read

Wanazuoni Wengi Wa Kisunni Wameacha Kuifanyia Kazi

Hakika kati ya mambo yanayozisibu riwaya hizi ni wanazuoni wengi wa kisunni kuacha kuzitumia, jambo ambalo linawajibIsha zisiwe na hoja.

Baada ya kutaja Hadithi za kukusanya, Tirmidhiy anasema: Kuzifanyia kazi hizi riwaya kwa masunni ni kutokukusanya kati ya Sala mbili isipokuwa safarini au Arafa.1

Watafiti wengi wa dini wameijibu kauli hii:

a). An-Nawawiy anasema: “Riwaya hizi zimethibiti ndani ya Muslim kama unavyoziona. Na wanazuoni wana tafsiri na madhehebu mbalimbali kuhusu riwaya hizi, na Tirmidhiy mwisho wa kitabu chake amesema: Ndani ya kitabu changu hakuna Hadithi ambayo umma umeafikiana juu ya kuiacha na kutokuifanyia kazi isipokuwa Hadithi ya Ibnu Abbas inayohusu kukusanya Madina bila ya hofu wala mvua, na Hadithi ya kumuua mnywaji wa pombe mara ya nne.”2

Hili alilolisema Tirmidhiy kuhusu Hadithi ya mnywaji wa pombe ndivyo lilivyo, yenyewe ni Hadithi iliyofutwa kwani ijmai imethibitisha hilo. Ama kuhusu Hadithi ya Ibnu Abbas hakuna ijmai inayothibitIsha kuacha kuifanyia kazi, isipokuwa kuna baadhi ya tafsiri ambazo tutaziashiria.3

b). As-Shaukaniy amemjibu At-Tirmidhiy kwa kusema: “Haijifichi kuwa Hadithi ni Sahih, na wala kitendo cha masunni wengi kuacha kuifanyia kazi hakitii dosari usahih wake, na wala hakiwajibishi kuporomoka hoja yake. Baadhi ya wanazuoni wameifanyia kazi kama ilivyotangulia. Japokuwa dhahiri ya maneno ya Tirmidhiy ni kuwa yeye haifanyii kazi lakini wengine wamethibitisha kuifanyia kazi, na kilichothibitishwa hutangulizwa.4

c). Al-Alusiy amesema: “Madhehebu ya kundi la maimamu linaruhusu kukusanya usipokuwa safarini kwa mwenye haja asiyefanya kuwa ni mazowea. Kauli hii ndiyo ya Ibnu Sirini, na Ash'habu mfuasi wa Malik.

Al-Khatabiy Ameinukuu toka kwa Al-Qufali As-Shashiy Al-Kabiru mfuasi wa Imam Shafy, na kutoka kwa Abi Is'haqa Al-Marwaziy na toka kwa jamaa kati ya watu wa Hadithi.

Ibnu Al-Mundhiru amechagua kauli hii, na inaungwa mkono na dhahiri iliyosihi toka kwa Ibnu Abbas` na iliy- opokewa na Muslim kuwa alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha Madina pasipo na hofu wala mvua. Akaambiwa: Kwa nini amefanya hivyo? Akasema: “Hakutaka yeyote apate taabu katika umma wake.”

Inatokana na taabu kwa maana ya uzito hivyo hajatoa sababu ya ugonjwa wala ya kitu kingine.
Kutokana na tuliyoyataja inafahamika kuwa kauli ya At- Tirmidhiy mwishoni mwa kitabu chake: Ndani ya kitabu changu hakuna Hadithi ambayo umma umeafikiana juu ya kuiacha na kutokuifanyia kazi isipokuwa Hadithi ya Ibnu Abbas inayohusu kukusanya Madina bila ya hofu wala mvua, na Hadithi ya kumuua mnywaji wa pombe mara ya nne. Inatokana na kutokufanya utafiti .

Ndio! Aliyoyasema kuhusu Hadithi ya pili ni sahih kwani wameeleza wazi kuwa Hadithi hiyo imefutwa na ijmai imethibitisha kufutwa kwake.5

d). Kwa ukosoaji huu imedhihirika kuwa hakuna hali ya kususa kuifanyia kazi Hadithi hii, na huenda masunni wengi hawajatoa fat'wa kulingana na makusudio ya Hadithi hizi kwa sababu ya ubora wa kutenganisha na kuzigawa kwa nyakati.

Lakini ubora huu unapingana na ubora mwingine, nao ni kuwa katika zama zetu hizi kitendo cha kutenganisha kinapelekea watu wengi wenye shughuli kuacha kuswali (kama tunavyoshuhudia kwa macho). Kinyume na kukusanya kwenyewe ambako kunarahisisha kuhifadhi Sala kwa kuziswali, kwa ajili hiyo ubora umegeukia upande wa pili, hivyo ni bora wanazuoni wa sheria wakatoa fat'wa ya kukusanya, na watie wepesi badala ya kutia uzito.

Allah (s.w.t.) anasema: “Mwenyezi Mungu huwatakieni yaliyo mepesi wala hawatakieni yaliyo mazito.”6 “Wala hakuweka juu yenu uzito katika dini.”7
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwani zipo dalili zina- zoruhusu kukusanya katika hali yoyote, tena ni dalili sahih na za wazi kama ulivyoona, bali ni Kitabu chenye hekima ndio kimebainisha hivyo.8

Hadithi Haielezi Kukusanya Kwa Kutanguliza Au Kwa Kuchalewesha.

