read

Alikusanya Kwa Sababu Ya Udhuru Usiyojulikana

Kwa kuwa kuainisha udhuru unaoruhusu kukusanya imekuwa ni jambo gumu hivyo baadhi yao wamepita njia ya kutokujulikana na kutokuwa wazi, hivyo wakadai kuwa alikusanya kwa sababu ya udhuru unaoruhusu hilo lakini bila kuuainisha.

Kati ya watu waliounga mkono dhana hii ni Mufti wa zamani wa Saudia Abdul-Azizi bin Bazi katika ufafanuzi wake mfupi wa Kitabu Fat-hul-Bari fi sharhi Sahihl- Bukhari Baada ya kudhoofIsha mtazamo wa Ibnu Hajar kuhusu maana ya kukusanya (kukusanya kimuonekano) kwa kusema: Kukusanya kwa namna hii ni dhaifu.

Akasema: Sahihi ni kuitafsiri Hadithi iliyotajwa kuwa alikusanya Sala zilizotajwa kwa sababu ya taabu iliyopatikana siku hiyo kutokana na ugonjwa uliozidi au baridi kali au matope na mfano wa hayo. Na dalili juu ya hilo ni kauli ya Ibnu Abbas alipoulizwa kuhusu ila ya kuku- sanya huku, akasema: “Ili asiutaabishe umma wake.”

Kisha (Ibnu Bazi) akapendekeza kukusanya huku akasema: Nako ni jawabu kubwa sahihi lenye kutibu.”1

Anajibiwa kuwa: Kukusanya huku na kule alikokudhoofisha kote ni dhaifu, kwa sababu kunapingana na riwaya na kitendo cha Ibnu Abbas, kwani yeye alikusanya Sala mbili huko Basra bila ya kuwa na ugonjwa mkali au baridi kali au matope.

Zaidi ya hapo ni kule kuenea kwa ila. Yaani kuuondolea taabu umma, kwani taabu haihusu hali za udhuru tu bali inajumuisha hata kuwalazimisha watu kutenganisha Sala kwa namna ya wajibu ndani ya maisha yao.

Hapa si vibaya kunukuu maneno ya Ibnu As-Siddiq yaliy- omo ndani ya kitabu chake kiitwacho Izalatul-Hadhari aman jamaa bayna salatayni fil-hadhar, amesema: “Hakika Mtume (s.a.w.w.) elieleza wazi kuwa alifanya hivyo kwa lengo la kuuondolea umma wake taabu.
Akawabainishia kuwa inaruhusiwa iwapo wakihitajia kufanya. Hivyo kusema kuwa ila ni mvua baada ya kuwa tayari Mtume na maswahaba wapokezi wameshabainisha ila yake ni nini, itakuwa ni kuzuwa dhahiri isiyokuwepo bali itakuwa ni kuwapinga maswahaba na kumkosoa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.

Kwa sababu laiti angefanya hivyo kwa ajili ya mvua basi Mtume asingeeleza kinyume, wala wapokezi wasingeacha ila husika na kushikilia ila ya kuondoa taabu.

Pia imepokewa toka kwa Mtume kuwa katika usiku wenye mvua alikuwa akimwamrisha mtu anadi: "Salieni majumbani kwenu”. Wala hawakutaja hili katika kukusanya, ndio itakuwaje wataje ilihali wameshakanusha mvua?

Akaongeza kwa kusema: “Hakika Ibnu Abbas mpokezi wa Hadithi hii alichelewesha Sala akakusanya kwa ajili ya kujishughulisha na hotuba, kisha akatumia hoja ya kitendo cha Mtume kukusanya. Hairuhusiwi kutumia hoja ya kitendo cha Mtume kukusanya kwa ajili ya mvua kuthibitisha kitendo cha kukusanya kwa ajili ya hotuba au somo.

Ilihali (Ibnu Abbas) alikuwa anaweza kusitisha kwa ajili ya Sala kisha baadae aendelee au amalize somo au hotuba uingiapo wakati wa Sala na wala asipate madhara yoyote wala taabu yoyote kama taabu na madhara yampatayo mtu atokapo wakati wa mvua na matope. 2

Matokeo: Sheria hii toka kwa Mtume aliyopewa na Mwenyezi Mungu ni sheria ya raha inayoweza kutumika zama zote na katika hali zote za maisha ya kisasa vyovyote yatakavyokuwa.

Atakayechunguza kwa undani maisha ya kisasa ya ki- Magharibi ya biashara na viwanda ataona kuwa kutenganisha kati ya Sala mbili hasa Adhuhuri na Al-Asr ni jambo gumu na taabu kwa Waisilamu hasa wafanyakazi na watumishi. Kiasi kwamba inafikia ima akubali taabu au aache Sala, na inawezekana ikampelekea kukataa faradhi.

Wanazuoni wa sharia wa kisunni wenye mwamko wachukulie umuhimu ndani ya ijtihadi na hesabu zao msamaha huu uliyotolewa na Uislamu, na wepesi ulioletwa na riwaya.

Wawatangazie watu waziwazi kuwa kuku- sanya Sala mbili Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha ni jambo lililoruhusiwa kisheria japokuwa kutenganisha ni bora.

Hivyo atakaetenganisha atapata ubora wa kutenganisha na atakayekusanya atakuwa katekeleza faradhi ndani ya wakati wake.

  • 1. Fathul-Bari fi Sharhu Sahihl- Bukhari, Juz. 2, Uk. 24 maelezo ya Abdul-Azizi bin Bazi
  • 2. Izalatul-Hadhari aman jamaa bayna salatayni fil-hadhari, 116- 120