read

Shaytani Waswas-Khannas

Katika tafsiri 'Majmaul Bayaan' na 'Al-Miizan fi Tafsiril Quran' Juzuu ya nne na Juzuu ya ishirini uk. 398 ya ‘Allamah Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai. Chapa ya pili 1974 Beirut. Ipo riwaya ifuatayo juu ya Istighfaar:

Baada ya kuteremka kwa Aya 3:135, Sheitani alikuja Makkah na kupiga sauti kubwa mno juu ya mlima Thur, ambayo iliwafanya mashabiki wake wote wakusanyike, nao walipokuja walimwona huyo amezongwa na mushkeli mkubwa sana na hapo hawakusita kumwuliza: "Je umekuwaje na hoja gani ya kutukusanya hapa?"

Akajibu:

“Imeteremka Aya isemayo kuwa Ummah wa Muhammad utasamehewa kabisa madhambi yake na masharti ya Tawbah yaliyokuwa yamewekewa Ummah yaliyotangulia, yameondolewa kwao. Na iwapo sisi hatukubuni mbinu dhidi yake, basi juhudi zetu zote za kuwapotosha hazitakuwa na athari yoyote kwani wao watakapofanya Tawbah, madhambi yao yatasamehewa yote kwa pamoja na hata kubadilishwa kuwa matendo mema."

Kwa hivyo nimekuiteni hapa ili tutafute mbinu za kukabiliana na swala hili ama sivyo sisi hatutakuwa na kazi yoyote ile."

Kila mmoja wao alitoa mpango wake aliinuka mmoja wa Masheitani, akasema: "Nitafanya hivi na vile......." Lakini hawakukubaliana naye, nao wengine pia walisema walivyokuwa wakiona, nao wote walikwenda wakipingwa mmoja baada ya mwingine.

Na hapo akainuka Waswas - Khannas, naye akasema: "Nitawatia watu katika hatia (madhambi) na papo hapo nitawasahaulisha Istighfaar (Tawbah) na nitawaambia kuwa :

"Ewe binadamu! Bado unao muda mwingi wa kufanya Tawbah, haraka ya nini? Huu ndio muda wako wa kustarehe na kufaidi umri wako! Siha yako na vile nguvu zako zinakuruhusu ufanye hivyo, hivyo starehe hadi utakapokuwa mzee, utafanya Tawbah kiasi utakacho!”

Kwa hayo, Masheitani wote walifurahi mno na yeye Khannas alikabidhiwa kazi hiyo hadi kufika siku ya Qiyama.

(Tafakari Sura an-Naas, 114, Ayah 1-4 :

Sema: Ninajikinga kwa Allah swt Mlezi wa wanaadamu,

Mfalme wa wanaadamu,

Mungu wa wanaadamu,

Na shari ya wasiwasi wa Shetani, Khannas

Hizi ndizo wasiwasi za Sheitani ambazo huwapotosha watu wengi hasa vijana ambao hudhani kuwa wao bado wanao umri mrefu wa kufanya Tawbah hapo mbeleni. Sisi twachukulia uzee ndio wakati wa kufanya Tawbah, lakini nani anayejua kuwa uzee huo ataufikia au atakufa kabla yake. Je siku hizi hatuoni kuwa wazee ndio waliobakia hai ambapo vijana wamekufa kwa magonjwa kama ukimwi? Na magonjwa mengine ambayo hayana hata muda wa kuyashughukikia vyema kama homa ya uti wa mgongo, n.k. Kwa hivyo fanya lile uliwezalo leo badala ya kungojea kesho, kwani unaweza kuugua vibaya sana na hata kufa! Jambo linalotubidi kujiambia ni :

"Sielewi ni lini mauti yangu itanifikia na kunichukua, labda hata sasa hivi ipo mgongoni mwangu ikinichukua, hivyo ni aibu kufika mbele ya Allah swt huku nimejitwisha mzigo mzito wa madhambi bila ya kufaidi fursa ya Tawbah!"

Je, ndugu zangu, Imani yetu haipo hatarini? Labda tukafa mauti isiyo ya Islam na ambapo Allah swt anatuambia tusife ile tukiwa Waislamu!

Quran Tukufu inatuambia katika Sura ar-Ruum, 30, Ayah 10:

Kisha ubaya ndio ulikuwa mwisho wa wale waliotenda uovu, kwa kukadhibisha Aya za Allah swt , na kwa haya walizoea kudhihaki.

Vile vile twaambiwa katika Sura Aali Imraan, 3, 132:

Na harakisheni kwa (njia ya kujipatia) Maghfirah kutoka Allah swt wenu!