read

Swali La Kwanza

Hebu na tufikirie ni madhahebu ipi yenye kumtukuza yule mtu Mtukufu ambaye yu Shahidi wa Karbala na inayozifuata nyayo zake, na ni ipi isiofanya hivyo.

Bila ya kusema mengi, ni madhehebu ya Shia yenye kumwamini Imamu Husayn (a.s.) kuwa yu mtu aliyeteuliwa na aliyewekwa na Allah (s.w.t.) na yu mrithi wa haki wa nafasi ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w). Shia wanaamini kwamba kila neno na kitendo cha Imamu (a.s.) ni katika kumtii Allah, vita yake na amani yake ni kioo cha amali chenye kufaa, na msimamo wake ndio mapenzi ya Allah. Kwa Shia, Imamu ni sehemu ya Nuru (Nuur) ya Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.), Nyama na damu ya Imamu ni nyama na damu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Kujitoa kwa ajili ya Imamu ni jukumu kuu. Kumtii kuna maana ya kuikamilisha imani yake mtu, na kwanza yeye Imamu katakasika kutokana na kukosea na makosa. Kumpenda Imamu ni kutimiza malipo ya Utume wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Allah (s.w.t.) anasema:

"...Sema (ewe Rasuli Wetu Muhammad): kwa hayo, siombi ujira wowote kwenu ila mapenzi (yenu) kwa karibu (zangu)..."(Qur'ani, 42:23).

Imamu katakasika kutokana na kila aina ya uchafu, uwe wa kimwili au wa kiroho. Allah (s.w.t.) anasema:

"...Hakika Allah anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Ahlul Bayt (wa Rasuli Wetu Muhammad) na kukutoharisheni kwa tohara kamili." (Qur'ani 33:33)

Imamu yu mwana wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Allah (s.w.t.) anasema:

"...Lakini atakayekuhoji kuhusiana na hayo baada ya kukufikia elimu, basi sema: "Njooni tuwaite wana wetu na wana wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu na nafsi zetu na nafsi zenu..."(Qur'ani 3:61)

Imamu yu ua la Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na anatokana na Mtukufu Mtume (s.a.w.w), kama alivyosema Mtukufu Mtume (s.a.w.w) mwenyewe, pale aliposema: "Husayn anatokana na mimi, na mimi ninatokana na Husayn." Imamat (Uimamu) wake hautegemeani na upatano wa watu wala kiapo cha utii cha watu.

"Yeye yu kiongozi wa vijana wa Peponi." Yu mtakatifu (kutokana na dhambi na kukosea) tangu kuzaliwa kwake hadi kufariki dunia kwake. Itikadi hii juu ya Umaasum (Utakatifu wa Maimamu) ni maalumu kwa Mashia tu, na wasiokuwa Mashia hawashiriki kwenye itikadi hii. (Ingawa wanavyuoni wakuu wasio Shia wanaweza kuthibitisha Uma'sum wa Maimamu).

Waislamu wasio Shia, hasa wale wa madhehebu ya Hanafii na Shafii wote, na wengi wa Hambali (Wafuasi wa Imamu Ahmad Ibn Hambal) wanamtambua Imamu Husayn (a.s) kuwa na haki na Yazid kuwa yu mwenye makosa. Kuzitaja rejea zote hapa kutaifanya orodha hiyo kuwa ndefu sana. Hivyo nitazitaja baadhi tu ya rejea hizo, nilizozichagua miongoni mwa waandishi walioandika juu ya jambo hili:

1. Allamah Shahabuddin Abul Abbas Ahmad bin Muhammad Qastalani, aliyefariki kwenye mwaka wa 923 Hijiria, mwenye kitabu chake kiitwacho: "Irshad Alsari Sharh Sahih Bukhari", Juzuu 2, ukurasa wa 139.

2. Bwana Ibn Jawzi (aliyefariki mnamo mwaka 1200 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Al-Radd Alal Mutaassib Alanidil Man 'Min Dhulm Yazid."

3. Bwana Sibt Ibn Jawzi (aliyefariki mnamo mwaka wa 1257 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Tazkiratu Khawassil Ummam".

