Kukusanya Sala Mbili Pasipo Na Safari Kwa Ajili Ya Udhuru

Jambo lililo mashuhuri ni kuwa inaruhusiwa kukusanya kati ya Magharibi na Isha kwa ajili ya udhuru kinyume na Hanafiyya ambao hawajaruhusu kukusanya kwa hali yoyote ile isipokuwa msimu wa Hijja uwapo Arafa au Muzdalifa.

Ama wanaoruhusu kukusanya nao wametofautiana kwa namna zifuatazo:

Je ruhusa inahusu mvua tu au inajumuisha udhuru mwingine?

Je ruhusa inahusu Magharibi na Isha au inajumuisha Adhuhuri na Al-Asr?

Je ruhusa inahusu kukusanya kwa kutanguliza tu au inajumuisha kukusanya kwa kuchelewesha?1

Yafuatayo ni maneno yao kuhusu sura hizo tatu: Ya kwanza: Dhahiri toka kwa Shafy ni kuwa ruhusa inahusu mvua tu.

As-Shiraziy amesema: “Inaruhusiwa kukusanya Sala mbili katika hali ya mvua. Hairuhusiwi kukusanya kwa ajili ya hali ya upepo mkali, tope, ugonjwa na giza."2

(1). Ibnu Rushdi amesema: “Shafi ameruhusu kukusanya usipokuwa safarini kwa ajili ya mvua, mpaka aliposema ama kukusanya kwa ajili ya ugonjwa usipokuwa safarini ni kuwa Malik ameruhusu iwapo atahofia kuzimia au ana ugonjwa wa tumbo, lakini Shafy kakataza hilo.3
(2). Akasema ndani ya kitabu As-Sharhul-Kabiru kuwa: Na je ni ruhusa hilo - kinyume na mvua - kwa ajili ya tope na upepo mkali wenye baridi, au kwa mwenye kuswalia nyumbani au msikitini huku njiani kuna mvua nyingi.4

Ya pili: Yaani je ruhusa inahusu Magharibi na Isha tu au inajumuisha Adhuhuri na Al-Asr? Ibnu Rushdi amesema: “Shafy ameruhusu kukusanya usipokuwa safarini kwa udhuru wa mvua usiku au mchana, ama Malik yeye ameruhusu usiku akakataza mchana.5

An-Nawawy amesema: “Shafy na jamaa wamesema inaruhusiwa kukusanya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha katika hali ya mvua. Imam wa haramaini akaeleza kuwa inaruhusiwa kukusanya Magharibi na Isha wakati wa Magharibi, wala hairuhusiwi kati ya Adhuhuri na Al- Asr, na haya ndio madhehebu ya Malik.

Al-Mazny amesema: “Hairuhusiwi kwa hali yoyote. Madhehebu ya kwanza ndiyo yanayotokana na maelezo ya Shafy, ya zamani hadi mapya.”6

Ya tatu: Yaani ruhusa inahusu kukusanya kwa kutanguliza bila kujumuisha kukusanya kwa kuchelewesha.

A-Shirazy amesema: “Ni ruhusa kukusanya Sala mbili katika hali ya mvua katika wakati wa Sala za kwanza, na je inaruhusiwa kuzikusanya katika wakati wa Sala za pili?" Hapa kuna kauli mbili: Shafy amesema ndani ya Al-Imlau: “Inaruhusiwa kwa sababu ni udhuru unaoruhusu kukusanya katika wakati wa Sala ya mwanzo hivyo ikaruhusiwa kukusanya katika wakati wa Sala ya pili kama kukusanya kwa safarini.

Akasema katika Al-ummu: “Hairuhusiwi kwa sababu iwapo akichelewesha huenda mvua ikakatika hivyo akawa kakusanya bila udhuru."7

Huu ni ufupi wa kauli katika nukta hizi tatu. Pia wao wana tofauti katika sehemu nyingine ambazo hakuna haja ya kuzitaja.

Baada ya kutambua hilo la muhimu ni kuwepo dalili juu ya ruhusa ya kukusanya kwa udhuru usipokuwa safarini.

Wamethibitisha hilo kwa Hadithi mbili:Inayoonyesha kuwa inaruhusiwa kukusanya usipokuwa safarini katika hali yoyote ile, hivyo wakaichukulia katika hali ya mvua au udhuru wowote ule.

Bukhari ametoa toka kwa Ibnu Abbas` (r.a.) kuwa Mtume aliswali Madina rakaa saba na rakaa nane, yaana Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha.8

Ibnu Rushdi amesema: “Ama kuhusu kukusanya usipokuwa safarini bila udhuru wowote ni kuwa Malik na wanazuoni wengi hawaruhusu, lakini hilo limeruhusiwa na wengi kati ya kundi la dhahiri na Ash’habu ambaye ni kati ya wafuasi wa Malik.

Sababu kubwa ya kutofautiana kwao ni tofauti yao kuhusu ufa- hamu wa Hadithi ya Ibnu Abbas`, hivyo wapo waliy- oitafsiri kuwa ilikuwa ni katika hali ya mvua kama alivyosema Malik, na wapo walioichukulia kuwa ni hali yoyote.
Aliyoipokea Ibnu Abbas` kuwa Mtume alikusanya Adhuhuri na Al-Asr na kati ya Magharibi na Isha Madina bila ya hofu, safari wala mvua. Akaulizwa Ibnu Abbas: Alitaka nini katika hilo? Akasema: “Alitaka asiutaabishe umma wake.”9

Dhahiri inaonyesha kuwa kukusanya wakati wa hali ya mvua ni jambo lililokuwa linajulikana kabla, ndio maana Ibnu Abbas` alijaribu kubainisha kuwa kukusanya huku hakukuwa ni kwa lengo la mvua au nyudhuru nyingine bali ilikuwa ni msamaha kwa lengo la kutokuutaabisha umma wake.

Hivyo ikiruhusiwa kukusanya katika hali isiyo ya safari kwa udhuru wowote, basi kukusanya safarini bila udhuru wowote itakuwa ni hiyari kati ya hukumu za safari. Kwa sababu msafiri atakusanya Sala mbili safarini bila udhuru.

Ama yule asiye safarini yeye atakusanya kwa ajili ya udhuru au kwa lengo lingine. Ama tukisema kuwa inaruhusiwa kukusanya bila udhuru wowote usipokuwa safarini, basi haitakuwa kukusanya kati ya Sala mbili ni kati ya hukumu za safari.

Mpaka hapa maneno yametimia kuhusu sura ya tatu, hivyo imebakia sura ya nne.

  • 1. Tuliyoyataja ni vichwa vya tofauti zao, lakini matawi yake ni mengi hatuna haja ya kuyaingilia
  • 2. Al-Majmuu: Juz. 4, Uk. 258, Kifungu cha matni
  • 3. Bidayatul-Mujtahid: Juz. 1, Uk. 173-174 mahali pawili
  • 4. Al-Mughni, Juz. 2, Uk. 118
  • 5. Bidayatul-Mujtahid, Juz. 1, Uk. 173
  • 6. Al-Majmuu: Juz. 4, Uk. 260
  • 7. Al-Majmuu: Juz, 4. Uk. 258
  • 8. Katika sura ya nne utaona vyanzo vya riwaya hizi.
  • 9. Katika sura ya nne utaona vyanzo vya riwaya hizi.