read

Alikusanya Sala Mbili Kimuonekano

Wengi wanaojaribu kutatua suala hili hukimbilia kudai kuwa haikuwa ni kukusanya kwa halisi kama kukusanya kwa safarini, bali ilikuwa ni kukusanya kwa kimuonekano, yaani Mtume alichelewesha Adhuhuri mpaka ulipobakia muda wa rakaa nne ndipo akaswali Adhuhuri na baada ya kumaliza tu ukawa umeingia wakati wa Al-Asr akaswali Al-Asr, hivyo akawa kakusanya Sala mbili huku akiwa kaswali kila moja ndani ya wakati wake.

Hili ndilo linalodhihirika toka kwa wengi wanaofafanua Hadithi; na yafuatayo ni maelezo yao: An-Nawawiy amesema: “Wapo waliofasiri kuwa ni kuchelewesha ya mwanzo mpaka mwisho wa wakati wake kisha aiswali ndani ya wakati wake, hivyo baada ya kumaliza ukawa umeingia wakati wa Sala ya pili akaiswali, hivyo Sala yake ikawa katika muonekano wa kukusanya.”

Kisha akapinga akasema: “Kauli hii nayo ni dhaifu au batili kwa sababu inapingana na dhahiri kwa namna isiy- otegemewa. Kwa sababu kitendo cha Ibnu Abbas tulichokitaja katika hotuba kisha kutoa kwake Hadithi kama hoja ya usahihi wa kitendo chake, kisha kuthibitisha kwake Abu Huraira bila kukanusha ni hoja tosha katika kupinga tafsiri hii.1

An-Nawawiy alipasa amjibu kwa hoja tuliyoitaja nayo ni kuwa: Mtume alikusanya Sala mbili kwa lengo la kuuondolea umma wake taabu, na kukusanya kwa namna hiyo iliyotajwa kunataabisha zaidi kuliko kutenganisha.

Ibnu Quddama amesema: “Kukusanya ni hiyari, hivyo ingekuwa kukusanya ni kwa namna waliyoielezea basi ingekuwa ni taabu zaidi kuliko kuiswali kila Sala wakati wake. Kwa sababu kuiswali kila Sala wakati wake ni wepesi zaidi kuliko kulinda mwisho wa wakati, mwisho ambao unalingana na muda wa kuswali Sala ya mwanzo tu bila wakati kubaki.

Pia laiti kukusanya kungekuwa ni kwa namna hiyo basi ingeruhusiwa kukusanya kati ya Al-Asr na Magharibi na Isha na Asubuhi. Ilihali hakuna tofauti kati ya umma kuwa kufanya hivyo ni haramu. Hivyo kuzifanyia kazi riwaya kwa ufahamu uliyo karibu ni bora zaidi kuliko kulazimisha maana hiyo.2

Pia Al-Muqaddasiy ndani ya kitabu As-Sharhu Al-Kabiru3 amejibu tafsiri hii kama alivyojibu Ibnu Quddama, tamko ni moja katika vitabu vyote viwili hivyo ndio maana tumetosheka na tamko la Ibnu Quddama.

Ndio, Kulingana na tuliyonukuu toka kwao ni kuwa wao wamemjibu yule aliyefasiri ruhusa ya kukusanya Sala mbili kwa msafiri kwa tafsiri ya kukusanya kimuonekano.

Hivyo kwa kuwa sababu ya kukusanya katika hali zote mbili (Msafiri na asiye msafiri) ni moja, nayo ni kuuondolea umma wake taabu na uzito huku kukusanya kwa muonekano kukiwa ni taabu na uzito zaidi kuliko kutenganisha basi tunathibitisha maneno yao katika mada hii. (Kukusanya bila udhuru katika hali isiyo ya safari).

Dhahiri ni kuwa jina kukusanya, kijamii halimlengi mtu aliyechelewesha Adhuhuri akaja kuiswali mwisho wa wakati wake na akaiharakisha Al-Asr akaiswali mwanzo wa wakati wake, kwa sababu huyu kaswali kila Sala ndani ya wakati mahususi kwa Sala husika.

