read

Al - Badau

Al-badau ni tuhuma miongoni mwa tuhuma ambazo wapinzani wa Shi’a wanaieneza dhidi yao kwa msukumo wa kimadhehebu bila ya kutazama kwa kina katika kusoma hoja ambazo Shi’a wamefahamu kutoka kwayo. Bali wapinzani wa Shi’a wanazidi kuelekeza tuhuma na kuwalaumu kwa sababu yake hadi Al-badau imekuwa ni moja ya tofauti za kimadhehebu ambazo zimetenganisha Shi’a na wasio kuwa wao.1

Badau kwa Shi’a ni kuongezeka umri na riziki na kupungua kwake kutokana na vitendo.2

Wanadai baadhi ya waandishi kwamba badau wanayoisema Shi’a ni kudhihiri kwa Mwenyezi Mungu yaliyokuwa hayafahamiki kwake. Na kauli hii ni batili, Shi’a wako mbali nayo. Lakini badau kwao ni kudhihiri baada ya kufichwa na sio kudhihiri baada ya kufichikana, Mwenyezi Mungu wakati kinadhihiri kitu kwake tayari yeye ana elimu tangu awali ya hili linalodhihiri kwake." Amesema Imam Swadiq (a.s): "Hakika hakidhihiri kitu kwa Mwenyezi Mungu isipokuwa kitakuwa katika elimu yake kabla ya kudhihiri kwake," na amesema (a.s): "Hakika Mwenyezi Mungu haidhihiri kwake ambako kumetokana na kutokujua."3

Na badau ipo katika itikadi ya Sunni ispokuwa haikufanyiwa utafiti kwao kama ilivyofanyiwa katika Shi’a.

Amepokea Bukhariy kutoka kwa Abu Huraira kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) Amesema: "hakika watu watatu katika Bani Israili wana mbalanga, kiziwi na kipofu ilidhihiri kwa Mwenyezi Mungu kwamba awape mtihani."4

Na kisa ni kirefu katika sahihi Bukhariy na mahala pa ushahidi hapa ni kauli yake (s.a.w.w) (Badaa lillahi) (ilidhihiri kwa Mwenyezi Mungu). Mtume (s.a.w.w) amenasibisha Albadau-ambayo wanaisema Shi’a kwa Mwenyezi Mungu, je, watajibu? Hao wapinzani ambao wanatuhumu Shi’a juu ya itikadi yao hii? Na katika Sahihi Muslim kutoka kwa Anas bin Malik amesema: "Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) anasema: "Anayependa akunjuliwe riziki yake au arefushiwe umri wake basi na auunge udugu wake."

Amesema Nawawiy katika kusherehesha Hadith: Ama kuahirisha mauti humo kuna suala mashuhuri nalo ni kwamba mauti na riziki zimekadiriwa haziongezeki wala hazipungui, inapokuja ajali yao hawacheleweshwi hata saa moja wala hawawahishwi. Na maulamaa wanajibu majibu sahihi juu ya hilo.

Jibu la pili- Ni kwamba kuhusu yanayodhihiri kwa Malaika, katika lauhul-mahfudh na mfano wa hayo, inadhihirika kwao katika lauhul-mahafudh kwamba umri wake ni miaka sitini isipokuwa akiunga udugu wake anazidishiwa arobaini, na Mwenyezi Mungu mtukufu anajua yatakayomtokea kwa ajili ya hiyo, nayo ndiyo maana ya kauli yake (s.a.w.w) "Anafuta anayotaka."

Na anathibitisha humo kulingana na elimu ya Mwenyezi Mungu na ambayo yametanguliwa na kudra yake kwamba hakuna ziada bali ni mustahili. Na kwa yaliyodhihiri kwa viumbe yanatupa picha ya kuongezeka, na ndio kusudio la Hadith.5

Haya ambayo ameyataja Nawawiy ndio badau halisi ambayo wanaisema Shi’a, na Aya aliyotolea dalili kwayo, ya kuunga mkono itikadi hii, ndio ile ile wanayoitolea ushahidi Shi’a.

Amesema Dkt. Hamid Daud Hanafiy: "Ilipokuwa badau ni katika sifa za viumbe, kwa sababu kufanya kitu kisha kukifuta inaonyesha fikira inayojitokeza, na kusahihisha baada ya kukosea na kufahamu baada ya kutokujua, hivyo wanafikra wengi wamepuuza akili za Mashi’a kwa kunasibisha badau kwa Mwenyezi Mungu mtukufu, na Shi’a wako mbali ambapo kilichobainikiwa kwao na kwa Maulamaa wa Kisuni ni kwamba elimu ya Mwenyezi Mungu ni ya zamani imeepukana na mabadiliko na kufikiri ambavyo ni katika sifa za viumbe.6

  • 1. Islaamunaa uk: 210
  • 2. Awailul-maqaalati-ya Sheikh Mufiyd
  • 3. Usul-kaafiy J: I uk:148
  • 4. Sahihi Bukhariy kitabul- Ambiyai - Hadith abras wa a'amaa wa aqirasu fiy bani Israil
  • 5. Sahihi Muslim sharhe ya Nawawiy kitabul-biru wa swilatu wa adaabu babu swilatu rahmi wa tahariymi Qatwi'uhu
  • 6. Utangulizi wa "kitabu cha Aqaudul - Imamiyah uk: 25