read

Kukusanya Sala Mbili Bila Udhuru Usipokuwa Safarini Kwa Mujibu Wa Sunna

Kuna riwaya nyingi zinazodhihirisha haki kuhusu ruhusa ya kukusanya Sala mbili bila udhuru pasipokuwa safarini, riwaya hizo zimepokewa na waandishi wa Sahih sita, Sunan na Masanidi. Hivyo tuanze aliyopokea Muslim kwa sanadi na tamko kisha twende kwenye yale waliyonukuu wengine.

1. Ametuhadithia Yahya mwana wa Yahya amesema: Nilisoma kwa Malik toka kwa Zuberi toka kwa Said bin Jubair toka kwa Ibnu Abbas alisema: ‘Mtume aliswali Adhuhuri na Al-Asr pamoja, Magharibi na Isha pamoja bila ya hofu wala safari.”

2. Ametusimulia Ahmad bin Yunus na Aun bin Salam wote toka kwa Zuhayri, Ibnu Yunus alisema: “Ametusimulia Zuhayri, ametusimulia baba Zuberi toka kwa Saidi bin Jubair toka kwa Ibnu Abbas` alisema: ‘Mtume aliswali Adhuhuri na Al-Asr pamoja Madina pasi na hofu wala safari.’ Baba Zuberi akasema: ‘Nikamuuliza Said, kwa nini alifanya hivyo? Akajibu: Nilimuuliza Ibnu Abbas kama ulivyoniuliza akasema: ‘Alitaka asimpe taabu yeyote katika umma wake.'”

3. Ametusimulia Abu Bakr bin Abi Shaybat na Abu Kuraybi wamesema: Ametusimulia Abu Muawiya na ametusimulia Abu Kuraybi na Abu Said Al-Ashaju (tamko ni la Abu Kuraybi) walisema: ‘Alitusimulia Wakiu wote kutoka kwa Al-A’amash toka kwa Habibu bin Abi Thabit, toka kwa Said bin Jubairi toka kwa Ibnu Abbas alisema: ‘Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina pasi na hofu wala mvua.’

Katika hadith ya Wakiu amesema: Nikamwambia Ibnu Abbas: Kwanini alifanya hivyo? Akasema: Ili asiupe taabu umma wake. Katika Hadithi ya Abu Muawiya ni kuwa Ibnu Abbas` aliambiwa: Alitaka nini katika hilo?

Akasema: Ili asiupe taabu umma wake.

Ametusimulia Abu Bakr bin Shaybat, ametusimulia Sufiani bin Uyayna toka kwa Amru toka kwa Jabiri bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas alisema: “Niliswali na Mtume wa Mwenyezi Mungu rakaa nane pamoja na saba pamoja.

Nikasema: Ewe baba As-sha’shau, nadhani alichelewesha Adhuhuri na akaharakisha Al-Asr, akachelewesha Magharibi akaharakisha Isha. Akasema: “Na mimi nadhani hivyo.”1

Kama atakusudia kukusanya kwa kimuonekano basi dhana yake si kitu haisaidii haki chochote. Muda si mrefu utakufikia ufafanuzi kuhusu kukusanya kimuonekano.

Ametusimulia Abu Rabiu Az-Zaharany, ametusimulia Hamadi bin Zaid toka kwa Amru bin Dinari toka kwa Jabiri bin Zaid toka kwa Ibnu Abbas kuwa, Mtume aliswali Madina rakaa saba na nane,2 Adhuhuri na Al- Asr, Magharibi na Isha.

Amenisimulia Abu Rabiu Az-Zaharany. Ametusimulia Hamadi toka kwa Zuberi bin Al-Khariti toka kwa Abdallah bin Shaqiqi alisema: “Siku moja Ibnu Abbas alitutolea muhadhara baada ya Al-Asr mpaka lilipokuchwa jua na nyota zikaanza kuonekana.

