read

Itikadi na Athari ya Mazingira

Hakika mazingira na nyakati mara nyingi zimekuwa na athari kubwa katika kupanga fikra ya binadamu na mwelekeo wake, ambapo urithi wa kimazingira unakuwa kadiri muda unavyopita pamoja na kuzoeleka, kimaneno na kitabia unakuwa ni ukweli thabiti ambao hawezi kuuepuka; mwanadamu akitokewa na jambo linalopinga itikadi zake, athari za kifikra za jamii yake ambazo zimeshatawala katika mishipa yake zinajitokeza bila kuhisi na kusimama kidete kupinga kila anayezikhalifu, lakini Mwislamu ambaye ni mtu adhim, dini inamlazimisha kukaribisha fikra za wengine na kuzijadili kwa uhuru na kwa maudhui.

Tukiuangalia umma wa Ki-Islamu tutaukuta uko makundi mengi “kila kundi linafurahia liliyonayo”1 kila kundi miongoni mwa makundi ya Ki-Islamu linaona fikra zake kuwa ni katika vitu ambavyo havipaswi kupingwa2. Na unapojadili fikra za wengine basi unaonekana utabeba mila zao na utamaduni wao, pamoja na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anawalingania waislamu wawe wazi kwa Ahlul-kitabu tukiachilia mbali kuwa wazi baina yao, amesema Mwenyezi Mungu (Sema: Enyi Ahlul-kitabu njooni katika neno la sawa baina yetu na baina yenu, tusimwabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu na wala tusimshirikishe na chochote.3

Kwa nini waislamu wasiwe wazi baina yao? Kwa nini watu wa dini moja wasiwe na muamala baina yao? Je, kila mmoja wetu amechagua madhehebu yake kwa fahamu na kujua? Na baada ya kusoma na kuhakiki au amejiungaje? Lazima tukubali kuwa jambo hili litakuwa gumu sana tutakapopata mambo yanayohusiana na itikadi, mila na mambo ya kurithi ambayo yameota mizizi ndani ya mishipa yetu na nafsi zimeyazoea.

Kama utamuuliza kijana aliyezaliwa katika mji wa Najaf, je, utakuwa Shi’a kama utazaliwa na wazazi wa Kisunni? Vivyo hivyo kama utamuuliza aliyezaliwa Halab, je, utakuwa Sunni kwa njia hii kama utakuwa umezaliwa katika mji wa Najaf katika familia ya kishi’a? Hapa hawatatofautiana kati yetu watu wawili kuhusu jawabu - Hapana - ambalo tutalisikia bali tunaweza kuweka jawabu mwanzo, kuwa ni katika mambo ya kawaida ambayo hakuna ikhitilafu humo.

Tanmbihi hii peke yake inatosha kutuweka wazi juu ya ukweli halisi na inatosha kutuletea mshangao wa muamala huu mgumu, na kukimbiana unaopatikana baina yetu. Kasumba zimetufikisha kiasi hicho cha hatari, hadi kasumba kwa kitu chochote tulichokizoea mazoea makubwa zaidi kuliko kuwa kwetu tayari kushikamana na hukumu ya kisheria iliyothibiti…….

Ni kipi kinanifanya katika itikadi yangu – nijisalimishe - ni madhehebu yangu niliyoyarithi kutoka kwa baba zangu na jamii yangu ndogo kuwa ndio haki pekee? Na kwamba ndio picha iliyokamilika zaidi ya dini ya Uislamu Mtukufu kiasi kwamba hailingani na madhehebu mengine katika daraja la ukamilifu? Ni nini kilichonipelekea kwenye itikadi hii? Ni Qur'an Tukufu, Sunna takatifu, akili sahihi au ni taasubu ambayo haina mashiko?

Kwa nini nisiweze kuitakidi kuwa madhehebu mengine ni kama madhehebu yangu? Je, si nitaulizwa kesho juu ya sababu ya kufuata kwangu na itikadi yangu ya kidini?

Swali hili muhimu ndio ambalo ni wajibu niwe na msimamo madhubuti…… mbele ya ukweli huu, hakuna pa kukimbilia kwani sote tuko sawa katika majukumu, jukumu la kutafuta, kuhakiki na kisha kuchagua msimamo sahihi wakielimu usiegemee upande wowote na usivuke mipaka. Na sote tuko sawa katika hoja ya kurejea misimamo yetu kisha kuijenga upya katika misingi sahihi.4

  • 1. Suratul-Mu’minoona:53
  • 2. Nadharia hii ni yenye makosa na ameilaumu Mwenyezi Mungu katika kitabu chake kauli hii ni kama kauli ya washirikina wa kiarabu: “Hakika sisi tumewakuta baba zetu wako katika mila na sisi ni wenye kuwafuata nyendo zao” (Zukhruf. 23)
  • 3. Surat Ali-Imraan: 64
  • 4. Manhaju fiyl intimail - madhihabi - kitabu cha Swaibu Abdul-hamid Uk. 15-30