read

Utangulizi

Ni pale tu tunapofikiri na kutafakari juu ya mwongozo na hadithi zilizosimuliwa na Mtume (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt wake (a.s.) tunapoweza kutambua zile hazina walizoacha kwa ajili yetu sisi. Johari hizi za hekima zinaangaza njia kuelekea Mbinguni kwa kutupatia ushauri na maarifa katika kila hatua kwenye maisha yetu.

Kwa bahati mbaya, nyingi ya johari hizi zinapatikana kwa Kiarabu na Kifursi tu, na kuwaacha wasomaji wa Kiingereza (na lugha nyingine) kijisehemu tu cha kile kinachopatikana, hivyo kuwalazimisha kutegemea moja kwa moja juu ya taarifa za kilimwengu ili kuziba pengo hili.

Mbili ya johari hizi ni mafundisho ya kiislam ya mahusiano ya kijinsia baina ya mwanaume na mwanamke, na upatikanaji wa mtoto halali wa ‘kiungu.’

Taarifa hizi kwa hiyo, zimetafsiriwa kutoka kwenye vitabu mbalimbali vya Kifursi na kukusanywa katika kitabu hiki cha mwongozo. Ni matumaini yetu kwamba hiki kitawapatia wasomaji wa Kiingereza mwon- gozo wa Kiislam utakaounganishwa na kutumika sambamba na taarifa nyingine zote zinazopatikana, kumuwezesha mtu sio tu kupata manufaa yake katika dunia hii, bali kumsogeza mtu karibu na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na Pepo.

Taarifa za ndani ya kitabu hiki cha mwongozo zimeegemea kwenye vyanzo sahihi na vya asili vya mafundisho ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na Ahlul-Bayt wake (a.s.). Mahali ilipowezekana, hadithi kutoka kwa watu hawa watukufu zimejumuishwa ili kuupa umuhimu ule msingi imara wa Kiislam unaounga mkono yale mapendekezo yaliyotolewa, na vilevile kumtia moyo msomaji katika kuwa mzoefu na maneno ya viongozi wetu katika Uislam. Kwa nyongeza, uingizwaji wa hadithi hizi unatia msisitizo umuhimu unaowekwa na Uislam katika kila kipengele cha maisha, kamwe bila kutuacha sisi tukikosa mwongozo katika hatua yoyote ile.

Katika hatua hii ni muhimu sana kueleza kwamba inawezekana kuwa hao Ahlul-Bayt (a.s.) wamezisimulia hadithi hizi katika muda mahususi, mahali au hali, ambayo taarifa kwa bahati mbaya hazijatufikia sisi. Tumejaribu kiasi cha uwezo wetu kuwaletea hadithi kama zilivyosimuliwa katika vyanzo, ili kwamba ziweze kuwa na manufaa na mafanikio.

Kitabu hiki kinaanza na mjadala kuhusu ule usiku wa harusi, pamoja na amali ambazo zimependekezwa kwa ajili ya usiku huu, kuwawezesha Bwana na Bibi harusi kuanza hatua hii mpya ya maisha yao katika njia nzuri zaidi iwezekanavyo. Kisha hii inafuatiwa na mahusiano ya kijinsia na umuhimu wake katika Uislam, na vilevile mapendekezo kwa ajili ya matendo hayo na nyakati ambazo muungano wa kijisia haswa unaoshauri- wa au usiporuhusiwa.

Mlango juu ya kanuni za kifiqhi zinazotoa taarifa muhimu katika namna rahisi unafuata. Kanuni zote za kifiqhi ni kwa mujibu wa Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Hasan as-Sistaniy. Muqallidin (wafuasi) wa mujtahid wengine wanashauriwa kurejea kwenye risala zao wenyewe juu ya milango hii.

Kuhusu mahusiano ya kijinsia, upangaji wa familia na kipindi cha kushika mimba, mapendekezo ya kiislam yamepewa umuhimu sana kuhusiana na vyakula, matendo na nyakati zake, ili kuandaa mazingira kwa ajili ya kutengeneza mtoto wa halali na mzuri, insha’allah.

Mara tu unapopatikana ujauzito, wote mama na baba wanahitaji kutambua majukumu wa wajibu wao, ili kuwawezesha kuyatimiza haya katika namna nzuri iwezekanavyo. Kwa mara nyingine tena, mapendekezo kwa ajili ya vyakula, matendo na madua vimeainishwa, ili kuanza kumrutubisha na kumlea mtoto huyo kuanzia kwenye hatua hizi za mapema akiwa ndani ya tumbo la mama yake.

Vitendo vinavyopendekezwa kwa ajili ya kujifungua kuliko salama na kwepesi na kwa ajili ya kile kipindi cha mara tu baada ya kujifungua hapo tena vinajadiliwa, kuendelea hadi wakati wa kunyonyesha, ambako kunajulikana kama moja ya haki za mtoto. Hili, halafu linafuatiwa na kanuni muhimu za ziada ya kifiqhi juu ya mama, zikishughulika hasa na suala la nifaas (ile damu anayoona mama baada ya kujifungua).

Mwisho lakini sio kwa umuhimu wake, kitabu hiki kinamalizia na mlango juu ya malezi ya watoto, pamoja na nukta arobaini juu ya namna ya kutendeana na mtoto wako, kudukiza au kuingiza kidogo kidogo mapenzi kwa Ahlul-Bayt (a.s.) ndani yao na vidokezo na ushauri wa kuhifadhi Qur’ani kwa wazazi na watoto.

