read

Kisimamo Pamoja na Salafia

Salafia wanakhalifu kundi la Sunnatu wal-Jamaah katika kuchukua mafunzo ya Ki-Islamu, wakati ambapo Sunni wote wamefuata maimamu wanne na wanafanya ibada kulingana na fatwa zao, salafia wanawachukulia mabwana hawa ni kama maulamaa wengine wa waislamu, na wala uislam haujafungamanishwa kwao tu, bali kufahamu uislamu sahihi ni kurejea kwenye kitabu na Sunna kwa kunukuliwa na sahaba yeyote. Na aliyekuja baada yao.

Sisi tuna-afikiana nao katika kutegemea Kitabu na Sunna kama misingi miwili ya Ki-Islamu lakini je, inawezekana kuchukua Sunna kutoka kwa sahaba yeyote, vyovyote itakavyokuwa sira yake bila yakuiangalia hali yake kama ilivyo manhaji ya salafia? Au ni wajibu tumwingize katika kanuni ya kukosoa na kurekebisha na kusoma maisha yake, na kama utathibiti msimamo wake na umadhubuti wake katika kunukuu, ndio inachukuliwa kutoka kwake? Amepokea Bukhariy kutoka kwa Abu Wail; amesema Mtume (s.a.w.w): "Mimi nitawatangulia kwenye birika, wataletwa kwangu wanaume miongoni mwenu hadi nitakapotaka kuwapa maji watazuiliwa dhidi yangu; Nitasema: Ee mola masahaba wangu, nitaambiwa: "Hujui waliyoyazusha baada yako."1

Na katika riwaya nyingine: "Watanijia watu nawajua na wananijua, kisha kutawekwa kizuizi
baina yangu na wao.2

Na kutoka kwa Abu Huraira, hakika yeye alikuwa amesimulia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) amesema: "Watanijia siku ya Qiyama kundi kati ya masahaba wangu watazuiliwa kufikia birika, nitasema: Ee Mola wangu masahaba wangu. Itasemwa: "Hakika wewe hujui waliyoyazua baada yako, hakika wao waliritadi na kurudi nyuma.3

Hadith hizi zinaeleza wazi kuingia masahaba motoni na tatizo hilo liliwapata salafia, hivyo wakafasiri kuwa waliokusudiwa katika Hadith ni wanafiki na walioritadi, na tafsiri hii sio sahihi.

Riwaya inabainisha sababu ya hawa kuingia motoni nayo ni kuritadi na kuzua,…na mnafiki haritadi kwa sababu yeye hakusilimu asilani na historia haikututajia chochote juu ya uzushi wa wanafiki.4

Tafsiri ya kuwa ni walioritadi inapingwa kwa sababu sehemu kubwa kati yao walioritadi katika uhai wa Mtume (s.a.w.w) vipi atasema kuingia kwao motoni? Na wala hawajazua kitu katika dini bali waliritadi tu na si vinginevyo, kuna riwaya inayosema: "Baada ya maswahaba kuingizwa motoni Mtume atasema: 'Sioni akiwaacha isipokuwa kama mfano wa ngamia wasio na mchungaji."5

Ibnu-Hajary ameseama: Na 'hamalu' kwa fataha mbili: Ni ngamia asiye na mchungaji na maana yake ni kwamba "Hataingia katika birika miongoni mwao isipokuwa wachache kwa sababu ngamia asiyekuwa na mchungaji katika ngamia ni wachache ukilinganisha na wengine.”6

Na imekuja katika kamusi "Lisanul-Arabi na Nihayatu ya Ibnu Athiri" yaani watakaofaulu kati yao ni wachache kwa maana ya uchache wa ngamia wenye kupotea.7

Kwa kuongezea haya hakika kuna riwaya kutoka kwa maswahaba walio karibu na Mtume walikiri wenyewe kuzua na kubadilisha baada ya Mtume (s.a.w.w), nazo zinafasiri Hadith zilizotangulia kiasi kwamba hakubaki kwa salafia taawili yoyote au kisingizio katika Hadith ya birika (hodhi).

Amepokea Bukhari kwa sanadi yake kutoka kwa Alau bin Abdi Musayabu, kutoka kwa baba yake amesema: "Nilikutana na Baraa bin Aazib akasema: "Umefaulu; ulikuwa sahaba wa Mtume na ukambayi chini ya mti." Akasema: "Ewe mtoto wa ndugu yangu hakika wewe hujui ambayo tumeyazua baada yake."8

Anasi bin Malik amesema: "Sijui kitu kati ya yaliyokuwa katika wakati wa Mtume (s.a.w.w) isipokuwa machache;" akaulizwa na sala? Akasema: "Si mmepoteza humo mliyoyapoteza."9