Amesema: “Hakika kukusanya kunakojulikana ni kuswali Sala zote mbili pamoja ndani ya wakati wa mojawapo, hivi huoni kukusanya Sala mbili Arafa na Muzdalifa ndivyo kulivyo?"4

Dalili Za As-Shaukaniy Za Kuthibitisha Kuwa Kukusanya Kulikuwa Kwa Kimuonekano

Kisha As-Shaukaniy ni kati ya watu wanaounga mkono kuwa kukusanya kulikuwa ni kwa kimuonekano. Ameunga mkono hilo kwa hoja tatu:

Ya kwanza: Riwaya aliyoitoa Malik katika Al-Muwatwau na Bukhari, Abu Daud na An-Nasaiy toka kwa Ibnu Mas'udi kuwa alisema: “Sikumuona Mtume akiswali Sala nje ya wakati wake isipokuwa Sala mbili alikusanya Magharibi na Isha Muzdalifa na siku hiyo akaswali alfajiri kabla ya wakati wake.”

As-Shaukaniy akasema: Ibnu Mas'ud kakataa namna yoy- ote ya kukusanya na akaihusisha na kukusanya Muzdalifa tu, japokuwa yeye mwenyewe ni kati ya watu waliyopokea kukusanya kwa Madina kama ilivyotangulia.

Hivyo inaonyesha kuwa kukusanya kulikofanyika Madina ni kukusanya kwa kimuonekano, kwani laiti ingekuwa ni kukusanya kwa halisi basi riwaya zake zingepingana, na ni lazima tukusanye riwaya hizi kwa namna itakayowezekana. 5

Anajibiwa:

Kwanza: Ibnu Mas'udi si hoja kwa sababu amehusisha kukusanya na Muzdalifa tu ilihali kuna riwaya nyingi zinazoonyesha kuwa Mtume alikusanya Muzdalifa na Arafa, hivyo dhahiri ya Hadithi hii inaachwa wala haitegemewi, wala haisihi kuwa alama ya kuainisha makusudio ya kukusanya katika riwaya za mada hii.

Pili: Ibnu Mas'udi mwenyewe amepokea kukusanya kwa Mtume Sala mbili Madina, na akasema: “Alikusanya Mtume wa Mwenyezi Mungu Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha.”

Akaulizwa kuhusu hilo akasema: “Nimefanya hivyo ili umma wangu usitaabike.” 6

Umeshafahamu kuwa kukusanya kwa kimuonekano kunataabisha zaidi kuliko kukusanya kwa halisi, kwani kufahamu mwisho wa nyakati na mwanzo wake bila kukosea ilikuwa ni tatizo kwa zama zilizopita hivyo hakuna njia isipokuwa ni kutafsiri kukusanya kwa maana ya kukusanya kwa uhalisia.
Hii ni dalili kuwa riwaya inayohusisha kukusanya kwa Muzdalifa tu imeachwa na wala si hoja.

Ya pili: Aliyopokea Ibnu Jariri toka kwa Ibnu Umar amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alitujia akawa akichelewesha Adhuhuri na kuharakisha Al-Asr hivyo anazikusanya pamoja.

Anachelewesha Magharibi na anaharakisha Isha hivyo anazikusanya pamoja na huku ndio kukusanya kwa kimuonekano.”7

Anajibiwa kuwa Hadithi hii japokuwa inahusIsha kukusanya kwa kimuonekano lakini haichukuliwi kwa sababu muradi wake hauko wazi, kwani laiti akimaanIsha kuwa Mtume alifanya hivyo safarini basi imeshatangulia kuwa ukusanyaji wa Mtume safarini ulikuwa ni halisi.

Amepokea Muslim toka kwa Anas bin Malik kuwa alisema: “Ilikuwa Mtume akisafiri kabla ya kugeuka jua huchelewesha Adhuhuri mpaka wakati wa Al-Asr kisha anashuka na kuzikusanya pamoja.”8

Na katika riwaya nyingine toka kwake: “Hakika Mtume alikuwa aharakishwapo na safari huchelewesha Adhuhuri mpaka mwanzo wa wakati wa Al-Asr kisha anazikusanya pamoja, na anachelewesha Magharibi mpaka aje aikusanye na Isha mpaka wekundu wa Magharibi unapoondoka.” 9

Kama makusudio yake ni kuwa Mtume alikusanya kati ya Sala mbili kukusanya kwa kimuonekano ilihali hayupo safarini basi nadhani umeshajua jinsi riwaya zinazoonyesha ukusanyaji halisi zilivyonyingi, kiasi kwamba Hadithi ya Ibnu Abbas` na nyingine zimeweka wazi na ni alama tosha ya kutafsiri riwaya kwa maana ya ukusanyaji halisi, hivyo hatuwezi kuitupa Hadithi na kitendo cha Ibnu Abbas` eti kwa ajili ya Hadithi isiyokuwa wazi ya
Ibnu Omar.