4. Allama Ibn Hajar Al-Haitami (aliyefariki mnamo mwaka wa 974 Hijiriya), mwenye kitabu chake kiitwacho: As-Sawa'iq al-Muhriqah, ukurasa wa 132-134.

5. Imamu Jalaluddin Abdul-Rahman Ibn Abi Bakr Al-Suyuti (aliyefariki mnamo mwaka 911 Hijiriya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Tarikhul Khulafaa".

6. Shaikh Muhammad bin Ali Sabban (aliyefariki mnamo mwaka 1792 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Is'afur Raghbiin".

7. Allama Sa'duddin Mas'ud bin 'Umar Taftazani (aliyefariki mnamo mwaka 1389 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Sharh Aqaid Nasafi".

8. Shah Abdulaziz Dehlawi (aliyefariki mnamo mwaka 1824 Masihiya) mwenye kitabu chake kiitwacho "Sirrul Shahadatain".

9. Shah Abdulhaqq Dehlawi (aliyefariki mnamo mwaka 1642 Masihiya), mwenye vitabu vyake "Mada-rijun Nubuwwat" na "Ja-adhbul Qulub".

10. Maulana Abdulhai Firangi Mahali, mwenye kitabu chake kiitwacho "Fatawi," Juzuu 3, ukurasa wa 7.

11. Nawwab Siddiq Hassan Khan Bhopali (aliyefariki mnamo mwaka 1889 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Bughyatul Raid Fi Sharhil Aqaid".

12. Maulana Muhammad Matin Firangi Mahali, mwenye kitabu chake kiitwacho: "Wasilatun Najat", ukurasa wa 290.

13. Mufti Muhammad Akramuddin, mwenye kitabu chake kiitwacho: "Sa'adatun Kawnain Fi Fadhailil Hassanain."

14. Qadhi Muhammad Sulaiman, mwenye kitabu chake kiitwacho:

15. "Rahmatuh-Lil- 'Alamiin".

Majina haya machache ni mifano michache tu yenye kuwajumlisha wanachuoni wa kihanafiyah, Kishafi'i na Kihambaliya ambao wameweka sehemu ya Imamu Husayn kuwa ilikuwa ya haki na kwamba alikufa akiwa shahidi aliyedhulumiwa.

Kinyume na hivyo, wako Mahambaliya wanaoamini kuwa Ibn Taimiya ni kiongozi wao; na hivyo ndivyo waaminivyo Nasibi na Kharji, ambao ili kuwahadaa Masunni, hujitokeza kama Masunni. Watu hawa humchukulia Yazid kuwa ni khalifa wa kweli na hivyo, Mwenyezi Mungu na atusamehe, humchukulia Imamu Husayn (a.s) kuwa yu mwenye makosa aliyestahili kuuawa. Siku hizi, maoni ya namna hii yanatolewa na Mahmud Ahmad Abbasi, ambaye kitabu chake kiitwacho "Khilafat Muawiya wa Yazid" kimeziumiza hisia za Waislamu wengi. Kwenye siku za awali, kabla ya Ibn Taimiya (aliyefariki mnamo mwaka 728 Hijiriya), mtu mmoja aliyeitwa Abu Bakr Muhammad bin Abdullah bin al-Arabi (aliyefariki mnamo mwaka 543 Hijiriya) alijitokeza kwenye itikadi hiyo hiyo. Mtu huyo aliandika hivi:

"Husayn hakuuawa ila kwa upanga wa babu yake mwenyewe (yaani kwa mujibu wa kanuni za shari'ah), kwa sababu kililiwa kiapo cha utii kwa Yazid na hivyo Husayn alikuwa mwasi".

Maelezo ya huba yake kwa Yazid yaliyomo kwenye kitabu kiitwacho "Tazkiratul Huffaz" yanatosha kuwa utangulizi: "Hafidh, Allama, Qadhi, Faqihi, alifikia daraja la Ijtihad". Abu Bakr bin Al-Arabi alikuwa mwanafunzi wa Imamu Ghazali (aliyefariki mnamo mwaka 505 Hijiriya). Imamu Ghazali huyu ndie yule yule aliye maarufu kwa jina la Hujjatul Islam na anaaminiwa kuwa yu nguzo ya kanuni za kidini (za Kisunni) na mmoja wa wale ambao Fat'wa (hukumu ya Kiislamu) zao zilikuwa:

"Ni haramu kuhadithia juu ya Husayn na wafuasi wake kwenye hotuba, kwa sababu kufanya hivyo kunazaa chuki juu ya masahaba".

