read

Sura Ya Sita: Kutangazwa Kwa Uislamu

Kipindi kirefu cha matayarisho aliyotakiwa kuyafanya Muhammad ili aje kusimamia kazi zake na wajibu wake kama Mtume Mkubwa wa Mwisho wa Mungu hapa duniani kilikwisha.

Usiku wa upagani, makosa na ujinga vimekuwa vya muda mrefu, vyenye giza nene, vyenye kutia huzuni na majonzi. Mwanadamu alik­wisha fika katika hali ya kutokutambua kama kweli ingewezekana kuonekana hali ya kuleta matumaini.

Ilikuwa ni kwa sababu ya huruma za Mungu zisizo na kipimo ndizo zili­zo kumbusha shauku ya muda mrefu isiyotamkwa. Katika kutoa jibu kwa ombi lake (mwanadamu) la kimya, kimya "Jina" la Uislamu lili­chomoza kutoka kwenye bonde la Makka kushinda giza la ushirikina hapa duniani, na kutangaza ushindi wa imani ya Tauhid (Kumpwekesha Mwenyezi Mungu).

Muhammad alikuwa na umri wa miaka 40 alipoamriwa na Mwenyezi Mungu, kupitia kwa malaika Wake Jibril kutangaza Upweke Wake Tauhid, kwa watu wanaoabudu masanamu na washirikina wa ulimwen­gu wote, na kufikisha ujumbe wenye matumaini mapya na amani kwa jamii ya binadamu iliyokuwa inajihami wakati wote.

Kwa kukubali amri hii ya Mbinguni, Muhammad aliasisi mpango wa maana sana uitwao - Uislamu, ambao ulibadilisha majaliwa ya binadamu daima milele. Msingi wa madhumuni ya Uislamu, kama alivyoupokea kutoka kwa malaika Jibril, ulikamilishwa mbinguni, na sasa alitakiwa aufikishe kwa Jamii ya kibinaadamu.

Kabla hajapokea Ujumbe wake wa kiutume, Muhammad alikuwa akitu­mia mchana na usiku katika kusali na kutafakari wakati mwingine nyumbani kwake na wakati mwingine kwenye pango la jabali Hira, (kama ambavyo imeelezewa hapo kabla) kwa muda wa siku nyingi.

Siku moja, saa za jioni alipokuwa kwenye pango la Hira Malaika Mkuu Jibril alimtokea, na alimpa habari kwamba Mwenyezi Mungu alimteua yeye kuwa mjumbe wake wa mwisho hapa duniani, na alimwamuru afanye kazi ya kumwondoa mwanadammu kutoka kwenye vurugu ya dhambi, makosa na ujinga na kumleta kwenye mwanga wa Mwongozo, ukweli na ujuzi. Halafu Jibril alimwambia Muhammad "asome" Aya zifuatazo:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ {1}

خَلَقَ الْإِنْسَانَ مِنْ عَلَقٍ {2}

اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ {3}

الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ {4}

عَلَّمَ الْإِنْسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ {5}

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

“Soma kwa Jina la Mola wako Mlezi aliyeumba,
“Amemuumba binadamu kwa pande la damu,
“Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote!
“Ambaye amefundisha kwa kalamu.
“Kamfundisha mtu aliyokuwa hayajui."
(Qur'an Majid 96: 1-5).

-Aya hizi tano zilikuwa ndio ufunuo wa kwanza kabisa, na ziliteremsh­wa kwa Muhammad Mustafa kwenye Usiku huo Mkuu "au" "Usiku Uliobarikiwa" mnamo mwezi wa Ramadhani (Mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu) ya mwaka wa 40 wa Ndovu.

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنْزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ{185}

"Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa Qur'an kuwa ni mwongozo kwa watu, na hoja zilizowazi za uwongofu na upam­banuzi kati ya wema na Ubaya." (Qur'an Majid 2: 185)

إِنَّا أَنْزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ {1}

"Hakika sisi tumeiteremsha Qur'an katika Laylatul Qadri, Usiku wa cheo Kitukufu..."
(Qur'an 97:1)

وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ {2}

إِنَّا أَنْزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنْذِرِينَ {3}

"Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha,
"Hakika tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa..."
(Qur'an Majid 44:2-3)

"Usiku wa Cheo Kitukufu" "au" "Usiku Uliobarikiwa" hutokea wakati wa kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani, na inawezekana kuwa mwezi 21 au 23 au 25 au 27 ya mwezi huo. Kwa mujibu wa Hadithi. Na kwa mujibu wa kalenda ya Gregory, ufunuo wa kwanza uliteremshwa kwa Mtume tarehe 12, Februari, 610 kama anavyotaarifu

Mahmud Pasha al-Falaki wa Misri. Aya hizi tano zimo mwanzoni mwa Sura ya 96 ya Qur'an Majid. Jina la sura ni Iqraa (soma) au Alaq (Tone la Damu).

Katika maelezo yao kuhusu Muhammad Mustafa kupokea Ufunuo wa kwanza, Suni na Shia hawakubaliani. Kwa mujibu wa hadithi za Sunni, kutokea kwa Jibril ni jambo ambalo lilimshangaza Muhammad, na malaika alipomwamuru asome alisema "Siwezi kusoma."

Hii ilifanyika mara tatu, na kila mara Muhammad alipotamka kutokuwa na uwezo wa kusoma malaika alimbana tumbo. Hatimaye aliweza kukariri hizo Aya 5 kisha ndipo malaika naye alimwachia na kutoweka.

Malaika Jibril alipotoweka Muhammad ambaye alikwisha "tangazwa" kuwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alishuka kutoka kwenye majabali ya Hira na alikwenda nyumbani kwake akiwa na wasiwasi sana. Ni dhahiri, malaika Jibril kuingia ghafla pangoni ilisababisha kiwewe.

Alikuwa anatetemeka kwa sababu ya baridi, na alipofika nyumbani kwake alimwambia mkewe Khadija amfunike blanketi na alifanya hivyo. Baada ya hali ya woga kumtoka, alimwelezea mkewe kuhusu mkutano wake na Malaika Jibril ndani ya pango la Hira.