Watu wakawa wanasema: Sala! Sala! Mara akaja mtu mmoja wa koo ya Bani Tamim huku akisisitiza: Sala! Sala! Ndipo aliposema Ibnu Abbas: “Je unanifundIsha Sunna? Usiye na mama wee! Kisha akasema: ‘Nilimuona Mtume amekusanya Sala ya Adhuhuri na Al-Asr, na Magharibi na Isha.’ Abdallah bin Shaqiqi anasema: ‘Hilo likanitia shaka moyoni mwangu, mara moja nikaenda kwa Abu Huraira nikamuuliza, naye akathibitisha habari ya Ibnu Abbas kuwa ni kweli.”

Ametusimulia Ibnu Abi Omar. Ametusimulia Wakiu. Ametusimulia Amrani bin Hudayri toka kwa Abdallah bin Shaqiq Al-Uqayliy amesema: Mtu mmoja alimwambia Ibnu Abbas: “Sala!” Akanyamaza. Kisha akasema: “Sala!” Akanyamaza. Kisha akasema: “Sala!” Akanyamaza.

Kisha akasema: “Ee usiye na mama we!” Unatufunza Sala ilhali tulikuwa tukikusanya kati ya Sala mbili zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu.3

Haya ndiyo aliyoyanukuu Muslim ndani ya Sahih yake. Yafuatayo ni waliyonukuu wengine.

Ametoa Bukhari toka kwa Ibnu Abbas kuwa: “Mtume aliswali Madina saba na nane pamoja, Adhuhuri na Al- Asr, Magharibi na Isha. Ayubu akasema: ‘Huenda alikuwa ndani ya usiku wa mvua.’ Akasema, huenda.”4

Ametoa Bukhari toka kwa Jabiri bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas amesema: “Mtume aliswali saba pamoja na nane pamoja.”5

Ametoa Bukhari kwa kuivusha toka kwa Ibnu Omar na Abi Ayyub na Ibnu Abbas kuwa: Mtume aliswali Magharibi na Isha.6

Ametoa Tirmidhiy toka kwa Saidi bin Jubairy toka kwa Ibnu Abbas alisema: Mtume alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr na kati ya Magharibi na Isha Madina pasi na hofu yoyote wala mvua. Akasema: Akaambiwa Ibnu Abbas: ‘Alitaka nini katika hilo?’ Akasema: ‘Alitaka asi- upe taabu umma wake.' Baada ya kunukuu Hadithi hii Tirmidhy akasema: Hadithi ya Ibnu Abbas imepokewa toka kwake na watu zaidi ya mmoja, kaipokea Jabir bin Zaidi, Saidi bin Jubayri, na Abdallah bin Shaqiqi Al- Uqayliy. 7

Imam Ahmad ameitoa toka kwa Qatada amesema: “Nilimsikia Jabir bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas akisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina pasipo na hofu wala mvua.’ Ibnu Abbas akaulizwa: ‘Alitaka nini kinyume na hayo?’ Akasema: ‘Alitaka asiupe taabu umma wake.’8

Imam Ahmad ametoa toka kwa Sufiyani amesema Umar: Amenipa habari Jabir bin Zaidi kuwa alimsikia Ibnu Abbas akisema: Niliswali na Mtume wa Mwenyezi Mungu nane pamoja na saba pamoja. Nikamwambia:

‘Ewe Abu Shauthau, nadhani alichelewesha Adhuhuri na akaharakisha Al-Asr, Akachelewesha Magharibi akaharakisha Isha. Akasema: Nami nadhania hivyo.”9

Imamu Ahmad ametoa toka kwa Abdallah bin Shaqiqi alisema: “Siku moja Ibnu Abbas alitutolea muhadhara baada ya Al-Asr mpaka lilipokuchwa jua na nyota zikaanza kuonekana. Watu wakawa wanasema: “Sala! Sala! Alikuwepo mtu mmoja wa ukoo wa Bani Tamimu akaan- za kusema: Sala Sala! Ibn Abbas akaghadhibika akasema: Je unanifundisha Sunna?

