read

Mlango Wa 8: Baada Ya Kujifungua

Vyakula Vinavyopendekezwa

1. Tende Safi

1. Tende Safi 1

a) Imesimuliwa kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Kitu cha kwanza mwanamke anachopaswa kula baada ya kujifungua kiwe ni ratb (aina ya tende freshi), kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu alimwambia Hadhrat Maryam baada ya kumzaa Nabii Isa ale ratb.” 2

Alipoulizwa, “Je kama sio msimu wa ratb iweje?” Yeye akajibu akasema: “Basi ale tende tisa kutoka Madina, na kama hizo nazo hazi patikani, basi tende zozote tisa zitatosha. Hakika Mwenyezi Mungu amesema: “Naapa kwa Heshima na Utukufu Wangu, kwamba mwanamke yeyote ambaye amezaa hivi punde na akala ratb, nitamfanya mwanawe kuwa mwenye subira.’”

b) Imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba lisha tende aina ya Birmi kwa mwanamke baada ya kuzaa mtoto wake ili kwamba mtoto huyo awe jasiri na mwenye subira.

c) Kula tende sio tu kwamba kuna manufaa kwa mama huyo bali kuna athari kwenye maziwa ya kifuani vilevile, na pia ni kwenye manufaa zinapolishwa watoto.3 Kwa vichanga vinavyoanza kuzaliwa, imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba weka kajipande kadogo katika kinywa cha kitoto hicho, na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alifanya hivyo kwa Imam Hasan na Imam Husein (a.s.).

2. Maji Ya Mto Furati Na Khakhe Shafaa

2. Maji Ya Mto Furati Na Khakhe Shafaa4 (Juu Ya Kipaa Cha Mdomo Wa Mtoto)

a. Imesimuliwa kwamba maji ya Furati na khakhe shafaa yawekwe kwenye mdomo wa mtoto, na kama maji ya mto Furati hayapatikani, basi maji ya mvua badala yake.5Na6

b. Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba khakhe shafaa inapaswa kuwekwa kwenye kinywa cha mtoto, kwani hii inamkinga na maumivu na majonzi.7

c. Katika riwaya nyingine kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.), inasimuliwa kwamba yeye amesema: “Hakuna mtu ambaye anakunywa maji ya mto Furati na akayaweka kwenye mdomo wa mtoto isipokuwa kwamba yeye ni rafiki yetu, kwa sababu Furati ndio mto wa mu’min.8

3. Nyingineyo

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba wakati mtoto anapozaliwa, chukua kiasi cha maziwa kutoka kwa mama yake (kipimo cha mbegu ya adesi), yachanganye na maji na uweke matone mawili katika tundu ya pua ya kulia ya mtoto huyo, na kisha ya kushoto, na usome Adhana katika sikio lake la kulia na Iqaamah katika sikio lake la kushoto, kabla hawajakata kiunga mwana kutoka kitovuni mwake. Kama hili likifanyika, hofu haitamfika mtoto huyo kamwe na Umm Sabyaan (jinni subiani) hatamsumbua kamwe. 9

Matendo Yanayoshauriwa

1. Ukubalikanaji Wa Mtoto, Awe Wa Kiume Au Wa Kike

Kwa bahati mbaya, hata leo hii, wengi bado wanayo ile kasumba kwamba watoto wa kike hawafai na kuwashughulikia watoto wa kiume na wa kike kwa tofauti. Ambapo, iko wazi kabisa ndani ya Qur’ani Tukufu kwamba mtoto ni kiumbe cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Yeye anajaalia mtoto wa kiume kwa yeyote amtakaye na mtoto wa kike kwa amtakaye. 10

Inasimuliwa kwamba wakati pale Imam Zainul-Abidiin (a.s) alipobashiriwa habari njema za kuzaliwa kwa mwanawe, yeye hakuuliza iwapo kama alikuwa wa kiume au wa kike, bali hasa kwanza aliuliza, maumbile (umbo) yake yako sawasawa?

