read

Sura Ya 17: Khadija Na Wake Wenza Wa Mtume (S.A.W.W)

Jambo la kushangaza ni kwamba wanawake wote wa nyumba ya Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, walikuwa na udhaifu kama ilivyo kwa wanawake wengine. Wake zake wengine wal­isumbuliwa na wivu, na hawakuwa na haya kabisa kuuonyesha (huo wivu). Tukio kuhusu “asali” litadhihirisha jambo hili.

Mmojawapo wa wake zake Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikuwa Zainabu binti Jahash. Alijua kwamba mume wake alikuwa anapenda asali. Kwa hiyo alifanya mpango wa kuwa nayo aina hiyo ya asali. Ilitokea kwamba Zainabu alikuwa na sura nzuri kuliko wake wengine wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Alimtilia maanani sana. Hali hii ilis­ababisha wasiwasi kwa Bi Aisha binti Abu Bakr, mke mwingine wa Mtume. Aisha aliogopa isije mapenzi ya mume wake yakaelekezwa yote kwa Zainabu na kuwabagua wake wengine. Kwa hiyo, Aisha binti Abu Bakr na Hafsa binti Umar, mke wa tatu wa Mtume, walifanya mpango ambao madhumuni yake ilikuwa kumfanya mume wao achukie asali.

Sehemu nyingine ya Hadithi anasimulia Aisha mwenyewe. Imam Bukhari amemnukuu kwenye Kitabu chake cha Talaq (Talaka) na Kitabu cha Tafsiri (ya Sura ya Tahreem) kama ifuatavyo:

"Mimi na Hafsa tulibuni mpango huu kwamba wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu akimtembelea yeyote kati yetu, amwambie kwamba mdomo wake unanuka uvundo wa maghafir (Maghafir ina ladha tamu lakini inayo harufu mbaya. Muhammad Mustafa alikuwa hapendi jambo hili. Alikuwa hapendi harufu kali).

Ilitokea kwamba Hafsa alikuwa mke wa kwanza kutembelewa baada ya kubuniwa mpango huu. Mara Mtume alipoingia chumbani kwake alisema: "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Mdomo wako unanuka harufu ya Maghafir, "Alisema: "Sijala Maghafeer. Lakini nilipokuwa na Zainabu, alinipa asali nikala. Inawezekana kwamba asali ilikuwa na harufu ya maghafeer. Lakini, sitakula asali tena."

Hapa wake wa Muhammad Mustafa Aisha na Hafsa wanaonekana wanafanya hila dhidi ya mke wa tatu - Zainabu. Zainabu alikuwa hajafanya lolote baya kwa Aisha na Hafsa. Alikuwa binamu wa Mtume, Zainabu akimuona Mtume ni mtoto wa mjomba wake (anayezaliwa na mama yake).

Zainabu alimpenda mumewe naye mume alimpenda mke wake. Mke alijua vitu avipendavyo na avichukiavyo mume wake; kati­ka hali hiyo, alikuwa na aina fulani ya asali chumbani kwake ambayo alijua ni kitu anacho kipenda.

Mapenzi ya Muhammad kwa Zainabu yaliwasha miale ya wivu moyoni mwa Aisha. Ili kutuliza wivu huo, alitumia mpango akiwa pamoja na Hafsa dhidi ya Zainabu na kuutimiza. Ni dhahiri kwamba hawa wanawake wawili hawakumwamini mume wao katika kuwatimizia haki zao jinsi inavyopasa. Walifikiri kwamba Zainab anapendelewa na wao wanasahauliwa. Kama wangekuwa wanamwamini, hawangebuni mpango huo.

Abul Kalim Azad anasema kwamba wivu ni silika ya wanawake, na inaweza kuzielemea silika zingine zote walizo nazo. Anasema, Aisha, aliongozwa na silika hii ya kibinadamu kwa lengo la kutunga hila hara­ka haraka ambayo ingemfanya mume wao atumie muda mfupi kuwa na Zainabu kuliko alivyokuwa anafanya.