Maelezo ya Hadithi ya Sunni kuhusu tukio hili ipo kwenye makala iliyoandikwa na sheikh Ahmad Zaki Hammad, (Ph. D.) Chini ya kichwa cha habari; "Uwe na Matumaini" iliyochapishwa kwenye gazeti la Islamic Horizons of the Islamic Society of North America Plain field, Indianic Mei-June, 1987, kama ifuatavyo:

"Mtume (s.a.w.) katika hatua zake za mwanzo mjini Makka, alihofia kwamba kuteremshwa kwa ufunuo ilikuwa ni mguso wa kishetani ili kusumbua mawazo yake, kumchezea kiakili, kuvuruga utulivu na amani ya akili yake. Alihofu kwamba jini mojawapo lilimwingia. Alimuelezea haya Khadija. Hofu yake ilizidi kiasi kwamba... (na tafad­hali usishangazwe na taarifa sahihi iliyopo kwenye sahili Bukhari) Mtume (S.a.w.w.) alitaka kujiua ili asije akaguswa na shetani, apotosh­we, avurugwe na kuharibiwa."

Lakini kwa mujibu wa maelezo ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, ni kwamba; Muhammad Mustafa, mbali na kutokushangazwa, hakuhofish­wa na tukio la kukutana na Malaika Mkuu Jibril. badala yake alimkaribisha kama vile alikuwa anamtazamia. Malaika Jibril alileta habari njema kwamba Mwenyezi Mungu alimteua yeye kuwa Mjumbe wake wa mwisho kwa binadamu, na alimpongeza kuchaguliwa kuwa mpokeaji wa heshima kubwa kuliko zote kwa kiumbe wa hapa duniani.

Muhammad alikubali bila kusita ujumbe wa utume wala hakupata shida kukariri Aya za Ufunuo wa Mwanzo. Alizisoma au alizikariri aya hizo bila shida wala bila kuongozwa.
Kwa hakika Jibril hakuwa mgeni kwake, na pia alitambua kwamba yeye akiwa mtumishi wa Mwenyezi Mungu, wajibu wake ni kutekeleza ujumbe aliopewa na Mwenyezi Mungu. Muhammad alikwisha tayarishwa kuuendeleza ujumbe huo hata kabla Jibril hajamtembelea. Jibril alimpa tu ishara za kuanza.

Waislamu wa madhehebu ya Shia pia wanasema kwamba kitu kimoja ambacho Jibril hakufanya ni kutumia nguvu za kimwili kumbana Muhammad na kumwambia asome. Kama alifanya, kweli ingekuwa mtindo wa kioja wa kumfundisha Muhammad, uwezo wa kusoma -kwa kumbana au kumkaba. Pia Shia wanaendelea kueleza kwamba Muhammad Mustafa hakufikiria kujiua hata mara moja katika maisha yake, hata alipokuwa amehuzunishwa sana, na haikupata kutokea kwamba angeingiwa na "shetani" au "angepotoshwa, kuvurugwa au kuchafuliwa."

Katika mazingira haya, Waislamu wa madhehebu ya Shia wananukuu Aya mbili za Quran Majid ambazo zinaonekana kuwa na uhusiano wa kimantiki kuhusu kisa hiki: (Mwenyezi Mungu alimwambia Shetani) "Hakika wewe huna mamlaka juu ya waja wangu. Na Mola wako Mlezi anatosha kuwa ni wa kutegemewa."(Qur'an Majid 17:65)

Mwenyezi Mungu mwenyewe huwalinda waja wake waaminifu na wa kweli kutoka kwenye mfumo wa Shetani; hawezi kuwa na mamlaka juu yao, na hawawezi kubadilishwa, au kuvurugwa au kuharibiwa.

وَيُنَجِّي اللَّهُ الَّذِينَ اتَّقَوْا بِمَفَازَتِهِمْ لَا يَمَسُّهُمُ السُّوءُ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ{61}

"Na Mwenyezi Mungu atawaokoa wenye kujikinga kwa ajili ya kufuzu kwao. Hapana Uovu utakaowagusa, wala hawatahuzuni­ka".(Qur'an Majid 39:61)

Hakuna uovu ambao ungemgusa Muhammad, mteule wa Mwenyezi Mungu Mwenyewe. Chini ya ulinzi wa Mungu alikuwa salama, hivyo kwamba haguswi na ouvu wowote.

Aliishi chini ya mamlaka ya kishe­ria ya Mungu wakati wote. Hata hivyo, Muhammad alikuwa na wasi­wasi kuhusu ukubwa wa kazi iliyokuwa mbele yake.

Alielewa kwamba katika utendaji wa kazi yake, angekutana na upinzani mkubwa, wenye kuogofya na uliodhamiria kutoka kwa wapagani dunia nzima.

Hali ya shauku yake ilikuwa dhahiri. Kwa hiyo alikuwa na mawazo ya huzuni alipoondoka pangoni kwenda nyumbani kwake. Na kweli alimwambia Khadija amfunike blanketi alipoketi na kumwelezea yaliyo tokea huko pango la Hira.

Khadija aliposikia habari aliyoambiwa na Muhammad Mustafa, alimli­waza na kumhakikishia kwa kumwambia "Ewe mwana wa ami yangu, uwe na matumaini mema. Mwenyezi Mungu amekuteua wewe kuwa Mjumbe wake. Mara nyingi wewe ni mkarimu kwa jirani zako, unawa­saidia ndugu zako, unawapa yatima, wajane na masikini na mwema kwa wageni. Mwenyezi Mungu kamwe hatakutelekeza."

R.V.C,Bodley

"Mungu ni ulinzi wangu, Ewe Abul Qasim" Khadija alisema: "Furahi na uwe na matumaini mema. Yeye ambaye mikononi mwake maisha ya Khadija yanategemea, ni Shahidi wangu kwamba wewe utakuwa Mjumbe wa watu Wake!"

(Messenger, The Life of Mohammad, 1946).

Inawezekana kwamba Muhammad mara moja alizidiwa na fikira ya kuwajibika kwa Mwenyezi Mungu katika kutekeleza mzigo mkubwa mno wa kazi yake mpya, lakini, aliposikia maneno ya Khadija ya kumpa matumaini, haraka sana alijisikia mfadhaiko unapungua.