Kisha alipoambiwa kwamba mtoto huyo alikuwa mwenye afya njema na hakukuwa na dosari yoyote katika maumbile yake, yeye alisoma haya: “Alhamdulillahi al-ladhiy lam yakhluq miniy shaiyaan mushawwahaan”

“Sifa zote ni za Mwenyezi Mungu ambaya hakuumba kutoka kwangu kitu chenye umbo lisilo sawa.”11

Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Ni jambo la neema kwa mwanamke kwamba mtoto wake wa kwanza awe ni wa kike.”12

Imesimuliwa kwamba mabinti ni wema na neema na vijana ni fadhila. Mtu ataulizwa kuhusu fadhila alizopewa, ambapo wema na neema vitaongezwa.13

2. Kusoma Adhana Na Iqaamah

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ameeleza kwamba yeyote ambaye atazaliwa mtoto, anapaswa kumsomea Adhana kwenye sikio lake la kulia na Iqaamah kwenye sikio la kushoto, kwani hili ni ulinzi kutokana na uovu wa Shetani.14

Kwa kuongezea, katika simulizi nyingine imeelezwa kwamba mkunga au mtu mwingine lazima aambiwe amsomee Iqaamah katika sikio la kulia ili jinni asije akamsumbua mtoto, wala asije akawa mwendawazimu. 15

Imesimuliwa vilevile kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alithibitisha kwamba zilisomwa Adhana na Iqaamah kwenye masikio ya Imam Hasan (a.s.) na Imam Husein (a.s.), na pia Suratul-Fatiha, Ayatul-Kursi, mwisho wa Suratul-Hashir, Suratul-Ikhlaas, Suratul-Falaq, na Suratun-Naas.16

3. Nguo Za Mtoto

Kutoka kwenye hadithi wakati wa kuzaliwa Imam Hasan (a.s.) na Imam Husein (a.s.), ni dhahiri kwamba ni makuruhu kumfunga mtoto kwenye nguo ya manjano mara tu baada ya kuzaliwa; bali inapendekezwa kumfunika kwenye nguo nyeupe.17

4. Josho (Ghusl)

Imeelezwa katika kitabu Fiqh al-Ridhaa kwamba moja ya mambo yanay- opendeza (mustahab) lililosisitizwa sana (wengine wanadiriki hata kuliita la wajibu) baada tu ya kuzaliwa kwa mtoto ni kumpatia mtoto huyo Ghusl. Mtu lazima aweke nia kwamba ninampa mtoto huyu ghusl kwa ajili ya radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu na halafu kwanza aoshe kichwa chake, kisha upande wa kulia na halafu upande wa kushoto.18

Hata hivyo, inapasa ifahamike kwamba hili linapaswa kufanyika tu iwapo lina usalama kiafya na sio lenye madhara kwa mtoto huyo.

5. Kunyoa Nywele

5. Kunyoa Nywele 19

Hii inahusisha unyoaji wa nywele zote za mtoto (anayetoka tumboni) mara tu baada ya kuzaliwa, na kutoa dhahabu au fedha kulingana na uzito wa nywele hizo kama sadaqah. Halafu nywele hizo zizikwe ardhini. Inapendekezwa kulifanya hili katika siku ya saba baada ya kuzaliwa mtoto.

Nywele ni lazima zinyolewe zote kabisa bila kuacha kishungi au shole (sokoto) la nywele kwenye paji.Imesimuliwa kwamba mtoto mwenye kishungi aliletwa karibu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.); kisha Mtume hakumswalia mtoto huyo na akasema kwamba kishungi chake kinyolewe kiondoke.
Inashauriwa kwamba baada ya kunyolewa kwa nywele hizo, inapaswa akandwe kwa zafarani kichwani mwake. Ukandaji wa damu ya aqiqah hata hivyo unakataliwa kwa nguvu kabisa na umeitwa ni kitendo cha kijahilia.

6. ‘Aqiqah Na

6. ‘Aqiqah 20 Na 21

Hii inahusisha uchinjaji wa mnyama kwa jina la mtoto kwa ajili ya ulinzi wake. Aqiqah ni sunna iliyokokotezwa sana kwa yeyote yule mwenye uwezo (baadhi wamediriki hata kuiita ni wajibu), na ni bora kama itafanyi- ka katika siku ya saba baada ya kuzaliwa mtoto.22

Kiangalizo: Inashauriwa kwamba huo unyoaji wa nywele, utoaji wa dhahabu/fedha kama sadaka na Aqiqah vifanyike kwenye sehemu moja hiyohiyo na kwa wakati mmoja, ingawaje ni sunna kwamba unyoaji wa nywele ndio ufanyike mwanzo.

