Masunni Wanaoafikiana Na Imamiyya Katika Kila Kitu Kuhusu Suala Hili

Japokuwa kukusanya Sala bila udhuru ni kati ya mambo ya wazi katika fiqhi ya Imamiyya lakini suala hili si mahususi kwa Imamiyya peke yao bali kuna baadhi ya wanazuoni wa sheria wa kisunni wameafikiana nao katika suala hili.

Ibnu Rushdi amesema: “Ama kukusanya bila udhuru usipokuwa safarini hakika Malik na wanazuoni wengi wa sheria hawaruhusu, lakini wameruhusu hilo baadhi ya jamaa katika watu wa Dhahir na Ash'habu katika wafuasi wa Malik. Na sababu ya kutofautiana kwao ni tofauti yao kuhusu kuifahamu hadith ya Ibnu Abbas, hivyo wapo walioifafanua kuwa ilikuwa kwa sababu ya safari, na wapo walioichukulia katika hali yoyote ile.

Muslim katika Hadithi yake ameondoa kauli: ‘Bila ya hofu wala safari wala mvua.’ Hili ndilo waliloshikilia watu wa Dhahir.1

An-Nawawy amesema: Tawi: “Kuhusu madhehebu yao kuna kukusanya bila hofu, safari, mvua, wala ugonjwa. Madhehebu yetu (ya Shafy) na madhehebu ya Abu Hanifa, Malik, Ahmad, na jamuhuri ni kuwa hairuhusiwi.

Ibnu Al-Mundhir ameelezea kuhusu kundi linaloruhusu bila udhuru wowote. Akasema: Ibnu Sirin ameruhusu kwa ajili ya haja maalum au asipochukulia kama mazoea.2

Kwa namna yoyote ile la muhimu ni dalili si kauli, hivyo iwapo kauli zitaafikiana na dalili basi ni vizuri, na kama si hivyo basi marejeo ya mwisho ni dalili.

  • 1. Bidayatul-Mujtahid, Juz. 2, Uk. 374 chapa iliyohakikiwa
  • 2. Al-Majumuu, Juz. 4, Uk. 264