read

Sura Ya Tisa: Hamza Aukubali Uislamu - 615 A.D.

Muhammad Mustafa, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.), ingawa alikuwa salama kutokana na ulinzi wa ami wake Abu Talib, si kwamba yeye hakufanyiwa fujo na makafiri. Kila walipopata fursa ya kumnasa, hawakumkosa. Ilitokea wakati fulani, Abu Jahl alimkuta akiwa peke yake na alitumia lugha ya matusi machafu kumtukana Mtume.

Jioni hiyo hiyo, ami wake, Hamza bin Abdul Muttalib alirudi nyumbani kuto­ka safari ya kuwinda, mtumwa wake wa kike alimweleza kuhusu tukio la Abu Jahl kumtukana Muhmammad, na jinsi Mtume alivyo vumilia na kwamba yeye alishuhudia hayo kwa macho yake.

Hamza alikuwa shujaa, mwindaji na mwana michezo, na hakuwa anapendelea kujua yanayo tokea mjini Makka kila siku. Lakini, tabia ya Abu Jahl kwa mpwa wake ilimkasirisha mno hivyo kwamba alichukua upinde wake na kwenda kwenye mkusanyiko wa Maquraysh ambapo Abu Jahl alikuwa anatoa maelezo kuhusu matukio ya siku hiyo kwa wenzake, alimpiga kichwani kwa upinde na kuanza kutoka damu na akasema kwa sauti ya juu sana "Mimi pia nimesilimu na kuukubali Uislamu."

Hii ilikuwa changamoto kwa Abu Jahl lakini aliona kwamba ukimya ulikuwa sehemu muhimu sana ya ushujaa, na hakugombana (hakupam­bana) na Hamza, pia akawazuia marafiki zake ambao walitaka kuamka kwa ajili ya utetezi wake.

Hamza akawa Mwislamu wa dhati na shujaa wa Uislamu. Akawa rafiki mkubwa wa mpwa wake mwengine Ali bin Abi Talib, na ilikuwa ni wao wawili walioua wapiganaji wa jeshi la Makka kwenye vita ya Badr - vita ya kwanza ya Uislamu ambayo ilipiganwa miaka michache baada ya Hamza kuwa Mwislamu.

Vita ya Uhud ilikuwa vita ya pili ya Uislamu. Kwenye vita hiyo, Hamza alimuua mbeba bendera mmoja wa jeshi la wapagani wa Makka.

Walipo shambulia safu ya Waislamu, Hamza aliingia kati yao. Alikuwa anawakatakata miongoni mwao, huku akisonga mbele ambapo Wahshi mtumwa kutoka Abyssinia alitupa mkuki na kumchoma Hamza tumboni, alianguka na kufa hapohapo. Wahshi aliajiriwa na Hinda, mke wa Abu Sufyan na mama wa Muawiya kwa lengo la kumuua Hamza.

Kwenye vita ya Uhudi Waislamu walishindwa. Baada ya ushindi wao Hind, na wakatili wengine aliokuja nao kutoka Makka, waliikatakata miili ya Waislamu waliouawa. Hind alipasua tumbo la Hamza, akachukua ini na kulitafuna. Muhammad bin Umar Waqidi, mwanahis­toria, anasema kwamba, Hind alikoka moto kwenye uwanja wa vita, na akachoma moyo na ini la Hamza akala.

Hakutosheka na hilo, alikata miguu, masikio na pua ya Hamza akavitunga kwenye kidani chake na akaingia Makka akiwa amevaa kama alama ya ushindi.

Hamza alimuua Utba, baba ya Hind, kwenye vita ya Badr. Kwenye vita ya Uhud alikuwa na hamu ya kulipiza kisasi jambo ambalo lilikuwa linamnyima raha tangu vita ya Badr.

Muhammad Mustafa, Mtume wa Mungu, alisikitishwa sana na kifo na kukatwakatwa vipande mwili wa mkereketwa wa Uislamu kama Hamza. Alimpa vyeo vya "Simba wa Mungu" na "Mkuu wa Mashahidi."

Hamza alisilimu mnamo mwaka wa tano baada ya kutangazwa kwa Uislamu. Mwenyezi Mungu na Amridhie na Amneemeshe.