read

Sura Ya Nane: Kuhama Mara Mbili Kwa Waislamu Kwenda Abyssinia (Ethiopia) (615-616)

Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alishiriki katika huzuni zote na huzuni na maumivu ya mateso ya wafuasi wake ambao walikuwa wakiteswa kwa sababu ya kuamini Tauheed (Upweke wa Mungu) lakini hakuwa na namna ya kuwalinda. Ilipoonekana kwamba vurugu na mateso hayangepungua dhidi ya Waislamu toka kwa wapa­gani, aliwashauri waondoke Makka, wakimbilie Abyssinia nchi iliyokuwa inatawaliwa na mfalme Mkristo, aliyejulikana sana kama mtu muadilifu na mchamungu.

Baada ya ushauri huu, kundi la Waislamu; wanaume kumi na moja na wanawake wanne, waliondoka Makka na wakaenda Abyssinia. Kundi hili lilijumuisha watu kama Uthman bin Affan (Baadaye akawa Khalifa wa Waislamu) na Zubyr bin al-Awwan, binamu ya Mtume. Mtume alim­teua mmoja wa Masahaba wake wakuu, Uthmani bin Mazoon, kama kiongozi wa kundi hili.

Muhammad bin Ishaq

Mtume alipoona mateso ya Masahaba wake na kwamba ingawa yeye aliyakwepa kwa sababu ya msimamo wake kwa Mwenyezi Mungu na ulinzi wa ami wake, Abu Talib, hakuweza kuwapa ulinzi, aliwaambia: "kama mngeondoka kwenda Abyssinia (ni bora zaidi kwenu), kwa sababu mfalme (wa kule) hatavumilia uonevu, na nchi hiyo ni rafiki, hadi hapo Mwenyezi Mungu atakapo waondolea dhiki."

Bila kukawia Masahaba wake walikwenda Abyssinia, wakiogopa wasije wakamkana na kumkimbia Mungu na dini yao. Hii ilikuwa hijira ya kwanza katika Uislamu.

(The Life of the Messenger of God).

Hijra ya kwanza ilikuwa mnamo mwaka wa tano wa Wito (Kutangazwa Uislamu) yaani, 615 A.D.

Mfalme wa Abyssinia aliwakaribisha wakimbizi Waislaamu kutoka Makka kwenye himaya yake. Aliwapa hifadhi, na wakapata amani na salama, na walifurahia uhuru wa kuabudu.

Inasemekana kwamba baada ya kama mwaka mmoja, Waislamu wakim­bizi waliokuwa Abyssinia walisikia tetesi kwamba Maquraysh wa Makka waliukubali Uislamu. Kama ilikuwa hivyo, basi hapakuwepo na sababu ya wao kuendelea kuishi uhamishoni, na wakatamani sana kwenda kwao.

Kwa hiyo, walirudi Makka. Lakini walipokuwa Makka waligundua kwamba si tu kwamba taarifa za kusilimu Maquraysh zilikuwa za uongo bali waliongeza kasi ya kutesa Waislamu. Kwa hiyo, kwa mara nyingine waliondoka Makka lakini si wao tu. Safari hii Waislamu wengine wengi walikwenda nao Abyssinia. Kundi hili jipya lilikuwa na jumla ya watu themanini na tatu (wanaume) na wanawake kumi na nane, wakiwemo wakimbizi wa zamani na wapya; miongoni mwao akiwemo Abdur Rahman bin Auf, Abu Salma Makhzumi na Abdullah bin Masud.

Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alimteua Binamu yake Jaafar bin Abu Talib, kaka mkubwa wa Ali, kuwa kiongozi wa kundi hili.

Hijira ya pili ya Waislamu kwenda Abyssinia ilikuwa mnamo mwaka wa sita baada ya Wito (Kutangazwa kwa Uislamu). Yaani, 616 A.D.

Kuhama kwa Waislamu na kupokewa kwao Abyssinia, kuliwashtua Maquraysh. Walihofia kwamba Waislamu huko Abyssinia labda wangekusanya nguvu ya kupigana au wangepata washirika wapya, na halafu, wangerudi Makka na kuwakabili. Kwa hiyo, ili kuzuia tishio hili lenye nguvu, kama ambavyo waliona, waliamua kutuma ujumbe kwenye baraza la mfalme wa Abyssinia kumuomba awarudishe Waislamu Makka.

Wakimbizi wa kiislamu ambao walitegemea wangeachwa katika hali ya amani, walishangaa na kukasirika kuona ujumbe kutoka Makka unafika Abyssinia ambao uliongozwa na Amr bin Ass. Amr alimletea mfalme na watumishi wake zawadi za thamani ili ajipendekeze nazo kwao.

Mfalme alipowapa nafasi ya kuongea, kiongozi wa ujumbe wa Maquraysh alisema kwamba, Waislamu waliopo Abyssinia hawakuwa wakimbizi waliokimbia mateso lakini walikuwa watoro waliotoroka haki na sheria; na alimuomba awarudishe Makka.

Hata hivyo, mfalme, alitaka kusikiliza maelezo kutoka upande wa pili kabla ya kutoa uamuzi, na alimwita Jaafar bin Abi Talib, kiongozi wa wakimbizi, kujibu mashitaka dhidi ya Waislamu.

