Kukusanya Kati Ya Sala Mbili Safarini

Wanazuoni wengi wa Kiislamu wamekubaliana kuhusu kukusanya Sala mbili safarini isipokuwa Al-Hasan, An- Nakhai, Abu Hanifa na jamaa zake wawili.
Hivyo inaruhusiwa kukusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr kwa kutanguliza kwa kuziswali wakati wa Sala ya mwanzo, na kwa kuchelewesha kwa kuziswali wakati wa Sala ya pili, hii ni kwa wote isipokuwa kwa hao tu.

Na Magharibi na Isha wakati mmoja kwa kuzitanguliza na kuzichelewesha.

Sala zinazokusanywa ni: Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha katika wakati wa mojawapo ya hizo, huitwa kuku- sanywa hizo Sala za mwanzo Jam’u taqdiim, (kwa kutanguliza), na katika nyakati za Sala za pili huitwa Jam’u taakhiri (kukusanya kwa kuchelewesha).

As-Shaukani ametaja kauli mbali mbali kuhusiana na suala hili kwa namna ifuatayo: Wanazuoni wengi wa sheria wameruhusu kukusanya safarini kwa hali yoyote kwa kutanguliza na kuchelewesha, na kauli hii ndio ya maswahaba wengi na wanafunzi wa maswahaba na wanazuoni wa sheria huku miongoni mwao ni: At-Thaury, As-Shafy, Ahmad, Is’haqa na As- Shahaby.

Wengine wakasema: “Hairuhusiwi kukusanya kwa hali yoyote ile isipokuwa Arafa na Muzdalifa. Na hii ndiyo kauli ya Al-Hasan, An-Nakhai, Abu Hanifa na wenzake wawili.

Al-Laythu amesema: “Na kauli hii ni mashuhuri toka kwa Malik kuwa kukusanya kunamuhusu yule tu mwenye haraka na safari."

Ibnu Habibu amesema: “Kunamhusu mwenye kutembea." Al-Awzay amesema: “Hakika kukusanya safarini kunamhusu mwenye udhuru.”

Ahmad amesema: Inaruhusiwa kukusanya kwa kuchelewesha (taakhiri) na wala si kwa kutanguliza (taqdiim). Kauli hii ndio chaguo la Ibnu Hazm nayo imepokewa toka kwa Malik.

Hizi ndizo kauli sita: Hivyo ikiwa suala kwa ufupi wamekubaliana wote isipokuwa wachache kama ulivyowaona, basi ni lazima tujadili suala hili sehemu mbili:

Je? Kukusanya kunamhusu tu yule mwenye haraka na safari.

Je? Inaruhusiwa kukusanya kwa kuchelewesha tu wala hakujumuishi kukusanya kwa kutanguliza?

Ama sehemu ya kwanza tunasema, habari zinazoonyesha kitendo cha Mtume (s.a.w.w) ziko katika makundi maw- ili: Kundi moja linaweka wazi kuwa alikuwa akikusanya awapo na haraka na safari, au aharakishwapo na safari:

Ameandika Muslim toka kwa Nafiu toka kwa Ibnu Umar kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akikusanya kati ya Magharibi na Isha awapo na haraka na safari.1

Ametoa Muslim toka kwa Salim, toka kwa baba yake: “Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu akikusanya kati ya Magharibi na Isha awapo na haraka na safari."

Ametoa Muslim toka kwa Salim bin Abdallah kuwa baba yake alisema: “Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu anapokuwa na haraka ya safari, akichelewesha Sala ya Magharibi mpaka anapokuja kuikusanya na Sala ya Isha.”2

Ametoa Muslim toka kwa Anas toka kwa Mtume kuwa aharakishwapo na safari huchelewesha Adhuhuri mpaka mwanzo mwa wakati wa Al-Asr hivyo huzikusanya pamoja, na huchelewesha Magharibi mpaka anapokuja kuikusanya na Isha pindi mawingu mekundu yanapozama.3

Kundi la pili linaonyesha kitendo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu bila sharti lolote (iwapo ana haraka na safari).

Ametoa Muslim toka kwa Anas bin Malik amesema: “Iwapo Mtume akianza safari kabla ya kupinduka jua alikuwa akichelewesha Adhuhuri mpaka wakati wa Al-Asr, kisha hushuka na kuzikusanya pamoja. Na iwapo jua litapinduka kabla ya safari, basi huswali Adhuhuri kisha hupanda kipando.4

Ametoa Muslim toka kwa Anas amesema: “Ilikuwa Mtume akitaka kukusanya kati ya Sala mbili safarini basi huchelewesha Adhuhuri mpaka mwanzoni mwa wakati wa Al-Asr kisha huzikusanya pamoja.5

Abu Daud na Tirmidhy wamepokea toka kwa Maadh bin Jabal kuwa: “Mtume alikuwa katika vita vya Tabuk anapotaka kusafiri kabla ya kupinduka kwa jua akachelewesha Adhuhuri mpaka akaja kuikusanya na Al-Asr pamoja, na anapotaka kusafiri baada ya kupinduka jua, huswali Adhuhuri na Al-Asr pamoja kisha huondoka, na ilikuwa akitaka kuondoka kabla ya Magharibi, huichelewesha Magharibi mpaka aiswali na Isha pamoja, na ilikuwa akitaka kuondoka baada ya Magharibi huitanguliza Isha na kuiswali na Magharibi pamoja.6

Ahmad amepokea ndani ya Musnad yake toka kwa Abbas` (r.a.) toka kwa Mtume kuwa Mtume akiwa na safari alikuwa kabla ya kupanda kipando hukusanya Sala za Adhuhuri na Al-Asr iwapo jua limepinduka akiwa nyumbani kwake.