Khadija alimhakikishia na kumshawishi kwamba, pamoja na msaada wa Mwenyezi Mungu alio nao, atasimama kidete katika utendaji wake na atashinda vizuizi vyote.

Muhammad alikubali. Tangu wakati huo alitambua kwamba Khadija alikuwa "chombo" ambacho kingeimarisha ujasiri wake endapo ungetetereka, na angekuwa tegemeo la imani yake endapo angelegalega.

Aya ifuatayo pia inaunga mkono maoni ya dhehebu la Shia:

"Na tulipochukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Isa mwana wa Mariamu na tulichukua kwako ahadi ngumu, ili (Mwenyezi Mungu) awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia makafiri adhabu chungu." (Qur'an Majid 33:7­8)

Maoni ya Mfasiri

“Kuna dokezo za mkataba juu ya kila kiumbe kufuata Sheria ya Mungu, nayo ni sheria ya kuwepo kwao. Lakini kuna dokezo la mkataba maalu­mu na Mitume, uliotongolewa sawasawa na makini, kwamba mitume watatekeleza ujumbe wao, watatangaza kweli ya Mungu bila woga au upendeleo, na kuwa tayari wakati wote kufanya kazi yake katika hali yoyote. Hiyo inawapa mitume nafasi yao na hadhi na madaraka yao makubwa sana kuhusu watu ambao wamekuja kuwaelekeza na kuwaon­goza kwenye Njia iliyonyooka.” (A. Yusufu Ali).

Waislamu wa madhehebu ya Shia wanasema kwamba Mwenyezi Mungu alichukua mkataba kutoka kwa Muhammad wa kufikisha Ujumbe Wake wa Mwisho kwa Mwanadamu.

Kwa hiyo, hawakubaliani na wanahistoria ambao hudai kwamba Muhammad alishangaa, alishtu­ka na kuogopa alipotembelewa na Jibril. Wanasema, maonyesho kama hayo ya hisia, hayaafikiani na mwenendo wake, na hayalingani na tabia ya Mkataba wake ulio makini.

Baada ya muda mfupi, Jibril alimtokea tena Muhammad alipokuwa kwenye pango la Hira, na alimpa Ufunuo wa pili ambao unasomeka kama ifuatavyo:

"Ewe uliyejigubika! Simama uonye! Na Mola wako Mlezi Mtukuze!" (Quran Majid 74:1-3).

Amri kutoka Mbinguni ya "simama na uonye" ilikuwa ishara kwa Muhammad (aliyejigubika blanketi) kuanza kazi yake. Jibril alimweleza waziwazi kazi zake mpya na ya kwanza kabisa ilikuwa kuharibu ibada ya miungu ya uongo, na kusimika bendera ya Tauhid ­imani ya Upweke wa Muumba - hapa ulimwenguni, na alitakiwa kuwaita wanadamu kwenye Imani ya kweli - Uislamu. Uislamu maana yake ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu na kukubali kwamba Muhammad ni mtumishi Wake na Mjumbe Wake.

"Alif Lam. Hiki ni kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye nuru, kwa idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa." (Quran 14: 1).

Muhammad alitakiwa kuwaongoza wanadamu kutoka kwenye kina cha giza nene na kuwaleta kwenye nuru.

"Muhammad angewaongozaje wanadamu kutoka kwenye kina cha giza nene na kuwaleta kwenye nuru” Swali hili linajibiwa na Quran Majid kwenye aya ifuatayo:

"Kama tulivyo mtuma Mtume kwenu, anayetokana na ninyi, kukutakaseni na kukufundisheni Kitabu na hekima na kukufundisheni mliyokuwa hamyajui." (Qur'an Majid 2:151).

Qur'an iko sahihi na bayana katika kufafanua dhana ya kazi yake kwa ajili ya Muhammad Mustafa. Alitakiwa kuwaongoza wanadamu kutoka kwenye "dimbwi la giza" na kuwapeleka kwenye nuru, kwa:

1. Kukariri Aya za Mwenyezi Mungu,

2. Kuwatakasa wanadamu

3. Kuwafundisha wanadamu yale yaliyomo kwenye maandiko na hekima, na

4. Kuwapatia wanadamu ujuzi mpya.

Jibril na Muhammad walitoka nje ya pango. Jibril alimfundisha kutawadha (matendo ya kujitakasa kabla ya sala). Muhammad alitawadha, na halafu waliswali pamoja na Jibril akiongoza swala, ilipoisha Jibril aliagana na Muhammad na kupaa
Jioni hiyo, Muhammad alirudi nyumbani kwake akiwa anafahamu zake na makini kwa kazi yake mpya ya "kusimama na kuonya."

Alitakiwa kuhubiri Uislamu, Dini ya Mwenyezi Mungu, duniani pote, na alitakiwa kuanza kuifanya kazi hiyo nyumbani kwake kwa kuhubiri kwa mkewe.

Muhammad alimwambia Khadija kuhusu Jibril kumtembelea kwa mara ya pili, na kazi aliyo amriwa na Mwenyezi Mungu kuifanya ya kumlin­gania yeye kwenye Uislamu.

Kwa Khadija, uadilifu na unyofu uliotangulia wa mumewe, ulikuwa uthibitisho usiopingika kwamba yeye alikuwa mjumbe wa Mungu, na tayari aliukubali Uislamu.

Hakika, "uhusiano wa kiitikadi" kati yake na Uislamu, ulikwisha kuwepo. Kwa hiyo, Muhammed Mustafa aliupele­ka Uislamu kwa Khadija mara moja "aliutambua", na aliukubali kwa matumaini makubwa. Aliamini kwamba Muumba alikuwa Mmoja na Muhammad alikuwa Mjumbe Wake, na akatamka:

"Nashahadia kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu; nanashahadia kwamba Muhammad ni mja na Mjumbe Wake."

