read

Sura Ya Tano: Mwanzo Wa Kutangazwa Kwa Uislamu

Pamoja na ukweli kwamba nchi ya Arabuni ilikuwa dimbwi la dhuluma na ngome ya ibada za masanamu na kumshirikisha Mwenyezi Mungu, Muhammad mwenyewe hakushiriki katika uovu huo na hakutenda dhambi, na hakulisujudia hata sanamu moja. Hata kabla ya kutangaza kwamba alikuja kuanzisha Ufalme wa Mbinguni hapa Duniani, mwe­nendo na tabia yake ulionyesha maelekezo ya Qur'an Majid - Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Rasimu ya Uislamu.

Hata maadui zake hawakuweza kuonyesha tofauti baina ya tabia yake na maandiko ya Qur'an- wakati wowote - kabla na baada ya kutangaza ujumbe wake ya kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Baada ya Kutangaza ujumbe wake kama Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, alipiga marufuku uendeshaji wa mila za upagani. Lakini hakuna ushahidi kwamba kabla ya tukio hilo, yeye mwenyewe alikwisha jihusisha na tendo la upagani, au tendo lolote linalopingana na Qur'an.

Inaonyesha kama vile Qur'an Majid iliandikwa kwenye moyo wa Muhammad toka mwanzo hadi mwisho na inaonyesha pia kwamba ali­hubiri Uislamu hata kabla ya kutangazwa kwa ujumbe wake, lakini, kwa matendo yake na si maneno yake.

Matendo yake yalieleweka wazi kama maneno yake, na yaliitangazia dunia kwamba yeye alikuwa mtu wa aina gani. Hata hivyo, wapagani ndio waliompa jina la As-Sadiq (Mkweli) na Al-Amin (Mwaminifu), na watu hao hao ndio, baada ya miaka kupita, walimtesa, walimuwinda, walimtenga na walikuwa tayari kumpa zawadi mtu atakayemuua.

Mwenendo wa maisha ya Muhammad ulihubiri mahubiri ya kimya kimya!

Pamoja na kwamba wapagani wa kiarabu walikuwa wapotofu na wako­rofi, hata hivyo walivutiwa na ukweli na uliwavutia hata kama ulikuwa kwa adui. Walivutiwa na Muhammad kwa sababu ya ukweli wake, laki­ni mapenzi yao hayakuwazuia wao kufanya njama ya kutaka kumuua aliposhutumu ibada za masanamu na ushirikina. Hawakupenda kitu kingine kama kumuua tangu hapo alipowaambia waingie kwenye Uislamu, lakini hawakuhoji hadhi yake na uaminifu wake.

Kwa jambo hili hapawezi kuwa na ushahidi wa kutokutuhumiwa zaidi kuliko tabia yao.

Raia wa Makka hawakupenda uaminifu wa Muhammad tu lakini pia walipenda uamuzi wake. Ilitokea wakati fulani, Maqurayshi walikuwa wanaijenga upya Kaaba, na kwenye mojawapo ya kuta zake ilitakiwa Jiwe Jeusi libandikwe. Palihitajika mtu alilete Jiwe Jeusi kwenye eneo la jengo, alinyanyue kutoka chini na kuliweka mahali pake ukutani. Nani angeifanya kazi hiyo?

Kila ukoo wa Quraysh ulidai heshima ya kustahili kufanya kazi hiyo lakini koo nyingine hazikuwa tayari kushindwa katika jambo hili.

Kutokukubaliana huko kulisababisha kutolewa hotuba zenye kuashiria vita, na haikupita muda mrefu watu walikuwa tayari kupigana. Mapigano hayo yangeamua nani angeweka Jiwe Jeusi kwenye ukuta.

Wakati huo huo mzee mmoja wa Kiarabu aliingilia kati, na kushauri kwamba badala ya kupigana na kuuana, Wakuu wa koo wangoje mpaka kesho yake asubuhi waone nani angekuwa mtu wa kwanza kuingia kwenye eneo la Al-Kaaba, na halafu wapeleke kesi hiyo kwake kwa uamuzi.

