read

Mlango Wa 10: Kanuni Muhimu Za Sheria (Fiqh)

Kwa Ajili Ya Akina Mama

Nifaas Ni Nini?

Kuanzia wakati pale kuzaliwa kwa mtoto kunapotokea, ile damu anayoiona mama mzazi ni Nifaas, madhali inasimama kabla au katika kukamilika kwa siku ya kumi. Ambapo katika hali ya Nifaas, mwanamke anaitwa Nafsa.

1. Ile damu ambayo mama anaiona kabla ya kutokeza kwa kiungo cha kwanza cha mtoto sio Nifaas.1

2. Inawezekana kwamba damu ya Nifaas inaweza ikatoka kwa muda mfupi tu, bali kamwe haizidi
siku kumi.2

3. Ni muhimu kwamba mtoto anakuwa kikamilifu. Hata kama mtoto mwenye upungufu (wa muda wa mimba yake) atazaliwa, ile damu anayoiona mama mzazi huyo kwa muda wa siku kumi itakuwa ni Nifaas. Maneno ‘kuzaliwa mtoto’ lazima yatumike kwake.3

4. Endapo mwanamke anakuwa na mashaka kwamba ameharibu chochote (mimba) au hapana, sio lazima kwa yeye kufanya uchunguzi, na ile damu ambayo inatoka katika hali hiyo sio Nifaas. 4

Mambo ambayo ni wajibu na yale ambayo yamekatazwa au kuharamishwa kwa mtu aliyeko katika hali ya Nifaas.

Kwa msingi wa tahadhari, kukaa ndani ya Msikiti na vitendo vingine ambavyo vimeharamishwa kwa mwanamke mwenye hedhi vilevile vime- haramishwa kwa mwanamke Nafsa na vile vitendo ambavyo ni wajibu kwa mwanamke mwenye hedhi pia ni wajibu kwa Nafsa.5

Nifaas Inachukua Muda Gani?

Inawezekana kwamba damu ya Nifaas ikaweza kutoka kwa muda mfupi tu, lakini kamwe haizidi siku kumi. Kwa kutegemea tabia ya kawaida ya mwanamke mwenye hedhi, kanuni za urefu wa Nifaas zinatofautiana kama ifuatavyo:6

1. Kwa Mwanamke Mwenye Tabia Ya Kudumu Ya Hedhi:

a. Nifaas yake itakuwa sawa na kitambo cha muda wa hedhi.

b. Kama tabia yake ni chini ya siku kumi, baada ya muda huu anayo fursa ya kuacha swala yake hadi siku kumi, au afanye kama mustahadha (mwanamke aliyeko kwenye hali ya Istihaadha); hata hivyo, ni bora kuziacha swala kwa siku moja (zaidi ya idadi ya zile siku alizokuwa na kipindi kabla ya mimba).

c. Endapo hata hivyo, damu hiyo itaendelea kuonekana hata baada ya siku kumi, basi siku zote baada ya kipindi na kawaida cha hedhi, mpaka ile siku ya kumi, itakuwa ni istihaadha, na ni lazima afanye kadha ya kila kitendo cha ibada ambacho hakikufanyika katika wakati huu hadi siku ya kumi (kwani atakuwa amefuata kanuni za istihaadha baada ya siku ya kumi kwa vyovyote).

d. Anapokuwa kama mustahadha, ni lazima ajiepushe kutokana na vitendo haramu kwa mwanamke Nafsa vile vile mpaka siku ya kumi na nane.

Kwa mfano: Kama muda wa hedhi ya mwanamke wakati wote imekuwa ni siku sita na damu yake ikamtoka kwa zaidi ya siku sita, anapaswa kuzifanya siku sita kama Nifaas na ile siku ya 7, 8, 9, 10, (kama kutokwa na damu hakuzidi siku kumi) itakuwa ni fursa ya hiari yake ama kujizuia na vitendo vyote vya ibada au kutwaa kanuni za istihaadha.