Muhammad, mjumbe mpya wa Mwenyezi Mungu, alimpata mfuasi wake wa kwanza wa Uislamu Khadija - mkewe. Alikuwa wa kwanza, wa kwanza kabisa kuthibitisha imani ya Tauheed (Upweke wa Mwenyezi Mungu) na alikuwa wa kwanza kabisa kukubali kwamba, Muhammad ni Mjumbe wa Mungu kwa watu wote duniani. Alikuwa Mwislamu wa kwanza.

Muhammad "aliutambulisha" Uislamu kwa Khadija. Alimweleza maana ya Uislamu, na alimwingiza kwenye Uislamu. Alimwambia kwamba utiifu na upendo kwa Mwenyezi Mungu ndio msingi wa mfumo wote wa Uislamu.

Halafu Muhammad alimuonesha Khadija jinsi ya kutawadha na kusali. Khadija alitawadha na wote wawili wakasali, Muhammad akiwa Imamu. Baada ya sala, wote walimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa neema ya dini ya Uislamu. Pia walimshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema za sala ambayo kwayo Aliwahudhurisha Kwake.

Khadija aligundua kwamba, Sala ndio "lango" la kuingia kwenye Baraza ya Mwenyezi Mungu ya Rehema na neema Zake, na huruma Zake.

Watumishi wanyenyekevu wa Mwenyezi Mungu wanatakiwa kupita kwenye "Lango" hili ili wafike kwenye Baraza Yake na waweze kupata Rehema na Neema na Huruma kutoka Kwake. Pia alijua kwam­ba Sala katika wakati wote ilisababisha upya na utakaso.

Khadija ni Mwislamu wa kwanza - wa kwanza kabisa kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu - baada ya mumewe. Sasa basi yeyote atakaye orod­hesha majina ya watu wa mwanzo kusilimu, jina lake litakuwa la kwan­za. Sasa haidhuru ni nani anaorodhesha orodha ya watu wa mwanzo kabisa kuingia Uislamu, Siku zote jina lake litakuwa la mwanzo.

Hapana mwanahistoria mla rushwa anayeweza kubadilisha jambo hili. Heshima ya kuwa Mwislamu wa kwanza ni ya Khadija, na itakuwa ya kwake daima Milele.

Baada ya kuingia kwenye Uislamu, Khadija alifuata imani ifuatayo:

Sema: "Kwa hakika, Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye Njia iliyonyooka, Dini iliyo sawa kabisa, ambayo ndiyo mila ya Ibrahim aliyekuwa mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina."

Sema: "Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. Hana mshirika. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu." (Qur'an 6:161-163)

Washington Irving

Baada ya Muhammad kukutana na Jibril kwa mara ya kwanza, alikuja kwa Khadija akiwa anatetemeka na kufadhaika. Khadija aliona kila kitu kwa jicho la imani. "Ni habari njema ulizozileta", alisema kwa mshangao, "kwa Jina Lake, ambaye roho ya Khadija ipo chini ya uwezo wake, kuanzia sasa ninakutambua wewe kama Mtume wa taifa letu." Aliendelea kusema, "Furahi, Mwenyezi Mungu hakupi usumbufu wa kuanguka kwenye fedheha Je, hukuwa wewe kipenzi cha ndugu zako, mwema kwa jirani zako, mpaji kwa masikini, mkarimu kwa mgeni, mwaminifu kwa neno lako, na wakati wote ni mtetezi wa kweli.?"

(Life of Muhammed)

A. Yusufu Ali

Katika umri wa miaka 25 Muhammad aliunganishwa katika mkataba mtakatifu wa ndoa na Khadija Mkubwa mwanamke mwenye daraja kubwa ambaye alimfanya kuwa rafiki yake wakati ambapo hakuwa na utajiri wowote, Alimwamini wakati umashuhuri wake ulikuwa hauju­likani, Alimtia moyo na alimwelewa katika bidii zake za kiroho, Alimwamini ambapo miguu yake ilikuwa inatetemeka, Aliitika wito na kupigana na upinzani, mateso, matusi, vitisho na maumivu, Na alikuwa msaidizi wake wa maisha kwa kipindi kirefu hadi kufa kwake, na kuju­muishwa na watakatifu wakati akiuwa na umri wa miaka 51. Mwanamke bora, mama wa wale waaminio.”

(Introduction to the translation and Commentary of the Holy Qur'an).

Wakati Muhammad alipoamriwa kuwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, binamu yake Ali bin Abu Talib aliyekuwa bado mdogo, alikuwa na umri wa miaka kumi, pamoja na umri wake kuwa mdogo, alionyesha uwezo mkubwa wa kushika mambo yake, na alipewa uwezo mwingi wa kuju­muika kwenye shughuli za kidini za mlezi wake.

Kwa hiyo, alitangaza kwa shauku kubwa kile alichokiamini kwamba Mungu ni Mmoja, na Muhammad alikuwa mjumbe Wake.

Na baada ya muda mfupi, alianza kusali pamoja na Muhammad na Khadija. Alitaka kwenda mbele ya Mwenyezi Mungu akiwa amefuatana na mjumbe Wake Mwenyewe.

Muhammad Mustafa alimfundisha Ali namna ya kutawadha na kusali, kuanzia hapo, Muhammad hakuonekana anasali bila ya Ali kuwepo.

Mvulana huyu pia alikariri Aya za Quran hapo hapo zilipoteremshwa kwa Muhamad. Katika hali hii, Ali alikua pamoja na Quran. Hakika, Ali na Quran "walikuwa" pamoja kama "mapacha" nyumbani kwa Muhammad Mustafa na Khadija Bibi Mkuu.

Ali aliishi kwenye mazingira ya kusisimua ya maadili ya Kiislamu.

Kwa kitendo cha unyonyaji huu (wa elimu), Uislamu ukawa sehemu ya damu ya Ali bin Abu Talib, mfuasi mdogo wa Muhammad. Uislamu ukawa umbile kabisa la utu wake.

Muhammad, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alimpata Khadija kuwa Mwislamu wa kwanza mwanamke na alimpata Mwislamu wa kwanza mwanamume - Ali bin Abi Talib.