Muhammad Mustafa aliwaambia Aisha na Hafsa kwamba hangekula asali tena. Tamko hili liliwafurahisha wote wawili kwa sababu labda waliamini kwamba mpango wao ulikwisha fuzu. Lakini, hapohapo Ufunuo uliingilia kati na kulikemea jambo hilo kwa aya ifuatayo:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ لِمَ تُحَرِّمُ مَا أَحَلَّ اللَّهُ لَكَ ۖ تَبْتَغِي مَرْضَاتَ أَزْوَاجِكَ ۚ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {1}

"Ewe Nabii! Kwa nini unaharamisha alicho kuhalalishia Mwenyezi Mungu? Unatafuta kuwaridhisha wake zako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Qur'an 66:1).

Hadhrat Aisha na Hafsa hawakutaka mume wao ale asali, na alikubali kwamba hangefanya hivyo, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) Mwenyewe alimkumbusha yeye kwamba ni halali kabisa kula asali na kwamba asi­jinyime raha ya kula kitu hicho.

Muhammad Mustafa kama ilivyokuwa kawaida, alirudi chumbani kwa Zainabu na alifurahia kula asali kama alivyofanya kabla ya tukio hilo.

Maria Mkipt

Mnamo mwaka wa 10 A.H. gavana wa Misri, alimpeleka mtumwa mwanamke aitwaye Mariya Mkipt, kwenda Madina kama mjakazi kum­tumikia Muhammad Mustafa. Baada ya muda mfupi Mariya alipata fursa ya kupendwa na kukaa nyumbani mwake Mtume. Alimpenda na yeye alimpenda. Mary alizaa mtoto wa kiume aliyeitwa Ibrahim. Ibrahim alizaliwa wakati wa mwisho wa uhai wa baba yake. Baba yake, alimpenda sana.

Ibrahim alikuwa zawadi maalum ambayo Mwenyezi Mungu aliwapa watumishi wake, Muhammad Mustafa na Maria Mkipt.

لِلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ يَهَبُ لِمَنْ يَشَاءُ إِنَاثًا وَيَهَبُ لِمَنْ يَشَاءُ الذُّكُورَ {49}

أَوْ يُزَوِّجُهُمْ ذُكْرَانًا وَإِنَاثًا ۖ وَيَجْعَلُ مَنْ يَشَاءُ عَقِيمًا ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ قَدِيرٌ {50}

"Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anam­tunukia amtakaye watoto wa kiume na wakike na akamfanya amtakaye tasa." (Qur'an 42: 49-50).

Muhammad Mustafa na Maria Mkipt walibarikiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuzaliwa mtoto wa kiume, Ibrahim. Walimshukuru yeye kwa baraka kubwa iliyojaza furaha maisha yao na nyumba yao.

Lakini kuzaliwa kwa Ibrahim halikuwa tukio la kufurahisha kwa wake wengine wa baba yake.

D.S. Margoliouth

Miaka ya mwisho ya uhai wake, Mtume ilichangamshwa kwa kipindi fulani kwa kuzaliwa mtoto wa kiume ambaye mama yake alikuwa Maria Mkipt ambaye alimuita kwa jina la Ibrahim muasisi wa kubuniwa (sic) wa dini yake. Mama huyu baada ya kufanyiwa wivu mkubwa sana na wake zake wengine ambao walikuwa hawana watoto, tukio hili lenye kheri liliwasababishia maumivu makali ndani ya mioyo yao, ambayo yalipunguzwa haraka na kifo cha mtoto Ibrahim (ambaye aliishi miezi kumi na moja tu).

(Muhammad and the Rise of Islam, London)

Mmojawapo wa wake zake Mtume ambaye kuzaliwa kwa Ibrahim kulimuumiza sana moyo wake, alikuwa Bi Aisha. Bi Aisha bila shaka alikuwa na wivu dhidi ya Maria -mke mwenza mpya, na alimchukia.

Bahati mbaya chuki yake haikuelekezwa kwa Maria peke yake; chuki hiyo ilivuka mpaka na kuelekezwa kwa mtoto wake mchanga. Aisha alimchukia Ibrahim. Haikupata kutokea kwamba angempenda Ibrahim, si tu kwamba alikuwa kipenzi cha Mtume, lakini pia kwamba alikuwa mtoto mchanga. Lakini kama Aisha alikuwa hawezi kujizuia kuona wivu na chuki na alishindwa kuonyesha mapen­zi kwa mtoto huyo, angalau angejifanya kumpenda, kumfurahisha tu baba yake. Lakini Aisha hakuweza hata kufanya hivyo.

