read

Kukusanya Sala Mbili Bila Udhuru Pasipo Safari

Imamiyya wameafikiana kuwa inaruhusiwa kukusanya Sala mbili bila ya udhuru wowote pasipo safarini, japokuwa kutenganisha ni bora.

Sheikh Tusi amesema: “Inaruhusiwa kukusanya Sala mbili kati ya Adhuhuri na Al-Asr na kati ya Magharibi na Isha, uwapo safarini au usipokuwa safarini na katika hali yoyote ile. Wala hakuna tofauti kati ya kukusanya wakati wa Sala ya mwanzo au wakati wa Sala ya pili.

Kwa sababu wakati wa baada ya kupinduka jua ni wakati wa kushirikiana, na wakati wa baada ya Magharibi ni wakati wa kushirikiana pia kama tulivyobainisha.1

Hakika upande wa madhehebu ya Imamiyya haina maana kuwa kukusanya Sala mbili ni kuiswali Sala nje ya wakati wake wa kisheria, bali muradi wake ni kuiswali katika muda usiyo wa ubora. Hivyo ufuatao ni ufafanuzi wa madhehebu yenyewe:

Kutokana na maelezo toka kwa Maimamu wa Ahlul-Bayt Imamiyya wamesema kuwa jua likipinduka basi umeingia wakati wa Sala mbili, yaani wakati wa Adhuhuri na Al-Asr, isipokuwa Sala ya Adhuhuri huswaliwa kabla ya Al-Asr, hivyo wakati uliyopo kati ya kupinduka jua na kuzama kwake ni wakati wa kushirikiana kati ya Sala mbili hizo.

Isipokuwa muda wa kutosha rakaa nne kabla ya kuzama kwa jua ni muda mahususi kwa ajili ya Sala ya Adhuhuri, na muda wa kutosha rakaa nne mwishoni mwa wakati ni wakati mahususi kwa ajili ya Sala ya Al-Asr, na muda uliyopo kati ya nyakati hizo mbili ni wakati wa kushirikiana kati ya Sala mbili.

Hivyo akiswali Sala ya Adhuhuri na Al-Asr katika muda wowote kati ya kupinduka jua na kuzama kwake atakuwa kaswali Sala hizi ndani ya wakati wake, kwa sababu ni wakati wa kushirikiana kati ya Sala mbili hizo.
Isipokuwa muda wa kutosha kuswali rakaa nne toka mwanzo wa wakati ni mahususi kwa ajili ya Adhuhuri hivyo haisihi kuswali Al-Asr humo.

Na muda wa kutosha kuswali rakaa nne mwishoni mwa wakati ni mahususi kwa ajili ya Al-Asr hivyo haisihi kuswali Adhuhuri humo.

Hii ndio hali halisi ya madhehebu, kwa ajili hiyo mwenye kukusanya Sala mbili nje ya wakati mahususi ametekeleza faradhi ndani ya wakati wake, hivyo Sala yake inakuwa ni kutekeleza (ndani ya wakati) na wala si kulipa.

Hivyo ni kuwa kila Sala ukiachilia mbali wakati wake wa kusihi bado ina wakati wake wa ubora. Hivyo wakati wa ubora wa Sala ya Adhuhuri ni kuanzia kupinduka kwa jua mpaka kivuli cha kitu kilichosimama kufikia urefu wa kipimo cha kitu chenyewe, baada ya kile kivuli cha mwanzo cha kabla ya kupinduka jua kuwa kimeondoka au kimetoweka.

Na mashuhuri ni kuwa wakati wa ubora wa Al-Asr ni kuanzia pale kivuli kinapolingana na kipimo mpaka pale kinapokuwa mara mbili ya kipimo husika.

Kwa wakati wa Magharibi na Isha hujulikana kuwa likizama jua zimeingia nyakati mbili mpaka nusu ya usiku.

Wakati wa mwanzo ni mahususi kwa ajili ya Magharibi kwa muda wa kutimiza Sala nzima, na wakati wa mwisho ni mahususi kwa Isha kwa muda wa kutimiza Sala nzima, na wakati uliyopo kati ya muda huo ni wakati wa kushirikiana.

Hivyo kila Sala kati ya Sala mbili hizi ina wakati wa ubora. Wakati wa ubora wa Magharibi ni kuanzia kuzama kwa jua mpaka kuondoka kwa wekundu wa Magharibi, na wakati wa ubora wa Isha ni kuanzia kuondoka kwa wekundu wa Magharibi mpaka theluthi ya usiku.2

Mara nyingi anayewashangaa Imamiyya kukusanya kati ya Sala mbili hudhani kuwa mwenye kukusanya huswali moja ya Sala mbili nje ya wakati wake, lakini amesahau kuwa mwenye kuswali huwa ameiswali nje ya wakati wa ubora lakini huwa ameiswali ndani ya wakati wa kusihi, na wala si ajabu Sala kuwa na nyakati tatu.

