenganisha - kwa amri wake zake wengine kutoka kwenye kundi la wanawake bora.

Khadija alikusanya katika utu wake sifa zote hizo zinazo mfanya mtu kuwa bora. kama angepungukiwa na yoyote katika sifa hizo, mume wake hangemweka kwenye kundi la walio bora. Na hakuna ushahidi wowote kwamba alikuwa na kasoro hizo, ambazo zinasemekana kwa kanuni kuwa ni tabia za kimaisha ya wanawake.

Tabia mojawapo ya udhaifu wa wanawake ni wivu. Khadija hakuwa na wivu wa aina yoyote. Alikuwa mwanamke aliyeona ukamilifu, furaha na kutosheka katika kutoa msaada. Alikuwa mlezi karimu wa masikini. Alikuwa anajisikia mwenye raha wakati anawapa chakula wenye njaa na huzuni. Matendo ya kuwalisha na kuwaliwaza wenye njaa na huzu­ni haikulazimu juhudi ya dhamira kwa upande wake; kwake matendo hayo yalikuwa kawaida yake.

Kama vile ambavyo Khadija alivyokuwa hana wivu, pia alikuwa habezi. Kitu kimoja ambacho kamwe hakukifanya, ni kuumiza hisia za mtu. Hakumtania mwanamke yeyote, hakujaribu kumdhalilisha mtu yeyote; kamwe hakumdharau mtu yeyote; kamwe hakukasirika na kuchukia na hakujiingiza katika kutoa maamuzi. Hakutamka neno baya au neno la kashfa dhidi ya mtu yeyote. Alikuwa na moyo wa kuelewa, alikuwa mtu wa kujihusisha sana na hisia za wanawake wanyenyekevu na masikini sana, na alidhikika kwa sababu ya dhiki ya wengine.

Kuna wakati ambapo Khadija aliitwa Binti wa Wafanyabiashara na Binti wa Makka. Halafu kuna wakati ambapo aliamua mali yake nyingi imi­likiwe na Uislamu.

Alikuwa tajiri sana lakini baadaye akawa masikini kwani hakuwa na kitu. Alibadilisha mfumo wa maisha ya starehe na kuendesha maisha ya dhiki. Lakini hakuna kilichobadilika katika tabia yake. Alikuwa mwenye furaha, karimu, mkamilifu kama mwanzo. Alitumia muda mwingi sana kujitolea kumtumikia Mwenyezi Mungu, na Mjumbe Wake, na kama ilivyo kawaida, kamwe hakusahau ustawi wa umma wa Waumini. Aya ifuatayo inatoa maelezo kuhusu alivyo:

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِنَفْسِهِ وَمِنْهُمْ مُقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ {32}

"Na wako wanaokwenda mbele kabisa katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kubwa." (Qur'an 35 : 32)

Khadija, aliyemkamilifu, alikuwa mstari wa mbele kufanya "Matendo mema." Alikuwa na hali ya msukumo wa utakatifu ndani mwake. Kupitia "matendo yake mema" akawa mpokeaji wa neema za hali ya juu kutoka Mbinguni.

Khadija alikuwa mwanamke aliyekamilika, mke aliyekamilika wa Muhammad Mustafa, Mama aliyekamilika wa watoto wao, na Mama aliyekamilika wa Waumini.

Imani kwamba Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma ilikuwa kama springi ambapo ndipo Khadija alipata majibu ya mafanikio ya maisha yake. Yeye aliyepewa kile Quran inachokiita Qalb Salyim (moyo mtulivu) aya ya 89 kwenye Sura ya 26. Qalb Salyim au moyo tulivu,

A. Yusuf Ali mfasiri na mfafanuzi wa Quran Majid ametoa maana ifu­atayo: "Moyo uliotakasika, na usio athiriwa na maovu yanayotesa wengine. Kwa sababu kwa lugha ya Kiarabu moyo unaeleweka kama kiini cha hisia maono na akili, na matokeo ya tendo, ina jumuisha tabia yote."

Ulinganifu wa tabia ya Khadija ilikuwa ishara ya Qalb Salyim yake. Khadija alizaliwa na "Qalb Salyim" (moyo mtulivu) kama vile tu wale wateule wa Mwenyezi Mungu wanavyo zaliwa nayo. Ni moyo uliokuwa unabubujika imani, kuutumikia Uislamu. Mapenzi na shukurani kwa Mwenyezi Mungu.