Kiangalizo: Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba Aqiqah sio sawa sawa na kafara (qurbaanii)

7. Utahiriwaji Wa Wavulana

7. Utahiriwaji Wa Wavulana23

Kutahiri ni wajibu juu ya wavulana, na pamoja na kunyoa na Aqiqah, inapendekezwa kwamba yafanyike yote katika siku ya saba baada ya kuzaliwa kwa mtoto, ingawaje hili likifanyika kabla ya hapo hakuna madhara.24

Kama haikufanyika wakati huo, ni sunna kwamba ifanyike hadi wakati wa balehe ya mtoto huyo, ambapo baada ya hapo ni wajibu juu ya kijana huyo mwenyewe kuifanya. Hata hivyo, wanavyuoni wengine wameeleza kwamba pale mtoto anapokaribia kubalehe, ni wajibu juu ya mlezi kumfanyia. Hasa imesimuliwa kutoka kwa Imam Ali (a.s.) kwamba mtu anayekuwa muislam anapaswa kutahiriwa, hata kama ana umri wa miaka 80.

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba watoto wanapaswa kutahiriwa kwani kunafanya mwili kuwa msafi zaidi, kunafanya nyama za mwili kukua haraka, na ardhi inachukia sana mkojo wa mtu asiyetahiriwa.

Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwamba ardhi inakuwa najisi kwa siku arobaini kutokana na mkojo wa mtu asiyetahiri- wa, na katika riwaya nyingine, imesimuliwa kwamba ardhi inatoa mkoromo wa huzuni kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa sababu ya mkojo wake mtu asiyetahiriwa.

Imesimuliwa vilevile kwamba endapo utamtahiri kijana, na ile ngozi ya kifuniko ikakua tena na kufunika dhakari, mtahiri tena, kwa sababu ardhi inalalamika kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa muda wa siku arobaini kwa sababu ya kufunikwa kule kutahiriwa kwake.

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.): “Mtu yeyote ambaye hajatahiriwa asiongoze swala, na ushahidi wake haukubaliki, na endapo atafariki (katika hali hiyo) basi msimswalie kwa vile ameacha sunna kubwa sana ya Mtukufu Mtume, isipokuwa kama ameiacha kwa hofu ya kifo ambacho kingetokana na kutahiriwa kwake.” Inashauriwa kusoma du’a ifuatayo wakati wa kutahiri:25

“Ewe Mungu! Hakika (hili tunalofanya) limo katika njia ya Sunnah Yako na Sunnah ya Mtume Wako (s.a.w.w.) kukutii Wewe na dini Yako na kutimiza amri Yako, nia na kutekeleza sheria ambazo umeamua kuzifanya zifuatwe bila masharti. Kwa hiyo umempa muonjo wa joto la chuma kupitia kutahiriwa kwake na kufikwa na jambo ambalo kwa hakika Wewe unalijua vizuri zaidi kuliko mimi. Ewe Allah! basi mtakase na dhambi zake; umuongezee umri; na umuondolee kutoka mwilini mwake magonjwa ya mlipuko na maumivu; na uongeze utajiri wake; na umlinde kutokana na umasikini; kwani kwa hakika Wewe unajua zaidi na sisi hatujui kitu.”

8. Karamu (Walimah)

Hii inahusisha kuwalisha waumini juu ya kuzaliwa mtoto na kwa ajili ya kutahiriwa kwa mtoto huyo (hizi zinaweza kukusanywa na kufanywa kwa pamoja wakati mmoja). Inashauriwa kuwakaribisha ndugu na marafiki mnamo siku ya saba baada ya kuzaliwa kwa mtoto (au karibu na siku hiyo) kushiriki katika tukio adhimu la kuzaliwa kwa kichanga hicho. Imesimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Sherehe na karamu katika siku ya kwanza ni wajibu, kwenye siku ya pili ni vizuri, na kwenye siku ya tatu hiyo ni riyaa (yaani, ni kwa ajili ya watu wengine na sio kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu).” 26
Ni makuruhu kwa waalikwa wote kuwa ni matajiri, bali mchanganyiko wa matajiri na masikini sio tatizo.
Ni mustahab pia kwamba waalikwa waitikie huo mwaliko wa kwenye walimah huo

9. Kutoga (Kutoboa) Masikio

Kutoga masikio ya mtoto huyo ni jambo linalopendekezwa.27

10. Kugusana Kwa Mama Na Mtoto Na Kunyonyesha Na

10. Kugusana Kwa Mama Na Mtoto Na Kunyonyesha28 Na29

Moja ya vitendo bora baada ya kuzaa ni kuogesha mtoto huyo na kisha kumrudisha karibu na ngazo ya mama yake na kuwafunika na blanketi. Nusu saa baada ya kuzaliwa, mtoto anakuwa anatambua kabisa na mchangamfu, na ndio wakati muafaka wa kujizoesha kunyonya na mguso wa mama yake.

