read

Hati Ya Nyongeza

Makala hiyo hapo juu (iliyoandikwa kwa lugha ya Kiurdu) ilichapishwa kwanza kwenye gazeti la kila juma liitwalo Sarfaraz (Toleo la Muharram) la mwaka 1354 Masihiya). Makala hii ilichapishwa huko ikiwa imefanyiwa masahihisho fulani fulani na ikaungwa na ile makala yangu ya Kiurdu iitwayo "Karbala Shanasi" (toleo la pili la mwaka 1989, ukurasa wa 199-220).

Kwenye mwaka wa 1954 watawala wa Rasiya Uarabuni (ambao kwa makosa huitwa Saudi Arabia) walikuwa bado hawajatiwa kiburi na dola ya petroli. Hivyo, hawakuhisi kuwa walikuwa mashujaa mno kiasi cha kuyatangaza mapatano na mapenzi yao kwa Yazid. Hii ndio maana ilinibidi nizipange thibitisho za kiuandishi hizo hapo juu, ili kuonyesha uhusiano wao na wauaji wa Imamu Husayn (a.s.).

Kwenye miaka ya 1960 Mwarabu mmoja (ambaye nadhani ni Mwahhabiya), hapa mjmi Dar es Salaam aliniambia: "Nyie watu mlimwua Imamu Husayn". Nikamjibu: "Sawa! Lakini hebu, yasikilize haya ninayotaka kukueleza. Mimi nikasema:

La'ana Allahu ummat qatalat al-Husayn
Wa la'ana Allahu ummat dhalamat al-Husayn
Wa la'ana Allahu ummat sami'at bi dhaalika
faradhiyat bihi

"(Laana ya Allah na iwe juu ya watu waliomwua Imamu Husayn; na laana ya Allah na iwe juu ya watu waliomdhulumu Husayn; na laana ya Allah na iwe juu ya watu walioyasikia hayo (maovu aliyotendewa Husayn) na wakayaridhia)."

Kisha nikamwambia ayatamke maneno haya iwapo yu mkweli kwenye hilo dai lake. Yeye alikataa.

Kwenye mwaka 1973 bei ya petroli ilipanda kwa kiwango ambacho hakikuweza kutegemewa kabla yake. Sasa Mawahhabiya wa Saudia wakawa na uwezo wa kukodi kalamu na vinywa, kila mahali ulimwenguni na sasa wakaanza kuionyesha rangi yao halisi, Wizara yao ya Elimu, kwa ujasiri mkubwa ikachapisha na kuwatawanyia bure Mahujaji, kitabu kiitwacho:

Haqaiq 'an Amir al-Mu'minin, Yazid ibn Mu'awiyah
(Ukweli juu ya Amirul Muminin, Yazid ibn Mu'awiyah).

Mnamo tarehe 6 Aprili 1989, nilisimama kwenye soko kuu la mjini Karachi (Pakistan) nikiutazama msikiti mpya, mkubwa na wenye mnara mrefu sana. Kwenye kitako cha mnara huo ilikuwako sentensi ya Kiurdu iliyoandikwa kwa maandishi makubwa na yenye kuvutia machoni. Sentensi hiyo ilidai hivi: "Hadhrat Amiirul Muuminiin Yazid - Allah na Amwie Radhi - yu miongoni mwa watu wa Peponi."

Hivyo, mwuaji wa Seyyid wa vijana wa Peponi ataingia Peponi!

Inashangaza, au sivyo?

Lakini linaloshangaza zaidi ya hayo ni ule ufedhuli wao wa kuendelea kuwashutumu Mashia kuhusiana na mauaji ya Imamu Husayn (a.s.) kama ilivyofanywa na Mawahhabiya wa mjini Dar es Salaam mwaka uliopita na kumhimiza Al-Haj Muhsin Alidina kuitafsiri makala yangu ya Kiurdu.

Mawahhabiya waelekea kuielewa vizuri sana methali ya Kiarabu isemayo: "Kama huna haya basi fanya lolote lile upendalo."

Sayyid Saeed Akhtar Rizvi
5 Mei 1991.