read

Swali La Tatu

Kwa Mashia, Yazid na wauaji wengine wa Imamu Husayn (a.s.) ni Kafir na hivyo wamejitakia laana ya Allah iwe juu yao na juu ya wote wenye kuyafurahia matendo yao; na huwahesabu wote hao kuwa ni watu wa motoni. Mahanafiya, Mashafii na Mahambaliya wapenda haki nao humchukia Yazid na wauaji wengine wenye kustahili karipio kali zaidi.

Lakini Mawahhabiya na Manasibi huwapinga Mashia waziwazi kwa kuwa wanawahesabu wauaji wa Imamu Husayn (a.s) kuwa ni wenye kustahili sifa. Miongoni mwa wauaji hawa, baadhi yao waliweza hata kujinyakulia Ukhalifa na wengine wakapewa majina ya heshima kama vile "Saduq" (Mkweli zaidi) na "Thiqah" (Mwaminifu), na watu kadhaa miongoni mwao wamekuwa wapokeaji wa Ahadith za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwenye "Sihah Sitta" na kutokana na maelezo yao watu hujichukulia hukumu za kidini.

Sasa tutawataja hapa chini kila mmoja wao kwa jina na kumwonyesha alikuwa ni mtu wa aina gani.

1. 'Umr Ibn Sa'd Ibn Abi Waqqas

Huyu ndie aliyekuwa amiri jeshi wa majeshi ya Yazid. Baada ya Yazid na Ibn Ziad, yeye anahusika moja kwa moja na matendo maovu mno yaliyotendwa dhidi ya Imamu Husayn (a.s.). Aliviambia vikosi vyake vishuhudie kwamba yeye anamtupia Imamu Husayn (a.s.) mshale wa kwanza. Mwandishi wa kitabu kiitwacho "Tahdhi'b al-Tahdhib" anamwelezea mtu huyu kama ifuatavyo:-

"Yeye (Umar Ibn Sa'd) alizipokea Ahadithi za Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kutoka kwa baba yake na kutoka kwa Abu Sa'id al-Khudri, masahaba wawili wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na mapokezi yake yalitolewa na mwanawe (aliyeitwa) Ibrahim na mjukuu wake aliyeitwa Abu Bakr Ibn Hafs Ibn Hurith, na Yazid Ibn Abi Maryam, na Qatadah, na Zuhri, na Yazid Ibn Habib na wengineo."

"Mwana wa mtu huyu aitwaye Ijli amehadithia kwamba alikuwa na kawaida ya kuzihadithia Ahadith alizozipokea kutoka kwa baba yake na watu wengi wamezihadithia Hadithi walizozipokea kutoka kwake na yeye yu "Tabi'i" (Mwanafunzi wa Sahaba) na Thiqah (mwaminifu)".

Kwenye kitabu kiitwacho Taqribul Tahdhib imeelezwa hivi:-

"Umar Ibn Sa'd Ibn Abi Waqqas wa Madina, mkazi wa mjini Kufah, alikuwa ni Saduq (Mkweli). Lakini watu walimtweza kwa sababu alikuwa amiri jeshi wa jeshi lililomwua Husayn."

Kumbuka kwa, hii ni kauli ya Shaikhul Islam wa mawahhabiya, Ibn Hajar.

Ifuatayo hapa chini ni orodha ya wale waliozihadithia Ahadith zilizopokewa na 'Umar Ibn Sa'd:

i. Abu Ishaq Sabi'i

ii. Qatadah, na

iii. Imamu Zuhri.

Hawa ndio wale watu watatu ambao Mawahhabiya huwategemea kwa Ahadith zao na huwahesabu kuwa ni mabwana wa uhadithiaji wa Ahadith. Kutokana na hawa watu wote watatu kuyakubali mapokezi ya 'Umar Ibn Sa'd, kunamfanya mtu huyu kuwa msema kweli na mwenye madaraka. Zaidi ya hapo, uthibitisho zaidi unaotolewa ni kwamba Imamu Nasai, Ibn Majah na Bukhari wamezihukumu Ahadithi alizozihadithia.