Al-Qadhiy Sharafudini Al-Husein bin Muhammad Al- Maghribiy amesema ndani ya kitabu chake Al-Badru At- Tamamu fi sharhu Bulughul-Marami kuwa: “Hakika Hadithi ya Ibnu Abbas haisihi kuwa hoja kwa sababu haiainishi ni kukusanya kwa kutanguliza au ni kwa kuchelewesha, hiyo ni kama ilivyo dhahiri katika riwaya ya Muslim na kuainisha moja kati ya hizo ni kulazimisha.

Hivyo inawajibika kuhama kwenda kwenye lile la wajibu kwa kubakia katika Hadithi za nyakati zinazomjumuisha mwenye udhuru na asiye na udhuru kisha kumuainisha msafiri tu kwa kuthibiti kiainishi.9

Anajibiwa kuwa: Ibnu Abbas hakunukuu namna ya kuku- sanya kwa kuwa jambo lenyewe liko wazi, kwani kukusanya katika hali isiyo ya safari ni sawa na kukusanya katika hali ya safari, hivyo kama inavyoruhusiwa kuku- sanya kwa namna zote mbili uwapo safarini yaani kuku- sanya kwa kutanguliza na kwa kuchelewesha kama maelezo yalivyotangulia ndivyo hivyo hivyo hata usipokuwa safarini.

Kunyamaza kwa Ibnu Abbas na kitendo cha wapokezi kutokumuuliza kuhusu namna ya kukusanya ni dalili kuwa kutokana na maneno yake walifahamu kukusanya si mahususi kwa namna moja tu kati ya namna mbili, kwani laiti isingekuwa hivyo ingewalazimu kuuliza tena: Je, Mtume alikusanya kwa namna ya kutanguliza au kuchelewesha?

Linalounga mkono hilo ni umoja wa sababu iliyopo kwenye maneno ya Ibnu Abbas kwani inapatikana katika namna zote mbili.

Ametoa Muslim toka kwa Ibnu Abbas kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu alikusanya Sala mbili katika safari aliyosafiri katika vita vya Tabuk, hivyo akakusanya kati ya Adhuhuri na Al-Asr, Magharibi na Isha. Said akasema: ‘Nikamwambia Ibnu Abbas kitu gani kilimpelekea kufanya hivyo, akasema: “Alitaka asiupe taabu umma wake.”10

Hivyo kinachoupa nguvu uhusikaji wa namna zote mbili bila tofauti kati ya namna hizo ni kule kuenea kwa sababu nayo ni kuuondolea taabu umma wake, kwani kwa hakika taabu inayopatikana kwa kutenganisha Sala mbili inaondoka kwa kukusanya kwa namna yoyote ile kati ya namna mbili. Sawa iwe kwa kutanguliza au kuchelewesha.

Zaidi ya hapo ni kuwa Ibnu Abbas aliifanyia kazi Hadithi kwa sura ya kukusanya kwa kuchelewesha. Imeshatangulia kuwa Ibnu Abbas siku moja alihutubia baada ya Al-Asr mpaka jua likazama na nyota zika- chomoza; watu wakaanza kusema: ‘Sala! Sala!’ Akaja mtu toka ukoo wa Bani Tamimu akaanza kusisitiza kwa kusema: ‘Sala! Sala!’ Ibnu Abbas akasema: “Je unanifundIsha sunna? Ee usiye na mama we!" Mpaka mwisho wa Hadithi kama ilivyotangulia.

Kwa hakika ndugu msomaji ni kuwa mpinzani alipofika mbele ya riwaya hizi nyingi zinazoruhusu kukusanya dhidi ya kutenganiha, kisha akaona wanazuoni wengi wako kinyume basi kwa makusudi akaanza kushakia, na kwa ajili hiyo akaleta utata huu ambao unafanana na swali la Bani Israeli kwa Nabii Musa bin Imran kuhusu miaka na rangi ya ng'ombe jike.11

 • 1. Sunanut-Tirmidhiy, Juz.1, Uk. 354
 • 2. Taz. Al-Ilali, Juz. 2, Uk. 331 na Juz. 4, Uk. 384
 • 3. Sharh ya Sahih Muslim ya An-Nawawiy Juz. 5 Uk. 224
 • 4. Naylul-Awtwari ya As-Shawkaniy Juz. 3, Uk. 218 mlango wa kukusanya kwa asiye msafiri kwenye mvua au kingine.
 • 5. Ruhul-Maaniy, Juz. 15 Uk. 133-134 katka tafsiri ya Aya: “Simamisha Sala jua linapopinduka”
 • 6. Al-Baqara: 185
 • 7. Al-Hajji: 78
 • 8. Masailul-Fiqihiya ya Imam Sharaful-dini: 9
 • 9. Ameelezea As-Sayyid Muhammad bin Ismail As-Swanaaniy aju- likanae kwa jina la Al-Amiru ndani ya kitabu chake Subulus-Salami: Juz. 2, Uk. 43
 • 10. Sharhu ya Sahih Muslim ya An-Nawawiy, Juz. 5, Uk. 224 mlango wa kukusanya Sala mbili Hadithi ya 51
 • 11. Al-Baqarat; 2: 67-71