Muhammad bin Ishaq

"Ali alikuwa mwanamume wa kwanza kumwamini Mtume wa Mungu, kusali naye na kuamini ujumbe wake wa dini, alipokuwa na umri wa miaka kumi. Mungu alimpendelea kwa kulelewa na Mtume kabla ya kutangazwa Uislamu."

(The Life of the Messenger of Allah)

Muhammad Husayn Haykal

Wakati huo Ali alikuwa kijana wa kwanza kuingia Uislamu, alifuatiwa na Zayd bin Harithah, mteja (mtumwa aliyeachwa huru) wa Muhammad. Uislamu ukakomea kwenye kuta nne za nyumba moja. Baada ya Muhammad mwenyewe, waliosilimu na kufuata hiyo imani mpya walikuwa mke wa Mtume, binamu ya Mtume na mteja wa Mtume.

(The life of Muhammed, Cairo, 1935).

Maumaduke Pickthal

Wa kwanza kabisa miongoni mwa wafuasi wa Muhammed walio silimu ni mkewe, Khadija; wa pili binamu yake Ali, ambaye alikuwa mtoto wa kupanga, wa tatu mtumishi wake Zayd bin Harith aliyekuwa mtumwa wake.

(Introduction to the Translation of Holy Qur'an. 1975).

Abdullah Yusuf Ali

Kwa binamu yake Muhammad, Ali, aliyependwa sana, alizaliwa, alipokuwa na umri wa miaka thelathini, alionekana kama mfano wa mtu bora. Alikuwa mpole na mwenye hekima na mkweli na imara. Mtu ambaye alitumia nguvu zake zote na ustadi wake wote alipotakiwa kuweka ulinzi, Aliyachukulia maisha yake kuwa kitu kisicho na thamani alipotakiwa kuunga mkono jambo kubwa lenye kuthaminiwa sana, na ujasiri wake, akili yake, kujifunza kwake na upanga wake katika kum­tumikia huyu Mjumbe mkuu wa Mwenyezi Mungu.

Khadija aliamini, akitukuka katika imani kuliko wanawake wote; Ali, aliyependwa sana, kisha alikuwa mtoto wa miaka kumi, lakini mwenye moyo kama wa simba ( kwa ujasiri ), alitoa ahadi kwa imani yake, na tangu hapo alikuwa Msaidizi Mkuu wa Uislamu.

(Introduction to the Translation and Commentary of the Holy Quran).

Shahidi wa tatu aliyeukubali Uislamu alikuwa Zayd bin Haritha, mtumwa aliyeachwa huru na Muhammad, na kuwa sehemu ya familia yake.

Tor Andre

Zayd alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kukubali Uislamu, kwa hakika alikuwa wa tatu baada ya Khadija na Ali. (Muhammed, the Man and his Faith, 1960).

Ali bin Abu Talib alikuwa mwanamume wa kwanza kukubali Uislamu, na kutangulia kwake kukubali Uislamu hakuna shaka. Dk. Maulana Muhammad Jabal, mwana falsafa wa mashairi wa India na Pakistani, anasema mtu huyu hakuwa wa kwanza, bali "Mwislamu bora wa mwan­zo kabisa."

Ali alikuwa Mwislamu wa mwanzo kabisa kwa kuzingatia wakati. Hakuna mtu aliyemtangulia katika kukubali Uislamu. Lakini pia alikuwa wa mwanzo kabisa katika kuutumikia Uislamu na Mjumbe -Mtume wake kama ambavyo miaka iliyofuata ilivyokuja kuonyesha.

Muhammad bin Ishaq, mwandishi wa maisha ya Muhammad Mustafa anataarifu ifuatavyo kwenye kitabu chake -Sira:

"Ilipokewa kutoka kwa Yahya bin Ash'ath bin Qays al-Kindi kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake Afiif: Al-Abbas bin Abdul Muttalib alikuwa rafiki yangu aliyekuwa na desturi kwenda Yemen mara kwa mara kununua manukato na kuuza wakati wa maonyesho ya biashara.

Nilipokuwa naye Mina, alikuja mtu mkubwa kwa umri na alifanya kwa ukamilifu vitendo vyote vya kutawadha na baada ya hapo alisimama na kusali. Halafu akaja mwanamke kutoka ndani naye akatawadha na akasali.

Halafu alitokea kijana aliyekuwa anakaribia kuwa mtu mzima alitawadha, akasimama karibu naye akasali. Nilimuuliza Abbas wali­chokuwa wanafanya watu hao, na alisema kwamba alikuwa mpwawe, Muhammad bin Abdullah bin Abdul Muttalib, ambaye anadai kwamba Mwenyezi Mungu amemtuma yeye kuwa Mtume; mwingine ni mtoto wa kaka yangu, Ali bin Abi Talib, ambaye amemfuata yeye kwenye dini yake; wa tatu ni Khadija ambaye ni mkewe, mtoto wa Khuwaylid ambaye pia anamfuata yeye kwenye dini yake.”

Baada ya kuwa Mwislamu na Uislamu ulikwisha jikita moyoni mwake, Afiif alisema, "Lau vile ningekuwa wa nne." Mtu wa nne kushahidilia na kuukubali Uislamu, alikuwa Abu Bakr, mfanyabiashara wa Makka.

Mwanzoni, Muhammad alihubiri Uislamu kwa siri. Aliwalingnia kwenye Uislamu watu hao tu aliowaamini na ambao walikuwa marafiki zake binafsi. Wachache katika wale waumini wapya aliowasilimisha "hawakujionyesha" hapo Makka."

(Sira-Muhammad Ishaq)

Muhammad Husayn Haykal

Wakihofia kuamsha uadui na migogoro kutoka kwa Quraysh kwa sababu ya kuacha ibada za masanamu, Waislamu wapya hawakutaka kujulikana kwamba wamesilimu.

(The life of Muhammed, Cairo, 1935).

Miongoni mwa waliosilimu mwanzoni kabisa walikuwa Yasar, mke wake, Sumayya; na mtoto wao Ammar. Wao wanajulikana sana kwa sababu familia yao yote ilikubali Uislamu kwa pamoja, hivyo, wao walikuwa familia ya kwanza ya Kiislamu iliyo nje ya ile ya Mtume wa Uislamu.

