read

Maudhui Haya ni ya Nini?

Mtume (s.a.w.w) alitupa habari kwamba umma wake utagawanyika makundi sabni na tatu, yote yataingia motoni isipokuwa moja litaingia peponi.1 Na leo tunaona kwamba waislamu wako makundi mengi na kila moja linadai liko katika haki, na nimeona jambo hili ni muhimu sana na kwayo imesimama hatima ya waislamu, hivyo ni muhimu sana kwa kila mwislamu anayetaraji nusura siku ya Qiyama lazima ajitahidi kujua kundi hili na kulifuata.

Al-hamdulillahi mimi nimeshafanya hivyo, baada ya utafiti mkubwa, nimeshalipata kundi hili, imenithibitikia kwa dalili ya kiakili na ya kunukuu kwamba ndilo lenye kufaulu na nitathibitisha hayo katika utafiti huu.

Na ni ajabu kwamba Mwislamu anasoma Hadith hii ya kufarikiana na wala hafanyi wajibu wake wa kisheria, katika kutafuta kundi hili, kwa uhuru na kwa maudhui, ili aondoe dhima yake na akutane na Mola wake kwa moyo uliosafi.

Ni wajibu kwa Mwislamu baada ya kupita muda mrefu tangu kuja Mtume (s.a.w.w) na kutofautiana kwa madhehebu na maoni, mifarakano mingi na makundi, afuate njia ambayo anaamini kuwa inamfikisha katika kujua hukumu zilizoteremshwa kwa Muhammad (s.a.w.w) mwenye kuteremshiwa wahyi, kwa sababu Mwislamu anatakiwa kutekeleza kwa vitendo hukumu zote zilizoteremshwa katika sheria kama zilivyoteremshwa, lakini atajuaje kwamba hizi ndizo hukumu zilizoteremshwa, na ziko kama zilivyoteremshwa?
Na waislamu wametofautiana, makundi yamegawanyika, swala sio moja, ibada haziafikiani, wala vitendo katika muamalati zote haviko katika muundo mmoja.

Atafanyaje? Ni kwa njia gani atasali? Na ni muundo gani katika maoni atafuata katika ibada zake na muamalaati zake? Kama vile ndoa, talaka, mirathi, kuuza na kununua, kutekeleza adhabu kutoa fidia n.k.

Na wala haijuzu kwake kufuata baba zake na kubaki katika aliyowakuta watu wake na rafiki zake, bali ni lazima apate yakini kati yake na nafsi yake na baina yake na Mola wake, kwani hapa hakuna upendeleo, kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa, kutofungamana na upande wowote wala kasumba.

Lazima apate yakini kuwa amefuata njia bora, ambayo anaitakidi kuwa ametimiza dhima yake, baina yake na Mwenyezi Mungu katika majukumu aliyofaradhishiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na anayoamini kuwa hakuna adhabu juu yake wala lawama kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika kufuata kwake, na kuchukua kwake hukumu kutoka kwayo, na wala haijuzu kumgusa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu lawama ya mwenye kulaumu.

"Je, mwanadamu anadhani ataachwa bure"2

"Bali mwanadamu anaijua vizuri nafsi yake"3

"Hakika huu ni ukumbusho basi anayetaka afuate njia iendayo kwa Mola wake"4 na 5

  • 1. Rejea Hadith ya kufarikiana katika Mustadrk.ak J: 1 uk: 6.1-128 na Sunan Tirimidhiy J:5 uk:26 na Musnad Ahmad J: 2 uk: 332
  • 2. Suratul-Qiyama:36
  • 3. Suratul- Qiyama:41
  • 4. Suratul - Muzzammil: 19
  • 5. Aqaidul- imamiyah Muhammad Ridhaa Mudhafar uk:63-64