Endapo hata hivyo, anaona damu kwa zaidi ya siku kumi, zile siku zote za ziada ya muda wake wa desturi wa hedhi utahesabiwa kama siku za istihaadha na itabidi kufanya kadha ya swala zilizokosekana kuswaliwa kama alichagua kujizuia na vitendo vyote vya ibada katika ile siku ya saba, ya nane, ya tisa na ya kumi.

2. Kwa Mwanamke Ambaye Hana Desturi Ya Kudumu Ya Hedhi

a. Nifaas yake itakuwa kwa siku kumi, na zinazobakia zitakuwa istihaadha.

b. Ni tahadhari inayoshauriwa kwamba pale unapojichukulia kama aliye mustahaadha, ujiepushe na vitendo vilivyoharamishwa kwa mwanamke Nafsa kuanzia ile siku ya 10 hadi siku ya 18. Wakati kipindi cha Nifaas kinapokuwa kimekwisha: 7

Pale mwanamke anapokuwa amesafika kitohara kutokana na Nifaas, ni lazima achukue josho (ghusl) na afanye vitendo vya ibada. Endapo ataona damu tena mara moja au zaidi, kuna uwezekano namna mbili:

1. Jumla ya idadi ya siku ambamo damu inaonekana mara tu baada ya kujifungua na zile siku zinazoingilia kati wakati anapokuwa msafi kitohara ni siku kumi au chini yake, basi yote hiyo itakuwa ni Nifaas. Katika zile siku zinazoingilia kati, kama tahadhari, atachukua wudhuu na kuswali kama mwanamke mwenye tohara na kujiepusha vile vile na vitendo ambavyo ni haramu kwa mwanamke aliyeko kwenye Nifaas. Hivyo, endapo alifunga saumu, atazilipia kadha yake.

2. Endapo ile damu ambayo aliiona baadae itazidi siku kumi hapo tena, kanuni zinatofautika kutegemea juu ya tabia ya kawaida ya hedhi ya mwanamke huyo:

A. Kwa Mwanamke Mwenye Tabia Ya Kudumu Ya Hedhi:

Kama tahadhari, ni lazima aichukulie ile damu iliyoonekana baada ya kipindi cha hedhi cha kawaida kuwa ni istihaadha; kwa hiyo lazima afanye kama aliye mustahaadha, na vile vile ajiepushe na yale yote ambayo ni haramu kwa mwanamke nafsa.

B. Kwa Mwanamke Asiye Na Tabia Ya Kudumu Ya Hedhi:

Lazima azihesabu zile siku kumi za mwanzo kama Nifaas, na zinazobakia ziwe kama ni istihaadha. Kubainisha Hedhi. 8 Kanuni za kubainisha hedhi ya kwanza ya mwanamke baada ya kujifungua mtoto tena ni ya kutegemea juu ya tabia ya kawaida ya hedhi ya mwanamke huyo.

1. Kwa Mwanamke Mwenye Tabia Ya Kudumu Ya Hedhi:

a. Kama damu itaonekana mfululizo kwa mwezi mmoja au zaidi baada ya kumzaa mtoto, ile damu inayoonekana kwa zile siku zinazolingana na kawaidi yake ya hedhi itakuwa ni Nifaas, na ile damu inayoonekana baada ya hapo kwa muda wa siku kumi itakuwa ni istihaadha, hata kama itaangukia wakati mmoja na tarehe zake za hedhi ya kila mwezi.

b. Baada ya kupita kwa zile siku kumi za istihaadha, endapo kutokwa na damu kutaendelea, basi hiyo ni hedhi kama itaangukia kwenye siku za desturi ya kawaida, bila ya kujali kama inazo dalili za hedhi9 au hapana. Kama kuvuja damu hakutokei katika siku za hedhi ya kawaida, ni lazima asubiri mpaka zile siku za kawaida, hata kama itamaanisha kusubiri kwa mwezi au zaidi na hata kama damu ina dalili za hedhi.
Kwa mfano: Mwanamke ana tabia ya kudumu ya hedhi ya kuanzia tarehe 20 hadi 27 ya kila mwezi.