Mwingine aliyesilimu mwanzoni ni Abu Dharr el-Ghiffari wa kabila la Ghiffar, ambaye alijulikana miaka iliyofuata, kwa kupenda mno haki na kweli.

Kwa juhudi za Abu Bakr, mtu wa nne kusilimu, wakazi wengine wachache wa Makka walikubali kuwa Waislamu.

Miongoni mwao walikuwemo Uthman bin Affan, aliyekuja kuwa khalifa wa Uislamu; Talha; Zubayr; Abdur Rahman bin Auf; Sa'ad bin Abi Waqqas; na Ubaidullah Aamir bin al-Jarrah.

Abu Abdullah Arqam bin Abil Arqam alikuwa kijana wa miaka ishirini. Alikuwa wa ukoo wa Makhzum wa kabila la Quraysh, na alikuwa mfanyabiashara aliyefuzu. Aliishi kwenye nyumba kubwa yenye nafasi kwenye bonde la Safa. Yeye pia alisikia wito wa Uislamu na aliukubali, na aliweka nyumba yake - Dar-al-Arqam kwa matumizi ya Mtume wa Uislamu.

Mwanzoni Waislamu walikuwa wachache sana kwa idadi kiasi kwamba hawakuweza kusali sala zao ndani ya Al-Ka'aba au hadharani. Mtume alikubali na kumshukuru Arqam kwa kujitolea kwake, na Waislamu walikusanyika nyumbani kwake na kusali sala za jamaa. Dar-al-Arqam ikaitwa jina Dar-al-Islam taasisi ya ujumbe wa Uislamu, na ndio ilikuwa mahali pa kwanza walipokuwa wanakutana Waislamu.

Miaka mitatu ilipita katika hali hii lakini mnamo mwaka wa nne wa wito, Muhammad aliamriwa na Mwenyezi Mungu kuwaita ndugu zake kwenye Uislamu waziwazi.

"Na uwaonye jamaa zako wa karibu Quran 26:214.

Ndugu wa Muhammad walikuwa watu wote wa ukoo wa Bani Hashim na Bani al-Muttalib. Alimwamuru binamu yake, Ali, awaalike wazee wote kwenye karamu. Watu arobaini walihudhuria.

Wageni walikusanyika kwenye ukumbi wa nyumba ya Abu Talib, na baada ya kumaliza kula chakula, Muhammad, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alisimama na kusema nao. Miongoni mwa wageni waalikwa, alikuwepo Abu Lahab, ami yake Muhammad. Labda, Abu Lahab alik­wishasikia alichokuwa anafanya mpwawe kwa siri, na alihisi sababu ya wao Bani Hashim kualikwa kwenye karamu. Muhammad alipoanza tu kusema, Abu Lahab aliingilia kati kifedhuli, na yeye mwenyewe akahutubia mkutano huo:

"Ndugu, binamu na ami, msisikilize yanayosemwa na "msaliti" huyu na msiache dini ya wahenga wenu, endapo atawaita muingie kwenye dini mpya.

Kama mtakubali, basi kumbukeni kwamba mtaamsha hasira ya Waarabu wote na mtagombana nao. Hata hali ilivyo ninyi ni wachache sana. Kwa hiyo itakuwa kwa faida yenu kuendelea na dini ya jadi yenu."

Kwa hotuba yake fupi, Abu Lahabu alifaulu kuutumbukiza mkutano kwenye vurugu. Kila mtu alisimama na kurandaranda hapa na pale na kupigana vikumbo wao kwa wao. Halafu wakaanza kuondoka, na baada ya muda mfupi ukumbi ulibaki wazi.

Jaribio la kwanza la Muhammad la kusilimisha ukoo wake lilishindwa. Lakini hakustushwa na tatizo hili la mwanzo, alimwamuru binamu yake, Ali, awaalike tena wageni walewale kwenye karamu.

Baada ya siku chache, waalikwa walikwenda, na baada ya chakula cha jioni Muhammad aliwahutubia kama ifuatavyo:

"Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa huruma zake. Sifa zote anastahi­ki Mwenyezi Mungu na namwomba mwongozo wake. Namwamini Yeye, na ninaweka matumaini yangu Kwake. Yeye ni mwingi wa Neema na Mwenye kurehemu; Yeye ni Mwema na Mwenye Huruma."

Baada ya kumsifu Mwenyezi Mungu, Mtume aliendelea kusema "Nina shuhudia kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu; Yeye hana mshirika, na mimi ni mjumbe wake. Mwenyezi Mungu amenia­muru niwaite kwenye dini Yake Islam- kwa kusema: ‘Na onya ndugu zako wa karibu.’

Kwa hiyo, nawaonyeni kwamba acheni ibada za uongo, na ninawaiteni kushuhudia kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi mungu, na kwamba mimi ni mjumbe Wake. Enyi wana wa Abdul Muttalib, hakuna mtu yeyote ambaye amekuja kwenu na kitu kizuri kuzidi hiki ambacho nimewaleteeni. Kwa kuikubali (dini hii) mtakuwa na uhakika wa hali njema hapa duniani na Akhera. Ni nani basi, miongoni mwenu ambaye ataniunga mkono kufanya kazi hii kubwa mno? Nani atakaye nisaidia mzigo wa kazi hii? Nani atakaye kuwa naibu wangu, makamu wangu na waziri wangu?"

Walikuwepo wageni arobaini kwenye ukumbi. Muhammad alinyamaza ili atathmini matokeo ya maneno yake kwao. Lakini hakuna hata mmoja wao aliye jibu. Hakuna hata mtu mmoja miongoni mwa wasikilizaji aliyeonyesha kutikisika. Hatimaye, wakati kimya kilikwisha elemea mkutano, kijana Ali alisimama na kusema kwamba angemuunga mkono Mjumbe wa Mwenyezi Mungu; angegawana naye mzigo wa kazi yake; na angekuwa Naibu wake, Makamu wake na Waziri wake.

Lakini, Muhammad alimpa ishara Ali aketi chini, na alisema: "Ngoja! Labda mtu mwengine anayekuzidi umri atasimama."