Zile siku chache za mwanzo maziwa hayatengenezwi kwa wingi; hata hivyo, kiasi kile kinachotoka kinatosha, kinafaa na muhimu kwa mtoto aliyezaliwa punde. Ni muhimu sana kwamba kuchoka kwa mama na kukosa maziwa (kwa wingi) kusije kukatumiwa kama ni sababu ya kumlisha mtoto kwa chupa kwa hili linasababisha kucheweza kutengeneza maziwa kutoka kwa mama na mtoto kutokuwa na uwezo wa kunyonya sawa sawa. Vile vile kunaongeza uwezekano wa maambukizi kwa mtoto.

Aqiqah - Mtazamo wa karibu zaidi

Aqiqah - Mtazamo wa karibu zaidi 30

Umuhimu Wa Kufanya Aqiqah

Imesimuliwa kwamba maisha ya mtoto yameambatishwa na Aqiqah,31 na endapo kama haikufanyika, inamuanika mtu kwenye taabu na kifo. Kama ikicheleweshwa, ni sunnah juu ya baba mpaka kubalekhe kwa mtoto, na baada ya balehe, inakuwa ni sunnah juu ya mtoto mwenyewe.32

Imesimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba Aqiqah ni muhimu kwa mtu yeyote tajiri, na kama mtu ni masikini, anapaswa kufanya Aqiqah mara tu anapopata pesa, na kama hatapata pesa yoyote, basi ni sawa tu. Endapo mtu hakufanya Aqiqah, na akawa alifanya kafara (qurbaani), hii itatosha.

Imesimuliwa kwamba mtu mmoja alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Tumeomba kondoo kwa ajili ya Aqiqah lakini hatuwezi kupata hata mmoja, je, unashauri nini? Je, tunaweza kutoa thamani ya kondoo huyo kama sadaka badala yake?” Imam alijibu akasema: “Hapana, ombeni mpaka mpate mmoja kwani Mwenyezi Mungu anapenda ulishaji wa wengine …”

Umar ibn Yazid anasimulia kwamba yeye alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.): “Mimi sijui kama baba yangu alinifanyia Aqiqah au hapana.” Imam akajibu akasema: “Itekeleze wewe,” na hivyo akafanya Aqiqah katika umri wa utu uzima wake.

Katika riwaya nyingine imesimuliwa kwamba mtu mmoja alimuuliza Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba endapo mtoto atafariki katika siku ya saba, je, Aqiqah bado inapaswa kufanyika? Imam akajibu kwamba ikiwa mtoto atafariki kabla ya swala ya Adhuhuri, Aqiqah inakuwa sio lazima, bali endapo mtoto huyo atafariki baada ya Adhuhuri, basi itekeleze Aqiqah.

Ni Nini Kinachopasa Kichinjwe

Ni kawaida miongoni mwa ulamaa kwamba Aqiqah iwe ni kondoo, ngamia au mbuzi, na kwamba Aqiqah kwa ajili ya mvulana inapaswa iwe mnyama dume na Aqiqah kwa ajili ya msichana iwe mnyama jike.

Kama ni ngamia, anapaswa awe na umri wa miaka mitano. Kama ni mbuzi inapaswa awe na umri wa mwaka mmoja zaidi ya huo, kama ni kondoo, anapaswa awe angalau na umri miezi sita au zaidi na ni bora kama mwezi wa saba utakuwa umetimia.

Korodani zake zisikatwe na pia ni bora kama hazitapondwa vile vile. Pembe zake zisivunjwe (kiasi kwamba akatoa damu) na masikio yake yasikatwe. Asiwe mwembamba aliyekonda sana, wala asiwe kipofu, wala asiwe kilema sana kiasi kwamba kutembea kunakuwa ni kugumu juu yake.

Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba, kama ilivyosimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.), Aqiqah sio sawa na kafara (qurbaani) ambayo ina shuruti kali kwa ajili ya mnyama anayetolewa kafara.

Kwa hiyo, kama haiwezekani kutekeleza shuruti hizo hapo juu, kondoo yoyote yule ni sawa, ingawa aliyenenepa ni bora zaidi.

Dua Wakati Wa Aqiqah

Wakati33 wa kumchinja mnyama kwa ajili ya Aqiqah, du’a zifuatazo zinapasa kusomwa:

1. Mwishoni mwa du’a hii, mtu lazima ataje jina lake na jina la baba yake [kwa mfano, kama jina la baba ni Taahir na jina la baba yake ni Abdullah utasema, Taahir ibn (mwana wa) Abdullah] Dua hii inaanza na Aya za 78 na 79 za Suratul-An’am zikufuatiwa na Aya za 162 na 163 za Suratul-An’am hiyo hiyo:

“Enyi watu wangu! mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha (na Allah). Mimi nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi, hali ya kuwa nimewacha dini za upotovu, mimi si miongoni mwa washirikina. Hakika swala yangu na ibada zangu na uzima wangu na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola wa ulimwengu wote. Hana mshirika, na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa waliojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu). Ewe Allah! kwa hakika mnyama huyu anatoka Kwako na anarudi Kwako kwa Jina la Allah na Yeye Allah ni Mkubwa kuliko maelezo yoyote yanayoweza kutajwa juu Yake. Ewe Allah! shusha rehma na amani juu ya Muhammad na kizazi chake Muhammad na ikubali hii kutoka kwa (jina lako na jina la baba yako).”

2. Dua ifuatayo pia lazima isomwe wakati mnyama anapokuwa anachinjwa (mtoto huyo akiwa ni mvulana ama msichana).

“Kwa jina la Allah, na kwake Allah, na sifa zote ni zake Mwenyezi Mungu pekee, na Allah ni Mkubwa kuliko maelezo yoyote yanayoweza kuelezwa juu Yake. Kwa imani kamili kwake Allah na mapenzi kwa Mtume wa Allah (s.a.w.w.) na wana shukurani juu ya riziki ya Allah (s.w.t.). na kinga iliyotolewa kwa amri ya Allah na utambuzi kamili na mazingatio juu ya neema Zake juu yetu sisi Ahlil-Bayt.”

Kama mtoto ni mvulana, basi du’a ifuatayo pia inapaswa isomwe:

“Ewe Mungu! Umetuzawadia sisi mtoto mwanaume na Wewe unajua vizuri zaidi ni nini ulichotuzawadia sisi, na kurejea Kwako ni kile tuna- chokifanya sisi - hivyo basi ridhia kutoka (kafara) hili kutoka kwetu juu ya mila (sunnah) Yako na sunnah ya Mtume Wako, (rehma na amani juu yake na juu ya kizazi chake) na utuweke mbali na Shetani aliyelaaniwa. Kwa ajili Yako damu (ya mnyama huyu) imemwagwa, na Wewe huna mshirika na sifa zote njema ni Allah pekee, Mola wa ulimwengu wote.”

3. Dua ifuatayo pia ni lazima isomwe katika wakati wa kumchinja mnya- ma. Pale mtu atakapofikia mabano ya pembe, atataja jina la mtoto huyo na lile la baba yake [kwa mfano, kama jina la mtoto ni Jabir na jina la baba ni Kumayl, basi utasema: Jabir ibn Kumayl] na kisha uendelee na sehemu ya du’a iliyobakia. Maelezo ya kwanza ya du’a hii ni kwa sababa ya mtoto mvulana, du’a ya pili ni iwapo kama mtoto ni wa kike.

“Kwa jina la Allah na kwa Allah, Aqiqah hii (uchinjaji wa mnyama) ni kwa ajili ya [Jina la mtoto na jina la kwanza la baba yake]. Nyama yake badala ya nyama ya mtoto; damu yake badala ya damu yake mtoto; mifupa yake badala ya mifupa ya mtoto vyote vinatolewa Kwako. Ee Allah! ikubali hii kwa ajili kile ambacho kwacho mtoto huyu atakingwa na kuhifadhiwa, kwa jina la kizazi cha Muhammad, rehma na amani ya Allah iwe juu yake na juu ya kizazi chake.

