read

Sura Ya Nne: Ndoa Ya Muhammad Mustafa (s) Na Khadija

Msafara wa kibiashara wa Muhammad kwenda Syria ulikuwa ndio chanzo cha ndoa yake na Khadija.

Mtarjumi na mfasir wa Qur'an Majid, A. Yusuf Ali, anauliza swali: "Tunaweza kushangaa jinsi Yakuub alivyokutana tena na mwanawe Yusuf, au jinsi Musa alivyokutana na Harun, au jinsi Muhammad Mustafa alivyokutana na Bibi Khadija?"

La. Hatuwezi kushangaa. Ilikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu kwam­ba watumishi wake wawili- Muhammad na Khadija wangekutana kati­ka ndoa, na walioana.

Kuna taarifa isemayo kwamba mmoja wa marafiki wa Khadija alikuwa anatoka kwenye ukoo bora wa Makka jina lake Nafisa (au Nufaysa) binti Mumyah. Mwanamke huyu alikuwa na habari kwamba Khadija alikwisha kataa posa nyingi za ndoa. Alikuwa anashangaa kama pange­tokeza mtu katika Bara Arabu ambaye angekuwa wa kiwango alichoafi­ki Khadija. Marafiki hawa wawili walilizungumzia jambo hili mara nyingi.

Hatimaye, Nafisa alifanya mazungumzo ya mara ya mwisho kuhusu jambo la ndoa yake Khadija na akapata kutambua kwamba rafi­ki yake (Khadija) hakujali utajiri, cheo au uwezo wa mume mtarajiwa. Nafisa alijua kwa hakika kwamba rafiki yake Khadija alitaka kuolewa na mtu mwenye tabia nzuri, tabia inayokubalika. Khadija alitaka kuole­wa na mwanamume mwenye maadili mema na msimamo wa uadilifu.

Pia Nafisa (au Nufaysa) alijua kwamba alikuwepo mtu wa aina hiyo Makka na jina lake alikuwa Muhammad.

Kuna taarifa isemayo kwamba siku moja Muhammad alikuwa anarudi nyumbani kutoka Al-Kaaba, Nafisa alimsimamisha na mazungumzo yalifanyika kama ifuatavyo:

Nafisa: Ewe Muhammad, wewe ni kijana wa kiume na bado hujaoa. Wanaume ambao unawazidi umri, wamekwisha oa na wengine wamezaa watoto. Kwa nini hujaoa?

Muhammad: Bado sina uwezo wa mali; mimi ni fukara. Nafisa: Bila kujali ufakiri wako, ungejihisi vipi endapo ungemwoa mwanamke mwenye sura nzuri, tajiri, mashuhuri na mwenye kuheshimika?

Muhammad: Mwanamke huyu anaweza kuwa nani?

Nafisa: Mwanamke huyu ni Khadija, binti Khuwaylid.

Muhammad: Khadija? Inawezekanaje Khadija kukubali kuolewa na mimi? Unajua kwamba wanaume wengi matajiri na uwezo na wakuu wa makabila wamemposa na amewakataa wote.

Nafisa: Kama wewe upo tayari kumuoa Khadija, sema hivyo, na niachie mambo mengine mimi. Nitapanga kila kitu.

Muhammad alitaka kumwambia ami wake na mlezi wake, Abu Talib, kuhusu azima ya Nafisa, na kupata ushauri wake kabla hajatoa jibu.

Abu Talib alimfahamu Khadija kama alivyokuwa anamfahamu mpwa wake. Alikubali ushawishi wa Nafisa. Hakuwa na shaka kwamba Muhammad na Khadija wangekuwa wanandoa makini. Kwa hivyo, alilibariki pendekezo la ndoa yao.

Hapo hapo Muhammad alimtaarifu Nafisa kwamba pendekezo lake limekubaliwa na hivyo amepata mam­laka ya kuendeleza mazungumzo kuhusu ndoa yake na Khadija.

