read

Sura Ya 16: Khadija Na Muhammad Mustafa

Katika kipindi cha miaka kumi na tano ya mwanzo wa ndoa yake, kazi za Khadija zilikuwa zile hasa za mke na mama wa nyumbani.
Mwaka wa A.D. 610 Mwenyezi Mungu (S.w.) alimteua Muhammad kuwa Mjumbe Wake, na tangu hapo kazi za Khadija ziliongezeka. Zaidi ya kuwa mume wake, Muhammad alikuwa kiongozi na mlezi wake kati­ka malimwengu yote mawili hapa duniani na Akhera. Khadija alikuwa makini sana katika utendaji wa kazi zake kama mke na mama; na pia, sasa akajitambua katika kazi zake kama Mwislamu na Muumini wa kweli.

Alifurahi kwamba Mwenyezi Mungu alimteua mume wake kuto­ka miongoni mwa viumbe wote kuchukua ujumbe wa Uislamu kuufik­isha duniani, na yeye alijitolea nafsi yake, kwa moyo, akili na roho, kuhakisha kwamba kazi hiyo inatekelezeka ipasavyo na kuleta mafanikio

Wazazi wa Khadija, kama wale wa Muhammad Mustafa, walifariki akiwa bado mdogo sana. Kwa hiyo hakuwa nayo mapenzi ya huruma na upole wa wazazi kama ilivyokuwa kwa Muhammad. Khadija na mume wake walikuwa mayatima lakini hatimaye wote wawili wangekuwa watu wa kuwapa mapenzi na huruma mayatima wa dunia yote.

Kile walichopoteza kutoka kwenye mapenzi na huruma ya wazazi wao, walifanikiwa kupata mapenzi na huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenyewe (s.w.t) za milele na milele.

Khadija alipoingia nyumba ya Muhammad baada ya kuolewa, hakuonyesha kupenda kujikwatua kwa kutumia vipodozi, kuvaa mapambo ya gharama kubwa yaliyoingizwa kutoka nchi za nje na kad­halika. Baada ya ndoa yake, alikuwa na mapenzi ya kufanya kitu kimo­ja tu, nacho ni kumpa mume wake starehe na furaha.

Aliweza kufanik­isha hayo kwa kutumia nguvu zake zote kwa uthabiti. Alistarehe pale ambapo mume wake alikuwa na starehe na alifurahi tu ikiwa mume wake alikuwa na furaha. Furaha ya mume wake ilikuwa furaha yake. Alipewa kipaji hicho adimu na ule mkono stadi uliofanya nyumba ya mume wake kufana kama Pepo hapa duniani.

Wajibu aliofanya Khadija baada ya mume wake kutangaza ujumbe wake kama mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ulikuwa muhimu sana katika his­toria ya Uislamu.

Mara alipotoka nyumbani mwake, alipambana na matatizo. Wapagani walimtesa kwa matusi na walimuumiza kwa mikono yao. Kazi yake ilijaa matatizo, ugomvi na jirani wasio na adabu waliifanya kuwa ngumu zaidi. Lakini mara alipoingia nyumbani mwake, Khadija alimsalimia kwa tabasamu iliyomfanya afurahi. Alisema maneno ya kuchangamsha yenye matumaini na starehe na wasiwasi na woga wake wote ulitoweka.

Tabasamu na maneno ya Khadija yalikuwa kama kitulizo cha mateso aliyofanyiwa Muhammad na waabudu masanamu kila siku. Na kila siku Khadija alimtia moyo na kurejesha ari yake. Uchangamfu wake ulipun­guza shinikizo baya lililosababishwa na matukio wakati wa shughuli zake, na aliweza kupambana na maadui zake tena akiwa mwenye kuji­amini.

Khadija alikuwa ndio chanzo pekee cha furaha yake wakati wa vitisho na hofu. Huzuni na majonzi yalikuja kwa mfululizo kama maw­imbi, yakimtishia kumshinda, lakini mke wake alikuwepo wakati wote na kumwezesha apate ujasiri na ushupavu zaidi kuendelea na kazi yake. Kwake yeye mke wake alikuwa ngao ya kisaikolojia dhidi ya vurugu za Maquraysh zilizokuwa zinaongezeka mara kwa mara.