Aisha hakuweza kuonyesha mapenzi yoyote kwa Ibrahim, hata kwa ajili ya kujionyesha tu. Lakini kuna jambo moja ambalo angeweza kulifanya na hilo ni kujizuia kuonyesha hasira kwa mtoto huyo.

Ni jambo la kushangaza kwamba ambapo Aisha alikuwa amejaa hisia za chuki, wivu na kumkataa mtoto huyo, anaonyesha alikuwa hana upole ambao ni tabia ya wanawake duniani pote. Hakuonyesha upole wowote.

Kwa jambo la watoto, na hasa zaidi watoto wachanga hata mwanamke katili huonyesha upole kwao. Lakini si Aisha. Pamoja na kwamba hakuonyesha upole kwa mtoto mpendwa wa mume wake, alimtolea maneno ya kashfa. Hata hivyo Ibrahim hakuishi muda mrefu. Alifariki akiwa mchanga.

Muhammad Husayn Haykal.

"Wakati Maria alipomzaa Ibrahim, tukio hilo lilileta furaha kubwa kwa Muhammad, mtu ambaye umri wake ulizidi miaka sitini. Kwa sababu ya kuzaliwa kwa mtoto, nafasi ya mama yake - Maria pia ilipanda dara­ja. Muhammad sasa alimuona Maria kama mke mweye uhuru, hakika kama mtu anayefurahia nafasi iliyopendelewa sana.

"Ilikuwa ni kitu kisichoepukika kwamba kuzaliwa kwa Ibrahim kunge­washa moto kubwa wa wivu kwenye mioyo ya wake wengine wa Muhammad ambao wote walikuwa wagumba. Pia ilikuwa jambo la kawaida kwamba mapenzi ya Mtume kwa mtoto mchanga na mama yake, yaliongeza nguvu za wivu.

Muhammad alimkarimu kwa kumpa zawadi Salma, mke wa Abu Rafi, na yaya wa Ibrahim. Pia aligawa nafa­ka kwa fukara wote Madina. Alimpa Umm Sayr kazi ya kumlea Ibrahim. Mlezi huyu alikuwa na mbuzi saba na alitakiwa kumpa mazi­wa mtoto.

Muhammad alikwenda nyumbani kwa Maria kumuona mwanae kila siku na kumpakata mikononi mwake. Yote haya yali­chochea wivu miongoni mwa wake wengine waliokuwa wagumba. Swali ni kwamba hadi lini hawa wake wenza wa Maria wangeendelea kuvumilia machungu hayo.

"Siku moja, baba mpya mwenye fahari, Muhammad Mustafa aliingia chumbani kwa Aisha akiwa amembeba mtoto wake wa kiume mikononi mwake ili amwonyeshe Aisha. Alimwambia Aisha jinsi mtoto huyo alivyofanana naye mno. Aisha alimwangalia mtoto na alisema kwamba hakuona mfanano wowote naye. Mtume alipoonyesha furaha jinsi mtoto wake alivyokuwa anakua, Aisha alijibu kwa ukali kwamba mtoto yeyote akipewa kiasi cha maziwa anayopewa Ibrahim, angekuwa na mwili mkubwa na mwenye afya nzuri na nzito kama alivyo Ibrahim. Kweli kuzaliwa kwa Ibrahim ilikuwa sababu ya wake wenza wa Maria kuumia mioyo yao, hivyo kwamba walizidi kutoa majibu yenye kuumiza.
Hali hii ilifika kiwango ambacho Qur'an iliingilia kati kulaani. Bila shaka suala lote hili lilitia doa maisha ya Mtume pamoja na histo­ria ya Uislamu.

"Kwa kuwa Mtume alikuwa anawapa wake zake haki maalum na upen­deleo, wakati ambapo wanawake wa Arabuni walikuwa hawana thamani kabisa katika jamii, ilikuwa ni jambo la kawaida kwao kutumia vibaya uhuru ambao wenzao hawakupata kufurahia kabla yao.