Mara tu baada ya Abu Talib kuthibitisha ndoa hiyo, alimtuma dada yake, Safiya, kumuona Khadija, na kuzungumza naye kuhusu jambo hilo. Wakati huohuo, Nafisa alikwisha fanya mazungumzo ya awali, na Khadija alikuwa anategemea kupata mgeni kutoka nyumbani kwa wakwe wategemewa.
Khadija alimpokea Safiya kwa uchangamfu, alimkirimu, na kumwambia kwamba yeye Khadija alimteua mpwa wake Safiya kuwa mwenzi wake wa maisha bila masharti yoyote. Safiya ali­furahishwa sana na mafanikio ya ujumbe wake. Kabla hajaondoka kurudi kwao, Khadija alimpa Safiya kanzu nzuri sana na ambayo ali­ikubali kwa furaha na shukrani nyingi.

Abu Talib aliamua kutekeleza kanuni za desturi za ndoa. Alimpa Khadija zawadi, na aliwachukuwa kaka zake, Abbas na Hamza, wote watatu wakaenda nyumbani kwa Khadija na kulifikisha pendekezo la ndoa ya mpwa wake na Khadija rasmi. Khadija alikubali zawadi ali­zopewa na Abu Talib na kama ilivyotarajiwa alikubali pendekezo la ndoa. Pande zote mbili zilikubaliana na kuweka tarehe ya harusi.

Abu Talib mwenyewe alichukuwa madaraka ya matayarisho ya ndoa ya mpwa wake mpendwa. Kwa ajili ya tukio hilo lenye baraka, Abu Talib alileta kumbukumbu zote zenye kuheshimika sana za urithi wa familia. Vitu hivi vilikuwa pamoja na joho na fimbo ya Abdul Muttalib, mare­hemu, mkuu wa kabila la Bani Hashim. Bwana harusi alivaa joho na kuishika mkononi mwake ile fimbo. Abu Talib alimvisha kichwani Bwana harusi kilemba cheusi cha ukoo wake, na alivaa pete yenye kito cha kijani kwenye kidole chake. Pete hii, ilikuwa raslimali ya Hashimu bin Abd Manaf bin Qusayy - mnamo siku za nyuma.

Harusi ilihudhuriwa na wakuu wote wa Quraysh na mamwinyi wa Makka. Bwana harusi alipanda farasi mwenye kutembea kwa majivuno, na vijana mashujaa wa Bani Hashim walitikisa Majambia yao yaliyokuwa yanameremeta juu ya vichwa vyao wakati walipokuwa wana msindikiza kutoka nyumbani kwa Abu Talib kwenda nyumbani kwa Khadija. Wanawake wa ukoo wa Quraysh walikwisha mtangulia bwana harusi, na tayari walikuwa wanakirimiwa nyumbani kwa bibi harusi.

Nyumba ya Khadija ilipambwa kwa taa nyingi sana. Ndani ya nyumba, mashada ya taa zenye mapambo yalining'inizwa kwa minyiroro ya dha­habu kwenye dari, kila shada lilikuwa na taa saba. Wageni walifika wakati giza lilianza kuingia. Msimamizi mkuu wa eneo la makazi ya Khadija aliunda kamati ya kumkaribisha Bwana harusi na wageni mashuhuri. Kamati ya makaribisho iliwaongoza wageni ndani ya nyumba kupitia kwenye lango la juu na kuingia kwenye ukumbi wenye umbo la mstatili ambao kuta zake zilibandikwa vigae na dari yake ili­pakwa dhahabu. Wageni waliketi kwenye mazulia na mito.

Kwa madhumuni ya shughuli hii maalum, Khadija aliagiza washonewe sare watu wote wa nyumbani mwake - wanaume na wanawake. Wanaume walivaa vilemba vyenye kumetameta, mashati mekundu, na walivaa mikanda (mishipi) kwenye viuno vyao yenye rangi nyeusi. Mashada ya hariri yenye rangi ya pembe za ndovu yalishikizwa kwenye vilemba. Wasichana walivalia mavazi yaliyonakishiwa kwa kutonewa dhahabu na kumetameta. Walivalia taji dogo kichwani na lulu nyingi na vito vyenye kumetameta. Nywele zao ziliporomoka hadi kwenye mabega na kutoka kwenye mabega hadi kiunoni zilisokotwa kwa lulu.