Ya kwanza: Wakati mahususi ni ule wa kutosha rakaa nne mwanzoni mwa kuingia wakati, na wakati wa mwisho ni pale unapokaribia kwisha wakati. Au rakaa tatu baada tu ya kuzama jua na rakaa nne kabla kidogo ya nusu ya usiku.

Ya pili: Wakati wa ubora ambao tayari maelezo yake yameshatangulia kuhusu Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha.

Ya tatu: Wakati wa kusihi ambao ni wakati wote uliyopo kati ya vipimo viwili isipokuwa ule tu uliyo mahususi kwa moja ya Sala mbili, hivyo wakati wa kusihi unaju- muisha wakati wa ubora na ule wa baada ya ubora.

As-Swaduq amepokea kwa isnadi yake toka kwa Zararatu toka kwa Abu Jafar (a.s.) alisema: “Jua likipinduka umeingia wakati wa Sala mbili: Adhuhuri na Al-Asr.

Na jua likizama umeingia wakati wa Sala mbili: Magharibi na Isha ya mwisho.”3

Shekhe Tusi amepokea toka kwa Ubaydu bin Zararatu alisema: “Nilimuuliza Aba Abdillah kuhusu wakati wa Adhuhuri na Al-Asr. Akajibu: “Jua likipinduka umeingia wakati wa Adhuhuri na Al-Asr isipokuwa hii inakuwa kabla ya hii, kisha wewe unakuwa katika wakati ambao ni wa sala zote mbili mpaka jua lizame.”4

Riwaya zenye maana hii ni nyingi lakini sisi tunaishia hapa.

Hivyo ikiwa Sala zina nyakati tatu kama tulivyobainisha basi inatubainikia kuwa kukusanya si jambo baya isipokuwa kinachokupita ni wakati wa ubora wala si wakati asili wa Sala, kwa ajili hiyo imepokewa toka kwa Maimamu wa Ahlul-Bayt kuwa kutenganisha ni bora kuliko kukusanya, hivyo hapa tutataja baadhi ya riwaya zinazoruhusu kukusanya ili tupate baraka tu kwani suala hili kwenye fiqhi ya shia Imamiyya ni suala la wazi sana.

Amepokea As-Saduqu toka kwa Abdallah bin Sanani toka kwa Swadiq (a.s.) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Adhuhuri na Al-Asr kwa adhana moja na iqama mbili, na akakusanya Magharibi na Isha kwa adhana moja na ikama mbili, bila ya kuwa safarini na bila ya udhuru wowote.5

Pia amepokea toka kwa Is'haqa bin Ammar toka kwa Aba Abdillah alisema: “Hakika Mtume aliswali Adhuhuri na Al-Asr sehemu moja bila ya udhuru wala sababu yoyote. Umar akauliza: “Je kuna kitu kimezuka ndani ya Sala?” Akajibu: “Hapana isipokuwa nimetaka kuupa nafuu umma wangu.”6

Kulayny ametoa toka kwa Zararatu toka kwa Aba Abdillah amesema: “Mtume aliwaswalisha watu jamaa Adhuhuri na Al-Asr baada ya kupinduka jua bila ya udhuru wowote, na aliwaswalisha jamaa Magharibi na Isha kabla ya kuondoka wekundu wa Magharibi bila ya udhu- ru wowote, hakika alifanya hivyo ili aupe umma wake nafuu ya wakati.7

Na kuna riwaya nyingi ambazo amezikusanya shekhe Al- Hurru AlAamily ndani ya kitabu chake Wasailul-Shia. 8

Mpaka hapa umebainika mtazamo wa Shia Imamiyya kuhusu kukusanya Sala mbili.

  • 1. Al-Khilafu: Juz. 1 Uk. 588 mas'ala ya 351 Huko mbele utaona jinsi wakati ulivyobainishwa
  • 2. Angalia Al-Ur'watul-Wuthqa: Uk. 171. Kipengele cha nyakati za Sala
  • 3. Al-Faqihi: Juz. 1 Uk. 140. Pia inapatikana kwenye Hadithi ya 1 mlango wa 17
  • 4. At-Tahadhibu: Juz. 2, uk. 26
  • 5. Al-Faqihi: Juz. 1, Uk. 186 namba 886
  • 6. Ilalul-Sharaiu: 321 mlango wa 11
  • 7. Al-Kafiy: Juz. 3 Uk. 286 Hadithi ya 1
  • 8. Al-Wasailu: Juz.4 Uk. 220-223 mlango wa 32 kati ya milango ya nyakati.