read

Kukusanya Sala Mbili Kwa Mujibu Wa Kitabu (Qur’an)

Mwenyezi Mungu amesema: “Simamisha Sala jua linapopinduka, mpaka giza la usiku na Qur'ani ya alfajiri. Hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa” 1

Aya imebeba jukumu la kubainisha nyakati za Sala tano, hivyo iwapo tukisema makusudio ya giza la usiku ni nusu ya usiku basi wakati uliyopo kati ya kupinduka kwa jua na giza la usiku utakuwa wa Sala nne, isipokuwa dalili imeonyesha kuwa wakati wa Adhuhuri na Al-Asr unakomea kwa kuzama jua, hivyo wakati uliopo kati ya kupinduka jua na kuzama jua ni wakati wa kushirikiana kati ya Adhuhuri na Al-Asr.

Kama inavyokuwa wakati uliyopo kati ya kuzama kwa jua mpaka kuingia giza la usiku ni wakati wa kushirikiana kati ya Magharibi na Isha.

Na huenda mtu akafasiri giza la usiku kwa maana ya kuzama jua, hivyo Aya itakuwa imebeba jukumu la kubainisha wakati wa Adhuhuri, Al-Asr na Sala ya alfajiri bila kubainisha Magharibi na Isha. Na maarufu ni tafsiri ya mwanzo.

At-Tabarasiy amesema: “Katika Aya hii kuna dalili ionyeshayo kuwa wakati wa Sala ya Adhuhuri umerefushwa mpaka mwisho wa mchana, kwa sababu Mwenyezi Mungu alifanya wakati wa kuanzia kupinduka kwa jua ambako ndio kugeuka mpaka giza la usiku ni wakati wa Sala nne, isipokuwa Adhuhuri na Al-Asr zinashirikiana katika wakati mmoja nao ni kuanzia kugeuka kwa jua mpaka kuzama kwake.

Na Magharibi na Isha zinashirikiana katika wakati mmoja nao ni kuanzia kuzama kwa jua mpaka giza la usiku. Na Sala ya alfajiri ameitenganisha kwa kusema: ‘Na Qur'ani ya alfajiri’, hivyo Aya inabainisha wajibu wa Sala tano huku ikibainisha nyakati zake.2

Tuliyoyataja ndio maelezo aliyoyatoa Imam Al-Baqir (a.s.) aliposema: “Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume wake: ‘Simamisha Sala jua linapopinduka mpaka giza la usiku.’

Hizi ni Sala nne alizozipa majina Mwenyezi Mungu, akazibainisha na kuziwekea nyakati. Na giza la usiku ni nusu ya usiku. Kisha Mwenyezi Mungu akasema:

‘Na Qur'ani ya alfajiri, hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa,’ hii ni Sala ya tano.”3

As-Sadiq (a.s.) amesema: “Ndani ya Aya hiyo kuna Sala mbili mwanzo wa wakati wake ni kupinduka kwa jua isipokuwa hii ni kabla ya hii. Na kuna Sala mbili mwanzo wa wakati wake ni kuzama kwa jua mpaka nusu ya usiku isipokuwa hii ni kabla ya hii.”

Al-Qurtuby amesema: “Kuna watu wameona kuwa wakati wa Sala ya Adhuhuri unaanzia kupinduka kwa jua mpaka kuzama kwake, kwa sababu Mwenyezi Mungu ameuweka wajibu wake kutegemeana na kupinduka kwa jua na wakati wote huu ni kupinduka kwa jua. Kauli hii kaisema kwa upana Al-Awzay na Abu Hanifa. Ama Malik na Shafy wenyewe wameashiria kauli hii wakati wa dharura.4

Ar-Raziy amesema: “Laiti tukitafsiri giza la usiku kwa maana ya kuingia kwa giza la mwanzo, basi ibara giza la usiku itamaanisha mwanzo wa Magharibi, kwa maana hii nyakati zilizotajwa na Aya zitakuwa tatu: Wakati wa kupinduka kwa jua, wakati wa kuanza Magharibi na wakati wa alfajiri.”

Akasema: “Hili linapelekea kupinduka kwa jua kuwe ni wakati wa Adhuhuri na Al-Asr hivyo wakati huu unakuwa ni wa kushirikiana kati ya hizi Sala mbili.

Na mwanzo wa Magharibi uwe ni wakati wa Magharibi na Isha, hivyo uwe ni wakati wa kushirikiana kati ya hizi Sala mbili. Hii inapelekea kuruhusiwa kukusanya katika hali yoyote ile kati ya Adhuhuri na Al-Asr Magharibi na Isha, isipokuwa dalili inaonyesha kuwa kukusanya bila udhuru pasipo na safari hairuhusiwi, hivyo ikalazimika iruhusiwe kukusanya kwa ajili ya udhuru wa safari, mvua na udhuru mwingine.”5

Aliyoyahakiki Ar-Razi katika mada hii ni ukweli mtupu, lakini kuiacha kwake haki kwa hoja ya: ‘Hakika kukusanya bila udhuru wowote pasopo na safari hairuhusiwi kwa kuwa kuna dalili juu ya hilo,’ni dhana tu.

Ni dalili ipi iliyopo inayokataza kukusanya bila udhuru wowote, je, dalili ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu? Huku Kitabu kwa mujibu wa uhakiki wake kinaruhusu kukusanya. Au ni Sunna? Baada ya muda utaona jinsi maelezo ya Sunna yanavyoruhusu.

Lakini pia umeshajua jinsi Masunni walivyosema kuwa inaruhusiwa, zaidi ya hapo ni kuwa Maimamu wa Ahlul- Bayt nao wameruhusu. Hivyo baada ya Kitabu, Sunna na ijmai hakuna hoja nyingine kama ilivyo ‘baada ya Abadan hakuna kijiji kingine.’6

  • 1. Israa; 17:78
  • 2. Maj'maul-Bayan, Juz. 3, Uk. 434
  • 3. Nuru-Thaqalain, Juz. 3, Uk. 202 Hadith ya 377
  • 4. Al-Jamiu-liah'kamil-Qur'ani, Juz. 1, Uk. 304
  • 5. Tafsirul-Kabir, Juz. 12, Uk. 27
  • 6. Mara ngapi Imam Ar-Razi amehakiki na kuongea lile lililo haki ambalo yeye mwenyewe anastahiki kulifuata lakini huliacha kwa hoja ya kipuuzi. Angalia aliyoyahakiki kuhusu kupaka miguu miwili katika tafsiri ya: “Na mpake vichwa vyenu na miguu yenu mpaka vifundoni.” Na yale aliyozungumza kuhusu makusudio ya “Wenye mamlaka katika ninyi” katika tafsiri ya Aya: “Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi". Na sehemu nyingine kama hizi.