Mapambo ya chumba cha Bibi harusi yalikuwa mazuri sana, na hakika hayakuzidiwa kwa ustadi. Hariri iliyoning'inizwa na nguo iliyotariziwa kwa rangi nyingi nyororo, ilipamba ukuta; na busati, jeupe laini lili­tandikwa sakafuni. Moshi wa ubani ulichomoza kutoka kwenye chate­zo cha rangi ya fedha na almasi inayometameta, johari ya rangi ya bluu na rubi.

Khadija, bibi harusi, aliketi kwenye jukwaa lililofunikwa kwa nguo iliy­onakishiwa kwa urembo mwingi wa kufuma. Alionekana mchangamfu na kung'aa kama jua linalochomoza. Kichwani kwake alivaa taji la dha­habu na lulu yenye thamani na uzuri wa kushangaza. Gauni lake, lenye mchanganyiko wa rangi nyekundu iliyoiva na kijani, ilirashiwa dhahabu na kuwekwa mapambo ya lulu na Zamaradi. Walikuwepo wanawake wawili wa kumsaidia yeye binafsi, kila mmoja wao alikuwa amevalia taji la dhahabu, gauni la hariri lenye rangi ya zambarau, na makubazi yaliyotapakaa vito. Baada ya wageni wote kuketi kwenye nafasi zao, Abu Talib, mlezi wa Bwana harusi, alisimama na kusoma hotuba ya harusi.

"Utukufu na sifa zote ni zake mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na dunia, na shukrani zote ni Zake kwa neema Zake zote, riziki na huru­ma. Ametuleta sisi hapa duniani kutokana na vizazi vya Ibrahim na Ismael. Alitufanya sisi waangalizi wa Msikiti na kuwa viongozi wa Nyumba yake, Al- Kaaba, ambayo ni kimbilio la viumbe wake wote. Baada ya utangulizi huu Abu Talib aliendelea:

"Mpwa wangu, Muhammad bin Abdullah bin Muttalib, ni mtu mzuri kuliko wote katika jamii ya binadamu kiakili, hekima, uzao ulio safi, utakatifu wa maisha yake mwenyewe, na kwa heshima ya familia. Anazo dalili zote za mtu ambaye hatimaye atakuwa mtu mkubwa.
Anamuoa Khadija binti Khuwayled kwa mahari ya vipande 400 vya dhahabu. Natangaza kwamba Muhammad na Khadija sasa ni mume na mke. Mwenyezi Mungu na awabariki wote, na Awe Mlinzi wao.”

Kwenye hotuba yake, Abu Talib alitangaza kwamba ukoo wa Bani Hashim walikuwa warithi wa Ibrahim na Ismail, na walikuwa wabebaji au wachukuaji wa urithi huo. Kwa hiyo, hawakuchafuliwa na ibada ya masanamu.

Abu Talib alipomaliza hotuba yake, Waraqa bin Naufal alisimama kuso­ma hotuba ya harusi kwa niaba ya bibi harusi. Alisema: "Sifa zote na utukufu wote anastahili kupewa Mwenyezi Mungu.

Tunashuhudia na kukiri kwamba yale ambayo umeyatamka kuhusu Bani Hashim ni kweli. Hapana mtu anayeweza kukanusha ubora wao.

Kwa sababau ya uzuri wao, tunakubali ndoa ya Khadija na Muhammad. Ndoa yao inaziunganisha familia zetu mbili na kuoana kwao imekuwa chanzo cha furaha kubwa kwetu. Enyi Walezi wa Quraysh, nawatakeni kuwa mashahidi kwamba ninaridhia Khadija kuolewa na Muhammad bin Abdullah kwa mahari ya vipande 400 vya dhahabu. Mwenyezi Mungu na ajaalie ndoa yao iwe ya furaha.”

