read

Sura Ya 18: Khadija Na Aisha

Hadhrat Aisha hakuwaonea wivu wake wenzake aliokuwa anaishi nao tu nyumbani kwa Muhammad Mustafa, bali pia mke mwenzake ambaye alikwisha fariki muda mrefu - yaani Khadija. Hakika alikuwa ana­muonea wivu zaidi Khadija, kuliko mke mwenzake yeyote aliye hai. Alimuonea Khadija wivu mwingi mno hivyo kwamba alikuwa na des­turi ya kutamka makaripio makali dhidi ya jina lake.

Abbas Mahmud al-Akkad anasema kwenye kitabu chake, "Aisha":

"Aisha hakuonyesha hisia kali kiasi hicho cha wivu kwa mke mwenza­ke yeyote isipokuwa Khadija. Sababu yake ni kwamba Khadija alik­wisha jitengenezea nafasi yake moyoni mwa mume wake ambayo haku­na yeyote awaye angeweza kuichukua. Muhammad Mustafa alikuwa anazikumbuka sifa za Khadija usiku na mchana.

Muhammad Mustafa wakati wote alikuwa anawasaidia masikini na wagonjwa. Wakati fulani, Aisha alimuuliza mume wake sababu ya kufanya hivyo, alisema: "Khadija aliniambia niwafanyie wema na mapenzi watu hawa. Hili lilikuwa tamanio lake la mwisho."

Aisha aliposikia hivi, alilipuka kwa hasira na kung'aka: "Khadija! Khadija! Inaonyesha kama vile kwako wewe hakuna mwanamke mwengine hapa duniani isipokuwa Khadija."

Mtume alikuwa mtu mwenye uvumilivu mwingi mno. Lakini baada ya Mtume kusikia kauli ya ukali ya Aisha, aliacha kuzungumza naye.

Kama tukio hili linaonyesha jinsi Khadija alivyokuwa anawapenda masikini na wagonjwa, inaonyesha pia jinsi Mtume alivyokuwa anam­tukuza. Muhammad Mustafa alifanya kufuatana na matakwa yake (Khadija) bila kujali chuki ya wazi ya Aisha kwa mke mwenzake. Kwa hakika, alifanya mambo kufuatana na matakwa ya Khadija kipindi chote cha uhai wake. Je! Hakujua kwamba kumbukumbu yoyote ya Khadija ilimkasirisha Aisha? Bila shaka alijua.

Kwa hiyo alipomuuliza, kwanini alikuwa anawalisha masikini, anawapa nguo wasio na nguo na kuwali­waza wenye huzuni, angempa jibu la "tahadhari kubwa" ambalo halingechochea hasira zake. Lakini Mtume hakufanya hivyo. Alitoa jibu la kweli. "Ninatekeleza matakwa ya Khadija."

Je, hii ilikuwa ni sadfa kwamba fikira ya mwisho aliyokuwa nayo Khadija hapa duniani ilikuwa ustawi wa masikini, wagonjwa, mayati­ma, wajane na wasiojiweza? Hapana. Hakuna sadfa kuhusiana na hilo. Kila kitu alichofanya au alichosema Khadija, ilikuwa mpango uliok­wisha tayarishwa kwa lengo la kumfurahisha Mwenyezi Mungu. Na ali­tambua kwamba angefuzu kupata radhi ya Mwenyezi Mungu kwa kuwapenda na kuwatumikia wenye kuhitaji msaada miongoni mwa waja wake wanyenyekevu.

Zawadi ya Khadija ilikuwa kuwafikia wenye njaa, masikini na wag­onjwa hata baada ya kifo chake. Msaada wake haukukoma wakati alipokuwa hai na alipofariki!

Jina na sura ya "Khadija vilichorwa moyoni mwa Muhammad Mustafa, na wala si mwenendo wa wakati au ghadhabu za Aisha zingeweza kufu­ta.

Hadhrat Aisha alitambua kwamba hangeweza kumshawishi Muhammad Mustafa asiendelee kumsifu Khadija na kuzungumza habari zake. Lakini utambuzi huo haukuwa kizuizi cha kumfanya Aisha aache desturi yake ya kumuonea wivu mke mwenzake (Khadija).