Nilimuona Mtume amekusanya baina ya Adhuhuri na Al-Asr, na Magharibi na Isha. Abdallah anasema: Hilo likanitia shaka moyoni mwangu, mara moja nikaenda kwa Abu Huraira nikamuuliza, akalikubali.10

Ametoa Malik toka kwa Saidi bin Jubairy toka kwa Abdallah bin Abbas kuwa alisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu aliswali Adhuhuri na Al-Asr zote pamoja, Magharibi na Isha zote pamoja pasipo na hofu wala safari.”11

Ametoa Abu Daudi toka kwa Saidi bin Jubairy toka kwa Abdallah bin Abbas` amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu aliswali Adhuhuri na Al-Asr zote pamoja, Magharibi na Isha zote pamoja pasipo na hofu wala safari.

Malik akasema: Mimi naona alifanya hivyo wakati wa mvua.

Abu Daudi ameitoa toka kwa Jabiri bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas alisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alituswalisha Madina nane na saba, Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha. Abu Daudi akasema: Ameipokea pia Swaleh bwana wa At-Tauamah toka kwa Ibnu Abbas akasema: ‘Pasipo na mvua.”12

Ametoa An-Nasai toka kwa Saidi bin Jubair toka kwa Ibnu Abbas kuwa: “Mtume wa Mwenyezi Mungu aliswali Adhuhuri na Al-Asr zote pamoja, Magharibi na Isha zote pamoja pasipo na hofu wala safari.”13

Ametoa An-Nasai toka kwa Saidi bin Jubair toka kwa Ibnu Abbas kuwa: Mtume alikuwa akiswali Madina akikusanya kati ya Sala mbili kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha bila ya hofu wala safari.

Akaambiwa: Kwa nini? Akasema: Ili asiupe taabu umma wake.” (3) Ametoa An-Nasai toka kwa Abi Shauthau toka kwa Ibnu Abbas amesema: “Niliswali nyumma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu nane zote pamoja na saba zote pamoja."14

Ametoa An-Nasai toka kwa Jabir bin Zaidi toka kwa Ibnu Abbas kuwa aliswali huko Basra Sala ya mwanzo na Al- Asr bila ya kitu kati yake, na Magharibi na Isha bila ya kitu kati yake. Alifanya hivyo kutokana na shughuli. Na Ibnu Abbas akadai kuwa Aliswali na Mtume wa Mwenyezi Mungu Madina Sala ya mwanzo na Al-Asr sijida nane bila ya kitu kati yake.15

Hafidh Abdu Razaqi toka kwa Daudi bin Qaysi toka kwa Swaleh bwana wa At-Tauamah kuwa alimsikia Ibnu Abbas akisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina pasipo na safari wala mvua.”

Akasema: ‘Nikamwambia Ibnu Abbas: Unadhani kwa nini alifanya hivyo?’ Akasema: ‘Ninaona ili aupe nafuu umma wake.”16

Ametoa Abdu Razaqi toka kwa Ibnu Abbas amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr Madina pasipo na safari wala hofu.
Akasema: ‘Nikamwambia Ibnu Abbas, unaona ni kwa nini alifanya hivyo?

Akasema: ‘Alitaka asimpe yeyote taabu katika umma wake.”17

Ametoa Abdu Razaqi toka kwa Amru bin Dinari kuwa Aba As-Shauthau alimpa habari kuwa Ibnu Abbas` alimueleza akasema: ‘Niliswali nyuma ya Mtume nane zote pamoja na saba zote pamoja Madina. Ibnu Jarihu akasema: ‘Nikamwambia Abu Shauthau mimi nadhani Mtume alichelewesha Adhuhuri kidogo akatanguliza Al- Asr kidogo. Abu Shaathau akasema: “Na mimi nadhania hivyo.”18

Nasema: Dhana ya Ibnu Jarihu si chochote japo Abu Shauthau ameiafiki, dhana haisaidii haki chochote.

Matokeo yake ni kuwa kukusanya kulikuwa ni kimfano si kihalisi, hivyo tutakubainishia udhaifu wa maana hii ya kukusanya kimuonekano, na kuwa kukusanya kimuonekano kunawajibisha taabu zaidi kuliko kutengan- isha, kwani kujua mwisho wa wakati wa Sala ya mwanzo na mwanzo wa Sala ya pili ni taabu zaidi kuliko kukusanya.

