read

Sura Ya 19: Khadija Na Uislamu

Leo hii Uislamu ni jeshi lenye nguvu kubwa kabisa duniani. Maadui wake hawawezi kufanya lolote. Uislamu ni kama gogo la mti mkubwa, ambalo dhoruba za duniani zimeshindwa kuling'oa. Hata hivyo, kuna wakati ambapo gogo hili kubwa sana lilikuwa mti mchanga, ambao uli­hitaji mtu wa kuulinda kutoka kwenye vimbunga vya waabudu masana­mu na ushirikina ambavyo vilitishia kuung'oa.

Waislamu wanaweza wakasahau lakini Uislamu hautasahau kwamba wakati wa uchanga wake, ilikuwa Abu Talib na Khadija walioulinda. Waliufanya Uislamu usidhurike. Abu Talib aliulinda uchanga wa Uislamu usidhuriwe na tufani ya wasioamini na upagani; na Khadija aliumwagilia Uislam maji ya utajiri wake. Khadija hakuruhusu Uislamu mchanga ufe. Hakika Khadija hakutaka hata kuruhusu Uislamu udhoofike kwa sababu ya uzembe. Kwa Abu Talib na Khadija, kazi yao kubwa sana ilikuwa kuulinda Uislamu. Walipenda Uislamu, na wali­yarithisha mapenzi hayo kwa watoto wao.

Kama Abu Talib na Khadija waliulinda Uislamu usidhuriwe na maadui wakati wa uhai wa Muhammad Mustafa, na wakauimarisha kwa kutumia dhahabu na fedha nyingi, watoto wao na wajukuu wao waliulinda usidhuriwe na maadui baada ya kifo chake, na waliuimarisha kwa kumwaga damu yao. Damu yao ilikuwa Takatifu sana kuzidi yeyote katika Uumbaji wote. Hata hivyo, hiyo ilikuwa damu ya Muhammad Mustafa mwenyewe - Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, wa Mwisho na Mkubwa kuliko Mitume wote.

Khadija alikuwa shahidi aliyeona kwa jicho lake Uilsamu ulipozaliwa. Aliutunza katika kipindi chake cha uchanga, wakati wa matatizo makubwa sana, na wakati wa ukuaji wake. Uislamu ulipewa umbo na sura ndani ya nyumba yake. Kama kuna nyumba yoyote inayoweza kuitwa mtoto mchanga wa Uislamu, basi ni nyumba yake.

Aliulea Uislamu. Kama nyumba yoyote ile ingeitwa chimbuko la Uislamu, basi ni nyumba yake. Nyumba yake ilikuwa makazi ya Qur'an Tukufu kitabu cha Allah, na chenye Sheria za Kiislamu, za kidini na za Kisiasa.

Ilikuwa ndani ya nyumba yake Hadija ambayo Malaika Jibril alikuwa anamletea Mjumbe wa Allah (s.a.w.w.) ufunuo kutoka Mbinguni kwa kipindi cha miaka kumi.

Khadija amekusanya alama za kwanza nyingi zaidi katika historia ya mwanzo wa Uislamu kuliko mtu mwingine yeyote. Alikuwa mke wa kwanza wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Alikuwa Muumini wa kwanza. Alikuwa binadamu wa kwanza kushahadia kwamba Muumba ni Mmoja tu, na kwamba Muhammad ni mjumbe Wake. Baada ya mume wake alikuwa mtu wa kwanza aliyesikia sauti ya Ufunuo.

Alikuwa mtu wa kwanza kusali sala ya Mwenyezi Mungu akiwa na mume wake. Wakati wowote alipokwenda kumsikiliza Mwenyezi Mungu, Khadija alikuwa karibu naye. Alikuwa wa kwanza kuwa Mama wa Waumini. Alikuwa ndiye mke pekee wa Muhammad Mustafa ambaye hakuishi maisha ya uke wenza. Mapenzi yote na urafiki wote wa mume wake, alipewa yeye peke yake.

Wakati Muhammad Mustafa alipotangaza ujumbe wake kuwa yeye ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na kuwaambia Waarabu waache kuabudu masanamu na aliwaita wakusanyike chini ya bendera ya Tauhid, dhoruba ya mawimbi ya huzuni ilimkabili. Washirika walitaka kumuua. Waligundua namna mpya za kumtesa yeye na walijaribu mara nyingi kumnyamazisha milele. Wakati huo wa shida na dhiki, Khadija alikuwa ngome yake. Ilikuwa kwa sababu tu ya Khadija na Abu Talib, washirikina hawakufanikiwa kuvuruga kazi yake ya kuhubiri na kutangaza Uislamu. Katika hali hii alifanya mchango wake muhimu sana kwa uhai na kutangazwa kwa Uislamu.

Khadija aliiwekea misingi viwango ambavyo vilifanikisha kuwepo kwa amani, uelewano, furaha na utimilifu ndani ya nyumba, na sifa hizo alizishikilia na kuonekana katika maisha yake alitoa mfano kwamba, ufunguo wa nguvu na furaha ya familia ni kiwango cha ukaribu wa huba baina ya wahusika wa familia.

Alionyesha haki na kazi za waume na wake. Viwango vilivyowekwa na yeye vilikuwa ndio rasimu ya maisha ya familia katika Uislamu. Muhammad Mustafa na Khadija walikuwa pamoja kwa miaka ishirini na tano, na katika kipindi hicho walitunga sheria zinazo yafanya maisha ya ndoa kuwa na mafaniko na yenye fura­ha. Tangu hapo dunia imeshindwa kupata sheria bora zaidi ya hizo, hata za kutumia kwa muda mfupi. Uislamu ulijumuisha sheria hizo katika mpango wake.

