read

Swali La Pili

Hebu sasa natuligeukie lile swali la upande wa pili na tuone ni madhehebu ipi inayomchukulia Yazid mwenye nuru ipi. Baada ya kulielezea lile swali la kwanza waziwazi, haipo haja tena ya kueleza kwa kirefu hapa, lakini ili kuzi-imarisha zaidi thibitisho hizo, hapa chini tunatoa maelezo zaidi.

Mashia wanamchukulia mtu huyu aliyelaaniwa (Yazid) kuwa yu adui na kila mtoto wa Kishia humwona Yazid na jadi zake wote kuwa ni kizazi kilicholaaniwa Al-Shajaratul Mal-'unnah kilichotajwa kwenye Qur'ani (kwenye aya isemayo:

"...Na hatukuifanya ile ndoto tuliyokuonyesha ila kuwa ni mtihani kwa watu, na (pia) ule Mti uliolaaniwa (Ash-Shajarata Mal'uunat) kwenye Qur'ani na tunawahofisha lakini haiwazidishii (chochote) ila uasi mkubwa." (Sura Bani Israil, 17:60)

Kinyume na hivyo, Mawahhabi ambao ni wafuasi wa Ibn Taimiya humwona Yazid kuwa ni Khalifa wa haki. Hapo juu tumekwisha kumtaja Abu Bakr Ibn Al-Arabi. Mullah Ali Qari, kwenye kitabu chake kiitwacho "Sharh Fiqh Akbar", kwenye ukurasa wa 84, na lbn Hajr Haithami (ambaye pia tumemtaja hapo juu) kwenye kitabu chake kiitwacho: "Sawa'iqul Muhriqah, kwenye ukurasa wa 11 na wa 12 wameonyesha hisia zao zenye nyuso mbili (huku na huku) kwa kumwingiza Yazid miongoni mwa Maimamu kumi na wawili ambao kuhusiana nao imepokewa Hadith ya Mtukufu Mtume (s.a.ww.) isemayo kwamba dini itabakia kuwa imara madamu wako Maimamu kumi na wawili.

Ibn Taimiyya na wafuasi wake Mawahhabi wamefanya kila walichokiweza kumwokoa Yazid kutokana na kulaaniwa: wakitoa Fatwa isemayo kuwa yeye alikuwa ni Mwislamu na Mwislamu ameharimishwa kumlaani Mwislamu mwenzie: au kumwekea lawama yote ya mauaji ya lmamu Husayn (a.s.) Ibn Ziad; au kuzusha Hadithi isemayo kuwa Imamu Husayn (a.s.) atamsamehe Yazid kwenye siku ya Kiyama. Kwa ufupi ni kwamba, kila hila iliyowezekana inatumiwa katika kumwokoa Yazid kutokana na laana.

Mshairi mmoja amejaribu kuzijibu hila hizi akisema:

"Enyi msemao kuwa tusimlaani Yazid au majeshi yake kwa sababu yawezekana kwamba Allah akamrehemu.

Kama Allah atamsamehe, ingawa kawatendea yote hayo Dhuria wa Mtukufu Mtume, basi hakika Allah Atakusameheni nyie nanyi kwa kumlaani Yazid".

Ukweli uliopo ni kwamba Mashia, Mahanafiya, Mashafi na Mahambaliya wenye kuipenda haki (akiwemo Imamu Ahmad bin Hambal mwenyewe) humchukia Yazid ambapo Manasibi na Mawahhabiya (wengi wao huwaghilibu watu kwa kujiita Mahambaliya) sio tu kwamba hawamlaani Yazid bali vile vile hujaribu kuwazuia watu wasimlaani.