Ushauri huo ulikuwa wa busara na wakuu walitumia hekima kuukubali. Asubuhi ya siku iliyofuata, lango la Al-Kaaba lilipofunguliwa wal­imuona mtu wa kwanza aliyeingia ni yule aliyepewa majina ya Sadiq na Al-Amin. Wote walifurahi kwamba alikuwa yeye, na wote walikubaliana kupeleka shauri lao kwake, na kuahidi kukubali uamuzi wake.

Muhammed aliagiza nguo iletwe na itandikwe chini. Halafu akaliweka Jiwe juu ya nguo hiyo, na alimtaka kila mkuu wa ukoo anyanyue mojawapo ya pembe ya nguo hiyo, na kubeba mpaka chini ya ukuta wa Al-Kaaba. Baada ya kufanyika hivyo, yeye mwenyewe alilinyanyua Jiwe na kuliweka mahali pake.

Uamuzi wa Muhammad ulimridhisha kila mmoja. Kwa kutumia hekima yake, alizuia yasitokee mambo ya kufedhehesha na aliondoa umwagaji damu.

Tukio hilo pia lilithibitisha kwamba wakati wa machafuko, Waarabu waliheshimu maoni yake. Walijua kwamba Muhammad alikuwa na sifa za kiwango cha juu kulingana na mizani ya maadili yao.

Muhammad alikuwa kiongozi wa binadamu aliyefanya kazi hiyo kwa msukumo wa wahyi.

Bwana Willam Muir

“Hali iliyosababisha fursa ya Muhammad kutoa uamuzi wakati Al-Kaaba ilipokuwa inajengwa upya na kuweka Jiwe Jeusi mahali pake, inavutia kuonyesha kwamba hapakuwepo na chombo chenye mamlaka kuu hapo Makka.”

(The Life of Muhammed, London, 1877).

Wakati huu Muhammad alikuwa na umri wa miaka 35. Mashavu yake yalionyesha rangi ya fedha iliyofifia. Alikuwa mtu ambaye aliyeipenda sana familia yake, alikuwa anawapenda sana watoto. Watoto wake wanaume, Qasim na Abdallah, walikufa wakiwa wachanga. Baada ya vifo vya watoto wao, yeye na Khadija walimchukua Ali kuwa mtoto wao wa kiume. Ali alikuwa mtoto mdogo zaidi ya watoto wote wa ami na mlezi wa Muhammad, Abu Talib.

Alikuwa na umri wa miaka mitano alipokuja nyumbani kwao, na aliziba pengo katika maisha yao, walim­lea na kumsomesha. Hadi alipokua, alikuwa katikati ya mapenzi yao.

Katika miaka iliyofuata, Ali alijionyesha kwamba alikuwa natija bora sana ya malezi na elimu ambayo Muhammed na Khadija walimpa. Ali alikuwa na bahati ya kuwa kijana hodari katika msafara wote wa Muhammad, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu.

“Mara baada ya Al-Kaaba kujengwa upya, Muhammad alijiliwaza kutokana na hasara ya kumpoteza mtoto wake mchanga Qasim kwa kumfanya Ali, mtoto wa rafiki yake na mlezi wake huko nyuma, Abu Talib, kuwa mwanawe.

“Ali wakati huo akiwa na miaka mitano au sita, wakati wote alikuwa na Muhammad na walionyeshana huba ya mzazi na mtoto.”

(The Life of Muhammed, London, 1877.)

Kama ambavyo imeelezwa kwenye kurasa za nyuma, Muhammad ali­jaaliwa akili ya tafakuri sana. Jinsi muda ulivyopita, alizidi kuwa kati­ka hali ya kutafakari, alikwisha gundua pango liitwalo Hira, lililopo maili tatu kwenye vilima vilivyopo Kaskazini Mashariki ya Makka.