Khadija aligeuza mawazo ya dhana na kuyaweka katika hali halisi. Maisha yake na Muhammad ni ushahidi madhubuti wa kweli hiyo. Kile alichokipatia dunia haikuwa mpangilio wa misingi au fikira za kinad­haria bali ni uzoefu wa hali halisi yenye nyakati nyingi za furaha iliy­otakasika, ndani ya Uislamu, miitikio stadi ya kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.

Kama ilivyotajwa huko nyuma, Waarabu wapagani walijihisi wame­poteza heshima yao yote. Heshima hiyo ilikuwa ile iliyowalazimisha kuua mabinti zao pindi wazaliwapo. Uislamu ulikataza desturi hii ya kishenzi kwa kuifanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, na kosa la jinai dhidi ya ubinadamu. Mbali ya kukataza kuua watoto wa kike, Uislamu pia umetoa hadhi, heshima na haki kwa wanawake na kud­hamini haki hizo.

Mwenyezi Mungu alitaka kuonyesha kwamba sheria za Uislamu zinatekelezeka. Kuonyesha utekelezwaji wa sheria hizo, na kuonyesha "Mfumo wa Maisha" ya Kiislamu, Aliteua nyumba ya waja Wake, Muhammad na Khadija. Bila Khadija, sheria za Kiislamu zingekuwa hazina maana. Hakika, inawezekana pia kwamba Muhammad Mustafa hangeweza kuzianzisha sheria hizo bila Khadija.

Moja ya Neema kubwa sana Muhammad Mustafa na Khadija waliy­oipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu (S.W.) ni binti yao Fatima Zahra. Kama ilivyo onyeshwa kwenye kurasa za nyuma, Fatima alizaliwa baada ya kufa kaka zake Qasim na Abdullah.

Fatima alikuwa na umri wa miaka mitano tu mama yake alipofariki. Baada ya kifo cha mama yake, Muhammad Mustafa, mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alikuwa baba na mama wa Fatima. Katika kumlea na kumkuza binti yake, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikuwa anaonyesha jinsi sheria za Kiislamu zitumikavyo. Kwa kuwa yeye ni kigezo cha Waislamu wote, wanatakiwa kumuiga katika matendo yake yote. Aliweka upendo mkubwa sana juu yake, na alionyesha heshima kubwa mno kwa binti yake.

Kote Makka na Madina, watu wengi mashuhuri kama vile watoto wa wafalme na viongozi wa makabila yenye nguvu, walikuja kumuona Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Alikuwa hasimami wakati wa kusalim­iana na watu hao.

Lakini kama alisikia kwamba binti yake Fatima Zahra alikuwa anakuja kumuona, alinyanyuka na kwenda kumsalimia, alim­sindikiza na kumuonyesha sehemu ya heshima inayostahili kuketi yeye. Hakupata kuonyesha heshima hiyo kwa mtu yeyote wakati wote kati­ka maisha yake, si kwa mwanaume au mwanamke!

"Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayompa amtakaye; na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu. (Quran 62:4)

Mwenyezi Mungu alimpa Fatima Zahra Ukarimu Wake, binti ya kipen­zi chake na Mjumbe Wake, Muhammad Mustafa.

Alikuwa tu binti wa Khadija, Fatima Zahra, ambaye alipata kupokea sifa kuu za Mbinguni kama isemavyo Qur'an Majid, Sura ya 76 Sura Dahr. Kwa hakika, Sura yote inasema habari zake na familia yake pamo­ja na mume wake Ali bin Abi Talib, watoto wake Hasan na Husain, na mtumishi wake Fizza.

Pia amekuwa fasili ya maandiko yaliyomo kwenye Sura Kauthar (108) "Mwenyezi Mungu alimpa Khadija mkwe ambaye ni Ali bin Abu Talib aliyeitwa baadaye Simba wa Mwenyezi Mungu; "Mkono wa kuume wa Uislamu;" na ngao na kikingio cha Muhammad Mustafa; na Alimpa wajukuu kama Hasan na Husein ambao walikuwa “Wapanda mabega ya Mtume wa Mwenyezi Mungu", na "Viongozi wa Vijana wa Peponi."

Bila shaka Uislamu unamaanisha matendo ya nyumba ya Khadija, na bila shaka Qur'an Majid ni lugha ya familia yake. Binti yake, Fatima Zahra na wajukuu zake, Hasan na Husain, katika kukua kwao wanazungumza Qur'an Majid. Alikuwa na uhusiano ulio sawa kwa Uislamu na Quran kama vile mwanga ulivyo kwa macho, mng'aro kwa lulu na harufu nzuri kwa ua waridi.

Hata lugha yenye msamiati wa kiwango cha juu hushindwa kuzisema au kuzisifia sifa za Khadija. Lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameahidi zawadi zake kwa wapendwa watumishi wake kama Khadija kwenye Aya zifuatazo za Kitabu Chake:

" Hakika wale walioamini na kutenda wema, basi hao ndiyo wema wa viumbe. Malipo yao kwa mola wao ni mabustani ya daima ambayo mito inapita mbele yake, wakae humo milele; Mwenyezi Mungu amewaridhia, nao wameridhika. (malipo) hayo ni kwa yule anayemuogopa Mola wake." (Quran 98:7-8)