read

Sura Ya Kumi: Umar Kusilimu Kwake Kuwa Muislamu - 616 A.D

Tukio lililokuwa kubwa mnamo mwaka wa sita baada ya Wito (Tangazo la Uislamu) ilikuwa kusilimu kwa Umar bin al-Khattab, Khalifa wa baa­daye wa Waislamu. Huyu alikuwa adui mkubwa wa Uislamu, na Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na alikuwa mte­saji mkubwa wa Waislamu. Mwanahistoria wa zama za sasa, Amin Dawidar, anasema kwenye kitabu chake.
Pictures from the Life of the Prophet, kwamba chuki ya Umar kwa Uislamu, na uadui wake kwa Muhammad Mustafa, ililinganishwa tu na chuki na uadui kwao na ule wa mjomba wake, Abu Jahl.

Inasemekana kwamba siku moja Umar aliamua, kwa ghadhabu kali, kumuua Muhammad Mustafa, na kuzima kabisa mwale wa Uislamu. Aliondoka nyumbani kwake akiwa na nia hiyo.

Kama ilivyoonyeshwa huko nyuma, Waislamu wakati huu (mwishoni mwa mwaka wa sita) bado walikuwa ndani ya nyumba ya Arqam bin Abil Arqam wakisali sala ya jamaa. Ndio kwanza walianza kukusanyi­ka wakati mmoja wao alichungulia dirishani, alimuona Umar anakuja akiwa ametoa upanga wake kwenye ala. Katika hali ya mshangao, ali­waambia wenzake alichokiona. Bila shaka, na wao pia walishtuka.

Lakini Hamza ambaye naye alikuwepo ndani humo, aliwahakikishia, na akasema kwamba kama Umar alikua anakuja kwa nia njema, basi haku­na tatizo, vinginevyo, yeye (Hamza) angemuua kwa upanga wake mwenyewe.

Lakini, ilitokea kwamba Umar alikuja kwa lengo la kusil­imu, na alifanya hivyo.

Hadithi inasimuliwa kwamba Umar alikuwa anakwenda Dar-ul-Arqam kwa lengo la kumuua Mtume ambapo mpita njia alimsimamisha, na akamtaarifu kwamba dada yake mwenyewe na mume wake walisilimu, na alimshauri ajisafishe yeye mwenyewe kwanza nyumbani mwake kabla ya kufanya jambo lolote litokanalo na dhana.

Muhammad Husayn Haykal

"Umar alikwenda Dar-ul-Arqam mwenye nia ya kumuua Muhammad na kuwapunguzia Maquraysh mzigo, kurejesha mshikamano wao ulioteketezwa, na kuanzisha tena heshima ya miungu ambayo Muhammad aliikemea vikali. Alipokuwa njiani alikutana na Nuaym bin Abdullah. Baada ya kufahamu madhumuni ya Umar, Nuaym alisema, "Kwa Jina la Mungu, umejidanganya mwenyewe, Ewe Umar! Unadhani kwamba Bani Abd Manaf watakuruhusu uwe hai mara baada ya kumuua Muhammad. Dada yako ni Mwislamu sasa. Kwa nini usirudi nyumbani kwako na kuiweka sawa?"

(The Life of Muhammed, Cairo, 1935)

"Umar alikasirika aliposikia hivyo. Haraka sana alibadili njia na kuelekea nyumbani kwa dada yake ili apeleleze kama madai hayo ni ya kweli. Katika kumjibu, dada yake alimpa jibu la moja kwa moja lakini la werevu."

Muhammad bin Ishaq

Umar alikwenda kwenye mlango (wa nyumba ya dada yake) na wakati huo huo Khabbab (sahaba wa Mtume) alikuwa anasoma Sura: Taha na pale jua litakapopinduliwa. Wapagani walikuwa na desturi ya kuyaita maandishi haya "uchafu." Umar alipoingia ndani, dada yake aling'amua kwamba alitaka kufanya madhara na walificha maandishi hayo waliyokuwa wanayasoma. Khabbab aliingia ndani haraka. Umar ali­uliza maneno gani ya kipuuzi aliyosikia wanasema? Dada yake alijibu kwamba hayo yalikuwa mazungumzo ya kawaida tu kati yao...”

(The life of the Messenger of God)

Umar alipandwa na hasira kwa kile alichodhani ni uwongo, na alimpiga dada yake usoni. Pigo hilo lilisababisha damu kutoka mdomoni mwa dada yake. Umar alitaka kumpiga tena lakini alipoona damu aliacha. Mara alionekana hana hasira, na halafu kwa sauti tofauti kabisa alim­womba dada yake amwonyeshe kile alichokuwa anasoma.

Dada yake aliona mabadiliko kwa kaka yake lakini alisema: "Wewe ni mwabudu masanamu mchafu, na siwezi kukuruhusu wewe kushika neno la Mwenyezi Mungu."

Haraka Umar alikwenda nyumbani kwake, akaoga, akarudi nyumbani kwa dada yake, akasoma maandishi ya Qur'an na halafu akaenda nyum­bani kwa Arqam ambako alishahadia Upweke wa Muumba na Utume wa Muhammad.

Sir William Muir anasema kwamba Umar alisilimu mwishoni mwa mwaka wa sita baada ya kutangazwa kwa Uislamu.

Sir William Muir

Umar alisilimu wakati wa Dhul Hijja, mwezi wa mwisho wa mwaka. Inasemekana wakati huo waumini walifikia wanaume 40 na wanawake 10, au kwa hesabu nyingine; wanaume 45 na wanawake kumi na mmoja.

(The Life of Muhammed, London, 1877)

Umar alikuwa na miaka zaidi ya thelathini aliposilimu.

Muhammad Husayn Haykal

"Wakati huo, Umar bin al-Khattab alikuwa mtu mzima mwenye umri wa miaka kati ya thelathini na thelathini na tano."

(The Life of Muhammad, Cairo, 1935).