read

Sura Ya Kwanza: Makkah Mnamo Karne Ya Sita

Mnamo Karne ya Sita A.D. Makka ilikuwa soko muhimu Arabuni. Mji huu ulikuwa kituo cha kimataifa cha biashara na uchuuzi. Mizigo kuto­ka India yenye bidhaa kama viungo, matunda, nafaka, vyombo vya ufinyanzi na nguo vilikuwa vikiteremshwa kwenye bandari za Yemen na kutoka hapo bidhaa hizo zilibebwa pamoja na zile za Arabu ya Kusini, kama vile kahawa, dawa, manukato na mafuta mazuri kwa kutumia ngamia kwenda Makka, na kutoka hapo kuendelea Syria hadi nchi zili­zozunguka bahari ya kati.

Makkah yenyewe ilikuwa kituo cha misafara mingi ya "udi na ubani" ya Arabuni na "viungo" vya India. Misafara mingine ilipitia Makka na Yathrib wakati inaelekea kaskazini ambako iliungana na misafara ya njia kubwa ya biashara ya hariri toka China.

Misafara kutoka kaskazini, pia ilisimama Makka. Ngamia na farasi wal­ibadilishwa hapo na mahitaji kujazwa tena hapo na halafu misafara huendelea hadi kwenye bandari za kusini ya rasi ya Bahari ya Arabuni.

Aidha, Makka ilikuwa kituo cha kubadilishana mali na bidhaa kwa ajili ya makabila ya Kiarabu yasiyo hamahama na yale yanayo hamahama; na ilikuwa sehemu ya kugawa bidhaa za kilimo na zilizotengenezwa na kupelekwa katikati ya Hijaz.

Makabila hayo yalikuja kutoka mbali katikati ya Arabuni na hata Arabia ya mashariki kwa madhumuni ya kununua bidhaa hizo ambazo zilikuwa hazipatikani nchini kwao. Sehemu kubwa ya biashara hii ya maingiliano ya makabila ilifanyika Makka kwa mfumo wa kubadilishana mali kwa mali.

Makuraishi wa Makka walikuwa kabila muhimu sana kutoka Magharibi ya Arabuni. Wote walikuwa wafanyabiashara wakubwa. Kwa kufanik­isha usafirishaji wa hariri kutoka China, bidhaa kutoka Afrika Mashariki na vitu vya thamani kutoka India - Makuraish walitawala biashara kati ya ustaarabu wa Mashariki na ule wa nchi za Bahari ya Mediterania. Ni dhahiri kwamba sehemu kubwa ya biashara hii ilikuwa ya bidhaa za anasa, lakini bidhaa za kawaida pia zilikuwepo kwenye biashara, kama vile nguo za rangi za zambarau, majora ya nguo, nguo zisizowekwa urembo wa kufuma na zile ambazo ziliwekewa nakshi ya dhahabu, zafarani, melimeli, majoho, mablanketi, mishipi, manukato ya mgando, mvinyo na ngano.

Kwa jinsi hii, uzalishaji, uuzaji, ubadilishaji na usambazaji wa bidhaa, kuliwafanya Makuraishi kuwa matajiri. Lakini palikuwepo na kitu kingine kilichowafanya kuwa matajiri. Al-Kaaba na Jiwe lake Jeusi lilikuwa mashuhuri, vilijengwa mjini Makka. Waarabu walikwenda Makka kuhiji na kuitembelea Al- Kaaba. Kwao Makka ilikuwa takatifu kama vile Jerusalem ilivyokuwa kwa Wayahudi na Wakristo.

Al-Kaaba ilikuwa hekalu kubwa la miungu wa masanamu waliomiliki­wa na koo za makabila mbalimbali ya Kiarabu. Mahujaji walileta sada­ka nyingi na zisizo za kawaida kwa ajili ya kuwafurahisha wale miun­gu-sanamu waliowaabudu. Mahujaji waliporudi makwao, makuhani wa hekalu walichukuwa sadaka zote kuwa mali yao. Misafara ya hija ilikuwa njia moja yenye kuwaingizia mali nyingi sana raia wa Makka.

Hata kama Makuraishi wa Makka wasingejishughulisha na biashara, bado wangenufaika na kutajirika kwa kazi za kutoa huduma mbalimbali ambazo walizifanya kwa kipindi cha mwaka mzima kuhudumia misa­fara ya biashara na mahujaji kutoka Kusini kwenda Kaskazini na kuto­ka Kaskazini kwenda Kusini. Lakini kama ambavyo imekwisha fahamika mwanzoni Makuraishi wengi walikuwa wafanya biashara hodari, kwa hiyo walileta utajiri mwingi Makka kutoka nchi jirani.

Ingawaje wafanya biashara wa Makka walipeleka msafara mmoja tu Syria na mmoja Yemen kwa kipindi cha mwaka mzima, palikuwepo na misafara mingine mingi sana midogo midogo ambayo ilifanya biashara katika sehemu nyingi za ghuba ya Uajemi mwaka mzima. Mingi ya misafara hiyo ama ilianzia humo humo Makka au ilipitia Makka kwen­da sehemu nyingine. Kwa hiyo, kulikuwepo na msongomano mkubwa wa misafara ya biashara Makka.

Misafara ilitofautiana kwa ukubwa. Kuanzia Misafara ya "wenyeji" iliyo na kiasi cha chini kabisa ngamia kumi, mpaka ya misafara ya "kimataifa" yenye wingi wa ngamia kiasi cha kufikia maelfu. Kupanga misafara ya biashara ilikuwa shughuli kubwa katika Bara Arabu.