“Kwa jina la Allah na kwa Allah, Aqiqah hii (uchinjaji wa mnyama) ni kwa ajili ya [Jina la mtoto na jina la kwanza la baba yake]. Nyama yake badala ya nyama ya mtoto; damu yake badala ya damu yake mtoto; mifupa yake badala ya mifupa ya mtoto vyote vinatolewa Kwako. Ee Allah! ikubali hii kwa ajili kile ambacho kwacho mtoto huyu atakingwa na kuhifadhiwa, kwa jina la kizazi cha Muhammad, rehma na amani ya Allah iwe juu yake na juu ya kizazi chake.”

Jinsi Gani Itakavyogawanywa?

Inashauriwa kwamba mifupa hiyo isije ikavunjwa; bali inapaswa kuten- ganishwa kwenye maungio yake. Ni bora vile vile kwamba nyama hiyo igawanywe ikiwa imepikwa (kwa angalau na maji na chumvi tu) na ngozi yake kutolewa kama sadaka.

Inapendekezwa kwamba miguu na mapaja ya aqiqah (hii inaweza kuh- esabiwa kama moja ya tatu au moja ya nne ya kondoo huyo kutegemeana na namna ya ugawaji) lazima itolewe kwa mkunga (au daktari) yule aliye- saidia wakati wa kujifungua na iliyobakia itolewe kwa watu iliwe kama sadaka. Ikiwa mkunga au daktari huyo ni Myahudi, basi thamani ya robo ya kondoo huyo lazima itolewe (kumpa yeye badala ya nyama).

Kama mtoto huyo alizaliwa bila ya mkunga au daktari, basi inapasa kutole- wa kwa mama ambaye anaweza kuigawa kwa yeyote anayemtaka yeye; ni lazima yeye aitoe kwa waislamu angalau kumi hivi, na kama anaweza kuigawa kwa wengi zaidi ni bora. Sio lazima kwamba nyama hiyo itolewe kwa masikini tu; hata hivyo, ni bora zaidi kwamba inatolewa kwa wachamungu na masikini.

Inashauriwa kwamba huyo baba na mama (na wale ambao wanawatege- mea wao, kama vile watoto wao na wazazi) wao hawali kutoka kwenye nyama iliyopikwa ya Aqiqah, na hii imesisitizwa hasa kwa mama.

Namna Inayopendekezwa Ya Kumpongeza Mtu Wakati Wa Kuzaliwa Kwa Mtoto

Inasimuliwa kutoka kwa Imam as-Sadiq (a.s.) kwamba alimpongeza mtu mmoja kwa mtoto ambaye Mwenyezi Mungu alikuwa amembariki naye kwa namna ifuatayo (kumekuwa na simulizi nyingi za namna hiyo kutoka kwa Imam Hasan (a.s.) vilevile): 34

“Mwenyezi Mungu akuruzuku na shukurani juu ya alichokujaalia, na akibariki kile alichokujaalia nacho, na amfanye afikie umri wa balekhe, na akujaalie na uadilifu wake mtoto huyu.35

Kumpatia Mtoto Jina

Umuhimu Wa Kumpa Mtoto Jina

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Kadhim (a.s.) kwamba wema wa kwanza ambao baba anaweza kuufanya kwa ajili ya mwanawe ni kumpatia jina36 zuri.

Ni haki ya mtoto kwamba wazazi wake wampatie jina zuri na kumtunza na kumtendea wema.37 Katika riwaya nyingine, imesimuliwa kwamba miongoni mwa haki za mtoto ni pamoja na jina bora, kumfundisha kuandika na kumuozesha wakati anapofikia umri wa utu uzima (balekhe).38

Wakati Gani Wa Kumpa Mtoto Jina

Inasimuliwa kutoka wa Imam Ali (a.s.): “Mtoto anapaswa kupewa jina wakati akiwa bado yuko tumboni, na kama hakupewa jina na mimba ikaporomoka, katika Siku ya Kiyama atakuja kumuuliza baba yake, “Kwa nini hukunipatia jina?” Mtukufu Mtume alimpatia jina Muhsin, mtoto wa Hadhrat Fatimah wakati akiwa yuko tumboni, na Muhsin huyu ni yule mtoto ambaye, baada ya kufariki kwa Mtukufu Mtume, yeye alikuwa bado yuko tumboni wakati Umar alipomfanya kuwa (afe) Shahidi.”