Ya tatu: Ameipokea An-Nasai toka kwa ibnu Abbas kuwa: Niliswali na Mtume Adhuhuri na Al-Asr pamoja, na Magharibi na Isha pamoja. Alichelewesha Adhuhuri aka- harakisha Al-Asr, na akachelewesha Magharibi akaharakisha Isha.

Na huyu ni Ibnu Abbas mpokezi wa Hadithi za mlango huu ametamka wazi kuwa aliyopokea kuhusu kukusanya ni kukusanya kwa kimuonekano.10

Anajibiwa kuwa: Tafsiri hii, yaani kauli: Alichelewesha Adhuhuri akaharakisha Al-Asr, na akachelewesha Magharibi akaharakisha Isha, si ya Ibnu Abbas bali ni ya Jabir bin Zaid, hiyo ni kwa alama ya Hadithi aliyoitoa Imam Ahmad toka kwa Jabir bin Zaid kuwa alimsikia Ibnu Abbas akisema:

“Niliswali na Mtume wa Mwenyezi Mungu nane pamoja na saba pamoja. Nikamwambia, ewe Aba As-Shauthau nadhania alichelewesha Adhuhuri akai- harakisha Al-Asr na akachelewesha Magharibi akaiharak- isha Isha. Akasema: ‘Na mimi nadhani hivyo.’11

Hii ni dalili ya wazi kuwa tafsiri iliyotoka kwa Abu As- Shauthau na wenzake, inatokana na wao kuzoea kutenganisha Sala na kuipa kila Sala wakati wake, hivyo wakadai kuipa kila Sala wakati wake ni faradhi isiyoachwa.
Hivyo walipojikuta mbele ya riwaya hizi nyingi wakashindwa kujua makusudio ya riwaya, hivyo kila mmoja akakimbilia njia yake na Abu As-Shaathau akatafasiri kukusanya kwa kimuonekano.

Alikusanya Kwa Sababu Ya Udhuru Wa Mvua

Hii ndio tafsiri ya tatu ambayo amekimbilia kwayo yule asiyeruhusu kukusanya Sala mbili katika hali isiyo ya safari.

An-Nawawiy amesema: “Kati yao yupo aliyetafsiri kuwa kukusanya ni kwa ajili ya mvua. Kauli hii ndio mashuhuri toka kwa wanazuoni wakubwa waliotangulia.”

Kisha akaijibu akasema: “Ni dhaifu kutokana na riwaya nyingine za pasipo na hofu wala mvua.” 12

Sababu kubwa ya kupatikana aina hii ya tafsiri ni kujaribu kulinganisha riwaya na fat'wa za wanazuoni wengi, kama si hivyo basi riwaya ziko wazi kuwa kukusanya ilikuwa bila udhuru wowote.

Iwapo utafuatilia maelezo ya riwaya tulizonukuu toka kwa Ibnu Abbas utaishia kusema kuwa kukusanya haikuwa kwa udhuru fulani bali kwa ajili ya kuuondolea taabu umma wake.

Hivyo katika baadhi ya Hadithi utakuta kipengele: Pasipo na hofu wala safari (Angalia riwaya namba 1, 2, 15, 16, 18 na 23).

• Katika nyingine. Pasipo na hofu wala mvua. (Angalia riwaya namba 3, 4, 11, 12, na 19).

• Katika nyingine: Pasipo na safari wala mvua (Angalia riwaya ya 22).

• Katika nyingine: Pasi na hofu wala sababu. (Angalia riwaya ya 26).

• Katika nyingine: Bila ugonjwa wala sababu (Angalia riwaya ya 28).

Zaidi ya hapo ni kuwa, ila iliyopokewa ndani ya riwaya ambayo ndio inapinga uwezekano huo iko wazi sana, na yafuatayo ni maelezo yake: Katika baadhi ya riwaya ila ni kauli yake: Alitka asimsumbue yeyote kati ya watu wa umma wake (Angalia riwaya namba: 2, 3, 11, 12, na 23.) Katika baadhi ya riwaya nyingine: Ili umma wake usiwe na taabu. (Angalia riwaya ya 19).