Uhuru huu uli­wafanya baadhi yao kumlaumu Mtume mwenyewe kwa ukali sana, kiasi cha kuvuruga mipango yake ya siku nzima. Mara nyingi hakuwajali baadhi ya wake zake, na aliwaepuka wengine kwa lengo la kuwazuia wasiendelee kutumia vibaya upendeleo waliopewa. Hata hivyo, mmoja wao alisongwa sana na wivu wake hadi akavuka mipaka yote ya staha. Lakini, Maria alipojifungua mtoto, Ibrahim, hawakuwa watulivu na walishindwa kujizuia.

Ilikuwa kwa sababu hii Aisha alikataa kwamba mtoto Ibrahim hakufanana na baba yake, kukataa ambako ni sawa na shutuma ya zinaa kwa masikini Maria asiye na hatia."

(The Life of Muhammed, Cairo, 1935)

Mwenyezi Mungu alimwokoa mtumishi Wake mpendwa, Khadija kuto­ka kwenye maudhi ya kulazimishwa na mila na desturi za nchi, kushirikiana kumuangalia na mapenzi kwa mume wake na wake zake (Mtume) wengine. Lakini kama alikuwa na mke mwenza angemfanya­je? Angekuwa na wivu dhidi yake? Kamwe. Kwa Khadija, wivu ulikuwa mbali sana naye kama ambavyo nguzo huachana. Hangewachukia wake wenzake au mke mwenzake. Wakati wa uhai wake hakumchukia jirani yake, mtumishi au mtumwa. Hakuwachukia hata wanyama, wala binadamu yeyote. Khadija alipita kwenye maisha akiwa ameneemeshwa sifa za kimalaika.

Baada ya kifo cha Khadija, Muhammad Mustafa alioa wanawake wengi. Lakini hakuna hata mmoja wao ambaye angeweza kulingana na Khadija kwa ubora. Miongoni mwao walikuwepo wanawake wenye historia tofauti tofauti, na walitoka kwenye tabaka mbalimbali za tabia. Inaonyesha baadhi yao kamwe hawakujua kwamba mume wao ni mteule wa Mungu Mwenyewe, na alikuwa na daraja na hadhi isiyoweza kufikiwa na binadamu mwingine yeyote.

D.S. Margoliouth

Ukaaji wa wake zake Mtume nyumbani mwake ulikuwa wa muda mfupi, kwa sababu ya tabia mbaya, ilitokea mara moja au zaidi ambapo wake zake Mtume wapya walifundishwa na wake wenzao wenye wivu misemo ya Mtume ambayo kwa ujinga wao waliitamka vibaya, jambo ambalo lilimfanya awafukuze (awataliki) bila kukawia. Mmoja wao ali­talikiwa kwa sababu ya kutangaza baada ya kifo cha Ibrahim kwamba kama baba yake angekuwa Mtume, hangefariki - matumizi ya ajabu ya "uwezo wa kuhoji".

(Muhammed and the Rise of Islam, London)

Kwa Muhammad Mustafa, tabia ya baadhi ya wanawake aliowaoa huko Madina, ilionekana kama vile ni utumbuizo mgeni kwa mwenendo wa Khadija. Mwenendo wa Khadija ulikuwa mzuri na mwepesi. Kila neno na tendo lake limepatana na lengo lake la kujaza furaha kwenye nyum­ba ya mume wake, na aliweza kufaulu kutambua hilo.

Muhammad Husayn Haykal wa Misri na Abul Kalam Azad wa India wamewanukuu wakusanyaji na wafafanuzi wa Hadithi ile isemayo kwamba Hadhrat Abu Bakr na Hadhrat Umar wakati fulani waliomba ruhusa ya kumuona Mtume.