Imesimuliwa kutoka kwa Maimam (a.s.) kwamba: “Mtoto wa kiume haz- aliwi kwetu sisi, Ahlul-Bayt, isipokuwa kwamba anaitwa Muhammad kwa siku saba, na halafu kama ikihitajika, jina hilo linaweza kubadilishwa au kuondolewa.”39

Imeelezwa ndani ya Fiqh al-Ridhaa kwamba weka jina (yaani, tangaza jina hilo kwa wengine) mnamo siku ya saba.

Majina Yanayopendekezwa

Kumwita mtoto kwa majina ya Ahlul-Bayt (a.s.) ni tangazo la wazi la mapenzi na urafiki kwao, na dini sio chochote bali ni mapenzi na urafiki wa Ahlul-Bayt (a.s.) kama Allah (s.w.t.). anavyoelezea ndani ya Qur’ani Tukufu, katika ile Surat al-Imraan; 3:31:

إِنْ كُنْتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ {31}

“Sema: Ikiwa ninyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni mimi Mwenyezi Mungu atawapenda …...” (Al-Imraan; 3:31).

Imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Baqir (a.s.) kwamba majina yanayofaa zaidi kwa ajili ya mtoto ni yale ambayo yanaashiria utumwa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kama vile Abdullah (mtumwa wa Allah), na majina bora zaidi kwa mtoto ni yale ya Mitume.

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema kwamba yeyote aliye na watoto wanne na akawa hajamuita yoyote kati yao kwa jina langu, huyo amenionea mimi.40

Inasimuliwa kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): “Katika nyumba ambamo majina ya baadhi ya watu wake ni yale ya mitume (a.s.), neema za nyumba hiyo hazitatoweka kamwe.41

Katika riwaya nyingine, imesimuliwa kutoka kwa Imam al-Kadhim (a.s.) kwamba umasikini na ufukara kamwe havitaingia kwenye nyumba ambamo jina la Muhammad, au Ahmad, au Ali, au Hasan, au Husein, au Ja’far, au Talib, au Abdullah, au Fatimah linapatikana.42

Imesimuliwa kutoka kwa Imam Husein (a.s.); “Kama ningekuwa na watoto mia moja, ningependelea kuwaita wote kwa jina la Ali.”43

Imesimuliwa kwamba mtu mmoja alikwenda kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na akauliza: “Ametujia (amezaliwa) mtoto wa kiume kwetu, je nimuite jina gani?” Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alijibu akasema: “Muite yeye jina bora kabisa katika majina niliyonayo mimi, nalo ni Hamza.”

Imesimuliwa kutoka kwa Jabir ambaye amesema: Nilikwenda kwenye nyumba ya mtu mmoja nikiwa pamoja na Imam al-Baqir na mtoto mmoja akatoka nje yake. Imam akamuuliza: “Unaitwa nani?” Yeye akajibu akase- ma. “Ninaitwa Muhammad.” Imam akamuuliza: “Ni lipi jina la cheo (kuniyah) chako?” Yeye akajibu: “Ni Abu Ali.” Imam akasema; “Wewe umejitoa kwenye ngome ya Shetani. Kwa kweli, kila wakati Shetani anapomsikia mtu akiitwa Ya Muhammad! au Ya Ali! anatoweka zake na wakati anaposikia mtu akiitwa kwa jina la maadui zetu, yeye anafurahia na anajifaharisha katika hilo.”

Katika hadithi nyingine, inasimuliwa kwamba mtu mmoja alikuja kwake Imam as-Sadiq (a.s.) na akasema kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alikuwa amemjaalia mtoto mwanaume, Imam akampongeza, na akasema, “Wewe umempatia jina gani? Yeye akajibu, “Nimemwita Muhammad.” Imam akageuzia kichwa chake kuangalia chini ardhini na akawa anaendelea kurudia jina hilo Muhammad mpaka uso wake karibu uguse ardhi.

Kisha akasema, “Maisha yangu, watoto wangu, wake zangu, baba yangu, mama yangu na watu wote wa dunia hii watolewe kafara kwa ajili ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Kwa sababu umempa jina lililobarikiwa kiasi hicho, basi usije ukamtukana na usiwe unampiga na usimkaribie kwa ubaya. Na ulijue hili kwamba hakuna nyumba ambamo hili jana la Muhammad linapatikana bali kwamba kila siku nyumba hiyo inafanywa kuwa tukufu na safi halisi.”