Katika baadhi ila ni:

• Kuurahisishia umma wake. (Angalia riwaya ya 22)

• Katika baadhi ya riwaya nyingine: Asiutaabishe umma wake iwapo mtu akikusanya. (Angalia riwaya ya 25).

• Katika baadhi ya riwaya nyingine: Ili umma wangu usi- taabike. (Angalia riwaya ya 30).

Hivyo mwenye kuzichunguza hizi riwaya anaamini kuwa kukusanya haikuwa kwa udhuru wa mvua wala safari, hofu wala ila nyingine, hivyo Mtume alikusanya Sala mbili Madina bila ya udhuru wowote, ikiwa ni amri toka kwa Mwenyezi Mungu ili aurahisishie umma wake, na ili asidhani mwenye kudhani kuwa kuipa kila Sala wakati wake ni faradhi ambayo hairuihusiwi kuikhalifu bali ni ubora usiyokatalika.

Hivyo kila mmoja ndani ya umma huu ana haki ya kuku-sanya bila kuipa kila Sala wakati wake.

Alikusanya Kwa Sababu Ya Mawingu Mbinguni

Miongoni mwao yupo aliyetafsiri kuwa kulikuwa na mawingu hivyo akaswali Adhuhuri. Kisha mawingu yakaondoka na ikabainika kuwa wakati wa Al-Asr umeshaingia basi akaswali Al-Asr. Dhana hii ni dhaifu sana, hivyo aliyoyataja An-Nawawiy yanatosha kuonyesha udhaifu wake amesema:

Japokuwa kuna mategemeo fulani ya dhana hii katika Adhuhuri na Al-Asr lakini hamna kabisa mategeneo ya dhana hii katika Magharibi na Isha. Tena kukusanya hakukuwa mahususi kwa ajili ya Adhuhuri na Al-Asr bali alikusanya Magharibi na Isha mpaka Ibnu Abbas akachelewesha Magharibi mpaka wakati wa Isha.13

Zaidi ya hapo ni kuwa laiti kukusanya kungekuwa ni kwa hali hiyo basi wapokezi wangeelezea wazi wazi. Hivi tunaweza kusema Ibnu Abbas alisahau sharti, au alikum- buka lakini hakulinukuu. Pia wenzake mfano wa Abu Huraira, Abdallah bin Omar na Abdallah bin Masudi.

Alikusanya Kwa Sababu Ya Ugonjwa

Baadhi ya wale wasiyopendezeshwa na kukusanya Sala mbili wametafsiri riwaya wakasema riwaya inamaanisha alikusanya kwa sababu ya udhuru wa ugonjwa au mfano wake. Mtazamo huu kaunukuu An-Nawawiy toka kwa Ahmad bin Hambali, Al-Qadhi Huseini mfuasi wa Shafi. Pia ameuchagua Al- Khatabiy, At-Tawaliy, na Al-Rawiyaniy wafuasi wa madhehebu ya Shafi.

An-Nawawiy ameuchagua akasema: Ndio mtazamo auchaguao katika tafsiri yake kutokana na dhahiri ya Hadithi na kitendo cha Ibnu Abbas` na uthibitisho wa Abu Huraira na kwa sababu ndani ya ugonjwa kuna taabu zaidi kuliko kwenye mvua. 14

Anajibiwa kuwa: Tafsiri hii ni dhaifu na haifai kama tafsiri nyingine kwani ndani ya riwaya hizo kuna: Bila hofu wala ila. Na katika nyingine kuna: Bila ugonjwa wala ila. Na linalozidi kubatilisha hoja hiyo ni kuwa Ibnu Abbas alikusanya kati ya Magharibi na Isha huku akiwa si mgonjwa wala hakuna ugonjwa. Bali alikuwa akihutubia watu na maneno yake yakarefuka mpaka muda wa ubora wa Magharibi ukapita hivyo akaswali Magharibi na Isha ndani ya wakati mmoja.