(M. Shibli, mtaalam wa historia kutoka India, anasema kwamba mahari ya Hadhrat Khadija ilikuwa vipande 500 vya dhahabu - Siira).

Amr bin Asad, ami yake Khadija mwenye umri mkubwa, naye pia alise­ma kwenye sherehe hiyo na aliyaunga mkono, kwa maneno yake mwenyewe, yale aliyoyasema Waraqa bin Naufal. Na alikuwa yeye ambaye kama mlezi, wa bibi arusi, aliridhika na kumtoa Khadija aolewe na Muhammad bin Abdullah. (Abu Talib alilipa mahari ya mpwa wake.)

Edward Gibbon

“Nyumbani na ng'ambo, wakati wa amani na vita, Abu Talib, ami wa Muhammad aliyekuwa anaheshimiwa sana, alikuwa kiongozi na mlezi wa kijana wake; wakati alipotimu miaka 25 alimuoa mwanamke tajiri mwenye daraja kubwa na mkazi wa Makka, ambaye aliuzawadia uaminifu wake kwa kukubali kuolewa naye pamoja na mali yake. Mkataba wa ndoa, katika jinsi rahisi ya kizamani, unasema kuhusu maelewano ya kimapenzi kati ya Muhammad na Khadija, unamwelezea yeye kama ni mtu hodari sana miongoni mwa kabila la Quraysh na unataja mahari ya wakia kumi na mbili za dhahabu na ngamia ishirini, ambayo ilitolewa kwa ukarimu wa ami wake.”

(Rejea: The Decline and Fall of Roman Empire)

Washington Irving

“Khadija alijaa imani ya kusisimua aliyokuwa nayo kwa msimamizi wake bora sana, Muhammed. Kwenye sherehe ya harusi yake, Halima ambaye alikuwa yaya wa Muhammed wakati alipokuwa mtoto mchanga, aliitwa na kupewa zawadi ya kondoo arobaini.”

(Rejea: The Life of Muhammed).

Wageni wote walimpa hongera Muhammad Mustafa siku ya harusi yake na walimtakia maisha ya furaha. Pia walimpongeza ami wake Abu Talib, kuhusu hafla yenye heri. Pande zote mbili Bwana na Bibi harusi, wali­washukuru wageni wao kwa uchangamfu.

Baada ya kwisha sherehe hizo, Mkuu wa Itifaki aliwaagiza watumwa kugawa chakula. Chakula kilikuwa kingi kupita kiasi kwani ilikuwa haijapata kutokea hapo Makka. Wageni walikula chakula kizuri sana na kila mlo ulikuwa wa mapishi ya aina yake. Wageni walituliza kiu kwa kinywaji kilichochanganywa na maji matamu yatokanayo na maua.

Baada ya chakula kila mgeni alipewa zawadi ya kanzu ya heshima, ili kuafikiana na mila za kale na uungwana wa Arabuni.
Wakati huo huo mkuu wa Itifaki alitangaza kwamba Bibi harusi alikuwa tayari kuondoka.

Ngamia jike aliyetandikwa mapambo ya kitajiri, alibe­ba kibanda mgongoni kwake, alikuwa anangoja kwenye lango la nyum­ba. Wageni wote walikusanyika sebuleni kumwona Bibi harusi akisindikizwa kwenye lango. Watumishi wake walimsaidia Bibi harusi kupanda kwenye kibanda cha harusi.

وَقَالَ ارْكَبُوا فِيهَا بِسْمِ اللَّهِ مَجْرَاهَا وَمُرْسَاهَا ۚ إِنَّ رَبِّي لَغَفُورٌ رَحِيمٌ{41}

"Na akasema: Pandeni humo kwa Bismillah, kwa Jina la Mwenyezi Mungu, kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu." (Qur'an 11:41)

Mmojawapo wa watumishi wa kike aliketi kwenye kibanda na Bibi harusi. Kwenye kichwa chake, alivalia tiara la maua na nywele zake zil­isokotwa kwa utepe wa buluu na ncha zenye lulu za kifahari. Alivalia bangili zenye nakshi ya vito vigumu na zenye kung'aa, na alishika kipepeo kilichopambwa na vito.