Katika riwaya nyingine inasimuliwa kwamba mtu anapaswa kumheshimu binti ambaye jina lake ni Fatimah na asiwe anamtukana yeye na kamwe asimpige.”

Majina ya kivyeo ya Hadhrat Fatimah (a.s.) yanaweza kutumika kwa maji- na ya mabinti:

Mubaraka: Aliyebarikiwa.
Tahira: Aliyetakasika.
Zakiyya: Mwenye hekima.
Radhiya: Aliyetosheka.
Mardhiyya: Aliyeridhiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu
Siddiqah: Aliye mkweli.
Muhaddathah: Ambaye Malaika wanazungumza naye.
Muhaddithah: Anayesimulia hadithi za Mtume (s.a.w.w.).
Zahrah: Mwenye nuru.

Majina Ambayo Hayapendekezwi Kutumika

Katika riwaya kadhaa imesimuliwa kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amekataza kumwita mtoto kwa majina yafuatayo: Haakim, Hakim, Khalid na Maalik.

Na amesema kwamba majina mabaya sana kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Harith, Maalik na Khalid. Na pale jina linapokuwa ni Muhammad, amekataza vyeo (kuniyah) vinne: Abu Isa, Abul Hakim, Abu Malik na Abul-Qasim, kwani vyote, majina na vyeo havikubaliki kwa Mtume (s.a.w.w.).

Katika riwaya moja, imesimuliwa kwamba mtu anapaswa kutomwita mtoto Yaasiin, kwani hilo ni makhususia kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) pekee.

 • 1. Halliyatul Muttaqin, Uk. 125-127
 • 2. Surat Maryam, 19:25
 • 3. Israar Khuuraakiihaa, Uk . 96
 • 4. Udongo mtakatifu wa Karbala, Iraqi.
 • 5. Hii inashauriwa tu kwenye maeneo ambapo mtu ana hakika kwamba maji ya mvua hayakuchafuliwa
 • 6. Al-Kafi, Jz. 6, Uk. 24 hadithi ya 4
 • 7. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 145-146
 • 8. Biharul-Anwaar, Jz. 104, Uk. 114, hadithi ya 33
 • 9. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 126
 • 10. Surat al-Shuraa (42:49)
 • 11. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 21
 • 12. Biharul-Anwaar, Jz. 104, Uk. 98, hadithi ya 64
 • 13. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 6, hadithi ya 8
 • 14. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 24, hadithi ya 6
 • 15. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 126
 • 16. Biharul-Anwaar, Jz. 104, Uk. 126, hadithi ya 86
 • 17. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 146
 • 18. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 130
 • 19. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 132
 • 20. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 120 - 133
 • 21. Aqiqah itakuja kuelezewa kwa kirefu chini ya - Aqiqah: Uchunguzi makini katika mlango huu
 • 22. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 15, Uk. 145, hadithi ya 17807
 • 23. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 134-135
 • 24. Halliyatul Muttaqiin, Uk. 134
 • 25. Kitabu, ‘A Mother’s Prayer’
 • 26. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 16, Uk. 455
 • 27. Wasa’ilush-Shi’ah, Jz. 16, Uk. 134
 • 28. Rayhaaney-e Behesht, Uk. 167
 • 29. Hili limeelezwa kwa kina zaidi katika Mlango wa 9: Kunyonyesha
 • 30. Hilliyatul-Muttaqin, Uk. 130 - 133
 • 31. al-Kafi, Jz. 6, uk. 25, hadithi ya 3
 • 32. Hilliyatul-Muttaqin, Uk. 150
 • 33. Kitabu, ‘A Mother’s Prayer’
 • 34. Hilliyatul-Muttaqin, Uk. 127
 • 35. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 17
 • 36. Hilliyatul-Muttaqin, Uk. 128-130
 • 37. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 15, Uk.128, hadithi ya 17748
 • 38. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 15, Uk.166, hadithi ya 17876
 • 39. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 18, hadithi ya 4
 • 40. Tahdhib al-Balaghah, Jz. 7, Uk. 438, hadithi ya 11
 • 41. Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 15, 129, hadithi ya 17751
 • 42. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 19, hadithi ya 8
 • 43. al-Kafi, Jz. 6, Uk. 19, hadithi ya 7