Pia ni kuwa, laiti ingekuwa kuchelewesha ni kwa ajili ya ugonjwa basi ingesihi kwa mgonjwa mweyewe binafsi si kwa yule asiye mgonjwa, lakini Mtume alikusanya yeye na swahaba zake wote, hivyo kudhania kuwa wote walikuwa ni wagonjwa ni dhana iliyo mbali na ukweli.15

Kutokana na tuliyoyataja ndio maana Al-Hafidhu Ibnu Hajari Al-Asqalaniy amesema: “Laiti angekusanya kwa sababu ya ugonjwa basi asingeswali na yoyote isipokuwa na yule mwenye udhuru kama wake. Na dhahiri ni kuwa aliswali na maswahaba zake. Hilo kalitamka wazi Ibnu Abbas katika riwaya yake.” 16

Huyu hapa Al-Khatabiy anaelezea ndani ya (Maalimu) toka kwa Ibnul-Mundhir kuwa alisema: “Wala hakuna maana yoyote ya kulinasibisha jambo hili na udhuru wowote kwa sababu Ibnu Abbas ameelezea ila yake akasema: “Alitaka asiutaabishe umma wake.”

Na imeelezwa toka kwa Ibnu Sirin kuwa alikuwa haoni ubaya kukusanya Sala mbili kwa sababu ya haja fulani au kitu fulani iwapo tu hafanyi mazowea.17

Muhakiki wa Sunanut-Tirmidhi baada ya kunukuu maneno ya Al-Khatabiy amesema: Na hili ndio sahihi inayopatikana ndani ya Hadithi. Ama tafsiri ya ugonjwa au udhuru au jambo lingine ni kulazimisha jambo wala halina dalili. Kwa kuchukua sahihi hii watu wengi wameondolewa taabu kwani kazi zao na mazingira yao magumu yanaweza kuwalazimisha kukusanya Sala mbili hivyo wakajikuta wanapata dhambi au wanataabika katika hilo, hivyo katika kukusanya kuna raha kwao na msaada wa kumtii Mwenyezi Mungu iwapo tu hawatofanya kuwa ni mazoea kama alivyosema Ibnu Sirin. 18

Aliyoyasema ni haki lakini (Ibnu Sirin) kabana kile alichokipanua Mtume kwani kahusisha kukusanya kwa mwenye haja tu. Ilihali Mtume amepanua kwa watu wote kwa amri toka kwa Mwenyezi Mungu kwa yule mwenye ila au asiye na ila.

Ndio hakuna shaka kuwa kuipa kila Sala wakati wake wa ubora ni bora kuliko kuiswali ndani ya wakati wa kushirikiana, kwa hiyo kwa mujibu wa sheria ni kuwa muda wa kutekeleza Sala ni mpana.

 • 1. Sharhu ya Sahih Muslim, Juz. 5, Uk. 225
 • 2. Al-Mughni, Juz. 2, Uk. 113-114 ameitaja alipokuwa akikosoa maneno ya yule aliyefasiri maana hii katika kukusanya kwa safarini. Hivyo kwa kuwa jambo ni moja ndio maana tumeitaja hapa.
 • 3. As-Sharhul-Kabiru fi Dhaylil-Mughniyi, Juz. 2, Uk. 115
 • 4. Maalimus-Sunan, Juz. 2 Uk. 53 Hadithi ya 1163, Aunul-Maabudu, Juz. 1, uk. 468.
 • 5. Naylul-Awtari min ahadithi Sayidul-Akhbari, Juz. 3, Uk. 217
 • 6. Angalia riwaya namba 30
 • 7. Naylul-Awtari, Juz. 3, Uk. 217
 • 8. Sharhu Sahih Muslim, Juz. 5 mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Namba 46 na 48
 • 9. Sharhu Sahih Muslim, Juz. 5 mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Namba 46 na 48
 • 10. Naylul-Awtari, Juz. 3, Uk. 217
 • 11. Musnad Ahmad, Juz. 1, Uk. 221
 • 12. Sharhu ya Sahih Muslim ya An-Nawawiy, Juz, 5. Uk. 225
 • 13. Sharhu ya Sahih Muslim: Juz. 5, Uk. 225
 • 14. Sharhu ya Sahih Muslim ya An-Nawawiy Juz. 5, Uk. 226
 • 15. Angalia Naylul-Awtari ya As-Shaukaniy Juz. 3, Uk. 216
 • 16. Fathul-Baariy, uk. 24
 • 17. Maalimus-Sunnani, Juz. 1, Uk. 65
 • 18. Sunanut-Tirmidhiy, Juz. 1, Uk. 358 Upande wa nyongeza kwa kalamu ya Ahmad Muhammad Shakir