Abu Dardai amebainisha balaa ya msiba na kubadilika hali ya watu waliyokuwa nayo katika zama za Mtume (s.a.w.w) Bukhary ameitoa amesema: Nilimsikia Salim anasema: Na nimemsikia Ummu Dardai amesema: "Aliingia kwangu Abu Dardai naye ni mwenye kukasirika nikasema: kipi kimekukasirisha?" Akasema: "Wallahi sijui chochote katika umma wa Muhammad isipokuwa wote wanasali."10

Mtume (s.a.w.w) alishabainisha hali ya maswahaba baada yake kwa sura iliyo wazi kutoka kwa Abdillahi bin Amr bin Aasi kutoka kwa Mtume (s.a.w.w) kwamba yeye amesema. "Zitakapofunguliwa kwenu hazina za Fursi na Roma nyinyi mtakuwa ni kaumu gani?" Abdu Rahmani bin Auf akasema: "Tutasema kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume wa Mwenyezi Mungu:" Mtume akasema: "au yasiyo kuwa hayo?"

"Mtashindana! kisha mtashindana! Kisha mtafanyiana njama, kisha mtachukiana au mfano wa hayo kisha mtawaendea masikini miongoni mwa muhajirina na watawakandamiza baadhi yao."11

Na katika Hadith ya Amri bin Auf, aliwasili Abu Ubaida na mali kutoka Baharaini, Answar wakapata habari ya kuwasili kwa Abu-Ubaida, wakahudhuria sala ya Alfajiri pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) Mtume aliposali akaondoka, wakamwashiria Mtume wa Mwenyezi Mungu, akatabasamu alipowaona akasema: "Nadhani mmepata habari kuwa Abu Ubaida amekuja na chochote kutoka Baharaini, wakasema: "Ndio ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Akasema; "Furahini na pendeni yanayokufurahisheni, wallahi siwaogopei ufakiri, lakini naogopa kwenu Dunia kuwanyookea kama ilivyowanyookea waliokuwa kabla yenu, mkaishindania kama walivyoishindania basi ikawaangamiza kama ilivyowaangamiza.12

Mtume (s.a.w.w) ametilia mkazo katika Hadith nyingine akiweka wazi humo kwamba Maswahaba zake watawafuata waliokuwa kabla yao, amesema (s.a.w.w): "Mtafuata nyendo za waliokuwa kabla yenu shibri kwa Shibri, dhiraa kwa dhiraa hata kama wataingia katika shimo la kenge mtawafuata."

Tukasema "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni mayahudi na manaswara? Akasema: "Ni nani basi?"13

Imetubainikia kwamba haiwezekani kwa Mwislamu kupata matumaini katika kuchukua kutoka kwa swahaba yeyote kama ilivyo manhaji ya salafia, tuna-afikiana nao katika Kitabu na Sunna, lakini watakaozifafanua kwa watu ni maimamu wa Ahlul-Bait kulingana na dalili zilizothibiti.

 • 1. Sahihi Bukhariy kitabul-fitani babu maaja fiy qaulilahi talaa wataquu- fitina laa twisibanna aladhiyna dhalamuu min khum khaswa
 • 2. Sahihi Bukhariy kitabul-fitani babu maaja fiy qaulilahi talaa wataquu- fitina laa twisibanna aladhiyna dhalamuu mii khum khaswa na sahihi muslimu kitabu fadhail babu ithibati haudhi nabiyinaa (s.a.w.w)
 • 3. Sahihi Bukhariy kitabu riqaqi babu fiyl-haudhi
 • 4. Haitaji chochote katika harakati zao dhidi ya uislamu na waislamu, je: Abubakar alikuwa mwerevu zaidi kuliko Mtume (s.a.w.w)? Hivyo akawavutia kati- ka uislamu na nyoyo zao zikawa safi au wao waliridhia hali ya kisiasa iliyokuwepo wakati huo na ikawastaajabishwa hivyo wakasimamisha njama zao walizokuwa wakimfanyia Mtume (s.a.w.w) na Qurani ikazifichua? Inanibainikia kuwa nukta hii ni muhimu sana kuifikiria na kuifuatilia
 • 5. Sahihi Bukhariy kitabu riqaqi fiy haudhi
 • 6. Fatuhul Bar J: 11 uk. 401
 • 7. Lisanul Arabi-J:15 uk. 135, Nihayatu fiy ghariybil Hadath J:5 uk. 274
 • 8. Sahihi Bukhariy kitabul- Maghaaziy babu ghazuwatil -hudaibiyah
 • 9. Sahihi Bukhariy kitabu Mawaaqiti Swalati babu tadhiyi'i swalati
 • 10. Sahihi Bukhary J:2. uk 159
 • 11. Sunan Ibni Maajah kitabu Ifitan babu fitnatul -maali
 • 12. Sunan Ibni Maajah kitabu Ifitan babu fitnatul -maali, Sahihi Bukhari kitabu maghazi J.5 199
 • 13. Tumeshataja baadhi ya matatizo ya salafia katika kitabu "Warakibtu Safinah"