read

Sura Ya 15: Ukarimu Wa Khadija

Khadija Bint wa Arabuni, na Muhammad Mustafa, walioana mwaka wa A.D. 595. Miaka kumi na tano baadaye, Muhammad aliteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mjumbe Wake. Kama Mjumbe wa Mungu, kazi yake ilikuwa kutangaza Uislamu hapa duniani. Kuanzia hapo, kila kitu kilibadilika kwa Khadija.

Alitoa wakfu utajiri wake wote kwa ajili ya Uislamu. Wakfu huo ulipatikana katika kipindi mwafaka kwa Uislamu. Khadija alimwambia mumewe kwamba utajiri wake wote umekuwa mali yake, na atumie utajiri huo kwa jinsi apendavyo.

Ukarimu wa Khadija ulikuwa mng’aro wa kiwenyewe.

Muhammad Mustafa “aliwekeza” utajiri wa Khadija kwenye Uislamu. Hapajafanyika “uwekezaji” mzuri kama huo katika historia ya binadamu. “Uwekezaji” huu ulikuwa hakikisho kwamba mwendo wa Uislamu hautsimamishwa au hata kudumazwa kwa sababu ya kusefu wa matumizi muhimu na msaada. Ulikuwa ni uwekezaji ambao, mpaka hii leo, unalipa “migawanyo” mingi na utalipa “migawanyo” kwa kila kizazi cha Waislamu, mpaka mwisho wa muda.

Lakini nyenzo ya utajiri haikuwa ya uwekezaji pekee ambao Khadija alifanya kwa ajili ya Uislamu. Vilevile aliwekeza muda wake, kipaji, nguvu na juhudi na moyo katika Uislamu, uwekezaji unaojulikana vinginevyo kama msimamo wa kujituma. Alitambua ndoto na matu­maini ya mume wake na alishiriki yote pamoja naye.

Nia ya Khadija kusaidia Uislamu ilikuwa dhahiri mno hivyo kwamba Mwenyezi Mungu (S.w.) alifurahi na kuuita utajiri huo wa Kwake Mwenyewe katika aya ifuatayo:

وَوَجَدَكَ عَائِلًا فَأَغْنَىٰ {8}

"Na akakukuta fakiri akakutajirisha" (Qur'an 93: 8)

Maelezo ya mfasiri:

"Mtukufu Mtume hakurithi utajiri wowote na alikuwa masikini. Mapenzi ya kweli, safi, na ya dhati ya Khadija si tu kwamba yalimwon­dosha na kumweka juu ya tamaa ya kupata, bali yalimfanya ajitegemee kwa mahitaji ya kidunia, mnamo siku za usoni za maisha yake, yal­imwezesha yeye kutumia muda wake wote kumtumikia Mwenyezi Mungu." (A.Yusuf Ali).

Mwenyezi Mungu alimtajirisha mtumishi wake, Muhammad, kwa mali ya Khadija.

Khadija na makundi mawili ya Wahamiaji Waislamu kwenda Abyssinia (Uhabeshi)

Makundi mawili ya Waislamu yaliondoka Makka mwaka wa 615 na 616 kuepuka mateso ya Maquraysh na walitafuta hifadhi Abyssinia. Jumla ya idadi ya wanaume na wanawake katika makundi yote mawili ilikuwa takriban mia moja.

Wakitolewa wachache katika kundi kama Uthmani na Zubayr, wakim­bizi wengine wote walikuwa masikini mno kiasi cha kushindwa kumudu gharama za usafiri kwenda Abyssinia. Nani aliyefanya mipango yote ya misafara kuipatia vifaa muhimu ikiwa ni pamoja na chakula na maji na gharama nyengine zote za kuwezesha kusafiri? Wataalamu wa historia hawajatoa jibu la swali hili.

Lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba Khadija aliipatia misafara vifaa na kulipa gharama za usafiri, na Waislamu wakawa na uwezo wa kukimbilia Abyssinia. Hapa Makka ni Khadija peke yake ndiye aliyekuwa na uwezo wa kudhamini uhamaji wa Waislamu wa kiwango hicho.