Khadija alikuwa na uelewa sawa ujumbe huu kama Muhammad alivy­ouelewa, na yeye alikuwa na shauku ileile aliyokuwa nayo mume wake kuona Uislamu unashinda upagani. Zaidi ya kuwa na shauku ya kuona Uislamu unashinda, yeye aliongeza msimamo na uwezo. Alifanya hivyo kwa kuhakikisha mume wake anafanya kazi ya kutangaza Uislamu tu, na kazi ya kutafuta riziki alifanya yeye. Kwa hiyo Khadija alimwezesha mume wake kuelekeza uangalifu wake wote, nguvu zake zote na muda wake wote katika kuendeleza Uislamu. Huu ni mchango wake muhimu alioufanya katika kazi ya mume wake kama mjumbe wa Mungu. Khadija alikuwa tegemeo ambalo alihitaji, kwa maneno yake A. Yusuf Ali, "miaka yote ya matayarisho yake."

Miaka ile kabla ya kutangazwa Uislamu, ilikuwa "miaka ya matayarisho" kwa utume wake.

(A.Yusuf Ali)

Mchana na usiku Muhammad alikuwa ndani ya pango la Hira na Mola wake Mlezi. Matatizo magumu aliyoyatafakari akilini mwake, magumu zaidi kuliko jiwe la kito jekundu litokanalo kwenye jabali lililomzungu­ka, matatizo ambayo si yake, lakini matatizo ya watu wake, ndio, na ya hatima ya mwanadamu, ya huruma ya Mungu na mgongano wa miaka mingi ya uovu na wema, dhambi na Rehema nyingi.

(The Holy Qur'an Introduction)

Inawezekana sana kwamba Muhammad, Mtume - Mteule, aliupangilia na kuuwekea msimamo Uislamu ndani ya pango la Hira. Sura ya Uislamu ilikuwa dhahiri na kuonekana wazi ndani ya maisha yake binafsi muda mrefu kabla hajatangaza kwamba alikuwa mjumbe wa Mungu. Hatujui kwa ufasaha "miaka ya matayarisho" ilidumu kwa muda gani hadi hapo alipofikisha umri wa miaka 40, msingi wa Uislamu ulikuwa akilini mwake.

Muda ulikuwa jambo la msingi katika mpangilio wa Uislamu, na Khadija alijua umuhimu wake kwa mume wake katika kazi yake kwa hiyo Khadija alitengeneza mazingira bora ambamo mume wake angepa­ta mafaniko ya muda, na kusababisha matokeo mazuri. Khadija alikuwa na kipaji cha kusoma hisia za mtu mwengine. Alikuwa anategemea matamshi yasiyotamkwa kutoka kwa mume wake na alien­delea kufanya kile alichotaka kufanya. Miaka ishirini na tano ya maisha ya ndoa, aliyafanya mawasiliano sahihi kabisa na ya karibu sana baina yake na mume wake.

Mnamo mwaka wa 10 baada ya Tangazo la Uislamu, Khadija alifariki dunia. Kifo cha mpendwa huonyesha jinsi mapenzi ya binadamu yanavyoathiriwa na tukio hilo lakini mapenzi ya Muhammad na Khadija hayakuwa ya kusitishwa na kifo; yalikuwa mapenzi ya milele daima. Khadija alipofariki, mapenzi ya Muhammad kwake hayakukatika.

Kwa hakika, mapenzi yake kwa Khadija yaliendelea kuongezeka hata baada ya kutoweka duniani. Hata kuwapo kwa wake zake tisa haikuwa sababu ya kuzuia ongezeko la mapenzi kwa Khadija, na mapenzi yake kwa marehemu, wakati wote yalikuwa yanatafuta namna ya kujionyesha.

Kama Khadija alimfanyia wema mtu wakati fulani na hata kama ali­fanya hivyo mara moja tu, Muhammad Mustafa alikumbuka na aliji­tahidi kuonyesha wema wa aina ileile kwa mtu huyo hata baada ya kifo chake, na alifanya hivyo mara nyingi iwezekanavyo.

Huko Madina, ilitokea Bibi kizee alikuja kumuona Muhammad Mustafa na akampa maombi fulani. Alimsalimia kwa upole, na alionyesha kuhusika sana na tatizo lake, na alimtimizia ombi lake hapohapo.

Alipoondoka Bibi kizee huyo, Aisha ambaye alikuwa mmojawapo wa wake zake, alitaka kujua mtu huyo ni nani. Alisema: "Wakati Khadija na mimi tulipokuwa Makka, mwanamke huyu alikuwa na mazoea ya kuja kumuona mara kwa mara."