Ili kuondokana na fadhaa za kutoka nje na usumbufu wa aina yoyote, wakati wa kutafakari, alihama jiji,
alikwenda kwenye vilima na alipi­tisha siku zake nyingi za msimu wa kipupwe huko katika pango la Hira.

Wakati mwingine Muhammad Mustafa alikwenda Hira peke yake, laki­ni mara nyingi alikuwa anamchukua Khadija na kijana mdogo Ali. Wote watatu walipitisha siku yote juu ya kilima cha Hira walirudi nyumbani jioni.

Kutoka kwenye majabali ya Hira, Muhammad aliweza kutazama mand­hari ya ukubwa wa mbingu na dunia, na kwa mshangao wa kimya ali­fikiria mahali zilipokutana.

Vipi mtu ataweza kutambua ukubwa wa Muumba Ambaye ameumba ukubwa huo na Ambaye huudhibiti wote? Kipi kilichokuwa cha kushangaza sana kama nyota zimemetukazo kati­ka anga iliyotulizana, au kama kuvutia sana kama yalivyo majaliwa ya mwanadamu? Na je, mtu yeyote anaweza kupima siri ya dhana mbili kubwa ambazo zimeshikilia ulimwengu - anga (Makan) na zama (Zaman)? Muhammad alitafuta majibu ya maswali ambayo hushika­mana na siri za kudumu za kuwepo kwa mwanadamu.

Kwa maoni yake, Uumbaji wote ulifunikwa kwenye ghaibu. Alitumia muda wa saa nyin­gi akitafakari juu ya akili ya kutisha na uthabiti wa Uumbaji.

Lakini kama ulimwengu ulivyokuwa wa siri, ilikuwa dhahiri kwa Muhammad kwamba ulitawaliwa na sheria zisizobadilika. Alikuwa takriban anaona utaratibu na mfumo huo ukifanya kazi, bila ya utarati­bu na mfumo huo matokeo yake yangekuwa vurugu tupu kwenye Uumbaji wa mbingu na dunia.

Miaka michache baadaye Muhammad alipowaambia Waarabu kwamba Mungu amemtuma miongoni mwao ili awe mjumbe Wake, walimpa changamoto wakimtaka awaonyeshe "mujiza." "Mujiza?" aliuliza Muhammad.

Kuona mujiza, walichotakiwa kufanya ni kufungua macho yao na kutazama kile kilicho wazunguka. Je! Si kweli kwamba ulimwengu umejaa miujiza? Kuna miujiza yenye kustaajabisha zaidi ya kuchomoza na kuchwa kwa jua, mwezi mpevu ulioko kwenye mwendo kukatiza anga, nyota zilizopo kwenye mizunguuko, mbingu yenye nuru na joto, mabadiliko ya majira, kina cha bahari kinachobadilika, na mapenzi ya mama kwa mtoto?

Kama ukubwa na utukufu wa Uumbaji ulijaza akili ya Muhammad mshangao, pia moyo wake ulijaa unyenyekevu. Inaweza kuwa ilitokea kwake kwamba kama akili haikuweza kumtambua Muumbaji na kazi zake nzito, labda mapenzi yangeweza. Kwa hiyo, aliruhusu akili kuzidi­wa na mapenzi - mapenzi kwa Muumbaji wake.

Pia Muhammad alitafakari kuhusu hali ya Waarabu, ibada zao za masanamu, tamaa yao ya kuua, na kuua watoto wa kike, na maisha yao yasiyo na maana, mwelekeo, matumaini na ya kuhuzunisha.

Lakini, miaka mingi ya "mazoezi ya kiroho" na uvumbuzi wake wa pekee kuhusu miliki ya roho, ilikuwa inakaribia kufikia mwisho.

Inawezekana alikwisha ona kwamba muda wa kuacha maisha ya kufikiri na kutafakari ulifika, na kwamba baada ya muda mfupu alikuwa anatumbukia kwenye utekelezaji wa vitendo na mapambano.