Abbas Mahmud al-Akkad wa Misri, anatoa maelezo kuhusu tukio lingine kwenye kitabu chake, "Aisha," kama ifuatavyo:

Siku moja Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikuwa anamsifu Khadija ambapo Aisha alisema: "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Kwa nini wakati wote unazungumza habari za yule mwanamke mzee ambaye ana ufizi uliovimba? Hata hivyo, Mwenyezi Mungu amekupa wanawake wazuri zaidi kuliko yeye." Muhammad Mustafa alisema: "Hapana Aisha! Mwenyezi Mungu kamwe hajanipa mke bora zaidi ya Khadija. Aliniamini wakati ambapo watu wengine walinikana. Alinipa utajiri wake wote ambapo watu wengine hawakufanya hivyo. Na zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu alinipa watoto kupitia kwa Khadija tu."

Inaonyesha kwamba chuki ya Aisha kwa Khadija ambaye aliidhihirisha mno ilimrudia yeye.Mume wake alimwambia kwamba Mwenyezi Mungu alinipa watoto kupitia kwa Khadija tu ambapo wake zake wengine hawakuweza kumpa mtoto yeyote yule.

Kuishi bila mtoto ni hali inayomuumiza sana mwanamke. Lakini aki­ambiwa kwamba yeye ni mgumba, maumivu yale hugeuka kuwa mate-so. Na kama ni mume wake mwenyewe ndiye anayemdhihaki kuhusu ugumba wake, basi maumivu hayo yanakuwa machungu.

Lakini Aisha hakuweza kuacha kumchukia Khadija. Yeye mwenyewe alisema wakati fulani; "Sijamwonea wivu mwanamke yeyote kwa kiwango ambacho nina muonea Khadija." Alionyesha wivu wake mara kwa mara na kila alipofanya hivyo alishawishi hasira ya aina ile ile kuto­ka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Mtoto wa mwisho wa Muhammad Mustafa na Khadija alikuwa binti yao, Fatima Zahra. Alizaliwa mnamo mwaka wa tano wa tangazo la Uislamu na miaka minane kabla ya Hijiriya. Kaka zake, Qasim na Abdallah, walifariki kabla yake. Ilikuwa ni ridhaa ya Mwenyezi Mungu kwamba nasaba ya Mjumbe Wake na rafiki, Muhammad Mustafa, ianzie kwa binti yake, Fatima Zahra. Fatima alikuwa furaha ya moyo wa baba yake, na mwanga wa macho yake. Alimtunza binti yake na wototo wake kama hazina zake kubwa sana. Kwake yeye, walikuwa, mfano wa fura­ha iliyotakasika - hapa duniani na Akhera.

Mara kwa mara Muhammad Mustafa alisafiri nje ya Madina kwa ajili ya kutangaza Uislamu. Ilikuwa ni kawaida yake kutanguliza jeshi lake, na yeye alikuwa wa mwisho kuondoka jijini.

Pia ilikuwa ni kawaida ya Muhammad Mustafa kwamba jambo la mwisho alilolifanya kabla ya kutoka Madina ilikuwa kwenda kwa binti yake, Fatima Zahra, aliye barikiwa na watoto wake. Alimkabidhi Mungu awape ulinzi na kuwaaga.

Kitu cha kwanza alichofanya Muhammad Mustafa aliporudi Madina, ilikuwa kwedwa nyumbani kwa binti yake. Alimuomba Mungu ambari­ki yeye na familia yake. Wakati wa safari zake nje ya Madina, hakuna alichokikosa mno kama watoto wa binti yake. Alipowaona, alisalimiana nao, aliwabusu, aliwabeba na kucheza nao. Siku moja alikuwa nao, basi uchovu kutokana na mwendo mrefu kwa miguu kwenye vumbi na joto la Arabia, ulitoweka, na hali yake kurudi kuwa ya kawaida.

Huu ulikuwa mpangilio wa maisha ya Muhammad Mustafa, na kamwe hakubadili. Maisha ya hisia zake yalizunguka nyumba ya binti yake.

Hadhrat Aisha hakushiriki kumpenda binti ya Mtume kama alivyofanya baba yake. Abbas Mahmud al-Akkad anasema kwenye kitabu chake, "Aisha":

Kwanza kabisa, Fatima alikuwa mtoto wa Khadija; na Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alimpenda Khadija sana hivyo kwamba wakati wote alikuwa anamsifia na kumpongeza. Aisha hakupenda hivyo. Kwa upande wa pili Aisha alikuwa hana mtoto. Wakati wowote alipomuona mume wake anacheza na watoto wa Fatima, alizidi kupata uchungu wa maumivu ya kukumbushwa kwamba yeye alikuwa mgumba. Uhusiano wa Aisha na Fatima haukuwa na huba.