Kikundi cha watumwa wa Kinubi walibeba mienge, walitembea mbele ya ngamia jike kulia na kushoto.

Bwana harusi naye pia alipanda farasi wake, na yeye, na ami zake, vijana wa Bani Hashim na wageni wao, walirudi nyumbani kwa Abu Talib katika hali na mavazi yale yale waliyoenda nayo mapema siku ile nyumbani kwa bibi arusi.

Wakati msafara huu ulioongozwa kwa mienge ya moto ulipofika nyum­bani kwa Abu Talib, mke wake na dada zake Abu Talib walimsaidia Bibi harusi kuteremka kutoka kwenye kipando chake, ngamia jike. Msimamizi mkuu alimkinga kwa mwavuli wa hariri nyeupe juu ya kich­wa chake na akamwongoza kwenye vyumba vya ndani zaidi kwenye nyumba hiyo.

وَقُلْ رَبِّ أَنْزِلْنِي مُنْزَلًا مُبَارَكًا وَأَنْتَ خَيْرُ الْمُنْزِلِينَ {29}

"Na sema; Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho wenye bara­ka, na Wewe ni Mbora wa wateremshaji."(Quran 23:29).

Kila kitu kilifanyika kwa usahihi wa kiwango cha juu sana. Mawasiliano yalikuwa mazuri sana toka mwanzo hadi mwisho.

Kuoana kwa Muhammad na Khadija ni tukio lililomfurahisha kila mtu lakini furaha ya Abu Talib ilivuka mipaka ya kawaida. Alikuwa na dukuduku la kumuoza mpwa mke mzuri. Dukuduku hili liligeuka kuwa furaha kubwa isiyo na kifani baada ya mpwa wake na Khadija kuoana. Haingekuwa rahisi kupata malingano kama hayo. Abu Talib alimshuku­ru Mwenyezi Mungu kwa furaha mpya aliyoipata, na furaha yake iliwa­pata pia ndugu zake, Abbas na Hamza na watu wengine wote wa ukoo wa Hashim.

Siku tatu baada ya harusi, Abu Talib alifanya karamu ya chakula kush­erehekea tukio ambalo tangu hapo mpaka sasa linaitwa "karamu ya wal­ima." Jiji lote lilinga'a kwa ukarimu wake. Kila mkazi wa Makka alikuwa mgeni mwalikwa wa karamu hiyo. Muhammad, ambaye alikuwa Bwana harusi, alikuwa anawakaribisha wageni. Yeye mwenyewe (Muhammad), ami zake, Binamu zake na vijana wote wa ukoo wa Bani Hashim, walijivunia kuwa wenyeji wa sherehe hiyo. Karamu hiyo ilidumu kwa muda wa siku tatu. Miaka mingi baadaye,
Uislamu uliifanya karamu ya walima kuwa kumbukumbu ya karamu ya Abu Talib aliyoifanya kwenye harusi ya Muhammad na Khadija, na kui­weka kama desturi ya ndoa zote za Waislamu. Abu Talib alikuwa mtu wa kwanza kuitekeleza. Karamu ya walima haikujulikana katika bara lote la Arabu kabla ya harusi ya Muhammed na Khadija.

Abu Talib alilazimika kufikiri kama ingewezekana ndugu yake mpend­wa Abdullah na mkewe Amina, Mwenyezi Mungu awateremshie rehe­ma zake, wao pia kama wangekuwepo kushuhudia na kuibariki ndoa ya mtoto wao, na kushiriki pamoja katika ile furaha yake (Abu Talib). Lakini hata kama Abbullah na Amina wangekuwepo, harusi ya mtoto wao hainge sherehekewa kwa fahari na tamasha kuzidi alivyofanya Abu Talib kama mlezi wa Muhammad.