Wakati wa uhai wake, Khadija alionyesha ukarimu na wema kwa watu wengi sana. Baada ya kifo chake, Muhammad Mustafa hakuwasahau watu hao waliokuwa wanapokea ukarimu na wema kutoka kwa Khadija, baada ya kifo chake, waliendelea kufanyiwa hayo na mume wake.

Kuhusu haya Aisha alisema: "Wakati alipochinjwa mbuzi au kondoo (nyumbani kwa Mtume), mjumbe wa Mwenyezi Mungu aliamuru nyama ipelekwe kwa wanawake ambao walikuwa marafiki zake Khadija. Siku moja nil­imuuliza kwa nini alifanya hivyo na alisema: Nawapenda watu wote ambao walimpenda Khadija."(Isaba, Vol. 4, P. 283)

Mwenyezi Mungu (s.w.t) Alimpa heshima mtumishi wake ampendaye, Khadija, kwa kutokuchangia mapenzi ya mume wake na wake wengine. Kipindi chote cha robo karne cha maisha ya ndoa, ni Khadija pekee ndiye alikuwa sahaba na rafiki wa mume wake, Muhammad Mustafa. Kila mmoja aliishi kwa ajili ya mwenzake na walipata machungu na matamu ya maisha wote pamoja.

Mwenyezi Mungu alimpa mtumishi Wake Khadija nafsi na tabia yenye sifa nyingi. Kama alivyoneemeshwa kwa wingi mno kupewa sifa hizo, yeye aliziimarisha kwa kuutendea wema Uislamu.

Khadija alizipamba sifa hizo kwa kumpenda Mwenyezi Mungu kwa kumtii mume wake na kuutumikia Uislamu. Upendo na kutumika kwake ni sifa zilizo mnyanyua Khadija na kumweka kwenye nafasi ambayo hakuna mke mwingine wa Muhammad Mustafa aliyeweza kuifikia. Khadija peke yake, kwa kemikali ya tabia yake aliifanya nyumba ya Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, kuwa kama kisi­wa cha amani, kutosheka na furaha katika bahari ya mapambano na ugomvi.

Iliamriwa huko Mbinguni kwamba Muhammad Mustafa lazima aoe mwanamke mwenye malezi mazuri na mwenye kuelewa sana katika Arabu yote.

Hapakuwepo mwanamke wa aina hiyo isipokuwa Khadija. Mwenyezi Mungu alikuwa na madhumuni ya pekee ambayo yange­timizwa na Khadija. Kwa hiyo, ndoa yao ilitengenezwa Mbinguni.

Abbas, Mahmud al-Akkad wa Misri anasema kwenye kitabu chake, “Aisha”: "Ilikuwa amri maalumu ya Mwenyezi Mungu kwamba mke wa mjumbe wake anatakiwa awe mwanamke mpole sana, mwema na aliyetakasika kama Khadija."

Khadija alikuwa mfano halisi wa uchaji Mungu, utakatifu na alikuwa mlezi wa ukamilifu wa kiwango cha juu na maadili ya juu sana. Inaelekea kwamba kama Muhammad Mustafa hakutokea, Khadija angeishi maisha ya pekee bila mume. Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, wakati fulani alisema kuhusu binti yake Fatima Zahra, kwamba hakuna mtu mwengine ambaye angemuoa isipokuwa Ali bin Abi Talib: Ingekuwa kweli kabisa kusema kwamba hapana mtu mwengine ambaye angestahili kumuoa Khadija isipokuwa Muhammad.

Kuhusu suala hili, A. Yusuf Ali, mfasiri na mfafanuzi wa Qur'an Majid anasema: Ilikuwa baina yake na Hadhrat Khadija, mwanamke na mke bora kuliko wote.

Alimuoa miaka kumi na tano kabla ya kupewa Utume; maisha yao ya ndoa yalidumu miaka ishirini na tano, na mapen­zi yao yalikuwa ya kiwango cha juu sana, yakilinganishwa katika kipi­mo cha kiroho na kijamii. Wakati wa uhai wa Khadija mume wake hakuoa mke mwingine, jambo ambalo si la kawaida kwa mtu mwenye hadhi kama yake miongoni mwa jamii yake.

Mkewe alipokufa, yeye alikuwa na umri wa miaka hamsini (50), na kwa sababu mbili tu, inaelekea kamwe hangeoa tena, kwa kuwa alikuwa anajiepusha sana katika maisha ya kidunia.