Jaafar alitoa utetezi usio sahaulika. Ifuatayo ni hotuba yake ikijibu maswali yaliyo ulizwa na mfalme Mkristo wa Abyssinia.
"Ewe mfalme! Tulikuwa watu wajinga na tuliishi kama hayawani wa msituni. Wenye uwezo miongoni mwetu waliwanyonya wanyonge. Hatukutii sheria yoyote na hatukutambua mamlaka yoyote isipokuwa ile yakutumia nguvu.

Tuliabudu masanamu ya mawe na miti iliyochong­wa, na hatukujua lolote kuhusu hadhi ya binadamu. Halafu Mwenyezi Mungu kwa huruma zake alituletea mjumbe wake ambaye alikuwa mmoja wetu. Tulikuwa tunafahamu kuhusu ukweli wake na hadhi yake.

Tabia yake ilikuwa mfano wa kuigwa, na alikuwa mzawa aliye bora wa Waarabu. Alitukataza kuabudu masanamu na alituita na kutuambia tumwabudu Mungu Mmoja. Alitushauri kusema kweli, na kuwapa ulinzi wanyonge, fukara, wanyenyekevu, wajane na yatima.

Alituamuru kuonyesha heshima kwa wanawake, na kamwe tusiwasengenye. Tulimtii na tulifuata mafundisho yake. Nchini mwetu, wapagani bado wapo wengi sana na walitukataza tusisilimu na kufuata imani mpya. Walianza kututesa, na ilikuwa kwa sababu ya kukwepa mateso kutoka kwao, hivyo kwamba tukatafuta na kupata hifadhi hapa kwenye himaya yako."

Jaafar alipomaliza kuhutubia, mfalme alitangaza kwamba aliridhika na ukweli wake, na aliongeza kusema kwamba Waislamu waliruhusiwa kuishi bila woga wowote. Usemi ambao ulimkasirisha sana Amr bin Al-As.

Lakini Amr bin Ass alipata fikira nyingine, ambayo alikuwa na uhakika ingemridhisha mfalme ambaye alikuwa Mkristo. Kama ingekubalika, alikuwa na uhakika kwamba ingebadilisha hali dhidi ya Waislamu, na wangerudishwa Makka.

Kwa hiyo siku iliyofuata, alirudi barazani na akamwambia mfalme kwamba lazima asitishe ulinzi kwa Waislamu kwa sababu walikana uungu wa Yesu (Isa) na walidai kwamba yeye ni binadamu kama wengine. Mfalme alipomuuliza Jaafar kuhusu jambo hili, alisema: "Uamuzi wetu kuhusu Yesu (Isa) ni kama alivyo funuliwa Mtume wetu, kwamba Yesu (Isa) ni mtumishi wa Mungu na Mtume wake, Roho Yake na Amri yake iliyotolewa kwa Mariam, bikira mtakatifu."

Mfalme alimwambia Jaafar: "Yesu (Isa) yu vilevile ambavyo umesema na hakuna zaidi ya hapo." Halafu akawageukia Waislamu na kusema: “Nendeni nyumbani kwenu na muishi kwa amani. Kamwe sitawaruhusu maadui zenu wawakamate."Alikataa kuwarudisha Waislamu Makka, alimrudishia Amr bin Al-As zawadi alizokwisha mpa na kuwaambia warudi walikotoka.

Washigton Irving

"Miongoni mwa wakimbizi waliokwenda Abyssinia, alikuwepo Jaafar, mtoto wa Abu Talib na kaka wa Ali, binamu wa Muhammed. Alikuwa mtu mwenye uwezo wa kujieleza na umbo la kupendeza sana. Alisimama mbele ya mfalme wa Abyssinia, na akamweleza imani ya Uislamu kwa hamasa na nguvu.

Mfalme ambaye alikuwa Mkristo wa dhehebu la Nestorian, aliona imani hizi zinafanana sana katika mambo mengi na kwa hiyo alikataa kabisa imani ya kuabudu masanamu iliyokuwa inakumbatiwa na Maquraysh hivyo kwamba, hadi hapo, badala ya kuwafukuza watoro, aliwakubali zaidi na kuwapa upendeleo na ulinzi maalum na akimrudishia zawadi alizokwisha mpa Amr bin Al-Ass na Abdullah na kuwafukuza hapo mahakamani."

(The Life of Muhammed).

Waislamu waliishi miaka mingi Abyssinia. Baada ya miaka kumi na tatu, walirudi Madina, si Makka - mnamo mwaka wa saba Hijiria (A.H.) (628 A.D.).- miaka saba baada ya Mtume wa Mungu kutoka Makka kwenda Madina. Kufika kwao Madina iligongana na ushindi wa Waislamu huko Khybar.

Jaafar bin Abi Talib alikuwa kiongozi wa Waislamu wote waliokwenda Abyssinia mwaka wa 615 na 616 A.D. inaonyesha kama vile alikuwa peke yake kutoka ukoo wa Bani Hashim aliyeondoka Makka kwenda Abyssinia na wakimbizi wengine. Watu wengine wote wa ukoo wa Bani Hashim walibaki Makka.