Ilifuata zamu ya Khadija kuonyesha ukarimu na wema wake. Ukarimu na wema yalikuwa mazoea yake makubwa. Na hafla gani ambayo ingemfaa zaidi au kupendelea kama si kwenye sherehe ya harusi yake kutosheleza hulka yake? Kwa hiyo, Khadija, alimwagiza mkuu wake wa Itifaki kutayarisha mipango kwa kuandaa karamu/tafrija kubwa kabisa ya chakula na kuweka historia katika Makka.

Hiyo ilikuwa karamu ya kukumbukwa kweli. Hata ombaomba wa Makka na makabila ya watu wanaohama hapa na pale na wanawake, walikuwa kwenye kundi la waalikwa. Watu walikula vyakula ambavyo kamwe hawajapata kuviona. Wale Waarabu wa jangwani ambao kamwe walikuwa hawajawahi kuonja kitu chochote isipokuwa maji ya chumvichumvi au yanayonuka katika maisha yao siku hiyo walikunywa maji ya waridi wakiwa wageni wa Khadija. Kwa muda wa siku nyingi wageni waalikwa matajiri na fukara, mashuhuri na wenye daraja la chini, mamwinyi na wanyonge, vijana na wazee walikula nyumbani kwa Khadija. Khadija aliwapa wageni waalikwa walio maskini, vipande vya dhahabu na fedha na nguo, na alijaza nyumba za wajane wengi na wato­to yatima mahitaji mengi ya muhimu ambayo hawakuwa nayo.

Khadija alikaa miaka mingi ya maisha yake akingojea mwanamume anayefaa kumuoa. Alipata mafanikio baada ya kungoja kwa muda mrefu alipojitokeza Muhammad, na wakaunganishwa katika ndoa takat­ifu.

Ndoa ya Muhammad na Khadija ilikuwa ya kwanza na ya mwisho kwa aina yake hapa duniani. Ilikuwa ni ndoa hiyo tu duniani pote ambayo ilipata neema za akhera na mali za hapa duniani. Ilikuwa ndoa ambayo ilipata rehema nyingi zisizo na kipimo na hesabu za peponi na hapa duniani.

Inawezekana kabisa kwamba katika Bara Arabu lote, hakuna mwanamke yeyote ambaye alipata kwenda nyumbani kwa mumewe na mahari nyingi kiasi hicho kama alivyofanya Khadija.

Ilijumuisha watumwa, wasichana, mbuzi na kondoo, na nguo zake binafsi za bei ghali, vitu vya ziada, vitu vya urithi visivyoweza kukadiriwa bei, mapambo, vitu vya thamani vya chuma, vito vya thamani na dhahabu nyingi na vipande vya fedha.

Mahari hii, ambayo haikutazamiwa kuwa hivyo kwa ubora na wingi wake, haikuwa zawadi aliyopewa Khadija, Bibi harusi na ami zake au kutoka kwa kaka zake.

Haya yalikuwa ni matokeo ya jitihada zake mwenyewe. Alizalisha mali hiyo kwa uangalifu wake, bidii yake, busara zake na uwezo wa kuona mbali kifikira.

Lakini huu haukuwa ndio tu utajiri aliokuja nao Khadija. Khadija pia alikuja na utajiri wa moyo na akili, na hivi vilikuwa havina kipimo na visivyokwisha. Katika miaka iliyofuata, Khadija aliyatajirisha pasipo kipimo maisha ya mumewe kwa kutumia vipaji hivyo.

Mara tu Khadija alipoolewa, alionekana kupoteza upendeleo wake kwenye biashara na milki yake ya biashara. Maisha ya ndoa yalibadil­isha tabia yake, kujitolea kwake, na wajibu wake. Alimpata Muhammad Mustafa, hazina kubwa kuliko zote hapa duniani. Mara Khadija alipompata Muhammad, dhahabu, fedha na almasi zilipoteza thamani; kwake Muhammad Mustafa Mjumbe mtarajiwa wa Mwenyezi Mungu na Mtume mtarajiwa wa Uislamu, akawa ndio tu, kitu cha kuelekeza mapenzi yake, uangalifu wake na bidii yake.