Abdu Razaqi ametoa toka kwa Amru bin Shuaybu toka kwa Abdallah bin Omar amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alitukusanyia bila ya kuwa safarini akakusanya Adhuhuri na Al-Asr.” Mtu mmoja akamwambia Ibnu Omar: “Unaona ni kwa nini Mtume alifanya hivyo.” Akajibu: “Ili umma wake usipate taabu iwapo mtu akikusanya.”19

At-Twahawiy ndani ya kitabu Maanil-athari amesema toka kwa Jabir bin Abdallah: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina kwa hiyari bila ya hofu wala ila.” 20

Al-Hafidh Abu Naiimu Ahmad bin Abdallah Al-Isfihaniy (aliyefariki mwaka 430 A.H.) ametoa toka kwa Jabir bin Zaidi kuwa Ibnu Abbas alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, na akadai kuwa yeye aliswali na Mtume Madina Adhuhuri na Isha.21

Abu Naiimiy ametoa toka kwa Amru bin Dinari amesema: “Nilimsikia Abu Shauthau akisema: “Ibnu Abbas` amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu aliswali rakaa nane zote pamoja, na rakaa saba zote pamoja bila ya ugonjwa wala udhuru."22

Ametoa Al-Bazari ndani ya Musnadi yake toka kwa Abu Hurayra kuwa alisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Sala mbili Madina bila ya hofu.”23

At-Tabaraniy ametoa ndani ya kitabu Al-Awsatu na Al- Kabiri toka kwa Abdallah bin Zaid kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha. Akaulizwa kuhusu hilo akajibu: “Nimefanya hivyo ili nisiupe taabu umma wangu.” 24

Hizi ni Hadithi thelathini tumezikusanya toka kwenye Sahih Sita, Masnadi na Sunnani.Tumefupisha maneno kwa kutoa riwaya hizi tu ili msomaji ajue kuwa ni Hadithi ambazo wanazuoni wa Hadithi na wakubwa wao wamezitilia umuhimu hivyo wakazihifadhi, na wala mtu hawezi kuzikataa na kuzikanusha. Na kuna riwaya nyingize zaidi ya hizi hatujazitaja kwa ajili ya kufupisha.25

Mtiririko huu wa wapokezi unakomea kwa watu wafuatao:

• Abdallah bin Abbas

• Abdallah bin Omar

• Abu Ayubu Al-Annswariy mwenyeji wa Mtume Madina

• Abu Hurayra Ad-Duusiy

• Jabiri bin Abdillah Al-Answariy

• Abdallah bin Mas'udi.

Riwaya zinaeleza wazi kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Madina kati ya Sala mbili pasipo na hofu, mvua wala sababu yoyote. Alikusanya ili kubainisha ruhusa ya kukusanya na kuwa kufanya hivyo ni sheria. Pia ili mtu asije akadhani kuwa kutenganisha ni lazima kutokana na yeye Mtume kuendelea kuswali ndani ya wakati wa ubora. Hivyo kwa kitendo chake cha kukusanya kimethibitisha kuwa kukusanya ni ruhusa japokuwa kutenganisha ni bora.

Kwa kuwa madhumuni ya riwaya yanapingana na madhehebu za kifiqhi zilizozoweleka hivyo baadhi ya watu wa Hadithi na wanazuoni wa fiqhi wamejaribu kuzilazimisha riwaya zifuate fat'wa za maimamu zao na kufanya fat'wa hizo ndio kipimo cha haki na batili.

Hivyo wengi wao wakaacha kuzitumia riwaya hizi isipokuwa wachache tu ndio waliozitumia wakatoa fat'wa kulingana na madhumuni ya riwaya, hao wametajwa majina yao na Ibnu Rushdi ndani ya kitabu chake Bidayatul-Mujtahidu. Na Wametajwa na An-Nawawiy ndani ya Al-Maj'muu kama ilivyotangulia.

Na kifuatacho ni sababu na nyudhuru walizozitoa waliokhalifu riwaya, nazo ni sababu na nyudhuru dhaifu kuliko nyumba ya buibui.