Ni dhahiri kwamba, kama Imamu Ghazali aliifikiria sehemu ya Imamu Husayn (a.s) kuwa ni ya haki, asingeharimisha kuihadithia.

Tukiyafikiria yote haya, mtu hatakuwa na jingine la kufanya ila kuamua kuwa, Ulama kama hawa hawamfikirii Imamu Husayn (a.s) kuwa yu mtu mtukufu na kwamba, kwa mujibu wa mauni yao, kukataa kwa Imamu Husayn (a.s) kula kiapo cha utii kwa Yazid kulikuwa ni kosa kubwa mno kiasi kwamba hadi hivi leo wanaandika kuwa, Mwenyezi Mungu na atusamehe Imamu (a.s) alikuwa na dalili za ukaidi.

Kabla ya Muhammad Abbasi, mtu mwingine aliandika kitabu kiitwacho "Shahidi A'zam" kilichojaribu kuonyesha kuwa "Yazid alikuwa khalifia wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na kwamba Husayn alimwasi Yazid bila ya haki wala sababu kwa kulilia madaraka. Nduguze walimshauri kutofanya hivyo, lakini hakuwasikiliza. Mwishowe, Gavana wa Yazid aliyeitwa Ibn Ziad, akimzuia Husayn na kutoleta mfarakano na baada ya kushindwa katika kuzitumia njia nyinginezo, kwa shingo upande, alimwua ili kuidumisha amani na umoja."

Mwandishi aliyeandikwa kwenye ukurasa wa mbele wa kitabu hicho alikuwa ni Abdul Kalam Asad, kwa mujibu wa umaarufu na cheo cha mwandishi huyo, kiwanda cha uchapishaji wa vitabu kiitwacho: "Islah Publication, Kujhwa (Bihar, India) kiliona kuwa ni muhimu kukijibu kitabu hicho na kikatoa kitabu kiitwacho "Shahadat 'Uzma", ambacho hadi hivi sasa kinapatikana. Baada ya Uhuru wa India, mtu fulani alimtahadharisha Maulana Abdul Kalam Asad (Waziri wa Elimu wa India wa wakati ule) kuhusiana na kitabu kilichochapishwa kwa jina lake. Maulana huyu hakuwa na taarifa zozote juu ya kitabu hiki na hivyo akatoa tamshi rasmi la kutojihusisha na kitabu hicho. Kukikana kwake kitabu hiki kulikuwa kwa haki kwa sababu huyo marehemu Abdul Kalam Asad angeweza kuandika juu ya Imamu Husayn (a.s.) akikirejea kitabu hiki. Kwa mfano, hebu itazame makala yake ndefu iliyoandikwa kwenye gazeti liitwalo "Al-Hilal" lililotoka mwezi wa Muharram (Mfunguo Nne) iliyochapishwa tena neno hadi neno kwenye gazeti la mjini Lahore (Pakistan), liitwalo "Inqilab", toleo la Shaban, 1927, na ambayo Sayyid Muhammad Hashim Marhum Patlavi aliinakili tena kwenye sehemu ya pili ya kitabu chake kiitwacho "Namoose-Islam", kwenye ukurasa wa 274 - 278.

Hata hivyo, wale wanaomfuata Ibn Taimiya na Ibn Al-Arabi na Manasibi wamesema moja kwa moja au kwa mifano tu kuwa Imamu Husayn (a.s.) hakuwa na haki.

Maelezo

Muhammad bin Abdullah bin Al-Arabi alimfunza itikadi hii mwanawe aliyeitwa Muhyuddin Ibn Al-Arabi, aliyeandika kitabu kiitwacho "Al-Futahatul Makkiyah", na aliyefariki mnamo mwaka 638 Hijiriya.