Muhammad alitoa tena wito wake lakini hakuna aliyejibu, na kimya chenye kuleta mashaka kilizidi kutanda. Kwa mara nyengine Ali aliji­tolea lakini Mtume aliendelea kusubiri kwamba labda mtu mwenye umri mkubwa kuzidi wake angetokeza, alimwambia azidi kungoja. Halafu akatoa wito kwa mara ya tatu, lakini hakuna aliyeitika. Hakuna hata mtu mmoja kwenye mkutano aliye onyesha kupendelea wito wake.Alitupa macho kwenye kundi lote na kuwatazama kila mmoja kwa makini laki­ni hakuna hata mmoja aliyetikisika. Baada ya muda mrefu alimuona Ali ananyanyuka na kutangaza kujitolea kumtumikia yeye kwa mara ya tatu.

Safari hii Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikubali kujitolea kwa Ali. Alimsogeza karibu naye sana, na akauambia mku­tano. “Huyu ni Waziri wangu, Mrithi wangu, na Naibu wangu. Msikilizeni na mzitii amri zake."

Edward Gibbon

Katika kipindi cha miaka mitatu, watu kumi na wane walisilimu, matun­da ya mwanzo kabisa ya ujumbe wa Muhammad; lakini mnamo mwaka wa nne aliingia kwenye kazi yake ya kiutume, na aliamua kuionyesha familia yake nuru ya dini ya kweli, alitayarisha karamu ya watu arobai­ni wa ukoo wa Hashim. "Marafiki na ndugu."
Muhammad aliwaambia watu wa mkutano. Nawapa zawadi, na ni mimi pekee ninayeweza kuwapa zawadi hii yenye thamani kubwa sana, hazina ya hapa duniani na dunia ijayo. Mungu ameniamuru niwaite nyinyi kwenye kumtumikia Yeye. Nani miongoni mwenu atanisaidia mzigo wangu? Nani miongoni mwenu atakuwa Sahaba wangu na Naibu wangu?

Hakuna jibu lililo­tolewa, hadi hapo kimya cha kustajabisha na wasiwasi, na kebehi ilivun­jwa na ujasiri wa Ali uliokataa kuvumilia, mwenye umri wa miaka kumi na mine. “Ewe Mtume mimi hapa ni mtu huyo, yeyote atakayepigana na wewe nitamn'goa meno yake, nitayararua macho yake, nitavunja miguu yake, nitapasua tumbo lake. Ewe Mtume, mimi nitakuwa Naibu wako."

Muhammad alikubali kujitolea kwa Ali kwa msisimko wa furaha na Abu Talib kwa shingo upande alilazimika kukubali heshima kubwa ya mwanaye.

(The Decline and Fall of Roman Empire)

Washington Irving

"Enyi wana wa Abd al-Muttalib", aliita Muhammed kwa shauku, "kwenu ninyi, kwa watu wote, Mwenyezi Mungu amewapa zawadi hizi za thamani sana. Kwa jina L ake, nawapa neema za hapa duniani na furaha ya milele ya kesho Ahera.

Nani miongoni mwenu atanisaidia mzigo wa kazi yangu? Nani atakuwa ndugu yangu, Naibi wangu, Waziri wangu?" Wote walinyamaza kimya; baadhi walikuwa wanashangaa; wengine walikuwa wanatabasamu kwa mshangao na kejeli.

Baada ya muda mrefu Ali, alianza kuzungumza kwa ari ya ujana, alijitolea kumsaidia Mtume ingawaje kwa kiasi fulani alikiri kwamba yeye bado mtoto na hana nguvu za musuli. Muhammed alimkumbatia kijana huyo mwema na alimsogeza zaidi kifuani mwake. Tazama ndugu yangu, Naibu wangu, Waziri wangu", alisema kwa sauti ya juu, sik­ilizeni maneno yake, na mheshimuni yeye."

(The life of Muhammed)

Bwana Richard Burton

"Baada ya kipindi kirefu cha kutafakari, ikiwa imechochewa na ushabi­ki wa kipumbavu wa Wayahudi, ushirikina wa Wakristo wa Syria na Uarabuni, na ibada za masanamu za kuchukiza zinazofanywa na wananchi wenzake wasioamini, pia mwenye shauku. na kuna roho ipi mashuhuri ambayo haijawa na shauku? Yeye (Muhammad) alidhamiria kuyarekebisha maonevu hayo ambayo yalisababisha ujumbe uliokuwa unateremshwa kuchukiwa na watu wenye ujuzi na kutokupendelewa na wafedhuli.

Alijitambulisha kama mtu aliyetiwa moyo miongoni mwa ndugu zake na watu wa ukoo wake. Hatua hii haikufaa, isipokuwa ilim­silimisha muumini mmoja mwenye thamani ya wapiganaji elfu moja, naye ni Ali, mwana wa Abu Talib.

(The Jew the Gypsy and El-Islam, San Francisco, 1898)

Ali alijitolea kumtumikia Muhammad, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na alikubaliwa. Kwa wazee wa kabila la Qurayish, tabia ya Ali ilionekana kama ya kuharakisha mambo na kutokuwa na adabu lakini baada ya muda mfupi alithibitisha kwamba alikuwa na ujasiri wa kufanikisha mambo kinyume na vile wengine walivyofikiri. Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alikubali kujitolea kwa Ali si tu kwa maneno ya kushukuru na furaha lakini pia alitangaza kwamba Ali alikuwa kuanzia muda ule Naibu na Waziri wake.

Tangazo la Muhammad lilikuwa la kweli na lisilo na shaka. Ni upumbavu kukwepa jambo la msingi kama watu wengine wafanyavyo, kwamba Unaibu wa Ali kwa Muhammad ulikomea kwenye ukoo wa Bani Hashim, kwa sababu mkutano huo ulikuwa wa Bani Hashim. Lakini Muhammad hakuweka mipaka kwa unaibu wa Ali. Ali alikuwa Naibu kwa Waislamu wote duniani na wakati wote.

Karamu ambapo Muhammad, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alim­tangaza Ali kuwa naibu wake inajulikana kihistoria kama "Karamu ya Dhul-Asheera." Jina hili linatoka ndani ya Qur'an (26:214).