 • 1. Kwa alama ya hadith ya tano ni kuwa Mtume alifanya hivyo alipokuwa Madina.
 • 2. Kutaja bila kufuata mpangilio kwani mpangilio ni nane na saba
 • 3. Sherhe ya Sahih Muslim ya An-Nawawiy Juz. 5 Uk. 213-218. Mlango wa kukusanya Sala usipokuwa safarini. Japokuwa huu ni mlango mahususi kwa ajili ya riwaya za kukusanya usipokuwa safarini lakini kanukuu riwaya tatu zinazoonyesha kukusanya Sala mbili safarini hivyo hatujazinukuu. Inawezekana aliziweka riwaya hizi katika mlango huu ili kuonyesha kuwa kukusanya katika hali isiyo ya safari ni vilevile kama unavyokusanya safarini
 • 4. Sahih Bukhari, Juz. 1, Uk. 110 Kitabu cha Sala mlango wa kuchelewesha Sahih Bukhari: Juz.1 Uk. 113, Kitabu cha Sala mlan- go wa wakati wa Magharibi.
 • 5. Sahih Bukhari: Juz.1 Uk. 113 Kitabu cha Sala mlango wa wakati wa Magharibi.
 • 6. Sahih Bukhari: Juz.1 Uk. 113 mlango wa Isha
 • 7. Sunanut-Tirmidhy: Juz.1, Uk. 354 Hadithi namba 187 mlango wa yanayozungumzia kukusanya usipokuwa safarini. Kisha angalia kuwa muhakiki kwenye ufafanuzi kataja njia za upokezi zilizopokea Hadithi hii toka kwa Ibnu Abbas. Pia At-Tirmidhy ana tafsiri isiyokubalika kuhusu Hadithi hii. Utaiona muda wake ukifika.
 • 8. Musnad Ahmad, Juz. 1, Uk. 223
 • 9. Musanad Ahmad Juz.1, Uk. 221 alidhania kuwa alikusudia kukusanya kimuonekano. Dhana hii si hoja hata kwa yeye mwenyewe mdhaniaji. Dhana haisaidii haki chochote
 • 10. Musnad ya Ahmad Juz. 1, Uk. 151
 • 11. Muwatta ya Malik Juz.1, Uk. 144 Hadithi ya 4 mlango wa kuku- sanya Sala safarini na pasipo safari.
 • 12. Rejea iliyopita, Hadith Na, 1214
 • 13. Sunanun-Nasai, Juz. 1 Uk. 290 mlango wa kukusanya Sala mbili usipokuwa safarini.
 • 14. Sunanun-Nasai, Juz.1 Uk. 290 mlango wa kukusanya Sala mbili usipokuwa safarini.
 • 15. Sunanun-Nasai, Juz.1 Uk. 286 mlango: Wakati ambao asiye safarini hukusanya Sala, na makusudio ya sijida
 • 16. -2- Muswanafu Abdu-Razaqi, Juz. 2 Uk. 555-556 Hadithi ya 4434, 4435.
 • 17. 1-2- Muswanafu Abdu-Razaqi, Juz. 2 Uk. 555-556 Hadithi ya 4434, 4435.
 • 18. Muswanafu Abdu-Razaqi: Juz. 2, Uk. 556 Hadithi ya 4436
 • 19. Muswanafu Abdu-Razaqi, Juz. 2 Uk. 556 Hadithi ya 4437
 • 20. Maanil-Athari, Juz.1, Uk. 161
 • 21. Hil-yatul-Awliyai, Juz. 3, Uk. 90 mlango wa Jabir bin Zaid
 • 22. Hulyatul-Awliya, Juz. 3, Uk. 90 mlango wa Jabir bin Zaid
 • 23. Musnadul-Bazari, Juz. 1, Uk. 283 Hadithi namba 412
 • 24. Al-Muujamul-Kabiri Juz.10, Uk. 269 Hadithi ya 10525
 • 25. Angalia Al-Maujamul-Awsatu, Juz. 2, Uk. 94. Kanzul-Ummal, Juz.8 Uk.246-251 namba 22764, 22767, 22771, 22774, 22777, 22778.