Anajifungua mnamo tarehe 10 ya mwezi, na anaendelea kuona damu kiasi cha mwezi au zaidi; Nifaas yake itakuwa siku saba, sawa na siku za hedhi yake, na itakuwa ni kuanzia tarehe 10 ya mwezi huo hadi tarehe 17; sasa, ile damu anayoendelea kuona kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 27, yaani kwa muda wa siku kumi, hii itakuwa ni isti- haadha hata kama inaangukia katika siku za tabia yake ya hedhi.

c. Kama hana tabia maalum ya muda wa kuanza kwa hedhi, lazima afanye juhudi ya kutambua hedhi yake kwa dalili zake, na endapo hiyo itakuwa haiwezekani (kwa sababu damu inayoonekana baada ya Nifaas mara nyingi hubakia ya namna moja kwa mwezi mzima au zaidi), basi anapaswa kutwaa tabia iliyopo kwa wakati huo miongoni mwa ndugu zake wa damu (mama, dada zake, na kadhalika) ili kuamua siku za hedhi yake. Kama hilo nalo haliwezekani, basi anayo hiari ya kuchagua kupanga siku zake za hedhi.10

2. Kwa Mwanamke Asiye Na Tabia Ya Kudumu Ya Hedhi:

a. Kama ilivyoelezwa mapema, ile damu inayoonekana katika ule muda wa siku kumi za mwanzo itafanywa kuwa ni Nifaas, na kuhusu zile siku kumi zinazofuatia itakuwa ni istihaadha. Damu itakayoonekana baada ya hapo inaweza ikawa ama ni hedhi au istihaadha, na ili kuhakikisha kama ni hedhi, anapaswa kufuata kanuni kama hiyo hapo juu, yaani, kuitambua hedhi kwa dalili zake, kwa tabia iliyopo wakati huo miongoni mwa ndugu zake wa damu, au kupanga siku zake mwenyewe za hedhi.

Mikojo Ya Mtoto

Kuvifanya vitu kuwa safi kitohara kutokana na mikojo ya mtoto anayenyonya: Endapo kitu chochote kinakuwa najisi kutokana mikojo ya mtoto anayenyonya, ambaye bado hajaanza kula chakula chochote kigumu, na, kama tahadhari, yuko chini ya umri wa miaka miwili, kitu hicho kitakuwa tohara kama kitamwagiwa maji mara moja juu yake, yakifikia sehemu zake zote ambazo zimenajisika. Kama tahadhari inayoshauriwa, maji yanapaswa kumwagwa juu yake mara nyingine tena. Kama ni zulia au nguo na kadhalika, haitakuwa lazima kuikamua.11

 • 1. Sheria za Kiislam, Kanuni ya 515
 • 2. Sheria za Kiislam, Kanuni ya 517
 • 3. Sheria za Kiislam, Kanuni ya 516
 • 4. Sheria za Kiislam, Kanuni ya 518
 • 5. Sheria za Kiislam, Kanuni ya 519
 • 6. Sheria za Kiislam, Kanuni ya 523, 524, 525, 526
 • 7. Sheria za Kiislam, Kanuni ya 520
 • 8. Sheria za Kiislam, Kanuni ya 525
 • 9. Dalili za hedhi: Kwa kawaida ni damu nzito na yenye joto na rangi yake ni ama nyeusi au nyekundu. Inatoka kwa nguvu na muwasho kidogo.
 • 10. Tafadhali rejea kwenye mlango wa Hedhi wa kitabu Risalah kwa taarifa zaidi.
 • 11. Sheria za Kiislam, Kanuni ya 162