Kukusanya Sala Mbili

Kukusanya kati ya Sala mbili kuna sura tofauti:

• Kukusanya Sala mbili Muzdalifa na Arafa.

• Kukusanya Sala mbili safarini.

• Kukusanya Sala mbili pasipokuwa safarini kwa udhuru kama vile mvua na tope.

• Kukusanya Sala mbili pasipokuwa safarini bila ya kuwepo udhuru wowote.

Hivyo sura mbili za kwanza ndizo zinazoingia katika hukumu ya safari na si sura mbili za mwisho. Wanazuoni wa sheria ya Kiislamu wamekubaliana kuhusu kukusanya Sala hapo Muzdalifa na Arafa lakini wametofautiana kuhusu kukusanya Sala eneo lingine lisilokuwa kaati ya hayo mawili. Hivyo sisi hapa tutazungumzia kwa ufupi sura moja baada ya nyingine huku tukitaja kauli zinazohusu suala hili na vyanzo vya kauli hizo.

1. Kukusanya Sala Mbili Muzdalifa Na Arafa

Wanazuoni wa sheria ya Kiislamu wamekubaliana kuhusu kupendelea kukusanya Sala Muzdalifa na Arafa na wala hakuna tofauti katika hilo.

Al-Qurtuby amesema: “Wamekubaliana kuwa ni sunna kukusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr wakati wa Adhuhuri uwapo Arafa, na kati ya Magharibi na Isha wakati wa Isha uwapo Muzdalifa, huku wakitofautiana kuhusu kukusanya sehemu nyingine zisizo hizo mbili.1

Ibnu Quddama amesema: “Al-Hasan na Ibnu Sirin na watu wa rai wote wamesema: “Hairuhusiwi kukusanya isipokuwa siku ya Arafa uwapo Arafa, na usiku wa Muzdalifa uwapo Muzdalifa."2

Amepokea Muslim toka kwa Jabir bin Abdillah kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikaa miaka tisa bila kuhiji, kisha akawatangazia watu mwaka wa kumi kuwa Mtume (s.a.w.w.) atahiji, hivyo watu wengi wakaenda Madina huku wote wakitaka waongozwe na Mtume na wafanye kama atakavyofanya.

Akaendelea mpaka akasema - mpaka alipofika Arafa akakuta quba limepambwa kwa madoa, akashuka hapo mpaka jua lilipopinduka, akaamrIsha aletewe ngamia, akaondoka mpaka alipofika ndani ya bonde akatoa hotuba - akaendelea mpaka akasema - kisha akaadhini na akakimu, akaswali Sala ya Adhuhuri, kisha akakimu akaswali Sala ya Al-Asr wala hakuswali chochote baina ya hizo mbili, - akaendelea mpaka akasema - akaenda mpaka akafika Muzdalifa, hapo akaswali Sala ya Magharibi na Isha kwa adhana moja na iqama mbili wala hakufanya tasbihi yoyote baina ya Sala hizo mbili.3

Kwa kuwa suala hili ni jambo linalokubalika kwa Waislamu wote basi tutafupIsha kwa kiasi hiki.

  • 1. Bidayatul-Mujtahid Juz. 1 / Uk. 170 chini ya anuani: sehemu ya pili kuhusu kukusanya Sala.
  • 2. Al-Mughny: Juz. 2, Uk. 112.
  • 3. Sahih Muslim: Juz. 4, uk. 39 - 42 mlango: Hija ya Mtume.