Na iwapo halijapinduka akiwa nyumbani kwake, basi huondoka mpaka unapofika wakati wa Al-Asr ndipo hushuka kisha hukusanya Adhuhuri na Al-Asr.

Na iwapo Magharibi itaingia akiwa nyumbani kwake basi hukusanya Magharibi na Isha pamoja, na iwapo Magharibi haijaingia akiwa nyumbani kwake huondoka mpaka Isha inapoingia ndipo hushuka na kuzikusanya pamoja.7

Baada ya As-Shaukany kunukuu riwaya hii akasema: Shafy amepokea riwaya hii katika Musnad yake kwa namna yake akasema: “Na akiondoka kabla jua halijapinduka huchelewesha Adhuhuri mpaka aje aikusanye na Al- Asr wakati wa Al-Asr 8

Nasema: Kanuni ni kuchukuwa chenye sharti maalumu na kukitanguliza kabla ya kisicho na sharti maalumu, hivyo kuziwekea riwaya zisizo na sharti maalum lile sharti maalum lililomo kwenye riwaya zenye sharti maalumu, ndio maana hata Anas kanukuu kitendo cha Mtume bila ya kuwa na sharti maalumu na mara nyingine kikiwa na sharti maalumu. 9

Naongeza kuwa riwaya zinazoonyesha kitendo cha Mtume ni dalili ya ufahamu si tamko la Mtume, na suala linapokuwa hivi linakuwa halina sifa ya kuwa au kutokuwa sharti, kwa sababu hali hii ya kuwa au kutokuwa sharti ni hali ya tamko si ya kitendo, na wala katika suala hili hakuna tamko lolote lililopokewa toka kwa Mtume bali ni kitendo alichokinukuu mpokezi, na huenda kitendo chake hiki kilikuwa kimekutana na hali ya kuwa na haraka na safari, na ikawa mpokezi hakutaja hali hii kwa kutegemea kuwa haihusiki na hukumu.

Kutokana na haya maelezo hakusanyi isipokuwa anapokuwa na haraka na safari. Na inawezekana ndilo aliloliashiria Ibnu Rushdi aliposema: “Kukusanya kumenukuliwa kwa kitendo tu.” 10

Na kinachoweza kuipa nguvu kauli ya pili (bila sharti maalum) ni kuwa sharti lililopo katika riwaya hizi (iwapo ana haraka na safari) ni miongoni mwa masharti yatokanayo na hali ya mara kwa mara, masharti ambayo huwa hayafahamiki kama sharti, hiyo ni mfano wa kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na binti zenu wa kambo walio katika ulinzi wenu, waliozaliwa na wake zenu mliowaingilia”11

Hakika binti wa kambo ameharamishwa, sawa awe katika ulinzi wa mwanaume au hapana, lakini mara nyingi mwanamke anapoolewa huenda na binti yake kwa mume wa pili.

Kwa ajili hiyo binti yeyote wa kambo ni haramu bila sharti lolote sawa awe katika ulinzi wa mwanaume au hapana.

 • 1. Sahih Muslim, Juz. 2, uk. 150 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala.
 • 2. Sahih Muslim, Juz. 2, uk. 150 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala.
 • 3. Sahih Muslim Juz. 2 Uk. 151 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala
 • 4. Sahih Muslim, Juz. 2, Uk. 151 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala
 • 5. Sahih Muslim, Juz. 2 Uk. 151 Kitabu cha Sala. Mlango: Ruhusa ya kukusanya Sala mbili safarini. Mlango wa Sala
 • 6. Sunan Abi Daud: Juz. 2, uk. 8 Kitabu cha Sala mlango: Kukusanya Sala mbili. Hadithi ya 1220
 • 7. Musnad Ahmad bin Hambal: Juz 5 Uk. 241, Sunan Abi Daud: Juz. 2, uk. 2 kitabu cha Sala mlango: Kukusanya kati ya Hadithi mbili 1220
 • 8. Naylul-Awtwar: Juz. 3, Uk. 213
 • 9. Bidayatul-Mujtahid: Juz. 1, Uk. 173 Chapa nyingine iliyohakiki- wa: Juz. 2, Uk. 374.
 • 10. Bidayatul-Mujtahid: Juz. 1, Uk. 173 Chapa nyingine iliyohakiki- wa: Juz.2 Uk. 374
 • 11. Nisaa; 4: 23