Walipoingia nyumbani kwake walimkuta amekaa kimya, na kuzungukwa na wake zake. (wanawake hawa walikuwa wanadai fedha nyingi zaidi kutoka kwa mume wao, kwani walisema kwamba hawangeweza kuishi kwenye umasikini). Umar alisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kama binti yangu alionekana au alisikika ananiomba fedha, kwa hakika ningezivuta nywele zake. "Mtume alicheka na kusema: "Hawa hapa wake zangu wamenizunguka na wananiomba fedha." Haraka Abu Bakr alinyanyuka na kuzivuta nywele za binti yake, Aisha; na Umar naye alifanya vivyo hivyo kwa binti yake Hafsa. Wote wawili Abu Bakr na Umar wali­waambia mabinti zao: "Mnathubutu kumuomba Mtume wa Mwenyezi Mungu kile ambacho hawezi kuwapeni?"
Walijibu: "La! Kwa jina la Mungu sisi hatumuombi kitu cha namna hiyo."

"Ilikuwa ni kuhusu mazungumzo haya baina ya Abu Bakr na mabinti zao;" anasema Muhammad Husayn Haykal, "kwamba Aya zifuatazo ziliteremshwa."

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لِأَزْوَاجِكَ إِنْ كُنْتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا {28}

وَإِنْ كُنْتُنَّ تُرِدْنَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنْكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا {29}

"Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya duni­ani na pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano mzuri." (Qur'an 33: 28, 29)

Ingawa inawezekana wake zake Mtume waliungana katika kudai fedha zaidi kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine muhimu kutoka kwake.

Aisha na Hafsa walikuwa wanadai kwa nguvu zaidi. Abdullah bin Abbas anasema kwamba wakati fulani alimuuliza Umar ibn al-Khattab ni nani kati ya wake zake Mtume ambao walikuwa wanasisitiza kudai fedha kutoka kwa mume wao, na alisema: "Aisha na Hafsa."

Mtume mwenyewe aliishi maisha ya kujinyima.Mara nyingi aliwahudu­mia kwanza masikini na wenye njaa ndipo akajihudumia yeye. Mfumo wa maisha yake waliokuwa wanaujua zaidi kuliko mwengine yeyote ni wake zake.

Kwa hiyo, walipomwambia kwamba maisha yalikuwa magumu kwa upande wao na kwamba alikuwa anatakiwa kupunguza ukali wake kwa kuwaongezea fedha, alishangaa. Alidhani labda wake zake wangemuiga yeye, na wangeishi maisha ya kujinyima sana kama yeye. Kwa hiyo aliona kwamba madai yao ya pamoja yalimshtua sana; alidhani labda yalichochewa na tamaa kubwa ya chakula na anasa zitokanazo na mali.

Abu Kalam Azad anasema kwamba, wake zake Mtume, hata hivyo, walikuwa binadamu, na wao pia walikuwa na mahitaji na matamanio ya kibinadamu. Kwa hiyo madai yao, yanaeleweka.

Hata hivyo, Mtume, hakufurahishwa na walivyofanya wake zake kwa hiyo alijitenga nao kwa mwezi mmoja.

Muhammad Huseyn Haykal

"Muhammad alijitenga na wake zake kwa mwezi mmoja na hakutaka kusema chochote kwa yeyote kuhusu wao. Wala hakuna mtu yeyote aliyethubutu kusema lolote kwake kuhusu wake zake.

Abu Bakar, Umar, na wakwe zake wengine pia walikuwa na wasiwasi sana kuhusu hatima yao ya kusikitisha iliyokuwa inawangojea "Mama wa Waumini" kwa kuwa sasa walijionyesha kwenye ghadhabu ya Mtume, na matokeo ya kuadhibiwa na Mungu. Hata hivyo ilisemekana kwamba Muhammad alimtaliki Hafsa, binti ya Umar, baada ya kutoa siri aliyoahidi kutoi­fichua.

Habari zilienea kwenye soko la Madina kuhusu kutalikiwa kwa wake zake Mtume. Kwa upande wao wake zake walitubu na kujaa hofu. Walijuta kwamba kuoneana wivu wao kwa wao iliwaelemea na kwam­ba walimtukana na kumkasirisha mume wao. Muhammad alitumia muda wake mwingi akiwa ndani ya nyumba ya stoo aliyokuwa anaimi­liki, ambapo alimweka mtumishi wake Rabah mlangoni kwa muda wote aliokuwa ndani. Ndani ya stoo alikuwa analala juu ya kitanda kigumu sana cha matawi makavu ya mtende.