Mambo mawili yaliyotawala ndoa zake zilizofuata ni:

1. Aliwaonea huruma na kuwaonyesha upole wajane walio na dhiki na hawangesaidiwa kwa namna nyingine yoyote katika hali ya jamii ile, baadhi yao, kama Sauda, walikuwa na watoto katika ndoa zao za zamani, hivyo walihitaji ulinzi;

2. Msaada katika kazi yake ya uongozi, kutoka kwa wanawake ambao walipewa maelekezo na kuwekwa pamoja katika familia kubwa ya Waislamu, ambapo wanawake na wanaume walikuwa na haki sawa za kijamii.

Muhammad Mustafa, Mtume wa Mwenyezi Mungu, alitumia fursa zote kuonyesha kuvutiwa kwake na mapenzi kwa Khadija na kutambua ukubwa wa kiwango alicho utumikia Uislamu. Alifanya hivyo, kwanza kabisa kutii amri ya Mwenyezi Mungu kama Kitabu chake kinavyose­ma kwenye Aya zifuatazo:

"… Na kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu…." (Sura Al-Baqara 2:231)
" ...Na neema za Mola wake Mlezi zisimulie..." (Sura 93:11 ).

Muhammad Mustafa mtumishi na Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alipokea upendeleo na ukarimu mwingi kutoka Kwake kupitia kwa Khadija - alizikariri na kuzitangaza.

Halafu, pili, Muhammad Mustafa alipenda kutaja matendo mema, makubwa ya Khadija aliyoyafanya katika kumtumikia Mwenyezi Mungu na Uislamu, kwa sababu ya kuonyesha mapenzi kwake (Khadija). Hii ilikuwa njia mojawapo ya kuonyesha mapenzi. Ilikuwa pia namna nyingine ya kujikumbusha muda waliyotumia yeye na Khadija wakiwa pamoja Makka.
Mtu anaweza akaona waziwazi kwam­ba katika kumbukumbu zake, fikra zake zilikuwa zinayatembelea maisha yake ya zamani; na pia mtu anaweza kugundua humo dalili za mambo aliyozoea zamani. Palikuwepo na muda katika maisha ya kila mtu ambapo alizidiwa na kumbukumbu ya mambo aliyoyazoea.

Waandishi wa vitabu viwili mashuhuri, Isaba na Istiab, wamemnukuu Bi Aisha akisema: "Wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu akiondoka kwenda popote, alimkumbuka, alimsifu na kumrehemu Khadija."

Jinsi muda wa maisha ya ndoa ulivyopita, mapenzi ya Muhammad na Khadija yalizidi kupenya kwenye mioyo yao kwa nguvu zaidi. Kwa mapenzi yake, aliondoa wasiwasi wake wote, woga na huzuni kama ilivyoelezwa hapo kabla. Kwa kutumia istiari ya mashariki: Khadija aling'oa miba yote katika maisha ya Muhammad Mustafa, badala yake, alipanda maua ya waridi ya mapenzi.

Maua hayo kamwe hayakunyau­ka; rangi, harufu na ubichi wao ulikuwa wa daima milele. Kama palikuwepo na ndoa iliyopendeza wakati wote, ndoa hiyo ilikuwa ni ile ya Muhammad na Khadija; ndoa hiyo ilikuwa mpya siku ya mwisho wake kama ilivyokuwa siku ilipoanza.

Khadija alikuwa hai moyoni mwake daima milele. Jina la Khadija lilikuwa mdomoni mwake wakati wote, na mapenzi ya Khadija yalijaa moyoni mwake. Hata kuzungumza juu yake na kumsifu kulimfanya Mtume afurahi.

Kila neno na tendo la Khadija lilidhihirisha busara zake. Katika kuch­agua mume wake, alionyesha uwezo wa kushangaza na wepesi wa kuelewa wa hali ya juu. Lakini uwezo na wepesi wa kuelewa ni vipaji ambavyo wanawake wengine vile vile wanaweza kuwa navyo, na Khadija hakuwa mwanamke pekee aliyepewa vipaji hivi. Maelezo kuhusu uamuzi wenye msukumo wa kimungu uliofanywa na Khadija kukubali kuolewa na Muhammad Mustafa ni kwamba kulifanywa chini ya mwongozo wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Mwenyewe. Kwa hiyo, hangeamua vibaya. Alipokutana na Muhammad, Mtume mteule, Khadija aliona Utukufu kwa mbali sana ndani yake, na alikabidhi hati­ma yake kwenye mikono yake iliyobarikiwa. Mikono hiyo ilinyanyua hatima yake, na kuifanya tukufu.