Kwenye hali hii, hakuna umuhimu wowote uwezao kupewa wale watu wa kawaida wanaojificha au yale maneno ya Ibn Mu'in pale aliposema:

"Ni vipi mwuaji wa Husayn aweza kuwa mwaminifu?"

Kwenye Sharhi yake ya kitabu kiitwacho "Mishkat", Mullah Ali Qari anayehesabiwa kuwa yu miongoni mwa waandishi wakweli juu ya tabia za wapokeaji wa Ahadithi) anafafanua, akisema:

"'Umar Ibn Sa'd yeye mwenyewe hakumwua Husayn na inawezekana kwamba kushiriki kwake kwenye jeshi lile kulitokana na ujuzi wake halisi (ijtihad) na inawezekana kutokana na kuteleza au kutenda dhambi? Hivyo basi, iwapo malango ya lawama yanafunguliwa kwa hasira, kwa ajili ya vitu kama hivi, basi wanachuoni watajikuta kwenye mashaka".

Kwetiye kitabu kingine kiitwacho "Mizanul-I'tidal" zaidi ya kuyaandika hayo kuwa Umar alishiriki kwenye vita dhidi ya Imamu Husayn (a.s.), aliongezea kusema:

"Utu wake ni mwema kiasi cha kutokana kabisa na lawama. Mpokeaji wa Ahadithi (aitwaye) Su'ba (kwa kutokana na mabwana wake) amepokea Ahadithi kutoka kwake na wamefanya vivyo hivyo watu wengineo nao."

2. Shimr Ibn Dhil-Jaushan

Huyu ndiye mchinjaji hasa wa Imamu Husayn (a.s.). Ibn Ziad alimfanya mtu huyu kuwa kapteni wa jeshi madhubuti la watu elfu nne, na akampa maagizo ya kwamba iwapo 'Umar Ibn Sa'd atasitasita kumshambulia Imamu Husayn (a.s.) basi amnyang'anye uamiri-jeshi wa jeshi hilo na auchukue yeye. Huyu naye yu kiongozi wa wapokeaji wa Ahadithi wa Mawahhabiya. Kwenye kitabu kiitwacho "Tahdibut Tahdhib" imeandikwa hivi:

"Shimr ibn Dhil-Jaushan Abu Nabighah Dhubyani amepokea Ahadithi kutoka kwa baba yake, na kutoka kwa Shamr amepokea (Ahadithi hizo) Abu Ishaq Sabi'i."

Hayo yameandikwa kwenye kitabu kiitwacho Mizanul I'tidal na kwenye kitabu kingine kiitwacho Isti'ab. Kwenye Tadhkiratul Hufadh inaelezwa zaidi hivi:

"Na kutoka kwake amepokea A'mash na Shu'bah na Thawri na Israil na Abul Ahwas na Abu Bakr Ibn Ayyash na Sufyan bin Ayniyah."

Maelezo ya Abu Ishaq Sabi'i (ambayo ndani yake ameeleza udhuru wa kutomlaumu Shimr) ni haya yafuatayo:-

"Shimr alikuwa akisali pamoja nasi, na alikuwa kila mara akisema: Ee Allah! Unajua kuwa mimi ni mtu mtukufu, basi unisamehe."

Abu Ishaq anasema: "Nilimwuliza: Ni vipi Allah Angeweza kukusamehe wakati wewe umeyasaidia mauaji ya mwana wa Mtume? Shimr akajibu: Ole wako! Ningefanyaje? Viongozi wetu wametuamrisha kufanya hivyo nasi hatukuwaasi! Kama tungewaasi, hali zetu zingekuwa mbaya zaidi kuliko kumwua Husayn."