(The Life of Muhammed, Cairo, 1935).

Baadhi ya wake zake Mtume walijionyesha wenyewe kuwa na wasi wasi sana. Wasiwasi wao usingemfanya kuwa na furaha sana katika maisha yake ya ndoa.

Profesa Margoliouth amenukuu Musnad ya Imam Ahmad bin Hanbali (Vol. IV, P. 221) kuhusiana na jambo hili, kwenye kitabu chake "Muhammad and the Rise of Islam kama ifuatavyo":

"Wakati wa usiku wa manane, yasemekana Mtume alitoka na kwenda makaburi ya Al-Baqi, na akawaombea msamaha wafu waliozikwa pale. Ni kweli kwamba aliwahi kufanya hivyo siku za nyuma; ambapo Aisha alimfuata nyuma kama mpelelezi alipoanza safari yake, akidhani kwam­ba alikuwa ameshawishiwa na baadhi ya mapenzi; lakini aliona kwam­ba mwisho wa safari yake ilkuwa ni makaburini."

Sura ya 66 ya Quran Majid iitwayo Tahrim, inazungumzia zaidi suala la tabia za wake zake Mtume. Mojawapo ya Aya zake imenukuliwa hapo juu kuhusu tukio la "asali." Aya zake za 4 na 5 zinasomeka ifuatavyo:

"Kama nyinyi mtatubia kwa Mwenyezi Mungu (Basi inataka mfanye upesi upesi) kwani nyoyo zenu zimemili upande kidogo. Na kama mtasaidiana juu yake (Mtume kumuudhi kwa mambo ya nyumbani, Mwenyezi Mungu atakuwa naye juu yenu.) kwani Mwenyezi Mungu ni kipenzi chake na Jibrili na waislamu wema wote; na zaidi ya hayo malaika pia watasaidia. (Mtume) akikupeni talaka, Mola wake atampa, badala yenu, wake wengine walio bora kuliko nyinyi;…. (Quran 66:4-5)

Hakuna makubaliano ya wafafanuzi wa Qur'an Majid na wanataaluma wa historia kuhusu tukio mahsusi linalorejewa kwenye Aya hizi mbili. Wengine wanasema kwamba Mtume alimwambia Hadhrati Hafsa jambo la siri kwa sharti kwamba hangelifichua. Hata hivyo, hakuweza kuificha siri hiyo na aliitoa kwa Hadhrati Aisha. Kukiukwa kwa uaminifu ndiko kuliko sababisha kemeo lililopita juu ya mmoja wao kwa ajili ya "kusal­iti amana, na juu ya wengine kwa ajili ya kuutia nguvu usaliti," Hivyo, "kusaidia kosa la kila mmoja wao."

Akizielezea aya za Sura ya 66 ya Qur'an Majid, A. Yusuf Ali, mfasiri na mfafanuzi wake anaandika ifuatavyo: "Nyumba ya Mtume haikuwa kama nyumba nyingine. Wake wenza watakatifu walitakiwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha tabia na unya­mavu kuliko wanawake wa kawaida, kwani wao walikuwa na kazi kubwa ya kufanya.

Lakini, hata hivyo, wao walikuwa binadamu na walikuwa na udhaifu wa jinsia yao, na wakati mwingine walishindwa kufikia kiwango cha kuridhisha.

Ujinga wa Hadharti Aisha wakati fulani ulisababisha matatizo: Akili ya Mtume iliudhika mno na hakuta­ka kukutana na wake zake kwa kipindi fulani.Hafsa, binti ya Hadhrati Umar wakati mwingine alikuwa mwepesi wa kutumia vibaya nafasi yake, na hao wawili walipokutana na kushauriana kwa siri, na kuzungumza na kufichua siri zao, walisababisha huzuni kubwa kwa Mtukufu Mtume ambaye moyo wake ulikuwa mwema na aliyeifanyia familia yake yote matendo mema kwa uvumilivu na huba ya mfano wa kuigwa.