Katika hali isiyo ya kawaida Sir William Muir amelitaja tukio hili la kihistoria kama "lisilothibitishwa."
Lakini nini kisichothibitika au kisi­cho cha kweli? Kuna kitu gani ambacho kingekuwa cha mantiki zaidi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kuliko kuanza kazi ya kutangaza Uislamu nyumbani kwake, na watu wa familia yake na ukoo wake, hususan, baada ya kuamriwa kwa hakika na Mwenyezi Mungu kuwaonya "ndugu zake wa karibu sana?"

Karamu ya Dhul-Asheera pale ambapo Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu, alimteua Ali bin Abi Talib kuwa Naibu wake, ni tukio la kihistoria na ukweli wake umethibitishwa na wanahistoria wa Kiarabu, baadhi yao ni hawa wafuatao:

1. Tabari, History , Juzuu ya pili uk. 217

2. Kamil bin Athir, History, Juzuu ya pili uk. 22

3. Abul Fida, History Juzuu ya pili uk. 116.

Alipoandika kuhusu Ali, wakati huu Sir, William Muir anasema: "Binamu yake Muhammad, Ali, akiwa na umri wa miaka 13 au 14, tayari alikwisha onyesha ishara za hekima na uamuzi tabia ambazo zimempatia sifa ya maisha ya akhera. Ingawa alikuwa na moyo thabiti, alikuwa hana msisimko wa nguvu ambao ungemfanya yeye kuwa mtangazaji wa Uislamu mwenye kuathiri. Tangu utoto wake alikua kati­ka imani ya Muhammad, na mahusiano yake ya mwanzoni yaliimarisha imani ya miaka ya utu uzima...”

(Life of Muhammed, London, 1877).

Tuna mashaka mengi kuhusu usemi wa Bwana William Muir kwamba Ali alikuwa hana msisimko wa nguvu ambao ungemfanya yeye kuwa na uwezo mkubwa wa kutangaza Uislamu. Ali hakupungukiwa nguvu au chochote.

Kwenye matatizo yote ya Uislamu, Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alimteua yeye kutekeleza majukumu ya hatari sana, na bila kusita aliyatekeleza.

Kama mhubiri, Ali alikuwa hana kifani. Hapakuwepo na yeyote mion­goni mwa masahaba wote wa Mtume ambaye alikuwa na uwezo wa kutangaza Uislamu kumzidi Ali. Alizitangaza Aya za mwanzo 40 za Sura Baraa (kinga), Sura ya 9 ya Qur'an, kwa wapagani wa Makka, akiwa kama mhubiri wa kwanza wa Uislamu, na kama mwakilishi wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Ali ndiye aliyeyaingiza makabila yote ya Yemen kwenye Uislamu.

Muhammad, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alimlea Ali kama mtoto wake wa kumzaa, na kama alikuwa amepungukiwa na chochote ange­jua. Alimtangaza Ali kuwa waziri wake, wasii wake na naibu wake wakati ambapo hakuna mtu ambaye angeweza kutabiri hatima ya Uislamu. Hii inaonyesha jinsi Mtume wa Uislamu alivyojiamini sana katika kipindi cha miaka 14.

Ali alikuwa alama ya matumaini na malengo ya Uislamu. Kwenye mapinduzi yaliyofanyika wakati wa karamu ya Dhul-asheera, Muhammad, Mtume wa Mungu, alikusanya nguvu na mawazo, bidii, juhudi ya vijana; Ali alikuwa nazo tabia zote hizo. Mambo mawili yali­tokea kwenye Karamu. Jambo la kwanza ni kwamba Mtume aliudhi­hirisha Uislamu hadharani; halikuwa jambo la kuficha; Uislamu "uliji­tokeza."

Kwenye Karamu ya ndugu zake. Muhammed "alivuka Rubicon - (kivuko ambacho haingewezekana kurudi nyuma tena)". Wakati ulikwishafika kwake yeye kuufikisha Uislamu nje ya ukoo wake kwanza kwa Quraysh wa Makka, halafu kwa Waarabu wote na mwisho, duniani pote. Jambo lingine ni kwamba alimpata Ali ambaye alikuwa ngome ya ujasiri, kujitolea na thabiti, na alikuwa na thamani kubwa kuzidi "wapiganaji" elfu moja ."

Imeelezwa kwamba baada ya siku kad­haa baada ya karamu ya pili ya Dhul-Asheera, Muhammad Mustafa ali­panda kwenye kilima cha Safa karibu na Kaaba, na aliita: "Enyi wana wa Fihr; Enyi wana wa Loi, Enyi wana wa Adi, na Quraysh wengine wote. Njooni huku na mnisikilize. Nina jambo muhimu sana la kuwaambia."
Wakazi wengi wa Makka waliposikia sauti yake, walikwenda kumsik­iliza. Aliwaambia; "Je, mngeniamini kama ningekuambieni kwamba jeshi la adui limejificha nyuma ya milima hiyo, na lilikuwa linawataza­ma ili lije kuwashambulia haraka sana kama mkilala au mkijisahua?" Walisema wangemwamini yeye kwa sababu walikuwa hawajamsikia akisema uongo.

Muhammad alisema: "Kama ni hivyo, hasi sikilizeni kwa makini. Mola wa mbingu na dunia ameniamuru kuwaonya ninyi kuhusu kipindi kibaya kijacho. Lakini kama mkizingatia, hamtaangamia…" Abu Lahab ambaye alikuwepo aliingilia kati kwa mara ya pili na kusema: "Kifo kiwe juu yako. Umepoteza muda wetu kutuambia hili tu? Hatutaki kukusikiliza. Usituite tena."

Tangu hapo Abu Lahab aliifanya ni desturi kumghasi Mtume popote alipokwenda. Kama alianza kusoma Qur'an au kusema jambo fulani, Abu Lahab alimkatiza au alimbabaisha. Chuki ya Abu Lahab kwa Muhammad na Uislamu pia ilifanywa na mkewe (Abu Lahab) Umm Jameel. Wote wawili walilaaniwa na Mwenyezi Mungu, kwa ukaidi wao, kwenye Sura ya 111 ya Kitabu Chake.