3. Hasin ibn Numayr

Mlaaniwa huyu aliongoza jeshi la askari elfu nne huko Karbala. Baada ya kuuawa kwa Bwana Muslim Ibn Aqiil, Ibn Ziad alimfanya Hasin ibn Numayr kuwa kiongozi wa jeshi la kufunga mipaka ya Kufah ili kuweza kumkamata Imamu Husayn (a.s.) atakapokuja huko. Hurr alikuwa na afisa wa chini yake. Baada ya masaibu ya Karbala, wakati wa kuzingirwa kwa mji wa Madina na Harram, alikuwa kiongozi wa Jeshi sababu kiongozi wa jeshi hilo aliyeitwa Muslim ibn Uqbah alikuwa mgonjwa; baada ya kuuteka mji wa Madina Muslim ibn Uqbah alipofariki, akawa kiongozi hasa wa jeshi lililouzingira mji wa Makkah. Yeye nae yu mpokeaji wa Ahadith kwenye Sihah. Kwenye kitabu kiitwacho Tahdhibat Tahdib imeelezwa hivi:

"Mwenye mazingira ya mji wa Madina alikuwa mmoja wa maamiri-jeshi wa Yazid ibn Mu'awiyah. Kisha mwenye kumzingira Ibn Zubair alikuwa amiri jeshi wa jeshi la Yazid. Yeye yu mtu maarufu".

Kwenye Mizanul-Itidal imeandikwa kuwa yeye kapokea Ahadithi chache tu, lakini halaumiwi kwa kuwa mmoja wa wauaji wa Imam Husayn (a.s.). Zaidi ya hapo, Bukhari, Abu Dawuud, Tirmidhi, na Nasai wapokeaji wanne maarufu sana wamezinukuu kwa uhakika Ahadithi zake kwenye vitabu vyao ambavyo ni miongoni mwa Sihah Sitta ambavyo Ahadithi zote zilizoandikwa humo zahesabiwa kuwa ni sahihi kabisa.

4. Muhammad ibn Ash'ath ibn Qais

Huyu alikuwa ni mwana wa nduguye Khalifa Abu Bakr na mwana wa Munafiq (mnafiki) mkuu aliyeitwa Ash'ath bin Qais na ni umbu lake Ju'dah binti Ash'ath mwuuaji wa Imamu Hassan (a.s.). Ibn Ziad alimtuma mtu huyu kwenye kupigana na Hadhrat Muslim bin Aqil, na huko Karbala, aliongoza kikosi cha askari elfu nne. Yeye naye anahesabiwa kuwa yu mpokeaji wa Ahadith, mkweli wa Ahlul Sunnah. Kwenye Tahdhibut Tahdhib anaelezwa hivi:

"Muhammad ibn Ash'ath ibn Qais Kindi Abul Qasim alikuwa yu mkazi wa mjini Kufah. Mama yake alikuwa ni umbu lake Abu Bakr Siddiq. Ibn Ash'ath amepokea Ahadith kutoka kwa babayake na 'Umar na 'Uthman na Ibn Mas'ud na Ayisha; na kutoka kwake amezipokea Ahadith hizo mwanawe (aitwaye) Qais na Shu 'bi na Mujahid na Zuhri n.k. Ibn Habban amemwingiza miongoni mwa watu waaminifu. Mwenye Sunnan ya Ibn Dawuud liko moja miongoni mwa mapokezi yake juu ya Abdul Rahman ibn Qais na iko Hadith moja kwenye Sunnan ya Nasa'i izungumziayo juu ya Funga. Abu Zubair Razi ameeleza kwa Ibn Zubair alimpa mtu huyu ugavana wa Mosul".

Kwenye kile kitabu kiitwacho Tahdhibut Tahdhib imeelezwa hivi:-

"Muhammad ibn Ash'ath ibn Qais Kindi ambaye jina lake la utoto ni Abul Qasim, ni mpokeaji (wa Ahadith) anayekubalika - yeye yumo kwenye kundi la pili (yaani yu miongoni mwa Tabi'in)."

Baadae Muhammad Ibn Ash'ath alidai Ukhalifa na Ulama wa Kiwahhabiya wanasema:

"Yeye yu miongoni mwa wale ambao watu waliwapa Ukhalifa kwa makubaliano ya pamoja".