Sehemu hii taarifa muhimu na za kuvutia ambazo kama zitashikwa kikamilifu, zinaweza kutumika ili kupata matokeo chanya na yenye manufaa kwa mtoto.

Ni muhimu kutaja nukta fulani fulani ambazo zinaweza zikazuka katika akili ya msomaji pale anapopitia kile kiwango kikubwa cha taarifa kilichokuwepo.
Kwanza, mapendekezo fulani yanaweza kuonekana kuwa maalum sana na mafinyu, kama yale ya nyakati ambazo mtu anapaswa na pale ambapo hapaswi kushika mamba, hata hivyo, ni lazima ikumbukwe kwamba Uislam sio dini ngumu, na mapendekezo haya hayapo ili kuweka vizuizi visivyo na lazima juu yetu. Bali kwa usahihi zaidi, mapendekezo haya yanawekwa pale kwa faida yetu, na Muumba ambaye anatujua vizuri sana kuliko tunavyojijua sisi wenyewe.

Juhudi ndogo kutoka upande wetu sisi zitakuwa zichukue matokeo ya muda mrefu ambayo tunaweza hata pia tusiyatambue. Kwa kweli ni muhimu kuona kwamba mengi ya mapendekezo yamebaki hivyo, ni mapendekezo tu. Tunayotakiwa kufanya sisi ni kuyaendea haya kwa nia sahihi, kuhakikisha kwamba vitendo vya wajibu vinafanyika na kujaribu kwa uwezo wetu wote na hayo mengine, na insha’allah Yeye atakuongoza katika njia iliyobakia.

Pili, wanawake wa Kiislam hususan hasa wanao wajibu wa nyongeza wakati wa ujauzito na baada, kwamba wasifanye yale mambo ya kiafya tu na ushauri unaopaswa kushikwa, bali na mambo ya kiroho pia. Hili zaidi hasa ni gumu kama mimba yenyewe ni ya matatizo. Kwa mara nyingine tena, mtu ni lazima azingatie akilini kwamba manufaa yanazidi gharama zenyewe.

Kwa nyongeza, sio lazima kwamba kila tendo moja lililopendekezwa laz- ima litekelezwe; bali mama mwenyewe lazima aone ni kipi kinachofaa zaidi kwake na kutekeleza kile anachoweza kukifanya kwa ubora wa uwezo wake wote na kuyaacha mengine mikononi mwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye ni Mjuzi wa yote. Hili hasa linafungamana vizuri kwa kuchukulia kwamba mapendekezo yenyewe yatakuwa na matokeo yanayotakiwa tu kama yakitendwa kwa moyo uliotulia na wenye amani, kuliko wenye wasiwasi na mfadhaiko.

Kweli, katika vipengele vyote vya maisha, Uislam umetoa umuhimu kwenye ‘njia ya kati’ na kukataza mambo ya kuzidi kiasi. Kadhalika, ni jambo la busara kukumbuka kwamba mapendekezo yaliyomo katika kitabu hiki, kila moja lina wakati wake na mahali pake, na hayapaswi kuingiliwa kwa nguvu kupita kiasi, wala kupuuzwa moja kwa moja.

Kwa mfano, moja ya mapendekezo kwa ajili ya mtoto mzuri ni kwamba baba anapaswa kula komamanga; hata hivyo, hii haina maana kwamba baba huyo afanye komamanga kuwa ndio tunda lake peke yake, na hata kulibadilisha kwa ajili ya milo yake mikuu kwani jambo hilo lina madhara na ni hatari. Ni pale tu ambapo njia ya wastani au ya kati na kati itakapofuatwa ambapo manufaa ya kina ya kiroho ya mapendekezo haya yanapokuja kufanya kazi na kuathiri maisha yetu.

Kwa kumalizia, kwa ajili ya mtazamo mpana kwenye maeneo haya, tungependa kupendekeza kwamba kitabu hiki kisomwe kwa kushirikiana sambamba na dua zilizomo kwenye kitabu ‘A mother’s Prayer’* (Dua za Mama) kilichotungwa na Saleem Bhimji na Arifa Hudda.

Tungependa kuwashukuru wale wote ambao wamechangia kwenye kitabu hiki kwa njia moja au nyingine, na kukisaidia wakati wote. Mwenyezi Mungu Mtukufu awalipe kwa ajili ya kila kitu..

Mwisho, tunaomba msamaha kwenu endapo kuna mapungufu yoyote au makosa ndani ya kitabu hiki; tafadhali tujulisheni na insha’allah, sisi tutajaribu kukiboresha kwa ajili ya wasomaji wa baadae. Maoni au ushauri mwingine wowote unakaribishwa pia. Wakati unapotumia kitabu hiki, tafadhali kumbuka familia zetu katika du’a zako, na pia Marehemu wote kwa kusoma Suratul-Fatihah.

Tunaomba kwa unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu atukubalie juhudi zetu hizi, na kama atatukubalia, basi tunaziwasilisha kwa Hadharat Ma’sumah (a.s.) ambao katika ujirani wao tumeikamilisha kazi hii, na Mtukufu Imam wetu wa zama, Imam Mahdi (a.s.).

“Sifa zote njema ni Zake Allah (s.w.t.). Mola wa walimwengu wote.”

*Kitabu hiki kinaweza kununuliwa kutoka Islamic Humanitarian Service kwenye Mtandao kupitia www.al-haqq.com. Ili kuwasiliana na mwandishi unaweza kutuma baruapepe kwa anuani tph@tph.ca.

Abbas na Shaheen Merali
1 Julai, 2005
Qum Shariif.