Mambo kama yalivyokuwa, hakupoteza uwezo wake mkubwa wa kupanga mambo, lakini badala ya kutumia uwezo huo katika biashara zake, aliutumia kwa kumtumikia mumewe. Aliyapanga maisha yake yote upya na kumfanya Muhammad Mustafa kuwa ndio mhimili wake wa maisha.

Khadija hakusitisha biashara zake nyingi mara moja. Alizisimamisha kwa awamu. Kwa hiyo, kwa viwango alisimamisha biashara ya kuin­giza mali ndani ya nchi na kutoa nje ya nchi ambayo baba yake ali­ianzisha.

Miaka iliyofuata baada ya ndoa yake, Muhammad alianza kusafiri tena na misafara ya Khadija kwenda Syria. M. Shibli, mtaalam wa historia kutoka India, anasema kwamba pia alikwenda Yemen. Popote alipokwenda, alipata faida kubwa. Khadija pia aliajiri Mameneja wengine ambao waliuza bidhaa zake, au walinunua bidhaa kwa ajili ya mauzo yake, na wao pia walipata faida. Lakini, msisitizo ulibadilishwa, badala ya kupanua biashara yake kama alivyokuwa anafanya kabla ya kuolewa, Khadija alianza kupunguza bidhaa polepole hadi hapo ambapo bidhaa zote ziliuzwa, na alikusanya fedha zote kutoka kwenye miradi.

Wakati Malikia wa Makka alipoingia nyumbani kwa mumewe, Muhammad Mustafa, awamu ya maisha yake ya furaha kubwa ilianza. Awamu hii ilidumu miaka ishirini na tano - hadi kifo chake. Mara moja Khadija alibadili maisha yake na kuafikiana na mazingira mapya. Tangu siku ya kwanza alianza usimamizi wa kazi yake ambayo ilikuwa kuyafanya maisha ya mume wake kuwa ya furaha na mazuri. Katika kufanya kazi hii alifuzu vizuri sana kama historia ya siku zilizofuata ilivyosadikisha kwa ufasaha kabisa.

Maisha ya ndoa yalifungua ukurasa mpya ya maisha ya Muhammad na Khadija. Jambo la msingi la "ukurasa" huu mpya ilikuwa furaha - fura­ha isiyo na dosari. Pamoja na kwamba ndoa yao ilipewa baraka za fura­ha, pia ilipata neema ya watoto. Mtoto wao wa kwanza, alikuwa wa kiume aliyeitwa Qasim.

Ilikuwa baada ya kuzaliwa Qasim, baba yake Muhammad Mustafa alipewa jina la Abul-Qasim - (baba wa Qasim) ­kufuatana na mila za kiarabu.

Pia mtoto wa pili alikuwa wa kiume. Jina lake lilikuwa Abdullah. Alipewa majina ya lakabu ya Tahir na Tayyib. Watoto wote wawili walikufa wakiwa bado wachanga.

Mtoto wa tatu na wa mwisho na ndio huyo tu aliyeishi muda mrefu miongoni mwa watoto wa Muhammad na Khadija alikuwa binti yao, Fatuma Zahra, mtoto wa kike. Ingawa Mwenyezi Mungu aliwatunuku zawadi nyingi, hakukuwepo na chochote kile kingine walicho kithami­ni zaidi ya binti yao. Fatuma alikuwa "mwanga wa macho" ya baba yake, na alikuwa "starehe ya moyo wa baba yake." Alikuwa pia "Kiongozi wa Wanawake wa Peponi." Baba na mama walimpenda sana, na alileta pamoja naye matumaini na furaha na baraka na huruma Zake Mwenyezi Mungu ndani ya nyumba yao.