Ukweli ni kuwa, hata sahaba maarufu wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) Anas ibn Malik alikula kiapo cha utii kwake na akamtii. (Soma kitabu kiitwacho Hayatul Hayawan, Juzuu 2. ukurasa wa 48.)

5. Shabth ibn Rab'i

Mlaaniwa huyu naye alikuwa miongoni mwa waliomua Imamu Husayn (a.s.). Yeye nae aliongoza kikosi cha askari kwenye masaibu ya Karbala. Kwenye kitabu kiitwacho Taqribu Tahdhib imeonyeshwa kuwa yeye nae yu mpokeaji wa Ahadith za Sihah na upokeaji wake umejipatia nafasi kwenye vitabu vya Abu Dawuud na Imamu Nasa'i.

6. Sumrah ibn Jundab

Alikuwa miongoni mwa maamiri jeshi wajeshi la Yazid. Yeye alikuwa ni sahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ambaye kuhusiana naye Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alitabiri akisema kuwa atakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. Hivyo basi, mwenye Sharh lbn Abil Hadid, mwenye Ma'arif cha Ibn Qatbiya na mwenye Isti'ab ameelezwa hivi:

"Mtume (s.a.w.w.) akiwa anazungumza na Sumrah, Abu Huraira na Hudhaifa bin Yaman alisema kwamba miongoni mwao vule atakayekuwa wa mwisho kufa atakwenda Motoni. Abu Huraira alikuwa kila mara akisema kwamba Hudhaifa alitutangulia kufa na ninategemea kuwa nitakufa kabla ya Sumrah. Hivyo, Sumrah ibn Jundab aliwaishilizia wengine katika kufariki dunia na alikiwepo kwenye mauaji ya Karbala. Imamu Husayn (a.s.) alipoitangaza azma yake ya kwenda Iraq, Samrah alikuwa kwenye jeshi la polisi la Ibn Ziad na alikuwa na desturi ya kuwashawishi watu kwenda kupigana dhidi ya Imamu Husayn (a.s.)."

Ingawa aliyatenda yote hayo, kwa sababu tu yu sahaba wa Mtukutu Mtume (s.a.w.w.) amewekwa kwenye kundi la kwanza la wapokeaji wa Ahadithi na mapokezi yake huzipamba Sihah kwenye Isti'ab imeandikwa hivi:

"Yeye alikuwa ni sahaba wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na wakazihadithia".

Hawa watu sita walikuwa ni maamiri-jeshi kwenye majeshi ya Yazid huko Karbala. Sasa tutawataja wale ambao uadui wao kwa Ahlul Bayt (a.s.) kwa ujumla na hasa kwa Imamu Husayn (a.s.) unajidhihirisha wenyewe. Miongoni mwao, wa kwanza wao ni Marwan ibn al-Hakam.

7. Marwan Ibn al-Hakam

Baba yake aitwaye Hakam alifukuzwa mjini Madina na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ambaye alimwita "guruguru mwana wa guruguru". Mwenye Isti'ab imeelezwa hivi:

"Ayisha alisemo. "Ewe Marwan! Ninashuhudia ya kwamba Mtume alimlaani baba yako ulipokuwo (bado u mbegu za uzazi) mwenye kiuno chake (hivyo basi wewe nawe umo kwenye laana hiyo)."

Marwan alikuwa na kawaida ya kumlami Amiirul Mu'minnin Ali (a.s.) mbele ya Imamu Hassan (a.s.) na akamzuia Imamu Hassan (a.s.) asizikwe karibu na kaburi la babu yake Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Walid (gavana wa Yazid mjini Madina wakati ule) alipomwita Imamu Husayn (a.s.) kula kiapo cha utii kwa Yazid na Imamu (a.s.) akaamua kuwa jambo hilo liahirishwe hadi siku ifuatayo, ni huyu Marwan ibn Hakam aliyemwambia Walid kuwa kama atamwachia Imamu (a.s.) aende, katu hataweza tena kumkamata na akamhimiza amwue Imamu (a.s.) pale pale. Huyu Marwan aliyefukuzwa mjini Madina na akafahamika kwa majina ya "Mfukuzwa wa Mtume (s.a.w.w.)" na "guruguru mwana wa guruguru" na aliyemshawishi gavana wa mjini Madina kumwuua Imamu Husayn (a.s.), alipandishwa cheo hadi kukifikia cheo cha Ukhalifa na akawa anazungumziwa kuwa yu mpokeaji Ahadithi wa kuheshimika. Kitabu kiitwacho Taqribut Tahdhib kinaandika hivi:

"Marwan aliushika Ukhalifa mnamo mwaka wa 64 Hijiriya."

Kwenye kitabu kiitwacho Tahdhibut Tahdhib imeandikwa hivi:-

"Marwan ibn Hakam amepokea Ahadith kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ingawa inadhihirika wazi wazi kuwa katu hakuzisikia hadithi hizo moja kwo moja kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe. Vile vile amepokea Ahadithi kutoka kwa 'Uthman na Ali (a.s.) na Zaidi bin Thabit, na Abu Huraira, na Bushra binti Safwan na Abdulrahman bin Aswad bin Abd Yaghuth. Na mwanawe 'Abdul Malik na Sahl bin Sa'd Sa'idy (ambaye yu mtu mzima kuliko Marwan), Sa'id ibn Musayyab, Urwah bin Zubair, Abu Bakr bin Abdulrahman bin Harith, Ubaidullah bin 'Abdullah, bin 'Utbah Mujahid na Abu Sufyan (Mawla wa Ibn Abi Ahmad) wamepokea Ahadith kutoka kwake. Marwan alikuwa ni Katibu wa Khalifa 'Uthman bin Affan na mwenye utawala wa Mu'awiya alifanywa gavana wa Madina. Baada ya kufariki dunia kwa Mu'awiya bin Yazid bin Mu'awiya watu walikula kiapo cha utii kwa Ukhalifa wake. 'Urwah bin Zubair alisema kuwa Marwan hatiliwi shaka kwenye mapokezi yake."

Mtu ahitaji kusema mengi zaidi baada ya kuiona hiyo orodha ndefu ya watu waliopokea Ahadith kutoka kwa mtu huyu? Haishangazi kumwona mtu huyu akizipamba kurasa za Sahih Bukhari, Sahih Muslim, na Sunan Abi Dawuud

8. Abdullah bin Hani Azdi

Adui mwingine wa Bwana wa Mashahidi (a.s.) alikuwa ni Abdullah bin Hani Azdi. Mtu huyu alikuwa ni askari wa jeshi la Hajjaj bin Yusuf. Alikuwa kila mara akisema: "Ninazo sifa nyingi ambazo hakuna yeyote yule aliye nazo. Kwanza, katu, hatujawahi kumsema kwa ubaya Khalifa Abdul Malk ibn Marwan; pili, wanawake wetu wameapa kwamba iwapo Husayn bin Ali atauawa, kila mmoja wao atatoa sadaka ngamia warefu kumi. Hivyo wote wakafanya hivyo (alipouawa Husayn), tatu, hakuna hata mtu mmoja miongoni mwetu ambaye, alipoambiwa kumtukana Abu Turab (Ali a.s.) hakufanya hivyo, na katika kufanya hivyo asiwajumlishe Fatima, Hassan, Husayn nao". (Taarifa hii inatoka kwenye : "Sharh Ibn Abil Hadid, Juzuu 1, ukurasa wa 195). Adui wa Ahlul Bayt (a.s.) wa aina hii na mchochezi dhidi ya Imamu Husayn (a.s.) anathi-bitishwa uaminifu. Tahdhib imeandikwa hivi:

("Abdullah bin Hani Azdi) yu mfuasi mwaminifu wa Hajjaj bin Yusuf Thaqafi; amethibitishwa na 'Ijli kuwa yu mtu mwaminifu na wa kutegemeka".

9. Dhahhaka bin Qais na Ziad bin Sumaiyya n.k.

Zaidi ya hapo Dhahhak bin Qais na Ziad bin Sumaiyya na wengineo waliokuwa na uhusiano maalum na Yazid ni miongoni mwa wale ambao mapokezi yao yanahesabiwa na Mawahhabiya kuwa ni yenye kutegemeka.

Mpaka hapo tumetoa upande nimoja wa picha hii. Upande mwingine wa picha hii ni wa yule mtu ambaye kwa kusukumwa na nguvu ya huba yake kwa Ahlul Bayt (a.s.) aliwakamata wale waliomchinja Imamu Husayn (a.s.) na akawaua, anatukanwa na kulaumiwa. Hivyo basi, Mukhtar ibn Abu 'Ubaidah Thaqafi Rahmatullahi Alaih) anatukanwa kama ifuatavyo:

"Mukhtar ibn Ubaidah alikuwa mwongo mkubwa. Haifai kuyakubali mapokezi yake yoyote ya Ahadith kwa kuwa sio tu kwomba alijipoteza, bali vile vile alijaribu kuwapoteza watu. Alidai kwamba Jibrili alimjia. Mukhtar yu mwovu kama Hajjal au yu sawa na yeye. Inasemekana kwamba yeye yu mwongo ambaye Hadith ya Mtume ilimzungumzia kwamba kutokana na kabila la Thaqaf atajitokeza mtu mwongo na mchochezi. Hadithi hii imo kwenye Sahih Muslim" (Taarifa hii imechukuliwa kutoka kitabu Lisanul Mizan).

Maelezo haya yanaweza kumfanya mtu kufikiria kwamba pengine Bwana Mukhtar alikuwa na tabia za namna hiyo hasa na hivyo Ulama wa Rijal wakamfanyia upinzani. Lakini tunapoyatazama maelezo yaliyomo kwenye Isti'ab tunaona kwamba chuki yote hii inatokana na kwamba Bwana Mukhtar aliwaangamiza wauaji wa Husayn (a.s.). Hii ndio sababu iliyowafanya wale walioyachukia matendo yake walitwae rungu na kumsema kwa maneno ya uovu. Hicho kitabu kiitwacho Isti'ab kimeandika hivi:

"Mukhtar alidai kwamba katika kuilipizia kisasi damu ya Husayn (a.s.) alikuwa yu mjumbe wa Muhammad ibn Hanafiyyah. Hivyo akaomba msaada wa Ibrahim ibn Malik Ashtar na akawarukia wauaji wa Imamu Husayn (a.s.) na akawaua. Allah aliwafanya wengi wa wauaji wa Husayn (a.s.) kufa mikononi mwa Mukhtar; na ni kwa amri yake kuwa 'Ubaidullah ibn Ziad aliuawa na Ibrahim. Hii ndio sababu kwamba Waislamu wengi wanampenda na wale wasiozipenda itikadi zake humtukana na kumtusi."

Kwa kauli nyingine ni kuwa kiini cha maelezo haya ni kwamba wafuasi na wapenzi wa wauaji wa Imamu Husayn (a.s.) humtukana Bwana Mukhtar.

Kutokana na maelezo hayo hapo juu ni rahisi kuamua kuwa, Mawahhabiya huwatukuza wauaji wa Imamu Husayn (a.s.). Kila kiongozi wajeshi hili la wauaji amezipamba kurasa za Sihah. Wengi wao wamepewa vyeo vya kuwa wakweli, ukweli na kukubalika. Kwa upande mwingine, licha ya kuwa wauaji, wachochezi wa mauaji ya Imamu Husayn (a.s.) na kufukuzwa na Mtukufu Mtume wamefanywa kuwa Makhalifa. Kwa upande mwmgine, mwenye kuilipizia kisasi damu ya Imamu Husayn (a.s.) kama vile Bwana Mukhtar Thaqafi anashu-tumiwa kwa kupotoka na kuwa-poteza watu na kuwa mwongo na kuwa mwovu zaidi ya Hajjaj - na Allah anajua ni yapi mengineyo wayasemayo juu yake.